Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XXIII ya Mwaka C wa Kanisa: Wafuasi wa Kristo wanahitaji nguvu na msaada wa Roho Mtakatifu ili kutimiza masharti ya kumfuasa Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XXIII ya Mwaka C wa Kanisa: Wafuasi wa Kristo wanahitaji nguvu na msaada wa Roho Mtakatifu ili kutimiza masharti ya kumfuasa Kristo Yesu.  

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka C: Msaada wa Roho Mtakatifu

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Ujumbe mkuu leo ni kuwa ukristo ni gharama; unadai kubeba Msalaba, kuchukia familia zetu, mali na hata nafsi zetu. Kwa mtazamo wa kibinadamu jambo hili si rahisi, lakini kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu inawezekana. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafuta msaada wa Roho Mtakatifu katika ufuasi.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 23 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu leo ni kuwa ukristo ni gharama; unadai kubeba Msalaba, kuchukia familia zetu, mali na hata nafsi zetu. Kwa mtazamo wa kibinadamu jambo hili si rahisi, lakini kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu inawezekana. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani ni sehemu ya sala ya Mfalme Sulemani alipomwomba Mwenyezi Mungu hekima ili aweze kutambua mema na mabaya na aweze kuwaongza watu wake katika haki na kweli. Somo hili latufundisha kumtegemea Mungu katika shughuli zetu za kila siku, hasa katika magumu na katika uamuzi wa jambo lolote kubwa likisema, kwa kuwa mawazo ya wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa; na mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko. Kwa shida tu tunayapambanua yaliyoko duniani, na yaliyo karibu nasi ni kazi kuyaona na ya mbinguni tusiyoyaona na shida zaidi.

Katika somo la pili Mtume Paulo anamwandikia Filemoni akimshauri ampokee Onesimo aliyekuwa amemtoroka, si kama mtumwa wake tena, bali kama ndugu halisi akisema; mimi Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Kwa ubatizo sisi sote ni ndugu, hakuna ubaguzi wowote ndiyo maana Paulo anasema, tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ni ndugu mpendwa kwangu mimi sana na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Yesu kupitia kinywa cha mwinjili Luka, anatufundisha kuwa katika kuitika mwito wa Mungu, ndugu na familia wanachukua mahali pa pili. Yesu anadai kuwa kumfuata Yeye ni sadaka na kunahitaji udumivu akisema, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Na mtu ye yote asiyeuchukua Msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Katika Injili ya Yohane Yn 13:34-35, Yesu anatufundisha akisema, “Amri mpya nawapa; pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi”. Leo anatufundisha tuwachukie wazazi, watoto, jamaa, mali zetu hata nafsi zetu wenyewe. Je, Yesu anajipinga? Jibu ni hapana. Ujumbe wa msingi na maana hapa ni kuwa kama wazazi, watoto, marafiki, jamaa zetu, mali na hata nafsi zetu, zinatufanya tutende dhambi ni afadhali tuachane na haya yote kuliko kwenda kinyume cha mapenzi Mungu. Uhusiano wetu na wanafamilia au marafiki haupaswi kupingana na uhusiano wetu na Kristu. Hii ndiyo gharama na amana ya kumfuasa Kristi na ya imani yetu, ndiyo gharama ya ufuasi wetu kwa Kristo na ndiyo gharama ya ukristo wetu. Jambo hili si rahisi kulipokea na wala si rahisi kuacha malimwengu. Hii ni kwa sababu mapendeleo ya mwili mara nyingi yanapingana na mapenzi ya Mungu kwani mwili wenye uharibifu, huigandamiza roho.

Mtazamo wa kidunia ni tofauti na mtazamo wa Kimungu, kama Paulo anavyotuambia, kuwa ujumbe wa Msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu, upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu (1Kor 1:18, 25). Hata jambo hili nalo ni ngumu kulielewe kwa akili zetu za kibinadamu kama anavyosema nabii Isaya, mawazo ya Mungu si mawazo yetu, na njia zake si njia zetu kama mbingu zilivyo mbali na dunia ndivyo yalivyo mawazo ya Mungu na yetu. Lakini tukiwa na moyo wa unyenyekevu na imani Mungu atatufunulia ukweli huu. Hii ni kwa sababu, matatizo ya maisha yanaleta changamoto kubwa sana kwa imani yetu kwa maana kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko. Akili zetu zinashindwa kubaini mambo ya Mungu katika uzuri wake na utamu wa mambo ya dunia huzifumba akili zetu, kwa shida tu, twayapambanua yaliyoko duniani, ndivyo anavyotuambia Yoshua Bin Sira katika somo la kwanza.

Hivyo tunamhitaji Roho Mtakatifu atufanye tuishi kama mwanafunzi wa Kristo, atufundishe kuyaelewa mambo ya Mungu, kwani mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye isipokuwa Roho wa Mungu” (1Kor 1:11). Mtume Paulo aliwaasa Wagalatia akisema, Basi nasema hivi, mwenendo wenu na uongozwe na roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Matokeo ya kuongozwa na roho ni Mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (Gal 5:16,22 – 25). Daima tuombe kuyapata hayo matokeo na kuyafanya yatawale maisha yetu. Tuwe wanyeyekevu na kukubali kufundishwa na Roho Mtakatifu tuwe na sikio sikivu kama anavyosema Nabii Isaya “Huniamsha sikio langu lipate kusikia kama wafundishwao” (Isa 50:4) tumwombe ayafungue macho yetu ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo. Tumsifu Yesu Kristo.

J23 Mwaka C
12 September 2019, 07:24