Kumbu kumbu ya Marehemu Wote: Ufufuko na uzima wa milele
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. -Dodoma.
Wapendwa taifa la Mungu, kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, Kanisa linawaombea marehemu wale wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na alama ya imani na sasa wanapumzika kwenye usingizi wa amani. Linawaombea ili watakaswe, ikiwa kama wanahitaji kutakaswa kabla ya kupokelewa mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele wakati miili yao inapobaki ardhini ikingoja kurudi kwa Kristo na ufufuko wa wafu. “sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba, katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu” (KKK 962). Hii ndiyo sababu kanisa linatolea sadaka ya misa kwa ajili ya marehemu. Mtakatifu Monika, Mama yake Mtakatifu Augustino, anaongezea thamani ufuhamu huu. Alipokuwa katika hatari ya kufa, aliwaomba watoto wake na kusema, “mnaweza kunizika popote mnapotaka lakini msinisahau katika Altare ya Bwana.”
Kanisa linasali na kuwaombea marehemu kusudi wapate msaada wa kiroho na waamini walio bado hai wapate matumaini ya uzima ujao mbinguni. Ni muhimu na vema kuwaombea wafu, kwani hata kama wamekufa katika neema na upendo kwa Mungu, inawezekana bado wanahitaji utakaso wa mwisho ili waweze kuingia katika furaha ya mbingu. Mtakatifu Ireneo anatupatia tafakari hii nzuri sana – utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai. Maisha ya mwanadamu, mkristo, mbatizwa huwa na aina mbili ya kifo. Kifo cha kwanza ni kwa njia ya ubatizo na imani – Rum. 1:6 – ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo - tumejiunga na Kristo aliyekufa na kufufuka kutoka kwa wafu. KKK 628 – ubatizo ambao alama yake ya asili na timilifu ni kuzamishwa, waashiria bayana kushuka kaburini kwa mkristo - anayeifia dhambi pamoja na Kristo ili aishi maisha mapya. Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima – Rom. 6:4; Kol. 2:12 .
Tumekufa na tumezikwa pamoja naye katika ubatizo, na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu; Efe. 5:26. Aina ya pili ya mauti aipatayo mkristo huwa sawa na ile impatayo mwanadamu ye yote, yaani ni wakati utokeapo utengano wa mwili na roho hapa duniani. Kama tunavyoshudia leo tunapoona kuwa ndugu yetu hayupo nasi tena kimwili. Ndugu zangu – KKK 990 – neno mwili laeleza mtu katika hali yake ya udhaifu na ya kufa – Mwa. 6:3; Zab. 56:5; Isa. 40:6. Hivi mwanadamu aliye katika hali ya mwili na aliye na mwanzo hufika kikomo. Hufikwa na mauti. Ila katika kitabu cha Hek. 1:13 – tunasoma kuwa, Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea; Rom. 5:12. Ila katika KKK 1008 na 413 tunaona kuwa; kifo ni tokeo la dhambi. Na kwamba mwanadamu ndiye asili ya mauti – kinyume cha muumba wake – Mwa. 3. Kifo cha kweli ni kifo cha mwenye dhambi.
Mamlaka funzi ya Kanisa, mfafanuzi halisi wa Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa hufundisha kwamba kifo kimeingia ulimwenguni kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu –Ingawa mwanadamu ana hali ya kufa, Mungu alimweka asife. Kifo kilikuwa ni kinyume cha mipango ya Mungu Muumbaji, nacho kiliingia ulimwenguni kama tokeo la dhambi – Hek. 2:23-24. Kifo cha kimwili, ambacho mwanadamu angekuwa huru nacho, ndiye adui wa mwisho wa mwanadamu ambaye lazima kumshinda – 1Kor. 15,26 – adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Mbele ya kifo fumbo la hali ya kibinadamu linakuwa kubwa sana - KKK 1006. Kwa namna moja kifo cha mwili ni kawaida, lakini kwa imani kwa kweli kifo ni mshahara wa dhambi – Rom. 6,23; - kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. Na katika Mwa. 2,17 tunasoma haya – walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. Lakini sisi tunamshukuru Kristo aliyetupatia matumaini mapya. Kwa wale wanaokufa katika neema ya Kristo, kifo ni ushirika katika kifo cha Bwana, ili kuwezza kushiriki pia ufufuko wake.
