Tafakari Jumapili 28 Mwaka C: Yesu, mwingi wa huruma na upendo!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Nyakati za Yesu kuna makundi manne ya watu walioonekana si tu wamekutwa na balaa na laana kwa sababu ya dhambi na makosa yao bali hata kuonekana kuwa sawa na wafu nao ni; maskini, mkoma, kipofu na yule asiyekuwa na watoto au mtoto. Hivyo wakoma kadiri hata ya Kitabu cha Mambo ya Walawi sura ya 13 na 14 tunaona walikatazwa si tu kuingia mijini na vijijini bali pia kuonekana sawa na makaburi. Na hata kwa nasibu inapotekea mtu mzima akakutana na mkoma alipaswa kupiga yowe la kumwamuru mkoma arudi mahali pake. Mtazamo wao ni kuwa magonjwa au maradhi yote ni matokeo ya laana ya dhambi ila ukoma kwa namna ya pekee si tu matokeo ya dhambi bali ni dhambi yenyewe iliyomfanya mtu kuwa najisi, hivyo lazima kutengwa si tu na hekalu na masinagogi bali hata na familia, ndugu, jamaa na rafiki na jamii nzima. Wakoma waliteseka si kutokana na ugonjwa wao. Hivyo kupona ukoma ni sawa na kufufuka kutoka wafu. Ni Mungu pekee ndiye angeweza kumponya mkoma. Na ndio sababu tunaona wakoma si tu walikuwa mbali na jamii na watu wengine bali pia mbali na Mungu kadiri ya mitazamo ya watu wa nyakati zake Yesu.
Ni kwa sababu hizi basi tunaona wakoma wanaokutana na Yesu katika somo la Injili ya leo, Jumapili ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa, wanasimama mbali na kumuomba Yesu awarehemu, awaonee huruma. Ombi lao kwa Yesu ni awatazame si kama wengine walivyowaona na kuwahukumu kuwa ni wadhambi na najisi bali awaangalie kwa jicho lake la Huruma na Upendo. Ni watu wenye njaa na kiu ya upendo na huruma. Wanasimama mbali na Yesu na kwa pamoja wanafanya sala yao ya kuomba huruma ya Yesu. Kwa kweli njaa na kiu yao kubwa si kupokea muujiza wa kupona ugonjwa wao bali kukosa huruma na upendo kutoka kwa wengine. Ni mateso makubwa kwao si kuwa na ngozi iliyopoteza uhai na kukosa hisia bali mateso makubwa mioyoni mwao kuwa mbali na wengine. Hivyo waliteseka kimwili lakini zaidi sana kiroho na kiakili. Yesu baada ya kuwaona tunaona hawatendei muujiza wa kuwaponya bali anawaalika sasa kurejea katika jumuiya zao kwa kwenda kujionesha kwa makuhani ambao kadiri ya Kitabu cha Mambo ya Walawi sura 14:2-7 ndio pekee walikuwa na mamlaka ya kuthibitisha kupona kwa mkoma na hivyo kuweza kumruhusu kurejea na kujumuika na jamii kama awali.
Hivyo Yesu anawaalika waanze safari ya kurejea maisha yale waliyoyakosa na kuyatamani, kuwa na familia na ndugu na jamaa zao. Hivyo tunaona hapa uponyaji wao hauji mara moja wanapokutana na Yesu bali wanapotii amri na maagizo ya Yesu hivyo wakiwa njiani kuitikia amri hiyo ndio wanapokea uponyaji kwa kutasasika tena ngozi zao. Ni kama tulivyosikia pia katika Somo la Kwanza kuwa Naamani anapona ukoma wake baada ya kuachana na Nabii Elisha. Mwinjili Luka katika sura ile ya 5:12 -1 6 tunaona uponyaji unapokelewa mara moja, nataka takasika ila hapa hali ni tofauti. Hapa tunaona ili kupokea uponyaji na kuwa huru tena lazima kutii agizo la Yesu nalo ndio kwenda na kuishi Neno lake, ni mchakato katika maisha yetu, ni safari ya kiroho ambayo tunaalikwa na Injili yake kwenda kuiishi na hapo ndipo tunaweza kuona muujiza mkubwa katika maisha yetu, yaani kupokea si tu uponyaji wa ngozi bali mabadiliko ya ndani, kuwa na imani kweli. Yesu anashangazwa kuwa anayerudi kushukuru na kumtukuza Mungu ni msamaria, ni mgeni, ni mpagani. Na ndio Yesu anamwamuru asimame na kwenda zake kwani imani yake imemponya.
