Tafakari Jumapili 28 Mwaka C: Shukrani ni tendo la imani!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayaangalia na kuyatafakari masomo ya dominika ya 28 ya mwaka C wa Kanisa. Dhamira kuu tunayoiona katika masomo haya ni shukrani. Masomo yanatualika kuwa watu wa shukrani kwa Mungu na kwa watu kwa wema ambao tunaupokea daima katika maisha yetu. Kimsingi shukrani ni tendo la imani kama inavyojidhihirisha katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Somo la kwanza (2 Fam 5:14-17 ) ni kutoka katika kitabu cha pili cha wafalme. Somo hili linaelezea tukio lilifuatia uponyaji wa Naamani chini ya nabii Elisha. Naamani alikuwa jemedari wa jeshi la mfalme wa Shamu hivyo hakuwa mwisraeli. Naamani alipatwa na ugonjwa wa ukoma. Kisha kusikia juu ya Mungu wa Israeli alifunga safari hadi kwa Nabii Elisha. Elisha akamwagiza akaoge mara saba katika mto Yordani naye akapona. Baada ya uponyaji Naamani alirudi kumshukuru Mungu. Alikiri imani kwa Mungu wa Israeli alitaka kuonesha shukrani yake kwa kumpa mtumishi wake matoleo yake ya shukrani lakini Elisha hakupokea. Naamani kama shukrani kwa Mungu akachukua udongo kutoka Israeli aende nao katika nchi yake ili kupitia udongo huo wa Israeli aendelee kumwabudu na kumtolea sadaka Mungu wa Israeli. Somo hili linakazia moyo wa shukrani ambao Naamani anauonesha. Naamani baada ya kuponywa anakiri kuwa ameponywa na Mungu wa Israeli na anawiwa kushukuru. Shukrani anayoitoa inakuwa ni ile shukrani inayodumu na tena inayomwongezea imani; shukrani ya kuchagua kumwabudu Mungu wa Israeli katika maisha yake yote.
Somo la pili (2 Tim 2:8- 13) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo. Katika somo hili, Mtume Paulo akiwa kifungoni anamwelezea Timoteo juu yake mwenyewe. Anamwambia anayavumilia yote kwa ajili ya wateule, yaani kwa ajili ya taifa zima la Mungu. Paulo anatambua kwa anateseka kwa ajili ya injili lakini zaidi ya hapo anatambua na hili anamfahamisha pia Timoteo kuwa mateso yake hayo ni sehemu ya injili yenyewe. Na ni kwa sababu hiyo anayastahimili yote ili taifa la Mungu lipate wokovu. Katika sehemu ya pili ya somo hili Paulo anamwandikia Timotheo kile ambacho amekirudia mara nyingi katika barua zake kuhusu kuyashiriki mateso ya Kristo. Katika waraka kwa Warumi aliandika “kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake kadhalika tutaunganika naye kwa mfano wa kufufuka kwake…ikiwa tulikufa pamoja na Kristo tutaishi pia pamoja naye (Rej. Rom 6:5, 8). Anapomwandikia Timotheo anaanza kwanza kwa kumwalika ajibidiishe kuzishika tunu hizo ili Mungu ampe taji anayostahili. Mwishoni anamkumbusha kuwa Mungu ni wakuaminiwa daima na hawezi kujikana. Hiki anamwandikia ili kiwe kichocheo cha kumuimarisha na kumtia moyo.
Injili (Lk 17:11-19) Katika injili ya dominika ya leo ambayo ni kutoka kwa mwinjili Luka, Yesus anakutana na watu kumi wenye ukoma. Wanamwomba rehema naye anawatuma waende wakajioneshe kwa makuhani. Wakiwa njiani wanatakasika. Mmoja wao ambaye Injili inamtaja kuwa alikuwa ni wa taifa la Samaria anarudi kushukuru. Uponyaji wa wakoma hawa unafanana na ule wa Naamani ambao ni somo la kwanza katika dominika ya leo. Ni uponyaji unaoonesha nguvu ya imani na hapo hapo kuonesha kuwa shukrani ni tendo la imani. Katika jamii ya kiyahudi ya wakati huo wagonjwa wa ukoma walikuwa wanatengwa na hawakuruhusiwa kuchanganyika na watu wengine. Endapo mgonjwa wa ukoma alipona, ilibidi aende kujionesha kwa kuhani na kuhani akishathibitisha kuwa amepona ndipo huyo angeweza kurudi kuishi kawaida na watu wengine. Tunachokiona katika Injili ya leo ni kuwa Yesu anawaambia wagonjwa hao waende kujionesha kwa makuhani hata kabla hawajaponywa.
