Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka: Huruma ni Jina jipya la Mungu
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo, yanatuonesha jinsi huruma ya Mungu ilivyo kuu, haina mipaka ni ya milele. Mungu daima yuko tayari kumsamehe mkosefu anayetubu. Waisraeli, Mwana mpotevu na Mtume Paulo ni mifano wazi inayotuonesha huruma ya Mungu juu ya yule atubuye dhambi zake. Huruma ni jina jipya la Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujitambua kwamba wao ni wadhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Hii ni neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi zinazotendwa na mwanadamu na kwamba, msamaha wake ni dawa makini dhidi ya dhambi. Mwenyezi Mungu kama iluvyokuwa kwa Baba mwenye huruma daima anawasubiri watoto wake kukimbilia huruma, kwa njia ya toba. Kitendo cha mwamini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu kinaonesha toba ya ndani, sala inayopaswa kujikita katika unyenyekevu wa moyo badala ya litania ya maneno mengi!
Somo la kwanza la kitabu cha Kutoka, linasimulia jinsi wana wa Israeli walivyomwasi Mungu kwa kujitengenezea mungu wa ndama wa dhahabu, wakaiabudi na kuitolea dhabihu. Kwa tendo hili wana wa Israeli waliivunja amri ya kwanza ya Mungu (Kut 20:3-6) na kwa namna hiyo walivunja agano na Mungu wao walilolifanya mlimani Sinai, Agano lililotanguliwa na tamko: “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri katika nyumba ya utumwa” (Kut 20:2), kisha ikafuata amri: “Usiwe na miungu mingine ila Mimi”. Kwa hiyo, Waisraeli walipojitengenezea ndama na kuiabudu na kuitolea dhabihu walivunja amri ya kwanza ya Mungu, wakatenda dhambi mbele ya Mungu. Mungu akaazimia kuwaangamiza na kuunda taifa jipya toka kwa Musa. Musa anachukua jukumu la kikuhani na kinabii, analiombea Taifa lake kwa Mungu wa kweli, akitolea sala ya kuomba msamaha na kufanya toba. Lakini maombezi ya Musa hayategemei mastahili ya watu wake, bali yanategea upendo aminifu na huruma ya Mungu kwa watu wake iliyo ya milele na isiyo na mipaka wala ukomo. Kwa ajili ya sala ya Musa, Mungu akaughairi uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.
Paulo alikuwa ni mpinzani wa Kristo, aliwatesa na kuwaua wafuasi wa Kristo kwa muda mrefu hadi alipokutana na Kristo akiwa njiani kwenda Damasko. Tukio hilo lilibadili msimamo na hali ya maisha yake na muono wake. Hakusita kukiri makosa yake yote na kuanza maisha mapya. Katika somo la pili la waraka wake wa kwanza kwa Timotheo anafafanua kuwa “Yesu Kristo alikuja ulimwenguni kusudi awaokoe wenye dhambi.” Naye anashukuru kwa msamaha, neema na baraka alizozipokea kutoka kwa Kristo akisema: Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri; lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Nasi pia tukifuata mfano wa Mtume Paulo, wa kuitikia mwito wa Kristo na kukiri madhaifu yetu, kuachana na maisha ya dhambi na kuanza maisha mapya tukiongozwa na Roho Mtakatifu, huku tukimshukuru Mungu, maisha yetu yatajaa furaha.
