Tafakari Jumapili 27 Mwaka C: Imani: Sakramenti, Maisha & Sala!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 27 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatuonyesha nguvu ya imani kwa Mungu mmoja. Kama mitume walivyomwomba Yesu awaongezee imani vivyo hivyo nasi tumwombe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo mkombozi wetu atuongezee imani na tuishuhudie katika maisha yetu ya kila siku hata katika magumu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume, “Porta Fidei” yaani “Mlango wa Imani” anasema kwamba, kwa njia ya upendo wake wa dhati, Kristo Yesu aliweza kuwavuta watu wa nyakati zote; kwa njia ya Kanisa lake, anaendelea kuwaalika wengine pamoja na kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, changamoto ambayo daima ni endelevu. Kanisa linakabiliwa na changamoto ya Uinjilishaji ili kuwawezesha waamini kutambua ile furaha ya kuamini na kushirikisha imani yao. Waamini wanapaswa kugundua upendo wa Kristo kila siku ya maisha yao; kwa kujitoa kwa ajili ya kazi za kimissionari, ili iweze kusonga mbele. Imani inakuwa pale tu inapomwilishwa kwa njia ya mang’amuzi ya upendo unaopokelewa kwa dhati na kuwashirikisha wengine kama mang’amuzi ya neema na furaha.
Kwa kuamini anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, imani inakuwa na kuimarika zaidi, kiasi kwamba, inakuwa ni vigumu kwa mwamini kuipatia kisogo, kwani hata upendo kwa Mwenyezi Mungu utakuwa unaimarika zaidi, kwani Yeye ndiye chemchemi ya upendo huo. Mama Kanisa anapenda kuadhimisha Mwaka wa Imani kwa ari kubwa zaidi, ili uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Tafakari kuhusu imani haina budi kuimarishwa zaidi, ili kuwawezesha waamini kumfahamu Kristo zaidi na kujishikamanisha na Injili, hasa wakati huu ambapo mwanadamu anashuhudia mabadiliko makubwa katika maisha yake. Ni kipindi cha kuungama imani kwa Kristo Mfufuka, ili kila mwamini aweze kuifahamu vyema, ili hatimaye, kuirithisha kwa kizazi cha sasa. Jumuiya, Parokia na Vyama vya Kitume vinachangamotishwa kutafuta njia ambayo itawawezesha kuungama imani yao hadharani katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Mama Kanisa anapenda kuona watoto wake wakiungama imani yao katika ukamilifu wake, kwa mwamko na ari mpya zaidi, kwa kujiamini pamoja na kuwa na matumaini makubwa zaidi.
Iwe ni fursa ya kuimarisha imani katika Liturujia na kwa namna ya pekee katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni changamoto kwa waamini kutoa ushuhuda unaoaminika. Waamini watambue maudhui yaliyomo kwenye Kanuni ya Imani wanayoungama, wanayoadhimisha, ishi na kusali; mintarafu imani inayomwilishwa katika maisha ya kila mwamini. Katika somo la kwanza Habakuki nabii katika Yuda wa kabila la Lawi, mmoja wa waimbaji wa hekaluni, jina lake likimaanisha “Kumbatia” anamnung’unikia Mungu kwa kutokusikia kilio chake na maombi yake kwa ajili ya taabu walizopata watu wa Taifa lake walioonewa. Habakuki aliona kwamba viongozi wa Yuda walikuwa wanawaonea maskini, kwa hiyo aliuliza swali kwamba ni kwa nini Mungu anawaruhusu watu hawa waovu kustawi. Mungu alimjibu Habakuki kwamba Wakaldayo wangekuja kuwaadhibu. Lakini Habakuki aliumia zaidi na hakuelewa ni kwa jinsi gani Mungu angeweza kuwatumia Wakaldayo ambao walionekana kuwa waovu kuliko Wayahudi waovu, ili kutekeleza hukumu dhidi yao.
Jibu la Mungu lilikuwa kwamba ili waache ouvu wao na wamrudie. Kumbe Mungu anweza kuwatumia waovu kuwaadhibu watu wake wanapotenda uovu ili waaache uovu wao. Lakini waovu anaowatumia Mungu kuwaadhibu watu wake, wakiisha kutimiza kusudi lake, huwaadhibiwa na adhabu yao ni kubwa zaidi. Ndiyo maana watu wa Yuda walipotenda dhambi ikiwa ni pamoja na kuabudu sanamu, Mungu aliwatumia Wakaldayo walio waovu zaidi kuwaadhibu na hatimaye, Mungu akawaadhibu pia Wakaldayo. Kama ilivyomshangaza Habakuki kuona waovu wakistawi huku wakiendelea kutenda dhambi nyingi wala Mungu hawaadhibu upesi ndivyo ilivyo hata nyakati zetu katika maisha yetu. Wakati mwingine tunamlalamikia Mungu na kumuuliza kwanini watu wema wanateseka na kuteswa na waovu, kumbe yawezakuwa ni kwasababu hawa watu wema wamemkosea Mungu naye anawaadhibu warudi kwake na mwisho wa waovu ni mbaya zaidi kwani adhabu yao ni ya milele.
