Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXV ya Mwaka C wa Kanisa. Uaminifu kwa Mungu na kwa mali ya jirani ili kujenga na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XXV ya Mwaka C wa Kanisa. Uaminifu kwa Mungu na kwa mali ya jirani ili kujenga na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. 

Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka: Uaminifu kwa Mungu na Jirani

Katika masuala ya kiuchumi, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayohitaji fadhila ya kiasi, ili kuratibisha kile kishawishi cha mtu kugandamana na malimwengu pamoja na fadhila ya haki, ili kumpatia jirani iliyo haki yake. Yote haya yanaongozwa na kuratibiwa na kanuni ya mshikamano kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Uaminifu kwa Mungu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 25 ya mwaka C wa Kanisa. Katika masuala ya kiuchumi, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayohitaji fadhila ya kiasi, ili kuratibisha kile kishawishi cha mtu kugandamana na malimwengu pamoja na fadhila ya haki, ili kumpatia jirani iliyo haki yake. Yote haya yanaongozwa na kuratibiwa na kanuni ya mshikamano kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Amri ya Saba inakataza wizi. Hapa kuna haja ya kutekeleza ahadi na kuheshimu mikataba kikamilifu; sanjari na kufuata kanuni, sheria na taratibu za jamii mahalia. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo ambayo Mama Kanisa anayapatia kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii.

Somo la kwanza (Amo 8:4-7 ) ni kutoka katika kitabu cha Nabii Amos. Amos alifanya utume wake wa unabii katika kipindi ambacho Israeli ilikuwa imeshamiri sana kiuchumi. Ushamiri huu lakini haukuendana na ushamiri wa kimaadili, ushamiri wa haki wala ule wa kiimani. Watu walifikiri tu namna ya kuzidi kukuza mitaji yao na kupata faida katika biashara zao. Faida hizi hata hivyo walizipata kwa kuwanyonya maskini. Asiyenacho hakuwa na thamani. Tunasikia nabii anawanukuu wakisema “tupate kuwanunua maskini kwa fedha na wahitaji kwa jozi ya viatu” kwani kwa hakika haki ya maskini iliweza kununuliwa kwa gharama ya kununua jozi ya viatu. Hali hii pia iliwaondoa katika uchaji. Waliona siku za ibada na uchaji ni kupoteza muda wao wa kufanya biashara. Nabii anawanukuu tena wakisema “mwezi mpya utaondoka lini tupate kuuza nafaka? Na sabato itaisha lini tupate kutandaza ngano”?  Kwa hayo yote nabii Amos anawaonya kuwa wale masikini wanaonyonywa katika biashara na kunyimwa haki zao, Bwana kwa hakika hatazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo.

Somo la pili (1 Tim 2:1-8) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timoteo. Huu ni waraka wa kichungaji ambao Paolo anauandika ili kutoa maelekezo ya kichungaji katika makanisa na jumuiya ambazo Paulo mwenyewe alizianzisha. Hapa anamwandikia Timoteo aliyemweka kuwa Askofu wa Kanisa la Efeso ambalo yeye mwenyewe Paulo alilianzisha. Katika somo la leo Paulo anawaasa kutambua jukumu lao la kuwaombea watu wote hasa viongozi na wenye mamlaka ili jamii nzima iishi kwa utulivu na amani. Katika mazingira ya kihistoria ambapo ukristo ulionekana ni adui wa watawala hasa kwa dola ya kirumi, jibu na mtazamo wa Paulo ulikuwa huo. Kuonesha kuwa ukristo haupingi viongozi na watawala ila unapinga uovu popote pale ulipo bila kujali itikadi. Mtume Paulo kwa kuhimiza sala kwa ajili ya viongozi anaonesha kuwa ukristo unapopinga uovu haumaanishi kujenga uadui na watawala bali unafanya hivyo ili kutetea ukweli na tunu za msingi za kibinadamu kama anavyokusudia Mungu mwenyewe muumbaji.

Injili (Lk 16:1-13) Katika Injili ya dominika ya leo Yesu anafundisha juu ya mambo mawili. La kwanza ni juu ya uharaka wa kuupokea Ufalme wa Mungu. Uharaka unaohitaji akili ya kutambua na kung’amua mapema yale yaliyo mbeleni. Katika jambo hili Yesu anatoa mfano wa wakili aliyetakiwa kutoa mahesabu ya uwakili wake kwa sababu alikuwa hatarini kupoteza kazi. Kwa kujua alichokuwa anafanya na ili asikose wa kumkaribisha atakapofukuzwa kazi akawaita wadeni wa bwana wake na kuwapunguzia madeni yao. Injili haifafanui kama aliwapunguzia riba waliyopaswa kulipa au aliwaondolea asilimia aliyokuwa amewaongezea kama faida yake binafsi au tu alifanya hivyo kumpa hasara bwana wake ili yeye ajipatie marafiki. Katika yote hayo Yesu anasema wana wa ufalme huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru. Na ni kama anahoji, kwa nini linapokuwa suala linalohusu ufalme wa Mungu au mafaa ya kiroho busara ya namna hiyo haionekani? Jambo la pili, Yesu anafundisha kuwa uaminifu na wema hautokani na ukuu wa mamlaka au mali. Yeye aliye mwaminifu katika mambo madogo atafaulu pia kuwa mwaminifu katika yale yaliyo makubwa.

Liturujia J25
20 September 2019, 16:38