Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIV ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma inamwilishwa katika haki! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIV ya Mwaka C wa Kanisa: Huruma inamwilishwa katika haki! 

Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka: Huruma inamwilishwa katika haki

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 24 ya Mwaka C wa kanisa inatuchangamotisha kutafakari juu ya huruma ya Mungu. Huruma inayotangulia haki. Katika kutafakari huko tunafikia hatua ya kudaiwa kuangalia kwa undani uhalisia wa maisha yetu na mahusiano yetu na Mungu na wenzetu. Katika hali hii swala la kukubali au kukiri kosa linajitokeza wazi. Huruma inamwilishwa katika haki.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Dodoma.

Ndugu wapendwa Neno la Mungu jumapili ya leo latualika kutafakari juu ya huruma ya Mungu. Huruma inayotangulia haki. Katika kutafakari huko tunafikia hatua ya kudaiwa kuangalia kwa undani uhalisia wa maisha yetu na mahusiano yetu na Mungu na wenzetu. Katika hali hii swala la kukubali au kukiri kosa linajitokeza wazi. Wengi wetu tunatambua kuwa si jambo rahisi kibinadamu, yaani kukiri au kukubali kosa ingawa inawezekana. Wakati wetu huu tumepata bahati ya kushudia uwezekano huo. Huko nchini Afrika ya Kusini, Rais Nelson Mandela aliunda kamati iliyoitwa ya usuluhishi na upatanisho wa kitaifa. Mbele ya wengi ilionekana kitu kigumu na hatari lakini mwishoni ilipata mafanikio makubwa. Ni mahali hapa mtenda maovu na aliyetendewa walipata nafasi ya kukutana uso kwa uso, kukaa pamoja, mmoja akikiri kosa lake dhidi ya mtendewa, kuomba msamaha na msamaha kufikiwa. Tunafahamu kuwa tendo la upatanisho ni jambo gumu sana kwani hata mtenda jema aweza kuonekana tishio mbele ya baadhi ya watu pale anapodai haki yake.

Tunaona katika Neno la Mungu siku ya leo uwezekano wa mwanadamu kutenda dhambi. Tunaona Waisraeli wakitenda dhambi na hata mwana mpotevu. Kwa upande mwingine katika injili tunaona ukuu wa huruma ya Mungu inayookoa.  Katika somo la kwanza twaona jinsi watu wanavyokosa subira na katika kujaribu kumpata Mungu kwa namna yao wanatenda dhambi. Musa alikuwa amekwenda kuongea na Mungu, watu wanachoka kumsubiri na wanamwomba Haruni amtengeneze ndama. Hasira ya Mungu dhidi ya jambo hili inawaka lakini ombi la msamaha toka kwa Musa linawapa wokovuhuruma ya Mungu. Mungu anachukia dhambi lakini yuko tayari kutoa msamaha. Mtume Paulo anatambua ukuu huu wa huruma ya Mungu na anamshukuru Yesu kwa mema yote aliyomjalia. Ingawa sisi tulikuwa wadhambi, yeye hakuona dhambi zetu ila alituletea msamaha toka kwa Baba. Anatukomboa toka hali yetu ya zamani. Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.

Katika somo la Injili tunasikia habari juu ya kondoo aliyepotea, fedha iliyopotea na Mwana mpotevu. Katika ile mifano miwili ya kwanza hakuna hali ya dhambi wala utengano. Katika mifano hii miwili ya mwanzo na habari ya Mwana mpotevu twaona kwamba kanisa lataka kutoa wokovu. Dhambi ipo, hatuwezi kukataa, ndiyo maana upo wokovu. Haja ya kutambua, kurudi, kujipatanisha ndicho kiini cha injili ya Yesu. Kibinadamu ni vigumu lakini inawezekana. Ilitokea siku moja Mfalme wa Urusi alitaka kutoa msamaha kwa mmoja kati ya wafungwa katika gereza kuu la mji. Yeye alitaka kutoa msamaha kwa mfungwa atakayesema wazi kile kilichomsibu mpaka akawa pale gerezani. Kila mfungwa alidai kuwa ameonewa na hakutendewa haki kuwa pale gerezani. Mwishoni kabisa akatokea mfungwa mmoja aliyetamka wazi kosa lake na kukubali kuwa kuwepo kwake pale gerezani ilikuwa sawa kabisa. Huyu alikiri kosa lake. Mfalme akaamuru Bwana jela amfungue pingu na kumwacha huru kwa vile alikiri kosa lake.