Habakuki anaamini juu ya mamlaka ya Mungu na anauhakika kwamba Mungu ana haki katika njia zake zote na kwamba bado anaitawala dunia hata kama uovu bado unashamiri na ya kwamba iko siku Mungu atauhukumu na kuadhibu uovu na waovu wote na hatimye kuuangamiza kabisa usiwepo tena ndiyo maana hakukata tamaa kumuuliza Mungu mwisho wa matatizo hayo ni lini. Kumbe hatupaswi kuwa na mashaka juu ya nguvu na uwepo wa Mungu kwa uwepo wa uovu na waovu, cha maana zaidi kwetu ni kujikabidhi na kujiaminisha kwake Mungu muweza wa yote. Katika somo la pili la Mtume Paulo akiwa gerezani anamhimiza Timotheo ambaye alianza kuogopa kuhubiri Injili sababu ya madhulumu na kufungwa kwake Paulo, akimwambia kuwa akumbuke kuwa alipokea nguvu ya Roho Mtakatifu siku alipowekewa mikono. Hivi asiogope kutangaza Injili. Paulo anamwambia Timotheo, ndugu yangu, nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.
Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. Paulo kama Habakuki anaamini juu ya nguvu na uweza wa Mungu ambao haushindwi na chochote, licha ya kuwa yuko gerezani na anamtia moyo kijana Timotheo abaki katika imani hiyo na kuendelea kuihubiri mpaka kieleweke, ndivyo tunavyopaswa kuwa sisi tuliyoipokea imani kwa njia ya ubatizo na kuwekewa mikono na wazee wa Kanisa tukampokea na Roho Mtakatifu katika sakramenti ya kipaimara na kila siku kwa neno la Mungu na Ekaristi Takatifu tunaendelea kuimarishwa na kutiwa nguvu ili tuishihudie vyema imani yetu. Katika Injili ilivyoandikwa na Luka, mafundisho ya Yesu yanaonekana ni magumu kwa mitume hivyo wanasali na kuomba Yesu awaongezee imani.
Mtazamo huu wa Mitume haujatuacha salama mara nyingi tunaona mafundisho ya Kanisa aliyotuachia Yesu kuwa ni magumu na pengine ya ukandamizaji hatuwezi kuyaishi, basi nasi tusali kila mara sala hii ya mitume tuongezee imani ili tupate nguvu ya kuyashika na kuyaishi mafundisho ya Kanisa. Lakini jibu la Yesu kuwa, “kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeweza kuuambia mkuyu, ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6 latufundisha kuwa nguvu ya imani ipo katika kuweka tumaini lote kwa Mungu, na sio kutegemea nguvu zetu, mali zetu, akii zetu, mamlaka yetu bali ni katika kuweka tumaini letu kwa Mungu mazima mazima bila kujibakiza na bila mashaka wala wasiwasi wowote. Mfano wa mtumwa unafundisha, ukweli wa kuwa mtumwa hawezi jiinua na kujipongeza kwa kazi yake, zaidi ya kufanya na kutimiza wajibu wake kadiri ya mapenzi na matakwa ya Bwana wake. Na hivi ndivyo Mtume Paulo asemavyo, “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili” 1Kor 9:16.
Hakuna la kujisifia, zaidi ya kutimiza kwa uaminifu lile tupaswalo kutimiza. Sisi tumeumbwa na Mungu, kwaa ajili ya sifa na utukufu wake. Hivyo hatupaswi kujisifia kazi na mafanikio yetu bali yote yawe na kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, ili kwazo Mungu atukuzwe nasi tutakatifuzwe. Fundisho hili ni kinyume kabisa na mwono ule wa mafarisayo waliojiwekea mapambio kwa kazi zao na kusahau ukweli kwamba siyo kazi ndizo zinazotuhesabia haki, bali ni neema na kwanyo ni zawadi ya Kimungu kwetu. Kamwe hatuwezi jifananisha na vitu au idadi ya yale tuyatendayo, bali roho na upendo ule utusukumao kufanya mambo hayo hata kama ni madogo na macheche sana. Hivyo roho hiyo na upendo huo katika kutenda, na kwa kibali chake Mungu na kwa kadiri ilivyompendeza twahesabiwa haki. Ndiyo maana Yesu, anasema, “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10.
Kuna furaha ya kweli tunapojibandua kutoka vitu na mali, na kutovifanya ndio mwisho wa kila kitu ingawa twavihitaji hapa na pale. Tumruhusu Roho Mtakatifu atawale maisha yetu, atufundishe na kutuongoza vyema ili tuweze kutambua mipango na makusudi ya Mungu katika maisha yetu kwani Yesu anatuambia, “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, bali yote atakayoyasikia kutoka kwangu na kutoka kwa Baba atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh 16:13. Tukumbuke kwamba, tunaadhimisha Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 ili kuhamasisha ari na mwamko wa shughuli za kimisionari. Tunasindikizwa pia kwa sala, maombi na tunza ya Bikira Maria kwa tafakari ya Rozari Takatifu, muhtasari wa huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Tumsifu Yesu Kristo.