Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXVI: Lazaro & Tajiri jeuri!
Padre Reginald Mrosso, C.PP.S., - Dodoma.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini wanaolala mlangoni pa matajiri si kero inayopaswa kushughulikiwa kama “chuma chakavu” bali ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu sanjari na kubadili mfumo wa maisha, tayari kuwakumbatia na kuwasaidia wengine katika shida na mahangaiko yao. Huu ni mwaliko wa kujitahidi kumwilisha sehemu ya Injili la Lazaro maskini na tajiri asiyejali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zake. Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwinjili Luka anamchambua kwa kina na mapana Lazaro maskini, aliyekuwa anawekwa mlangono, akiwa na vidonda vingi naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyokuwa yanaanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakavilamba vidonda vyake. Hii ni picha ya tajiri na maskini aliyedharauliwa na kunyenyekeshwa kwa nguvu!
Maskini huyu alikuwa anaitwa Lazaro, maana yake “Mungu anatusaidia”. Kumbe, hapa kuna mtu mwenye historia, utu na heshima yake! Maskini mbele ya yule tajiri alionekana kuwa si mali kitu! Lakini kwa waamini ni mtu anayepaswa kufahamika, kwani ana sura, ni zawadi na utajiri mkubwa unaopaswa kukumbatiwa; kupendwa kwa kukumbuka kwamba, hata Mwenyezi Mungu katika ukamilifu wake, daima amekuwa akiwekwa pembezoni mwa maisha ya binadamu. Fuatilia kituko kifuatacho! Baada ya kifo na akiwa kwenye kiti cha hukumu, aliambiwa na Malaika, jina lako haliko katika orodha ya waingiao mbinguni. Hivyo nenda motoni. Yule mtu aling’aka kwa ukali, mbona sijafanya kitu? Malaika akamwambia na hii ndiyo hukumu yako. Kwamba hukufanya cho chote. Ndugu wapendwa, leo tunaalikwa kutafakari sana kuhusu wajibu wetu wa kikristo. Wengi wetu hudhani kwamba kutokufanya kitu ndilo jibu. Tunasahau kuwa sisi tunawajibu wa kufanya kitu na zaidi sana kwa mkristo ni wajibu si hiari.
Hiki ndicho alichokuja kufanya Bwana wetu Yesu Kristo Mwokozi. Sisi tulikuwa tumetindikiwa, tumetenda dhambi. Akawa kwetu sababu ya msamaha. Hata katika hukumu yetu ya mwisho, tutahukumiwa kwa matendo yetu. Angalia Mt. 25 – nilikuwa na njaa ukanipa chakula nk. Aliyehukumiwa ni yule ambaya anasema ni lini ulikuwa na njaa – anahukumiwa kwa kutokuona na kutokufanya cho chote. Mshangao huu utawakumba wengi wataosoma injili ya leo juu ya habari ya Lazaro na tajiri. Katika somo hili kuna mishangao mingi. Tujaribu kuiangalia. Hatuambiwi kwa mfano yule tajiri alipataje ile mali au kama alikuwa na lazima ya kumtunza Lazaro au kwamba yeye ni chanzo cha umaskini wake Lazaro. Hatuoni mahali ambapo Lazaro aliomba kitu kwa yule tajiri akanyimwa. Hatuoni kosa alilofanya yule tajiri dhidi ya Lazaro. Tunaona kuwa aliishi kama waishivyo watu waliofanikiwa katika maisha. Hapa tunatakiwa kutafakari sana maana ya injili ya leo na ujumbe wake kwetu. Hatuna budi kuwa macho hapa – kwa sababu mahangaiko yetu hapa ni kutaka kupata maisha mazuri, kufanikiwa katika maisha, kuishi vizuri n.k. Kwa nini huyu mtu alienda motoni?
Mara nyingi tunapofikiria dhana ya dhambi upo uwezekano wa kuishia tu kuomba msamaha kwa kukosa kwa mawazo, maneno na matendo. Hatukumbuki sehemu inayomalizika na kwa kutotimiza wajibu. Ndicho kilichomkumba yule tajiri. Angalia tena Mt. 25 … nilikuwa mgonjwa hukuja kunitazama n.k. Jambo lingine ambalo pia linatushangaza ni kwa nini Lazaro aende mbinguni? Hatuambiwi kuwa alikuwa mcha Mungu na wala kwamba alitenda jambo jema au kitu cha pekee. Tunaambiwa kuwa huu ni mfano pekee katika Injili ambapo jina la mhusika linatajwa. Hivi jina litasaidia sana kuelewa maana ya mfano huu. Jina Lazaro maana yake ni ‘Mungu ni msaada wangu’. Hivyo Lazaro si tu maskini bali maskini amwaminiye na kumtumainia Mwenyezi Mungu. Imani hii ilimsaidia kukutana na Abrahamu kule paradisi. Wazo kuu hapa ni kuwa utajiri au umaskini si mlango wa kuingia mbinguni. Kuamini na kumtumainia Mungu ndiyo jibu. Ndicho mtume Paulo katika somo la pili anasema utafute haki, utawa, imani, upendo, saburi, upole.
Ndugu yangu, kwa jinsi ulivyo, tajiri au maskini unaalikwa kuangalia nje ya wigo wako. Je, wewe una kitu gani au unapungukiwa na kitu gani? Je, kuna mhitaji ye yote aliye katika mazingira yako? Je, wewe una kitu gani cha kumsaidia mwingine? Je, umeshawahi kutoa msaada wo wote? Tukumbuke kuwa mwenye hitaji si maskini tu. Hata tajiri anayedhani kuwa na kila kitu bado ana hitaji fulani. Ona maajabu ya injili – maskini anatajwa kwa jina lakini jina la tajiri halitajwi. Ombi letu au sala yetu kwa Mungu ni kuoma neema na baraka ya kutumia kwa busara na hekima utajiri na pesa kwa haki na upendo/na kwa ukarimu mkubwa au wa pekee. Mtakatifu Jerome anasema ni tajiri zaidi, aliye maskini katika Kristo. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anasema hakuna aliye tajiri kwamba hana cha kupokea na hakuna maskini kiasi hicho kwamba hana cha kutoa. Tukumbuke wajibu wetu wa kikristo wa kufanya kitu. Kuwa baridi au kutokujali au kutokuona hali halisi itasababisha kupotea kwetu. Bwana wetu Yesu Kristo alikufa juu ya dhambi zetu. Na kwa sadaka yake msalabani sisi tukapata msamaha wa dhambi na tukajipatanisha na Mungu wetu. Tumsifu Yesu Kristo.