Mwinjili Luka si tu hapa anataka kutuelezea juu ya muujiza wa wakoma kumi bali zaidi sana anatualika kupata ujumbe kusudiwa katika Dominika ya leo. Basi nawaalika tutafakari zaidi. Wakoma kumi, idadi 10 kama vilivyo kumi vidole vyote vya mikono yetu au miguu yetu ndio kusema namba kamili, idadi kubwa ya wakoma waliopata kuponywa na kutakaswa na Yesu. Hivyo wakoma kumi wawanakilisha watu wote wa kila kabila, lugha na rangi. Ni sisi sote tu wakoma. Sote tu wagonjwa wa ukoma na hivyo tunahitaji kukutana na Yesu na kwa Neno lake tuweze kupokea uponyaji si tu wa ngozi bali wa ndani mwa kila mmoja wetu. Kwa kawaida Wayahudi hawachangamani na Wasamaria kwani walionekana ni wapagani na hivyo najisi, ila wanapokuwa wakoma na katika hali duni ya kusetwa na kutengwa tunaona hawa wanachangamana. Ni kama nasi katika maisha yetu ya kawaida kuna nyakati tunapojisikia wanyonge na duni hapo tunaungana na kuwa wamoja kuliko nyakati zile ambazo kila mmoja wetu anapojiona au kujisikia ana uwezo fulani.
Labda hata katika maisha ya kiroho ni mara ngapi tunapojiona wenye haki na safi tunawaangalia wengine kwa jicho la kaa chonjo, kaa mbali, kuwaangalia hata kwa jicho la hukumu na dharau? Mtakatifu Francisko wa Assisi si tu alimkumbatia na kumbusu mkoma bali akanywa maji aliyotumia kusafishia madonda ya mkoma. Ndio kusema alifuata mfano wa Yesu mwenyewe ambaya hakusita kuwakaribia wakoma na kuwaonjesha huruma na upendo wake tofauti na mfarisayo na viongozi wengine wa dini. Yesu hakuogopa kukaa na kula na kuambatana na wadhambi kama mafarisayo bali tunaona alikuwa rafiki wa wadhambi, ndio kusema alikaa na kula na kunywa nao ili kuwaonesha upendo na huruma yake. Mwinjili Marko 1:45 anatuonesha hata baada ya kuwaponya wakoma Yesu ilimpasa kukaa sehemu ya jangwani kwani asingeruhusiwa kuchangamana na jamii kwani aliwakaribia watu najisi, ndio kusema Yesu anakubali kujitanabaisha na watu najisi, watu walioonekana wadhambi na wasio na haki.
Ni Yesu anayekubali kuutwa ubinadamu wetu na kuja kukaa katikati yetu, ni Mungu aliye Mtakatifu anashuka kukaa katika uduni wetu, ni Upendo usio na kifani, ni Upendo wa ajabu, ni Upendo usi ona kujitafuta bali ni Upendo wenyewe! Wakoma wale wanakwenda kwa umoja na kutoa sala yao ya pamoja. Ni katika umoja tunaalikwa kila mara kumtafuta Yesu. Safari ya imani ni safari ya kuachana na ubinafsi wetu. Leo tunaona kila mmoja anaona mwenzake ana uhitaji wa kukutana na huruma na upendo wa Mungu. Ombi lao linakuwa moja, hitaji lao ni moja hakuna mmoja anayejiona ni yeye peke yake mwenye uhitaji bali wote kwa pamoja wanakwenda na kupiga kelele kutoa ombi na sala yao. Hata kama wanasimama mbali bado wanabaki na imani kuwa sala yao itamfikia Yesu, na ndio ishara ya mtu mwenye imani. Bila kujali hali na uduni wake na umbali wake na Mungu bado anakuwa na hakika kuwa sala yake itamfikia Mwenyezi Mungu. Hakuna umbali unaoweza kututenga na Mungu. Wakiwa njiani kama nilivyotangulia kusema sisi sote kama Kanisa la wasafiri tunaalikwa kwa kutii Neno la Yesu yaani Injili yake kupokea muujiza wa uponyaji na utakasaji.
