Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa udumifu katika maisha ya sala! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa udumifu katika maisha ya sala! 

Tafakari Jumapili 29 Mwaka C: Utamaduni wa udumifu katika sala!

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba sala ni zawadi ya neema na jibu la uamuzi wa upande wa waamini. Sala ni mapambano dhidi ya mtu binafsi na hila za Shetani, Ibili. Kwa kawaida mtu anapaswa kusali jinsi anavyoishi kwa sababu anaishi jinsi anavyosali. Waamini wanakumbushwa kwamba, kuna vizuizi na kushindwa katika Sala. Kesheni kwa moyo wa unyenyekevu! SALA!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu wa neno la Mungu ni kuwa tusichoke kusali kwa imani mbele za Mungu Baba yetu aliyetuumba. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba sala ni zawadi ya neema na jibu la uamuzi wa upande wa waamini. Watu mashuhuri kutoka Agano la Kale hadi Agano Jipya wanakiri kwamba, Sala ni mapambano dhidi ya mtu binafsi, hila za Shetani, Ibili. Kwa kawaida mtu anapaswa kusali jinsi anavyoishi kwa sababu anaishi jinsi anavyosali. Waamini wanakumbushwa kwamba, kuna vizuizi na kushindwa katika Sala. Kumbe, kuna haja ya kukesha kwa moyo wa unyenyekevu, ili kukabiliana na ukavu wa maisha ya kiroho, ili kuweza kukabiliana na vishawishi pamoja na vizingiti katika sala! Waamini wajenge tumaini la kimwana na kudumu katika upendo!

Somo la kwanza la kitabu cha Kutoka, linasisitiza juu ya nguvu ya sala ilivyo. Ukweli huo unaonekana kwa Waisraeli walipowashinda adui zao Waamaleki walipopigana nao huko Refidimu kwa maombezi ya Musa, maana kila alipoinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Ndiyo maana ilibidi Musa akae juu ya jiwe, Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, nayo ikathibitika hata jua lilipokuchwa Yoshua akashinda vita. Katika somo la pili Mtume Paulo anaendelea kumshauri, kumtia moyo na kumuonya kijana Timotheo ashike kweli zote za maandiko matakatifu alizofundishwa tangu utoto wake ambayo yaweza kumhekimisha hata apate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Tena asichoke kuhubiri Neno la Mungu, awe tayari, wakati ufaao na wakati usiofaa, akaripie, akemee, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.

Maonyo haya leo hii yanatuhusu nasi kwani ni maonyo matakatifu yatokayo kwenye vitabu vitakatifu vilivyoandikwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, hivi maonyo yake ni ya milele na kwa vizazi vyote. Kwa maana kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. Sisi nasi kwa ubatizo wetu tuliipokea imani kama watoto wachanga, tukakuzwa kwa kushibishwa na neno la Mungu, sakramenti ya kipaimara ikatuimarisha na Ekaristi Takatifu inaendelea kutupatia nguvu hivi tuna kila sababu ya kuishika na kuiishi imani yetu bila woga wala wasi wasi wowote. Katika Injili ilivyoandikwa na Luka kwa kutumia mfano wa kadhi dhalimu, ujumbe wa Yesu unakazia mambo mawili, kwanza ni kwamba Mungu hana kinyongo na mtu anayehitaji msaada wake na pili, sisi sote tunahitaji msaada wa Mungu, hivyo tumwombe msaada siku zote bila kuchoka wala kukata tamaa.

Katika mfano huu kuna wahusika wakuu wawili ambao kila mmoja ana ujumbe mahususi. Kwanza ni hakimu au kadhi dhalimu: Huyu ni mtu mwenye madaraka ya kuamua kesi kisheria; Ni mwamuzi baina ya pande mbili au zaidi katika mgogoro. Mhusika huyu katika Injili ana sifa mbili; Hamchi Mungu na Hajali watu. Hakimu wa namna hii hawezi kuangalia haki iko wapi. Hali hii inajidhihirisha kwa namna alivyoichukua kesi yam ama mjane kwamba kwa muda mrefu hakutaka kumtetea, kwani kwa kutokumcha Mungu wala kumjali binadamu, kwa hakimu wa namna hii ni lazima awe mla rushwa na mjane hakuwa na uwezo wa kutoa rushwa. Mhusika mwingine ni mama mjane: Mjane ni mwanamke aliyefiwa na mume wa ndoa na mume aliyefiwa na mkewe anaitwa mgane. Kwa Wayahudi Katika Agano la Kale, mjane alitazamwa kuwa mtu aliyehitaji ushauri, ulinzi na faraja ya pekee kwasababu ya upweke aliokuwanao.