Tuna uhakika kuwa kwa njia ya Kristo – tunapata uzima mpya – Rum. 8:29, - maana wale aliowajia tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu. 2Kor. 5:17, - hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. Yoh. 14: 5-6 – Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia na kweli na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Yoh. 3,5 – Yesu akajibu, amini, amini, nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Mk. 16:16 – aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa. Mtume Paulo anaelezea mauti na aina fulani ya ukombozi – Rum. 7:1…. Kwa kifo cha huyo mtu – tunakombolewa na maisha ya zamani – Rum. 7:1-5. – kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata tukaizalia mauti mazao.
Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya Andiko. Mtume Paulo akiongea juu ya kifo chake anasema 2Tim 4:7-8 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.” Mtume Paulo aliwekeza katika Kristo na matumaini yake ni kuupata uzima wa milele. Tena ana hakika ya hilo. Anatualika nasi tuwekeze katika Bwana. Pengine swali ambalo mwanadamu asumbuka nalo baada ya fumbo la kifo ni hili. Wafu wanafufuka namna gani? KKK 997 – kufufuka maana yake nini? Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu, uipandayo haikui isipokufa, nayo uipandayo hupandi mwili ule utakaokua ila chembe tupu … hupandwa katika uharibifu, hufufuliwa katika kutoharibika; wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu…maana sharti huu uharibikao, uvae kutoharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa – 1Kor. 15,35-53.
Kwa kifo, mtengano wa roho na mwili, mwili wa mtu huoza, pindi roho yake huenda kukutana na Mungu ikingojea kuunganika na mwili uliotukuka. Mungu, kwa uwezo wake mkuu, atairudishia kwa hakika miili yetu, uzima usioharibika kwa kuiunganisha na roho zetu, kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu. Siri iliyo kuu na ngumu - KKK – 1005 – ili kufufuka pamoja na Kristo, ni lazima kufa pamoja na Kristo; ni lazima kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana – 2Kor. 5,8 – lakini tunao moyo mkuu, nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Katika kwenda huko, yaani kifo, roho hutengana na mwili – Fil. 1:23. Nayo itaungana na mwili wake siku ya ufufuko wa wafu. . – Rum. 8,11 – lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Ili tufufuke ni lazima kufa pamoja na Kristo. Hapa ndipo mwanadamu anapata mahangaiko. Tunapata shida sana kupokea hili. Tunatamani uzima wa milele lakini kifo kinatusumbua mno.
Na zaidi sana katika wasiwasi huo mwanadamu huendelea kujiuliza -– nani atafufuka? KKK – 998 - Watu wote waliokufa. Wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu - Yoh. 5:29; Dan. 12:2 –tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na tena – namna gani? KKK 999 – kwa namna ya Kristo. Kristo amefufuka pamoja na mwili wake hasa – tazameni mikono yangu na miguu yangu ya kuwa ni Mimi mwenyewe. – Lk. 24:39, lakini hakuurudia uzima wa kidunia. Wakati huo huo walio wake Kristo watafufuka pamoja na miili yao wenyewe waliyo nayo sasa, lakini mwili huo utageuzwa katika mwili mtukufu, katika mwili wa kiroho – Fil. 3:21; 1Kor. 15:44. Ni Msalaba wa Kristo pekee unaoweza kutupa majibu na sababu za hayo mateso tunayoyashuhudia kutokana na kifo. Lakini pia msalaba hutoa majibu kwa fumbo ambapo kwa sasa ni vigumu kulielewa kwani lipo juu ya uelewa wetu.
Kwa hiyo tuna uhakika kuwa kifo cha Kristo ndilo jibu ambalo Mungu analitoa katika nyakati zote mbili za furaha na uchungu. Ufufuko wa mwili huonyesha kwamba baada ya kifo hakutakuwa na uzima wa roho peke yake bali kwamba hata miili yetu yenye hali ya kufa itapata tena uzima – Rom. 8,11 – lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Mwadilifu, maana yake asiye na dhambi, afungamanaye na Mungu, hafi kabisa – Hek, 11,26 – lakini wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu mpenda roho za watu, maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Mungu aliye hai ametuumba sisi ili tuwe hai. Hivyo kifo si mwisho wa maisha yetu.
Mwisho wa maisha yetu hapa duniani ni mwanzo wa maisha mapya na Mungu. Ndivyo inavyotufundisha imani yetu. Kifo hakina sauti ya mwisho. Ushindi wa msalaba ndiyo matumaini yetu. Kristo ameshinda dhambi na mauti. Ndiyo matumaini yetu. Nasi tunaalikwa kuwekeza katika matumaini hayo. Matumaini yetu ni uhai, tena ule wa kimungu. Tuongozwe na matumaini haya. Tutafakari tena na Mt. Ireneo – UTUKUFU WA MUNGU NI MWANADAMU ALIYE HAI.