Tafakari Jumapili 31 Mwaka: Zakayo Mtoza Ushuru: Huruma ya Mungu
Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.
Leo Msafara wa Yesu umeingia Yeriko ukitokea Galilea kuelekea Yerusalemu. Mji wa Yeriko ulikuwa bondeni wakati Yerusalemu ulikuwa mlimani. Ardhi ya Yeriko ina rutuba na kuna mitende mingi. Uchumi wa Yeriko ulikuwa wa juu hadi wanauchumi wake walifanya biashara na nchi mbalimbali zinazozunguka bahari ya kati ikiwa ni pamoja na Misri. Yeriko kulikuwa na ofisi kuu ya malipo ya kodi za mapato. Hivi kulishamiri pia utajiri wa mali za ufisadi na rushwa zilizohalalishwa na Serikali. Yesu alipokaribia Yeriko alikutana na kipofu:“Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia akiomba sadaka.” Yesu anamponya kusudi amwone Yesu na amfuate. Siku ya leo Yesu anakata mitaa ya Yeriko ili watu wamwone. “Naye Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake.” Katika pitapita yake akakutana na mtu mmoja tajiri tena mkuu wa watoza ushuru aitwaye Zakayo. Kwa Kiebrania Zakai maana yake ni msafi, mnyofu.
Mtoza ushuru kwa lugha ya Kigiriki anaitwa “Telones”, kumbe Zakeo ni “Archi-telones” yaani “Mkuu wa watoza ushuru". Wale wale mafisadi! Mtoza ushuru alipata kibali cha kuongeza kodi ya mapato na kinachozidi kinaingia mfukoni mwake, hadi raha! Aidha Mkuu wa watoza ushuru ilimbidi pia kutoa kiapo kwa Mfalme na kutolea sadaka kwa miungu ya mfalme. Kwa hiyo Zakayo alimsaliti Mungu (kwa kuabudu miungu) na alisaliti pia taifa lake kwa ajili ya mali na mafanikio ya maisha. “Baniani mbaya kiatu chake dawa!” Aidha Zakayo kama Mtoza ushuru aliishi maisha ya kifahari sana, kwake daima alikuwa anakula “Bata kwa mrija” kiasi angeweza kujisemea. “Miaka hii iliyokubakia, ni ya kuponda mali, kula, kunywa na kutulia.” Kumbe Zakayo hakuwa na amani wala raha moyoni licha ya utajiri wake. Hali ya kutoridhika inaonekana katika pilikapilika za nguo kuchanika kama tutakavyoziona. Yaani Zakayo aliwania sana kumwona Yesu.
Nadhani alishasikia jinsi Yesu alivyokuwa anawachamba mafisadi na wenye mali. Mathalani yule mkulima aliyejikusanyia mazao na kujengea maghala mapya, alimtukana: “Mpumbavu.” Pahala pengine aliwalaani: “Ole wenu matajiri, kama hamtolei mali zetu mnaharibu maisha yenu.” Aidha kwa kijana tajiri aliwaambia watu: “Angalieni jinsi ilivyo ngumu kwa tajiri kuingia mbinguni.” Aidha, Zakayo alivutiwa tu na Yesu kwa vile alisikia kuwa yu rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi. Hivi “Alitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani.” Katika pilikapilika zake Zakeo anapambana na vigingi: Kigingi cha kwanza: “Zakeo hakuweza kumwona Yesu kwa sababu ya umati wa watu.” Kumbe, jamii ya watu inaweza kukuzuia kukutana na Yesu. Kwa hiyo, inabidi kuiangalia sana jumuiya. Kama unakuwa “bendera fuata upepo” yaani hujinasui na fikra mbovu za vikundi namitandao ya kijamii huwezi kamwe kuwa na jibu la maswali ya msingi ndani ya nafsi yako.
Kwa hiyo wewe mkristo unaalikwa kuwa mwangalifu sana na vikundi mbalimbali vya dini hasa vile vinavyojiona vinamfuata Yesu kwa karibu na sehemu nyingine "wanajimwambafai" kwa kujiita eti “wanaharakati”. Yaani jumuiya ya wajuaji na vijumvi sana wa Injili. Kumbe yawezekana hawana zaidi ya kile walichofundishwa kabla ya komunio ya kwanza na kipaimara. Sasa wanabaki kumzuia anayetaka kujua zaidi juu ya Yesu. Hapa tunaweza pia kuwaona hata Mitume wanaoandamana kabisa na Yesu yaani wakleri na watawa. Kwa vile hata nao ni binadamu wanaweza kuwa kizuizi cha kumwona Yesu kwa makwazo wanayoonesha. Baada ya kushindwa kumwona Yesu, Zakayo angeweza kukata tamaa na kurudi nyumbani kuendelea na maisha yake. Lakini Zakayo anatufundisha kutokukata tamaa na kulaumu. Anachofanya Zakayo ni kujitambua udhaifu wake kwamba yeye “alikuwa mfupi wa kimo.” Kwa hiyo akafikiri haraka namna ya kujiongeza, kwa maana alijua: “Urefu siyo akili na ufupi si umaskini.” Zakayo anataka kuuona ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu. Pahala pekee anapoweza kumwona Yesu mubashara ni kuuparamia mti wa Mkuyu.
