Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Sadaka na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muweza wa yote! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Sadaka na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muweza wa yote! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 28 ya Mwaka: Sadaka ya Shukrani

Kwa njia ya Kristo Yesu, Mama Kanisa anaweza kutoa sadaka ya sifa katika shukrani kwa ajili ya kila kitu ambacho Mwenyezi mungu amekifanya chema, kizuri, na sawa, katika kazi ya uumbaji na katika ubinadamu. Wazo kuu katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 28 ya Mwaka ni ujenzi wa utamaduni wa kumshukuru Mungu, chemchemi ya wema, ukarimu na utakatifu wa maisha.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Katika Injili tunaona Yesu anamponya mwenye ukoma. Na mmoja anarudi kushukuru. Ni kwa nini arudi tu mmoja kushukuru? Tena mpagani. Sababu za kweli na za kufikirika za kukosa kutoa shukrani zaweza kuwa nyingi. Moja ya hizo yaweza kuwa – sasa tumeshapona, tunahitaji nini zaidi? Kukosa shukrani ni kuwa mbinafsi, ni kutanguliza mahitaji yangu kabla ya wengine.  Richard Braunstein anasema ni rahisi kutoa bila kupenda ila si rahisi kupenda bila kutoa.  Huyu alitambua upendo wa Kristo. Anatambua alichopata. Amepona katika shida yake. Anashukuru. Ndugu zangu, sehemu kubwa ya mafundisho ya Yesu inatawaliwa na miujiza na tunaona katika Agano Jipya jinsi watu walivyo na kumbukumbu zaidi ya miujiza aliyofanya Yesu kiasi kwamba huwezi kumtaja Yesu bila kutaja miujiza aliyofanya. Hata Yesu mwenyewe anaonesha hilo kwamba miujiza ni uthibitisho wa utume wake wa kimasiha – Mt. 11:4 … nendeni mkamweleze Yohani habari ya mambo mnayosikia na kuyaona: vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakata, viziwi wanasikia, wafu wanafufuka na maskini wanahubiriwa habari njema.

Ndugu zangu, hatuna budi lakini kutambua kuwa miujiza haijitoshelezi kwa yenyewe, na pia lengo lake si maigizo au aina ya mazingaombwe. Miujiza ni kichocheo na zawadi ya imani. Hii ni alama tu na husaidia kuvuta msisitizo kwa kile inachomaanisha. Kinyume chake itakuwa kilio. Twaona Yesu akisikitika, baada ya kuongeza mikate, watu wale hawakuelewa tendo hilo lilimaanisha nini – Mk. 6:51-52 – akaingia chomboni na upepo ukakoma. Wakastaajabu kupita kiasi. Kwa maana muujiza wa mikate ulikuwa umeipata ufahamu wao. Mioyo yao ilikuwa bado mizito. Tunaona pia katika Injili kuwa miujiza haikuwa wazi sana. Wakati mwingine huwa na ufahamu chanya au hasi. Huwa chanya pale yanapopokelewa na watu kwa mtazamo wa furaha, inapoamsha imani katika Kristo na kutoa matumani katika ulimwengu huru bila magonjwa na vifo. Huwa hasi inapotokea kuwa watu wanadai miujiza – Yoh. 6:30 – wakamwambia, basi, utafanya ishara gani, tupate kuona na kusadiki? Utafanya nini? Maelezo yafuatayo ya hao watu na uelewa wao ulikuwa tofauti kabisa mpaka Yesu alipowafafanulia na baada ya kuelewa wanamwomba Yesu awape huo mkate. Ndipo Yesu anasema mimi ndio huo mkate.

Hali hii ipo katika ulimwengu wetu huu. Kwa upande mmoja wapo wanaotafuta miujiza kwa hali yo yote ile na wanaodai miujiza hii huishia hapa – kama ukamilifu wa dai lao. Kuna upande mwingine pia wa wale wanoakataa nafasi ya miujiza kabisa katika maisha. Tunasoma katika Biblia kuwa miujiza ni ishara za wokovu na zinazoleta ufunuo kutoka kwa Mungu – Yn. 2:11 – mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana mji wa Galilaya. Alionesha utukufu wake, na wafuasi wake wakamsadiki. Miujiza ya Yesu ilifungamana na utangazaji wake wa ufalme wa mwisho wa Mungu – Mt. 4:23 – alizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao na kuitangaza injili ya ufalme. Akaponya kila ugonjwa na maradhi katika watu.; Lk. 13:32. Petro na Paulo wanakishuhudia kipaji cha namna hiyo hiyo kutoka kwa Mungu – Mdo. 3:1-11 – habari ya uponyaji waliofanya Petro na Yohane kwa yule kiwete katika lango la hekalu – kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, inuka na tembea; Rum. 15:19 – kwa nguvu ya ishara na miujiza, kwa uwezo wa Roho wa Mungu. Hivyo nilizunguka nchi toka Yerusalemu mpaka Ilirikumu nimemaliza kutangaza Injili ya Kristo kila mahali.

Kwa maelezo haya haiwezekani kutafsiri miujiza kadiri ya mapenzi yetu au kuyachukulia kama jambo la mzaha tu au jambo rahisi sana linaloweza kutokea katika maisha yetu. Baada ya ufahamu kama huu tunasema nini leo tunaposikia wahubiri mbalimbali wanaodai kwamba ni watenda miujiza? Tukirudi katika masomo yetu ya leo tunaona kuwa mojawapo ya lengo la mwandishi wa vitabu vya wafalme lilikuwa ni kuonesha jinsi Mungu wa Israeli alivyofunua mapenzi yake katika historia. Somo la kwanza la leo laonesha hilo. Tendo la kupona Naaman, mpagani katika taifa la Israeli laonesha hilo lengo. Naaman anatoa zawadi ambayo Elisha anakataa, ila Naaman anaomba kuchukua udongo toka Israeli na kuupeleka Siria, nchi ya kipagani. Lengo lake ni kujenga altare kwa udongo huo ili apate kumwabudu Mungu wa kweli. Hata mataifa ya kipagani yanatambua ukuu huu wa Mungu wa kweli.  Lakini kinachoonekana hapa ni nguvu ya Mungu ya kuponya wagonjwa au magonjwa. Uwezo huu wa Mungu uko wazi katika maandiko. 

Injili ya Luka inajulikana kama Injili ya wokovu kwa watu wote. Ni mwinjili pekee wa Agano Jipya anayenukuu habari ya Naaman mpagani akitambua ukuu na mapenzi hayo ya Mungu kwa wokovu wa wote. Hatuna budi kutafakari sana neno la Mungu siku ya leo na kufikiria matokeo yake. Tumeona nafasi ya Mungu katika kumponya mwanadamu. Upo pia uwezekano wa kukosa nafasi hiyo ikiwa tutapoteza kuishi mapenzi yake Mungu. Tumeona uwezekano wa kwenda kwa wapagani – kina Naamani, Msamaria n.k.  Hatuna budi kujiuliza ni kwa kiasi gani sisi tulio wake Mungu tunafaidika na utukufu huu wa Mungu. Isijekutokea kuwa siku ya mwisho wale tuwaonao na kuwaita wapagani wakapona kabla yetu na kurith maisha na uzima wa milele. Ni kwa kiasi gani au kwa namna gani tumetoa au tunatoa shukrani zetu kwa Mungu aliyetuumba kwa kuishi na kutimiza mapenzi yake? Tumsifu Yesu Kristo.

08 October 2019, 16:19