Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 27 Mwaka C: Bwana Yesu, tuongezeee imani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 27 Mwaka C: Bwana Yesu, tuongezeee imani! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 27 ya Mwaka C: Tuongezee Imani!

Kanisa halina budi kuwa ni sehemu ya maisha ya kila mwamini; mahali ambapo wanashibishwa kwa Neno la Mungu, Sakramenti na Katekesi. Kanisa ni uwanja ambapo waamini kwa njia ya ushuhuda: wanatangaza Injili ya upendo unaoonesha imani wanayokiri; wanayoiadhimisha; Imani wanayoimwilisha kwa kufuata Amri za Mungu: dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S., - Dodoma.

Kila mwamini anaalikwa kuwa mtakatifu, wito na mwaliko kwa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwamini mwenye imani thabiti hawezi kuyumbishwa na kinzani na migogoro inayoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia au kwa watu kupenda kukumbatia mawazo mepesi mepesi hata katika maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wanapaswa kumwongokea Mwenyezi Mungu, daima wakisaidiana katika hija ya maisha yao ya ndoa, ili kwa pamoja waweze kufikia utakatifu wa maisha. Hizi ni juhudi zinazowahitaji wanandoa kuimarishana katika imani, mapendo na matumaini. Waamini wanakumbushwa kwamba, hawawezi kamwe kuwa na Mungu kama Baba yao bila kuwa na Kanisa kama Mama yao, kama alivyosema Mtakatifu Cypriani; kila mwamini anapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa. Kanisa halina budi kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa kila mwamini; mahali ambapo wanashibishwa kwa Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Katekesi ya kina.

Kanisa ni uwanja ambapo waamini kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao wanatangaza kwa ujasiri mkubwa Injili ya upendo unaoonesha imani wanayokiri kwa vinywa vyao, imani wanayoiadhimisha kwa njia ya Sakramenti za Kanisa; Imani wanaojitahidi kuimwilisha kwa kufuata Amri za Mungu ambazo ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Utangulizi huu utusaidie kuyaelewa mafumbo ya Kanisa kama sehemu mpango mkakati wa Mwezi Oktoba 2019. Tunasoma toka Waraka kwa Warumi – 1:17 - …’ mwadilifu ataishi kutokana na imani’. Nabii Habakuki anaonesha wazi imani hii katika somo la kwanza. Dhamira ya imani inaongoza tafakari yetu leo. Ufahamu wa msingi au maana rahisi kabisa ya imani inasema kuwa ni kuamini au kutomwamini Mungu. Hii lakini siyo aina ya imani inayoonesha kuwa mmoja au ni mkristo au ni mwislamu au ni mwamini fulani. Katika Ebr. 11:6 tunasoma kuwa ‘pasipo imani haiwezekani kupenda, kwa maana anayependa kumfikia Mungu hana budi kusadiki kwamba Mungu yupo na kwamba kumfikia Mungu hana budi kusadiki kwamba Mungu yupo, na kwamba anawatunza wenye kumtafuta’.

Hii ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya imani au kuamini. Kutoka hapa tunaweza kuongea au kuona tofauti za kiimani zilizopo - ya kikristo, ya kiislamu au imani nyingine ye yote ile. Habakuki alihubiri kipindi wana Waisraeli wakiwa utumwani. Shida yake kama Ayubu na Zaburi 74 – inaoenekana kuwa wakati wana wa Mungu wanateseka, wabaya wananawiri. Katika Hab.1:13 – twaona Nabii anaongea na Mungu – ndiye wa kwanza katika historia ya Israeli kuongea kwa ukali kiasi hicho; anamwambia Mungu mbona hufanyi kitu? Inaonekana jibu la Mungu ni kuwa hata katika hali hii Mungu anafanya kazi, watu waendelee kuwa na imani – 2:4. Katika somo la pili – Paulo anaandika akiwa gerezani na anaongea kuhusu mwenendo mwema wa wachungaji na kulinda mafundisho ya imani. Anamwalika Timoteo achochee karama ya Mungu dhidi ya roho ya woga. Anamwalika amshuhudie Kristo aliyetuokoa na kumwalika kutoa ushuhuda na kuwa na uvumilivu. Anamhimiza akomae katika imani, kuishi ushuhuda na kufundisha ukweli.

Katika somo la Injili: Mitume wanaomba waongezewe imani. Tuzo toka wa Mungu haidaiwi kama walivyofikiria mafarisayo. Mwaliko ni kuwa tuishi imani yetu. Ni nini sababu ya manunguniko haya?  Katika Injili Yesu hatuambii tutembee njiani tukiamuru mikuyu ing’oke. Tusikae tukisubiri tulipwe kwa yale tufanyayo ila tunatakiwa kutimiza wajibu ipasavyo. Kumtumikia Yesu ni wajibu wa pekee na unaodai sadaka, hata ya msalaba. Ili kuweza kufanya jambo la pekee ni lazima imani yetu iwe ya pekee ili kile kilicho cha ajabu kionekane cha kawaida na kawaida kionekane cha pekee. Tunaalikwa kuishi, kutazama na kutenda ulimwenguni humu kwa jicho la kimungu. Tunaona mtazamo huu katika somo la kwanza – mtu wa imani anaweza kuongea na Mungu. Katika somo la pili, Mtume Paulo anaonesha imani hiyo anapomwambia Timoteo aichochee karama ya Mungu.  Tunaalikwa tuutambue wito wa Mungu kwa upendo ili tuweze kumwita Mungu – Baba, na kumtumikia Kristo kwa upendo kama wana wa mwanga.