Mwinjili Luka leo anatupa mifano mitatu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Kondoo aliyepotea, Shilingi iliopotea, na Mwana mpotevu. Mifano yote mitatu yaonyesha furaha ilivyo kuu mbinguni, juu ya mkosefu anayetubu na kumrudia Mungu. Ili kulielewa fundisho hili ni muhimu kutambua kwamba mifano yote mitatu inawalenga Mafarisayo na Waandishi kwa chuki waliyokuwa nayo kwa wakosefu na wadhambi kiasi cha kumkosoa Yesu kwa kuwapokea na kushiriki nao chakula. Lakini pia tutambue kuwa mifano hii mitatu inategemeana na kukamilishana kwa yenyewe lazima kuisoma na kuielewa kwa pamoja katika utatu ulio katika umoja. Mifano miwili ya mwanzo yaani kondoo aliyepotea na shilingi iliopotea inasisitiza ukweli kwamba ni Mungu anayeanza kufanya jitihada za mwanzo kwa wongofu wa wakosefu; ni Mungu anayeondoka kwenda kuwatafuta waliopotea. Asili ya fumbo la ukombozi ni Mungu mwenyewe. Ndivyo tunavyopaswa kufanya hata sisi kuwatafuta na kuwasamehe waliotukosea. Fundisho kuu katika mifano hii ni kuwa msamaha huanza kutolewa na aliyekosewa bila kutegemea hali ya mkosefu.
Mfano wa Baba mwenye huruma unaweka msisitizo juu ya namna Mungu anavyoheshimu uhuru wa binadamu na kusubiri kwa shauku na hamu kubwa kurudi kwake mwenye dhambi kama baba mwenye huruma kwa mwana mpotevu. Mungu hatushurutishi kurudi kwake na kuomba msamaha bali anatupa mda akitusubiri kwa hamu kubwa turudi kwake na kusema nimekosa nihurumie naye mara anatusamehe na kutufanya tena watoto wake na kutukaribisha katika ufalme wake milele yote. Kimsingi baba mwenye huruma aliwapoteza watoto wake wote wawili. Tofauti ni kwamba yule mdogo alipotea nje ya nyumba kama kondoo aliyepotea nyikani na yule mkubwa alipotea ndani ya nyumba kama shilingi iliyopotea. Makosa ya mwana mpotevu ni mengi na mazito. Alidai urithi kwa baba yake wakati angali hai, hiyo ilikuwa sawa na kusema: “Baba utakufa lini? Baba kwanini unachelewa kufa? Baba huoni kuwa mda wako wa kuishi umeisha, kwanini unaendelea kutuzibia ridhiki yetu?” Pili aliuza urithi wake. Kwa tendo hilo, aliondoa mali toka katika familia yake na hivyo kutoiachia urithi tena.
Tatu alikwenda nchi ya mbali. Kwa tendo hilo aliinyima familia yake huduma yake na katika maisha ya kifamilia hayo ni makosa mazito sana. Huko alikokwenda alitumia mali za baba yake kwa anasa kama anavyosema kaka yake kuwa alikula na kunywa pamoja na makahaba. Mbaya zaidi ni kulisha na kutamani kula makombo ya nguruwe tendo ambalo lilikuwa haramu kwa Myahudi. Pamoja na hayo yote alipojichunguza moyoni, akajutia matendo yake, akaamua kurudi kwa Baba yake na kuomba msamaha. Mwana huyo alipoomba radhi alisamehewa, alifanyiwa sherehe, alirejeshwa katika familia. Hii ni kuonyesha huruma ya Mungu kuwa ni ya milele na upendo wake kwetu sisi wanae ni mkubwa kiasi kwamba hakuna dhambi kubwa ambayo Mungu hawezi kuisamehe isipokuwa kufuru kwa Roho Mtakatifu yaani kukata tamaa na kushindwa kuomba msamaha. Kwa upande mwingine yule mwana wa pili, naye alipotea lakini ndani ya nyumba kama shilingi.
Kwa kiburi, chuki na wivu anamkataa ndugu yake na hata kumwambia baba yake “mtoto wako huyu aliyekula mali zako pamoja na makahaba (Lk 15:28-30). Kumbe hata yeye ni mpotevu. Baba yake anatoka kumtafuta na kumsihi afurahi pamoja na familia yake. Baba mwenye huruma anafanikiwa kumpata mdogo. Je, atafanikiwa kumpata na huyu mkubwa? Kila mmoja ajiulize yeye ni kijana yupi aliyepotea ndani ya nyumba kama shilingi au aliyepotea nje ya nyumba kama kondoo? Iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma! Tumsifu Yesu Kristo.