Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIV ya Mwaka C wa Kanisa: Ukuu wa neema ya Mungu unamwilishwa katika toba na wongofu wa ndani shari muhimu katika kushiriki furaha ya uzima wa milele. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIV ya Mwaka C wa Kanisa: Ukuu wa neema ya Mungu unamwilishwa katika toba na wongofu wa ndani shari muhimu katika kushiriki furaha ya uzima wa milele. 

Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka: Neema, Toba na Wongofu!

Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 24 ya mwaka C wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya haki na amani ya ndani inayofikia utimilifu wake katika msamaha kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu una nguvu zaidi kushinda dhambi na ubaya wa moyo unaoendelea kumwandama mwanadamu katika historia yake.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 24 ya mwaka C wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya haki na amani ya ndani inayofikia utimilifu wake katika msamaha wa dhambi kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu una nguvu zaidi kushinda dhambi na ubaya wa moyo unaoendelea kumwandama mwanadamu katika historia yake. Kimsingi Fumbo zima la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu linaiadhimisha huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka kwa waja wake! Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, kama sharti maalum la kushiriki katika ukamilifu wa furaha ya Baba mwenye huruma!

Somo la kwanza (Kut 32:7-11, 13-14 ) ni kutoka katika kitabu cha Kutoka. Ni somo linaolezea dhambi kubwa na ya kwanza ya waisraeli kama taifa, nayo ni dhambi ya kumuasi Mungu. Musa akiwa mlimani Sinai waisraeli waliona amekawia wakamwendea Haruni na pamoja naye wakajitengenezea ndama wa dhahabu na kuiweka badala ya Mungu. Tendo hili linamkasirisha sana Mungu naye anakusudia kuwaangamiza wote. Musa akiwa bado mbele ya Mungu anatubu kwa niaba yao na kuwaombea msamaha. Mungu anaigeuza nia yake, anawasamehe. Kiini cha dhambi ya uasi ni mwanadamu kutoridhika na utendaji wa Mungu. Ni jaribio la mwanadamu kumfundisha Mungu namna ya kuwa Mungu. Na tena zaidi ya hapo uasi ni jaribio la mwanadamu kujifanya Mungu. Na ndivyo walivyofanya waisraeli.Wwaliona Musa anachelewa na waliona Mungu hajitokezi na wala hajibu tena kwa haraka kama walivyotaka wao, basi wakajiundia mungu wao. Ni bahati mbaya sana kuwa dhambi hii ilimhusisha pia Haruni aliyekuwa kuhani mkuu. Hili ni angalisho juu ya madhara ya dhambi. Dhambi ina madhara kwa jamii nzima na jamii inapoharibika taasisi zake hata zile za kidini zisipojiangalia zitaharibika pamoja na jamii nzima. Somo hili pamoja na yote hayo linaonesha huruma kubwa ya Mwenyezi Mungu, huruma inayoitikia kila sala nyofu ya kuomba toba na msamaha.

Somo la pili (1 Tim 1:12-17) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timoteo. Huu ni waraka wa kichungaji ambao Paolo anauandika ili kutoa maelekezo ya kichungaji katika makanisa na jumuiya ambazo Paulo mwenyewe alizianzisha. Hapa anamwandikia Timoteo aliyemweka kuwa Askofu wa kanisa la Efeso ambalo yeye mwenyewe Paulo alilianzisha. Katika somo la leo Paulo anafundisha juu ya ukuu wa neema ya Mungu, neema inayoweza kumbadilisha mtu, kubadilisha maisha yake na kuwa mtu mwema. Paulo anatumia mfano wa maisha yake mwenyewe kuonesha kuwa fundisho analotoa sio nadharia, yeye mwenyewe ni ni mfano hai. Anaeleza maisha aliyioishi hapo mwanzo, maisha ya dhambi, ya kuudhi watu na kulitesa kanisa la Mungu na anakiri kuwa aliishi hivyo kwa sababu alikuwa katika enzi ya ujinga kwa kutokuwa na imani. Hivyo anawasihi nao kuitumainia sana neema ya Mungu na zaidi ya hapo kushirikiana nayo ili neema hiyo ifanye kazi ndani yao.

Injili (Lk 15:1-32) Injili ya dominika ya leo inaendeleza dhamira ya somo la kwanza na ya somo la pili.  Kutoka kwa upotevu wa waisraeli kwa kutengeneza ndama ya shaba hadi kwa upotevu wa Paulo kwa sababu ya kuishi nje ya imani, Yesu anatoa mifano mitatu zaidi. Mfano wa kwanza ni wa mchungaji aliye na kondoo mia na anagundua kuwa kondoo mmoja amepotea. Huyu anawaacha kondoo 99 na kwenda kumtafuta yule aliyepotea hadi ampate. Na akimpata furaha yake hukamilika. Mfano wa pili ni wa mama aliyekuwa na shilingi kumi akapotelewa na shilingi moja. Mama huyu akafanya juhudi zote alizonazo kuitafuta shilingi iliyopotea: aliwasha taa, akafagia nyumba hadi pale alipoipata. Na alipoipata furaha yake ikatimia. Mfano wa tatu ni wa baba aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo akaomba urithi wake akachukua akaondoka nyumbani kwenda nchi ya mbali. Huko akatapanya mali kwa maisha ya uasherati hatimaye, akaingia katika uhitaji. Akaishi maisha magumu kuliko waliyoishi nguruwe. Alipoamua kurudi nyumbani baba yake alimpokea kwa furaha kuu kama baba ambaye alikuwa daima anamsubiri ili furaha yake na furaha ya familia nzima ikamilike.

Ufafanuzi J24

 

15 September 2019, 09:37