Wengi wetu hatufikii hatua hii ya kukiri na kukubali makosa. Na hii inagharimu sana maisha yetu na mahusiano kati yetu sisi na kati yetu na Mungu. Hakika haja ya kutambua, kurudi, kuomba msamaha na kujipatanisha ni muhimu sana. Kilicho wazi kattika Injili ni kuwa mwanadamu amepata nafasi ya kujipatanisha na Mungu. Mungu ametaka upatanisho nasi na kati yetu wenyewe. Ili upatanisho na msamaha utokee ni lazima Mungu aingilie kati. Sisi tunaalikwa kushiriki katika tendo hili takatifu. Mtume Paulo anasema mpatanishwe na Mungu. Na anasema kwa vile sisi ni watu wake Bwana, sisi ni viumbe vipya. Tendo halisi la upatanisho hutoka kwa Mungu, kwa njia ya mwanawe. Katika 2 Kor. 5:18 - tunasoma kuwa naye anatupa sisi huduma ya upatanisho.  Hivyo huu unakuwa ni wajibu na si hiari.

Habari ya baba mwenye huruma katika somo la Injili nayo yatupa changamoto kubwa. Lakini kubwa zaidi ni ile roho ya yule mtoto kutambua na kukiri kosa. Anaamua kufunga safari ya kurudi kwa baba na kuomba msamaha. Huyu anajitambua na kukiri kosa lake. Wengi wetu hatuwezi kufikia hali hii ya juu kabisa ya kiroho. Habari ya kaka anayechukia kurudi kwa ndugu yake inasikitisha sana. Pengine anawakilisha hali zetu sisi ambao hatuko tayari kuwa na huruma na msamaha. Anadai haki yake kwanza na kusahau tendo la huruma. Kwake huyu ndugu yake alikuwa tayari adui. Tunakumbushwa kuwa hatuna budi kuwa tayari kuukubali msamaha wa baba kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine. Tukumbuke moto ya mwaka huu wa huruma ‘ Basi iweni na huruma kama Baba yenu alivyo na hurma – Lk. 6:36 lakini pia tunaambiawa “heri walio na huruma, maana watahurumiwa – Mt. 5:7”. Ninapomalizia tafakari hii mfano huu utusaidie kuweka katika matendo neno la Mungu fundisho hili. Walikuwepo ndugu wawili; mmoja mkubwa na mwingine mdogo.

Kaka mkubwa alikuwa mtu mwema na mpole, lakini mdogo mtu alikuwa mwizi na jambazi. Mara nyingi kaka mkubwa alimsihi ndugu yake aache tabia hiyo mbaya bila kufaulu. Siku moja usiku wa manane yule mdogo akarudi amechoka, ametapakaa damu na hali yake kuwa mbaya. Alipoingia ndani tu neno alilosema kwa kaka yake ni kuwa sitaki kufa. Kaka mtu alitambua wazi kuwa huko alikotoka ameacha maafa. Kitambo kidogo mlango wa nyumba yao ukagongwa kwa nguvu. Na sauti ya kujitambulisha ya polisi ikasika. Kumbe, alikuwa akifukuzwa na polisi kwani huko alikotoka alikuwa amefanya ujambazi na kuua mtu. Kaka mtu alitafuta kila mbinu ya kumsaidia mdogo wake aliyekuwa amechafuka damu. Alitambua wazi kuwa huu ulikuwa mwisho wake. Polisi wakaanza kuvunja mlango. Katika kutaka kumwokoa, kaka mtu akaamua kuvaa mavazi yake yaliyojaa damu na polisi walipoingia ndani akakamatwa aliyeonekana na hatia. Baada ya hukumu adhabu ikawa ni kifo. Hivyo kaka mtu, aliyekuwa mwema, akafa badala ya kaka yake mdogo aliyekuwa jambazi, mwizi na muuaji.   Yaani, kwa hakika huruma inamwilishwa katika haki. Tumsifu Yesu Kristo.

13 September 2019, 17:10