Tafakari Jumapili 33: Msiogope, Kristo Yesu ni Mshindi!
Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.
Hapa duniani kuna mapambano na vita vya kudumu. Mapambano hayo ni kati ya wema na ubaya. Ujio wa Yesu duniani umepambisha moto zaidi vita hizo. Katika Injili ya leo Yesu amefika Yerusalemu na kuingia Hekaluni. Alipoona wanafunzi wake pamoja na watalii wanalishangaa Hekalu lilivyojengwa kiufundi, akachukua mwanya huo kwanza kuwakata kauli kwamba: “Haya mnayoyatazama siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.” Baada ya hapo akatoa tamko rasmi la hali ya hatari inayosubiriwa: “Taifa litapigana na taifa jingine, ufalme na ufalme mwingine.” Akaeleza pia kwamba kutakuwa na njaa na tauni. Mbaya zaidi walio upande wake (wema) wataburuzwa magerezani na wengine watauawa. Vita hivyo havikwisha, bali bado vinaendelea hadi leo. Ukweli ni kwamba sasa hivi hali ni tete zaidi. Uovu unatamba na kuonekana kama unashinda.
Bahati yetu wakristo ni kwamba katika vita vinavyoendelea, sisi tumeshamfahamu Mshindi. Tena mmoja mwenye mang’amuzi aliyeishapambana na vita hizo. Lakini hata yeye mwanzoni alitetereka na kuonekana kushindwa. Alipigika vibaya sana na maadui zake. Wakamtesa vibaya sana. Kumbe wakaja kukosea walipompambanisha na adui wa mwisho mkali zaidi yaani kifo. Kumbe huyo ndiye aliyesubiriwa kwa hamu apigane naye. Shujaa huyo ni Bwana wetu Yesu Kristu. Akakishinda kifo kwa kishindo kwa kufufuka kwake. Katika mapambano tuliyo nayo Wakristu, tumeshajinyakulia ushindi kwa sababu tunaye tayari Mshindi, Bwana wetu Yesu Kristo. Maandiko Matakatifu yanatuhakikishia hilo kwamba hata tukipigwa mabomu na kudhulumiwa hadi kufa kwa ajili ya imani, tuwe na uhakika kwamba mshahara na ushindi ni vya uhakika. Haijalishi kama madhulumu ni ya muda mrefu au muda mfupi, cha msingi ni kujua kwamba ushindi tunao. Tuna kila sababu za kumwaminia shujaa wetu YESU KRISTO Mshindi.
Matumaini haya ya ushindi dhidi ya uovu unayaona katika somo la kwanza (Mal 3:19-21). “Angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru, na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.” (Malaki 4:1) Kisha tunasikia ahadi ya Mungu kwa wale walio upande wake: “Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika miali zake.” (Mal 4:2) Yesu Kristo ndiye hilo jua la haki na miale yake inayoponya. Angalia tu jinsi alivyoponya wagonjwa. Kadhalika katika Injili ya leo tunayo matumamini dhidi ya madhulumu (Lk 21:5-19). Yesu anaongea juu ya madhulumu yatakayowapata wafuasi wake yatakayotokea kabla ya kubomolewa hekalu la Yerusalemu (na Warumi mwaka wa 70). Makuhani wakuu na Hekalu lao la Yerusalemu (uovu) walilidhulumu Hekalu Takatifu hai la Mungu yaani Yesu Kristo (wema), mapato yake unabii wa Yesu unaushuhudia hadi leo unapoona magofu ya Yerusalemu aliyoyasema: “halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.”
Aidha Yesu alisema kwamba wafuasi wake watakamatwa na kudhulumiwa, watatupwa gerezani, na wengine watauawa. Lakini akawatuliza, “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.” (Lk 21:19). Ukweli huu tunaushuhudia kwa Wakristo wanaodhulumiwa kila siku duniani. Wanavumilia na kutoa miili yao kama Yesu alivyosali alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu: “Twaeni mle nyote huu ndiyo mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu.” Sisi tumshukuru Mungu kwa vile hatuna madhulumu makali ya kidini kama wanayopata wenzetu sehemu nyingine, lakini kuna sintofahamu na rabsha za hapa na pale hata ndani ya ukristo zenye dalili ya udhulumu. Kadhalika hata katika nchi huru na yenye amani kama nchi yetu, inabidi serikali isimamie pia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Siyo tu uhuru wa kuabudu bali hata wa kusimamia misingi ya imani na kutolazimishwa kutenda mambo kinyume cha dhamiri zetu.
Aidha Yesu alisema: “Mtachukiwa na watu wote kwa jina langu.” Anachotutia nguvu Mshindi mkuu ni kuvumilia: “kwani kwa uvumilivu wenu mtaokoa maisha yenu.” Mkifuata ulimwengu mpya, mnaweza kudhulumiwa, lakini maisha yenu ya kweli, haki na upendo hakuna atakayethubutu kuyagusa kwa sababu hayo ni maisha ya watoto wa Mungu ambao wanajenga maisha ya kweli, ya haki na ya upendo utakaobaki na kudumu milele. Sala kwa Mikael Malaika mkuu ni ushahidi tosha kwamba kuna vita vikali vinavyoendelea kati ya wema na ubaya. Kristo ni mshindi! “Mikaeli Mtakatifu Malaika Mkuu, utulinde katika vita, uwe kinga yetu katika maovu na maoteo ya shetani, Mungu amtiishe, tunaomba sana, nawe Mkuu wa Majeshi ya Mbinguni kwa nguvu ya Mungu uwaangushe motoni shetani na pepo wabaya wengine wote, wanaozunguka duniani, ili kuzipoteza roho za watu. Amina.”