Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXV ya Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa kuheshimu mali ya wengine; Upendo kwa maskini pamoja na kujali mahitaji ya jirani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXV ya Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa kuheshimu mali ya wengine; Upendo kwa maskini pamoja na kujali mahitaji ya jirani! 

Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka: Uchu wa mali & Dhuluma kwa maskini!

Leo Mama Kanisa anatufundisha umuhimu wa kuwajali watu na mali zao; kwa kujikita katika fadhila ya kiasi, ili kuratibisha tabua ya kugandamana na mali ya ulimwengu huu: fadhila ya haki, ili kuhifadhi haki za jirani na kumpatia kila mmoja haki yake; fadhila ya mshikamano, kwa kumuiga Kristo ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, waja wake wapate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Mwanafalsafa Seneca anasema, sisi hatuna dhamana ya maisha bali tu wajumbe au mawakili wake. Historia ya Biblia na kwa namna ya pekee tukiangalia wito wa Abrahamu, tunaona kuwa kama mwanadamu anaambiwa aache nchi yake na anaahidiwa mengi. Hata Waisraeli wakiwa safarini, walitamani kuifika nchi ya ahadi. Tafsiri ya Mwa. 1:28 – yaonesha ahadi ya Mungu juu ya urithi wa dunia. Hali hii ya tamaa ya kurithi inaonekana wazi katika Biblia. Lakini pia historia yaonesha matokeo mabaya ya tamaa hiyo mbaya ya kutaka kuipata dunia – dhambi, dhuluma na matumizi mabaya ya hayo matunda ya dunia. Somo la kwanza laonesha hilo. Hata hivyo Nabii Amosi halaani matunda hayo ila namna yanavyopatikana na matumizi yake. Kwa sababu ya tamaa ya mali, wanatumia vibaya hata siku za mapumziko ya kidini. Hawakuona tena umuhimu wake. Waliuza hata makapi ya ngano ambayo yalikuwa ni halali kwa maskini. Aliye maskini anaumia zaidi na Nabii analaani hilo. Hata inabidi walipe hilo kwa kuwa watumwa. Nabii Amos alikuwa Nabii maskini mkulima na akawa bila woga anakemea madhulumu ya matajiri dhidi ya maskini.

Katika somo la Injili tunaona harakati mbalimbali za mwanadamu katika kupata mambo ya kidunia. Ujumbe uliopo waonesha jinsi mtu anavyoshughulika kwa nguvu na bidii na ujanja kupata anachotaka kumiliki. Kwa kifupi katika sehemu hii ya injili, hakuna hukumu mbaya au nzuri inayotolewa kuhusu umiliki wa mali.  Ila upo ujumbe juu ya matumizi mazuri ila ufalme wa Mungu utumike kama kielelezo. Mwishoni mwa injili – ipo wazi – mali ya dunia haiwezi kuchukua nafasi ya ufalme wa Mungu. Kuna utengano wazi juu ya njia zinazotumika ambazo ni mbaya (tamaa ya fedha na mali) na mwisho unaotegemewa (Ufalme wa Mungu). Mama Theresa wa Calcuta alipoanza rasmi utume wake kwa maskini, alimwokota barabarani mwanamke ambaye alishaooza mwili na nusu ya mwili wake kuliwa na funza Hata viongozi wa mji walimcheka sana kwamba haisaidii lo lote kufanya tendo hilo. Atafanya kwa wangapi? Kwa shingo upande, bwana afya wa Manispaa alimruhusu kutumia jengo /hekalu au sehemu ya hekalu ambapo watu hutumia kupumzika baada ya kuabudu. Lilikuwa jengo tupu. Toka hapo Mama Teresa alianza rasmi utume wake.

Mama Theresa wa Calcutta akawekeza utajiri wake wote kuwahudumia maskini hawa. Leo hii ni mtakatifu. Katika injili yaweza onekana kuwa Yesu anamsifu yule tajiri dhalimu. Kwa hakika anachosema Yesu ni kuwa tunatakiwa kutumia uwezo wetu wote na nguvu zetu zote kuupata utajiri wa kweli, yaani ufalme wa Mungu. Ndicho alichofanya mtakatifu Mama Teresa wa Calcuta. Mtakatifu Augustino wa Hippo anasema, maskini ni wajumbe na wachukuzi. Wanatuwezesha kuanza sasa safari ya kupeleka mali au vifaa vya ujenzi katika nyumba itakayojengwa katika ufalme ujao. Katika Injili, hatuoni yule wakili akijitetea kwa kosa lake. Alitambua wazi kosa lake. Ila hakukubali kushindwa. Anajipanga kujiokoa na kulinda hali na hadhi yake. Anapanga dili na wadeni wa bwana wake na wanakubaliana. Taarifa ikamfikia Bwana yule. Anamsifu kwa akili yake. Hata hivyo isionekane kuwa Yesu anaunga mkono ujanja huu dhalimu. Iko wazi kuwa huyu wakili anasifiwa kwa akili yake na werevu wake dhalimu lakini harudishwi kazini. Bado atatumikia kosa lake. Bila shaka huyu bwana atadai mali yake ilipwe au wakili dhalimu atumikie kifungo.

Ujumbe toka somo la pili unatusaidia kuelewa mwito wake Mwenyezi Mungu. Mtume Paulo anamsihi Timoteo kuishi maisha adili ya kikristo, undugu thabiti, maisha ya sala, uwajibikaji katika amani na haki mpaka kuufahamu ukweli kamili. Hakika ujanja ujanja katika maisha hauna tija. Tutafakarishwe na maisha ya Jenerali Gordon na itusaidie kuishi ujumbe wa neno la Mungu jumapili hii. Wakati serikali ya uingereza ilipotaka kumzawadia Jenerali Gordon kwa utumishi uliotukuka huko China, alikataa fedha na vyeo vyo vyote ila alikubali kupokea zawadi ya dhahabu ikiandikwa miaka yake 33 ya utumishi uliotukuka. Aliipenda sana zawadi hii. Baada ya kifo chake, hii medali haikuonekana po pote. Baadaye ikafahamika kuwa aliipeleka Manchester wakati wa njaa kali, akiagiza kuwa iyeyushwe na mauzo yake yatumike kununua chakula kwa ajili ya maskini. Katika tarehe iliyotumwa yaliandikwa maneno haya katika kitabu cha kumbukumbu ‘kitu cha mwisho nilichokuwa nacho duniani, nilichokithamini, nimekitoa kwa Bwana Yesu Kristo’. Ukarimu wa namna hii, ambao unafaa wengine ndiyo unatupa changamoto ya namna ya kuenzi Neno la Mungu jumapili ya XXV ya Mwaka C wa Kanisa. Tamaa ya mali na maisha ya ujanja ujanja hayana tija. Tumsifu Yesu Kristo.

17 September 2019, 14:15