Tutafakarishwe na mfano huu. Mtu aliyedondoka toka kilimani na akiwa anaporomoka akafanikiwa kukamata tawi. Lakini tawi lenyewe halikuwa imara na hakuweza kulitumia kurudi juu kilimani. Alijua wazi kuwa tawi likikwanyuka basi ndo mwisho wake. Mara anapata wazo la kumwita Mungu wake. Anatoa ombi na Mungu anamjibu; Je, waamini? Anajibu ndiyo. Mungu anamwambia nitakuokoa. Achia hilo tawi. Kwa sauti hiyo yule mtu akasita, akawa na wasiwasi. Je huyu mtu anaamini kweli? Jibu ni ndiyo. Tena anamwamini Mungu. Anaamini katika nguvu ya sala. Ila inakuwa vigumu kutekeleza mapenzi ya Mungu. Kwa nini?  Bila shaka wengi wetu tunajiona hapa. Kweli tunamwamini Mungu ila inakuwa vigumu kutekeleza mapenzi yake. Kweli tunaamini ila imani yetu ni ndogo sana au haba sana. Katika Injili tunaona mitume wakimwomba Bwana Yesu Kristo awaongezee imani. Kuna msemo usemao – asiyejua na hajui kwamba hajui, huyo ni mjinga. Ila asiyejua na anajua kuwa hajui huyo ni mwenye hekima.

Ndipo walipo mitume katika Injili ya leo. Wengi wetu tunakwama hapa. Tunakosa unyenyekevu wa kiakili. Kukosa ufahamu wa hali zetu na mahitaji sahihi ya mwili na roho zetu na kutokutafuta msaada sahihi kunagharimu sana maisha yetu na mahusiano yetu na Mungu. Ule mfano katika injili utusaidie kuweka katika matendo kile tunachoamini. Hata mmoja wetu asiseme amechoka katika kumtumikia Mungu. Wajibu wetu ni kutimiza mapenzi ya Mungu mpaka mwisho. Tunaalikwa kuwa watumishi waaminifu wa Mungu. Hatuna budi leo kuchunguza jinsi tunavyoishi imani yetu. Kuna hatari ya kubinafsisha imani. Yule kijana aliyeshikilia tawi na kusita na kukataa kutii sauti ya Mungu anawakilisha wale wote waliobinafsisha imani. Wale wanaoamini ila kwa imani haba. Bahati mbaya sana wengi wetu leo na katika ulimwengu wa sasa tunaamini kwamba imani ya kweli na sahihi ni ile ya miujiza miujiza. Ona jinsi watu mbalimbali wanavyohangaika toka imani moja hadi nyingine, toka kanisa moja hadi jingine kumtafuta Mungu.

Wengi wetu tunataka Mungu atimize mapenzi yetu, mahitaji yetu n.k. Tunakata kuamini katika miujiza kuliko katika Mungu ambaye aweza kufanya miujiza. Hakika imani ya kweli haipo katika jinsi Mungu anavyotimiza mahitaji yetu haraka haraka ila ni kwa jinsi gani tunamtumikia Mungu bila kuhesabu gharama. Tuendelee kama mitume kuomba Mungu aongeze imani yetu. Katika Ebr. 13: 7… tunasoma hivi – ‘wakumbukeni viongozi wenu waliowahubiria neno la Mungu. Kumbukeni mwisho wa maisha yao, mkaige imani yao. Yesu Kristo ni yule yule; jana, leo na milele’. Hakuna imani rahisi rahisi au Mungu wa haraka haraka au anayetimiza matakwa yetu kama tunavyotaka sisi. Katika somo la pili Mtume Paulo anaonesha wazi matokeo katika maisha yetu yatokanayo na kuwasha maisha yetu katika Roho Mtakatifu. Anasema tutaishi imani thabiti katika maisha yetu bila hofu ya mateso au kifo, tutaamini imara mafundisho sahihi kadiri ya mafundisho sahihi na tutalinda na kuendeleza kwa vizazi mafundisho sahihi ya imani kama tukiwasha maisha yetu katika Roho Mtakatifu.

Mtakatifu Ambrosi anasema kuwa hai katika kazi bila uaminifu moyoni ni kama kujenga nyumba nzuri katika msingi usio imara. Kadiri jengo linavyokwenda juu ndivyo linavyohatarisha maisha na uwezekano wa mwanguko mkali. Bila nguzo thabiti ya imani, kazi nzuri hazitaweza kusimama imara.  Tumsifu Yesu Kristo.

 

30 September 2019, 15:39