Ni mmoja aliye mgeni tena Msamaria ndiye anayerejea kushukuru na kumsifu Mungu. Tunaona Yesu akihoji na kuuliza iweje ni mmoja tu tena aliye mgeni ndiye amerudi kushukuru na kusifu. Labda hata nasi tunabaki na maswali juu ya mshangao wa Yesu kwani ni Yeye aliwaagiza waende wakajioneshe kwa makuhani, na hivyo yawezekana walikuwa bado katika mchakato huo na pengine baadaye au hata siku nyingine wangerudi tena na familia na ndugu na jamaa na marafiki zao ili kumshukuru na kumtukuza Mungu. Na kwa kweli yawezekana kabisa walirudi na kufanya hilo alilofanya Msamaria, ila basi tutafakari kwa nini mshangao huu kwa Yesu. Yesu kwa kweli hazungumzii juu ya shukrani na kumtambua kuwa ni Yeye ametenda muujiza huo mkubwa bali anazungumzia juu ya kumrudishia sifa Mungu. Ndio kusema kuweza kuonja wema na ukuu wa Mungu kwao. Ni Msamaria huyu aliyetambua kuwa ni mkono wa Mungu umemtendea Mungu, ni kutambua nguvu za Mungu ndani ya Yes una hivyo kurejesha sifa na shukrani kwa Mungu. Ni mmoja mwenye imani ya kweli kwa Mungu.
Na anaporudi inakuwa ni nafasi ya kukiri imani yake mbele ya Yesu. Ni wazi Wayahudi waliokulia katika mazingira ya dini tungelitegemea wawe wa kwanza kukiri imani, kutambua umungu wake Yesu bali imekuwa kinyume. Ni katika mazingira haya Yesu anabaki na mshangao na mshangao wake unakuwa na mashiko. Si kwamba wale kenda walikuwa waovu bali walikosa imani ya kweli pamoja na kuponywa maradhi yao hawakuweza kuonja upendo na wema na ukuu wa Mungu tofauti na mgeni yule. Waliendelea kuishi kwa kuongozwa na tamaduni zao, yaani dini ile ya kale na hivyo kukosa kumyambua Yesu kuwa ni sura halisi ya wema na upendo wa Mungu. Walibaki kuona kuwa Mungu anabaki katika dini ile ya kimapokea yaani kule hekaluni na katika masinagogi badala ya kumwamini Mungu katika Nafsi ya Mwana pekee wa Mungu. Ni Msamaria ndiye anayemtambua Yesu kuwa ni Kristo na Masiha na hivyo kupokea sio tu muujiza wa kupona ukoma bali ukombozi wa nafsi na roho yake. Muujiza ule umeweza kumsaidia pale ambapo Mungu mwenyewe anatualika sote kufika yaani kuwa na imani ya kweli nathabiti kwake.
Wapendwa sote tunaalikwa kupokea sio tu uponyaji bali wokovu kutoka kwa Yesu. Ni kumkiri Kristo kama alivyofanya mkoma yule msamaria. Kadiri ya Injili ya Luka wote kumi walipona ukoma wao ila mmoja tu aliye mgeni aliyepokea uponyaji na ukombozi. Mwinjili Luka anatumia neno la kigiriki ‘’sozein’’ kumaanisha msamaria yule alipokea uponyaji kamili kutoka katika kila uovu na ndio sawa na ukombozi wa kiroho. Mtakatifu Katharina wa Siena anasema ni roho zetu zenye ukoma wa kiroho zinazohitaji kwa nafasi ya kwanza uponyaji, hivyo nawaalika kwa pamoja tuzidi kumuomba Mungu bila kujali umbali tulipo kwani daima anazisikia sala na maombi yetu ili atuponye roho zetu na ukoma utokanao na maisha ya kale yaani maisha ya utumwa wa dhambi unaotutenga na Mungu na jirani. Tafakari njema na Dominika njema.