Kwa hiyo, “Akatangulia mbio.” Mbio hizi ni alama ya juhudi inayobidi kila mmoja awe nayo anapowania kitu cha maana. Kisha “akapanda juu ya Mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kupitia njia ile.” Mkuyu una majani mengi sana yanayokuficha na kukuwezesha kuona bila wewe kuonekana. Zakayo anataka kuficha aibu na mahangaiko yake ya ndani. “Bora lawama kuliko fedheha.” Kumbe, tukitaka kuuona Uso wa Kristo ulio ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, yatubidi kukwea Mkuyu. Mkuyu huo unaweza kuwa Maandiko Matakatifu (Biblia), Sakramenti za Kanisa, Kufunga na Kusali pamoja na matendo ya huruma au hata neno jema kutoka kwa jirani. Kwa sababu Yesu anapitia njia hiyohiyo. Utakutana naye tu. Sasa tukitanguzana na Zakeo tutaigundua sura ya Yesu Kristu kama alivyoigundua yeye. Mosi, Zakayo alijificha ili aweze kumwona Yesu bila mwenyewe kuonekana. Kinyume chake Yesu anatangulia kumwona Zakayo. “Yesu alipofika mahala pale, alitazama juu.”
Huu ndiyo ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu uliyojiakisi katika Mwana wake. Kwamba siyo Mungu anayekaa juu na kutumikiwa. La hasha, bali anamtumikia binadamu ili awe na furaha. Pili, Yesu ndiye anayetangulia kumwona mtu anayejisikia aibu kuonwa. Yesu anakuona na anakupenda kama ulivyo. Tatu, Yesu anamwita kwa jina: Zakayo! Kumbe, Yesu anatufahamu na kutuita kwa majina yetu tena anaona uzuri tu ndani mwetu. Nne, Upendo haupotezi muda. Yesu anamwamuru: “shuka upesi.” Uso huu wa Mungu katika Kristo umependa na upendo haupotezi muda. Tano, Yesu anazungumza juu ya sasa, hajali mambo yaliyopita. Yesu anamwambia: “Leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.” Yesu daima anabisha mlango wa moyo wako. Kutokana na upendo alio nao kwa mdhambi hivi anaona ulazima wa kukaa na Zakayo. Yaani,“Tumaliziane hapa hapa!” Zaidi, katika Injili ya leo tunashuhudia matukio ya mwendo kasi: “Yesu anaingia mji wa Yeriko; Yesu anakatisha mji wa Yeriko; Zakayo anakimbia kutangulia mbele; Zakayo anapanda mkuyu kwa haraka; Zakayo anaamriwa kushuka upesi; Zakayo anashuka kwa haraka.”
Lakini kuna utulivu, amani na usalama baada ya Yesu kuingia nyumbani kwa Zakayo. Kadhalika Zakayo ametulia na kufurahi. “Mgeni afike mwenyeji apone.” Kwa vyovyote anayemkaribisha Kristo nyumbani mwake anatulia, anapata faraja, amani na kufurahi. Nyumbani kwa Zakayo kulikuwa pia na marafiki zake wakijipongeza pamoja na Yesu. Lakini nje walisimama watu wakiona husuda na kubeza kitendo alichokifanya Yesu. “walinung’unika wote wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” Yesu anamwonesha Mungu anayewakwaza wenye haki anapoleta furaha kwa watu dhaifu na wadhambi. Yawezekana hata sisi tunaomzunguka Yesu tunaweza kupata taabu sana kumpokea Mungu mwenye Uso wa huruma na wa kushirikiana na wadhambi. Sasa tukione kitendo anachokifanya mtu aliyeiona sura ya Mungu katika Kristo Yesu. Kwanza, Zakayo akasimama, kwa Kigiriki ni “statheis” maana yake ni kuwa wima.
Neno hili linatumika pia kumaanisha ufufuko, upya wa maisha. Sifa pekee ya Yesu ni kumsimamisha mtu au kumwinua yule aliyetopea katika dhambi na ubaya wa moyo Kwa hiyo anayeigundua Injili (kama yule kipofu aliyeona) anaweza kusimama na kutembea kifua mbele akijua kinachotakiwa katika maisha, yaani kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, hadi raha! Pili Zakayo anafanya maajabu: “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.” Yaani, Yesu amemfungua macho na sasa ni mtu mpya anaweza kuona mambo ambayo kabla ya hapo hakuweza kuyaona. Kwanza anawaona fukara na wahitaji wanaomzunguka ambao kabla alikuwa kipofu aliwaona kuwa kama “dili” tu la kuwanyonya. Pili, mali ambayo ingempa “ujiko” na maana katika maisha, sasa anayaiona kuwa ni mali ya kuwagawia maskini. Kumbe, tukiwania kumwona Kristo Yesu, yeye atatuponya upofu wetu. Tutawaona wanyonge na kuwagawia haki yao.
Yesu anajibu: “Leo wokovu umeingia katika nyumba hii kwani hata huyu ni mtoto wa Ibrahimu.” Ukombozi unafika pale mmoja anapoacha ubinafsi na kufungua moyo kwa ajili ya wengine yaani kuwapenda. Wokovu unafumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi pamoja na kupania tena kuachana na dhambi. Fundisho la mwisho linapatikana katika hatima ya simulizi hili lote. Yaani tungependa kusikia zaidi kilichomtokea Zakayo. Lakini hatusikii tena chochote juu ya Zakayo. Kwa sababu Mwinjili anataka kutuachia siku hii tuweze sisi sasa kuifuata Sura ya Ufunuo wa Mungu iliyoakisiwa katika Kristo Yesu. Vituko vya maisha ya Zakayo; tajiri na mkuu wa watoza ushuru akikwea juu ya Mkuyu kwani alitamani kumwona Yesu. Licha ya mali na utajiri; cheo na dhamana aliyokuwa nayo ndani ya Jamii, bado alikosa amani, utulivu wa ndani na furaha hadi pale alipokutana na Yesu, akamkirimia: amani, furaha na wokovu! Akamwonjesha huruma na upendo wa Mungu kwa kumwita kwa jina!