Tafakari Jumapili 28 Mwaka C: UKIRO na Moyo wa Shukrani
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelium gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anasema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi ya wokovu wanawekwa huru na hivyo kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke hasi. Pamoja na Kristo daima, furaha inazaliwa upya! Baba Mtakatifu Francisko anasema, furaha ya Injili ndiyo chapa makini ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, furaha ya Injili daima ni mpya na ni furaha inayoshirikishwa; ni furaha inayoinjilisha, inayopendeza na kufariji, ili kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu anakazia mabadiliko ya umisionari wa Kanisa, upeo wa tatizo la kujiaminisha katika Jumuiya; utangazaji na ushuhuda wa Injili; mwelekeo wa kijamii katika mchakato wa uinjilishaji.
Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa Kanisa kuwa na mihimili ya uinjilishaji iliyojazwa nguvu na karama za Roho Mtakatifu pamoja na kutambua kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa na ni nyota ya uinjilishaji mpya. Ujumbe wa masomo ya leo ni iweni na moyo wa shukrani. Somo la kwanza kutoka kitabu cha pili cha Wafalme linasimulia jinsi Naamani, jemedari mpagani, mkuu wa Jeshi la Syria alivyoponywa ukoma wake na Nabii Elisha Myahudi baada ya msichana Msamaria aliyechukuliwa mateka na Waasyria kumwambia kuwa katika Israeli kuna mtu wa Mungu naye ataweza kumponya. Hivi ndivyo Bwana alivyoufunua wokovu wake machoni pa mataifa kama wimbo wa katikati unavyotuambia. Jemedari Naamani baada ya kupona alikiri kuwa Mungu wa Waisraeli ana wema na nguvu za kipekee kuliko miungu wa nchi yake. Naamani anataka kumshukuru Mungu kwa kumpatia Nabii Elisha zawadi. Nabii Elisha anakataa kuonesha na kukiri ukuu wa Mungu kwamba si yeye aliyemponya bali ni Mungu. Naamani anaomba udongo wa nchi ya Israeli ili akamjengea Mungu madhabahu amwabudu yeye peke yake.
Somo hili linatufundisha kuwa na moyo wa shukrani kwa wema wa Mungu kama Naamani jemedari mpagani pia kuwa na moyo wa kuwasaidia wenye shida kama msichana Msamaria na tuwe na unyenyekevu kama wa nabii Elisha. Katika somo la pili kutoka waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo, Paulo akiwa gerezani anaendelea kumsihi Timotheo na kumpa maagizo yake kuwa tukiteswa na kutolea uzima wetu kwa ajili ya kazi ya Yesu Kristo tutafufuka pamoja na Kristo na tutashiriki naye furaha ya mbingu. Tusipomwungama Kristo katika mateso, yeye atatukataa siku ya hukumu. Paulo anamwambia Timotheo, mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, kama inenavyo injili ambayo kwayo yeye Paulo ameteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo anastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Maneno haya ya Paulo yatutie nguvu nasi tusirudi nyuma kamwe na kuiacha imani yetu kwa sababu yoyote ile hata ikitupasa kujitoa sadaka kwani hiyo ndiyo shukrani yetu kwa Kristo aliyetoa maisha yake kwa ajili yetu na ndiyo njia ya kutufikisha katika uzima wa milele. Injili ilivyoandikwa na Luka inamleta tena mtu Msamaria mwenye imani kamili. Msamaria huyu baada ya kuponywa ukoma wake kama jemedari Naamani aliyeponywa baada ya kuaginzwa na msichana mtumwa msamaria kwenye Israeli kwa Nabii Elisha, anarudi kumshukuru Yesu Kristo. Hapo Wayahudi waliojiona taifa teule wanaaibishwa na huyu asiye Myahudi. Hivi ni onyo kwetu sisi wakristo tusije tukaaibishwa na wasio wakristo.