Wangeweza kujiuliza, waende kwa Makuhani kujionesha ili iweje wakati taratibu walizijua vizuri? Yesu aliwaambia waende kwa makuhani kwa sababu machoni pake aliona tayari wameshaponywa kwa imani waliyokuwa nayo kwake. Aliwahitaji waendelee kujikita katika imani hiyo hiyo na kuenenda katika matakwa ya imani hiyo ili uponyaji wao udhihirike. Na ndivyo ilivyokuwa. Katika hatua ya pili, baada ya kuponywa ni mmoja tu anarudi kushukuru. Na Yesu anasema ni huyo aliyerudi kumpa Mungu utukufu. Ni hapa Yesu anaisifu fadhila ya shukrani kwa Mungu na anamwambia msamaria “imani yako imekuokoa”.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo ya dominika hii ya leo yanaendeleza dhamira ya masomo ya dominika iliyopita, dhamira ya imani na nguvu ya imani katika kuyabadili maisha yetu. Tunaona kuwa ni imani inayotuunganisha na Mungu na ni imani inayotufungulia mlango wa kuuonja wema wake Mungu katika maisha yetu. Kwa imani, jemedari Naamani anaponywa ugonjwa wake wa ukoma chini ya nabii Elisha. Kwa imani wakoma kumi wanaponywa ugonjwa wao wa ukoma chini ya Yesu. Baada ya uponyaji ni nini kinafuata katika maisha? Baada ya Mungu kutugusa na wema wake ni nini kinapaswa kuendelea? Au tena baada ya imani kutufungulia mlango wa kupokea baraka za Mungu ni nini tunapaswa kufanya. Bila shaka sio kusimama mlangoni bali ni kuingia ndani na kuendelea kuishi katika uwepo wa neema hizo.
Masomo ya leo yanadokeza dhamira ya shukrani. Kuwa baada ya kuguswa na wema wa Mungu tunapaswa kuwa watu wa shukrani. Shukrani yenyewe ni tendo la imani na shukrani hii hutuwezesha kuendelea kuishi katia neema hizo ambazo Mungu anatujalia. Kwa moyo huu wa shukrani aliamua kuchukua udongo kutoka ardhi ya Israeli ili anaporudi nchini kwake aendelee kumtolea Mungu wa Israeli sadaka ya shukrani. Na katika Injili Msamaria anaporudi kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa uponyaji ndipo anapotunukiwa zawadi kubwa zaidi ambayo ni zawadi ya wokovu. Yesu anamwambia “imani yako imekuokoa”. Katika maisha yetu sisi waamini ndani ya kanisa, muunganiko huu wa imani na shukrani hujionesha katika adhimisho la Misa Takatifu. Misa Takatifu ni adhimisho la Ekaristi na Ekaristi maana yake ni shukrani. Kumbe, ni katika adhimisho la Ekaristi tunaalikwa kuiishi shukrani yetu kwa Mungu kila siku kwa ajili ya mema yote anayotujalia kwa njia ya imani. Ndiyo maana tunasali daima ili Mungu atujalie tufanane na Fumbo la Ekaristi, fumbo tunaloliadhimisha na kulishiriki kila siku katika maisha yetu. Mwenyezi Mungu atujalie neema ya kuwa watu wa shukrani na hasa zaidi tumtolee shukrani ile inayodumu katika maisha yetu, shukrani ya kumwabudu na kutembea daima katika njia zake. Amina.