Pia kulikuwa na nguo maalumu aliyovaa ili kumtofautisha na kahaba au mwanamke asiye mjane (Mwanzo 38:14). Kutokana na mazingira haya magumu aliyokuwa nayo ziliwekwa sheria za kuwalinda wajane ambazo zilihusu usalama wao, mashamba yao, watoto wao na mali zao. Laana ilitangazwa kwa wale ambao hawakuwafanyia haki wajane. Kitabu cha kumbukumbu la torati kinasema, alaniwe apotoshaye hukumu ya mgeni na yatima na mjane aliyefiwa na mumewe na watu wote waseme, Amina” (Kumb 27:19.). Katika Injili mhusika huyu ni maskini na ana shida. Hawezi kushinda kesi yake kwa kutoa rushwa. Shida aliyonayo anataka apewe haki zake ambayo haijatajwa wazi. Lakini katika unyonge na umaskini wake huu ana silaha moja tu, yaani udumifu katika kumwendea hakimu tena na tena kiasi cha kumchosha, hatimaye hakimu alimtetea na kumpa haki yake akisema, “Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima,” Lk 18:4b-5.

Kwa mfano huu wa Hakimu dhalimu na Mama mjane, Yesu anatufundisha kuwa, ikiwa hakimu huyu dhalimu, asiyemcha Mungu, tena hawajali wanadamu, alimsaidia mama mjane baada ya kusumbuliwa mara kwa mara akidaiwa atende haki: Mungu Baba yetu mwema tukisali na kudumu katika kumwomba daima atatusikiliza na kutusaidia. Lakini tusisahau sharti moja kuendelea kumuomba bila kuchoka. Tuige mfano wa Musa aliyeliombea taifa lake lishinde vita, tuige mfano wa Yesu mwenyewe aliyesali daima katika maisha yake ya hapa duniani na kabla ya kufanya tukio lolote daima alisali kwanza. Kabla ya kuwateua mitume wake 12 (Lk 6:12), katika miujiza aliyofanya daima aliimua macho mbinguni kwa Baba na kusali, kabla ya kukamatwa na kuteswa alisali katika bustani ya Getsemane, (Lk. 22:42).

Tutambue kuwa kusali ni sehemu ya maisha yetu. Sala ni kama mafuta yanayoifanya taa ya imani yetu ibaki ikiwaka daima. Tukipuuzia sala imani yetu inalegea taratibu na hatimaye itapotea kabisa. Tutenge muda wa kusali katika familia zetu, tushiriki sadaka ya misa takatifu Dominika na tushiriki sala katika jumuiya zetu ndogondogo. Wakati wa raha, tumshukuru Mungu; wakati wa shida tumwombe atusaidie. Na tunaposali tusitegemee kupata kila kitu tuombacho. Mungu hafungwi na muda, hivyo atatupa kile anachoona kitatusaidia kumtumikia yeye na jirani. Tumwombe Mungu atusaidie neema ya kutambua nguvu ya sala katika maisha yetu ya kumtafuta na kutumikiana hapa duniani. Tukisali bila kuchoka. Lakini tukumbuke kuwa sala ya mtu mchafu, mtu mwenye dhambi ni kelele mbele za Mungu.

Kumbe, tunaweza kuwa tunajitahidi kweli kila siku asubuhi, mchana na usiku, kutwa mara tatu na Mungu asitujibu. Tunapaswa kujiandaa vyema kwa kujipatanisha na Mungu kwa njia ya sakramenti ya kitubio ili tunaposali sala zetu ziwe na kibali machoni pa Mungu Baba mwenyezi. Tumsifu Yesu Kristo.

JP 29 Mwaka C

 

16 October 2019, 15:36