Tuwe na moyo wa shukrani. Mwinjili Luka anasema kuwa wenye ukoma walisimama mbali, wakapaza sauti wakesema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu. Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Maswali mawili ya kujiuliza: kwanini walisimama mbali na kwanini Yesu awaagize wakajionyeshe kwa makuhani? Ukoma ni ugonjwa unakula polepole sehemu za mwili wa mtu hasa vidole vyake vya mikono na miguu, masikio, pua na midomo. Wakoma hawakupaswa kuwakaribia watu wengine hivyo walifungiwa kengele ili wanapotembea watu wasikie wawapishe pia kama wanapita sehemu yenye watu walipaswa kufunika mdogo wa juu, na kupiga kelele, mimi ni najisi, mimi ni najisi ili wampishe. Wenye ukoma kumi walishika vizuizi vya Sheria hii na kubaki mbali na Yesu. Hata hivyo, wao wanapiga kelele kwa sauti kubwa hivi: “Ee Yesu, Bwana mkubwa, Uturehemu!” Yesu anawaamuru waende wakajionyeshe kwa makuhani kwa sababu kisheria makuhani walikuwa na mamlaka ya kuwatangaza waliopona ugonjwa huu na kuwapata kibali cha kuishi tena pamoja na watu wenye afya.
Wasamaria walikuwa hawachangamani wala hawapikiki chungu kimoja, walikuwa maadui. Wasamaria walionekana mbele ya wayahudi kuwa ni najisi na wadhambi kwani kihistoria, wasamaria ni mchanganyiko wa watu wa kabila la Efraimu na Manase walioishi katika Samaria mji mkuu wa ufalme wa kaskazini wa Israeli na makabila mengine walioletwa na mfalme wa Ashuru baada ya wayahudi wengine kuchukuliwa mateka (2 Wafalme 17:24; Ezra 4:2-11). Dini yao ilikuwa ni mchanganyiko wa imani na desturi za Kiyahudi na kipagani. Wayahudi hawa walioana na makabila yaliyoletwa wakaiacha dini yao wakaabudu miungu ya kigeni (2 Wafalme 17:26-28). Hivyo wayahudi asili waliporudi utumwani na kukutana na hali hii walichukizwa sana wakawatenga na kuwaona kuwa ni waasi hata wakajenga ukuta ili wasiweze kuingia tena Yerusalemu. Kilichowaunganisha msamaria huyu mmoja na wayahudi wale kenda ni ugonjwa wa ukoma. Mara nyingi matatizo yanatuunganisha na kutufanya tusahau tofauti zetu.
Hawa wakoma katika ugonjwa wao walisahau tofauti zao za Kiyahudi na Kisamaria. Walijiona kuwa wao ni wahitaji. Tatizo la kuungana katika shida tu ni kwamba shida ikiisha tunarudi kule tulikokuwa ndiyo maana msamaria alijitenga na kurudi peke yake. Baba wa Taifa la Tanzania mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwaonya watanzania kuhusu ukabila alisema kuwa wanajiona kuwa ni Wazanzibari au Watanganyika kwa sababu wako katika muungano, wakishajitoa katika muungano, dhambi ya ubaguzi inabaki pale pale na itaendelea kuwala. Nje ya muungano hawatasema tena sisi Wazanzibari bali watasema “Sisi Wapemba, ninyi Waunguja.” Hata sisi tukisha wabagua wengine iwe katika jumuiya, katika kazi au serikali hata sisi wenye hatutabaki wamoja tutaanza kubaguana sisi wenyewe. Kwa kuwa muungano utokanao na matatizo au mahitaji basi tuunganishwe na hitaji lisiloisha kwamba sote tunamhitaji Mungu hata uwe nani utamhitaji Mungu tu.
Uponyaji wa Naamani Jemadari, unaibua hisia za uchaji na utambuzi wa ajabu juu ya Mungu na kusema, "Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli,” 2 Fal 5:15. Tuyakumbuke kila mara matendo makuu anayotutendea Mungu na haya yatufanye tuwe na imani thabiti katika maisha yetu kwani mzaburi anasema msifu Bwana, moyo wangu; wala usizisahau fadhili zake” (Zab.103). Naamani anaahidi “kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana”. Nasi tuweke ahadi za kudumu imara katika imani ya Mungu mmoja iliyosimika na Yesu Kristo katika kanisa moja takatifu katoliki na la mitume. Tumsifu Yesu Kristo.