Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Haki na Amani
Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.
Ufalme ni cheo cha juu sana hapa duniani. Cheo hicho kinaendana na ukuu, nguvu, utawala na mamlaka makubwa ya Mfalme. Yesu lakini hakuwa kabisa na sifa kama hizo za Mfalme. Utawala na ukuu wa hapa duniani ni ule wa kutumia nguvu, wa kudhalilisha, wa kurubuni. Kwa kufanya hivyo, wafalme na wenye mamlaka wanaingia katika hatari kubwa sana ya kujidhalilisha na kudhalilisha mamlaka yao kwa namna nyingi sana. Lakini sera za serikali anayoongoza Mungu ni tofauti kabisa na za serikali za hapa duniani. Hata ukiangalia hali yake kutoka mwanzo “alipozaliwa kizizini.” Baadaye Yesu aliweza kuzidharau kabisa sifa hizo. Mathalani pale alipopewa ofa ya kushika dola ya ulimwengu mzima mradi tu amwabudu shetani, Yesu alijibu kifupi tu: “Mungu peke yake ndiye anayepaswa kuabudiwa” (Lk 4:5-8). Kadhalika alipokuwa msalabani raia walimrubuniwa kwa maneno mazuri kwamba kwa vile“Aliokoa wengine, mwache ajiokoe mwenyewe kama yeye kweli ni mpakwa (Kristo) wa Mungu” (Lk 23:35).
Lakini hakushawishika kutumia nguvu na mamlaka aliyonayo kujiokoa mwenyewe. Msingi wa thamani zilizompa ukuu, nguvu na mamlaka Bwana wetu Yesu Kristo ni Utumishi na Unyenyekevu. Akatuagiza wafuasi wake kwamba tukitaka kuwa wakuu hatuna budi tuwe kama watoto wadogo. (Lk 18:17). Aidha yatubidi kila siku kubeba misalaba yetu na kumfuata (Lk 14:27). Katika serikali ya utawala wa Kristo hakuna nafasi ya ufisadi, rushwa wala udhulumu kwa wanyonge. Watawala hawana budi kuheshimu na kujali masharti ya utawala. Kutokana na wakuu wa mataifa makubwa kutokuheshimu na kutojali masharti ya utawala, badala yake kutawala nchi kwa mabavu na mkono wa chuma, kinyume na masharti ya uongozi wa Kristo, ndiyo hali iliyompelekea Papa Pius XI kuingiza Sherehe ya leo katika Kanisa mwaka 1925. Katika Kanisa Sherehe hii inawelenga zaidi viongozi wote wenye mamlaka katika dini na jamii kijumla. Yesu ni mfalme wa haki, mpole na mnyenyekevu, anayeheshimu madaraka yake.
Hivi wote wanaokichezea cheo yaani wenye uchu wa vye, madaraka na wenye kuchuchumia ukuu, hao wote hawana nafasi katika utawala (ufalme) wa Yesu. Utawala wa Yesu unatetea wanyonge, watoza ushuru, wenye dhambi na wazinzi, kiasi hata wakuu wa ulimwengu huu kumwita majina ya maudhi: “mlevi na mlafi, rafiki ya watoza ushuru na wenye dhambi” (Lk 7:34). Mfalme anamkaribisha Ikulu mtu wa hadhi naa rika yake. Lakini Yeye anawapokea wanyonge waliotupwa na jamii. Mfalme anapewa zawadi kutoka kwa raia, lakini Yeye ndiye aliyewapa afya wagonjwa. Mfalme anavaa taji la dhahabu, lakini Yesu aliveshwa taji la miiba. Wafalme anakaa kiti cha kifalme, lakini kiti cha kifalme cha Yesu ni msalaba na akiwa msalabani anaongoza serikali yake. (Lk 23:35-43). Mfalme anazungukwa na walinzi, lakini waliosimama chini ya Msalaba walimrubuni ashuke msalabani ili kuonesh nguvu za Mwana wa Mungu Mfalme (Lk 23:35).
Utangulizi au "Prefacio" ya Misa inatupatia Kauli mbiu inayoainisha sifa za Ufalme wa Yesu kuwa ni: “Ufalme wa Kweli na Uzima; Ufalme wa Utakatifu na wa Neema; Ufalme wa Haki, Mapendo na Amani.”Mfalme huyo tunamwona katika Injili ya leo amesimama juu ya kiti chake cha enzi yaani Msalaba na kutundikwa mshtaka unaoonesha hadhi yake: “MFALME WA WYAHUDI”. Kwa bahati nzuri, kile kipindi cha maumivu makali ya kudhalilishwa kilikuwa cha mpito. Kisha Yesu akakirudia tena kiti chake alipoketi kuume kwa Mungu Baba yake. Haikuwa kazi rahisi kwa Yesu kuingiza sera za utawala wa Mungu katika ulimwengu wenye sera tofauti na zake. Sherehe ya leo inatukumbusha kuwa, tukitaka kuuenzi na kuutukuza ufalme wa Mungu, yatubidi kuachana na mambo yale ambayo ulimwengu unathamini. Aidha tuwe tayari kudhalilishwa kama alivyodhalilishwa Kristu juu ya Msalaba. Siyo rahisi kwa kanisa leo kulienzi Taifa la Ufalme wa Yesu katika Taifa linalofuata sera za kipagani na za kiulimwengu. Lakini kwa wale wanaojifia wenyewe na wanaojifunua zaidi kwa Yesu thawabu yao ya kuendana na kasi ya serikali yake anawaambia: “Amini, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.” (Lk 23:43).
Sherehe ya leo inawaalika viongozi wajihoji jinsi wanavyotumia nafasi zao: Je, Wanatumia kwa kujenga jumuiya ya haki au kujitanua tu mabawa na viota vyao? Je wanatumia madaraka yao kuwaumiza wengine au kuwapunguza mateso na masumbuko yao? Yesu ameshatuonesha jinsi ya kwenda na kasi ya utawala wake. Tusali sana ili mataifa na watu binafsi wawe wanyenyekevu angalao wa kuangalia kidogo jinsi Yesu alivyotumia nguvu na madaraka yake katika kujenga Ufalme na Utawala wa Mungu na kuiga. Tuyarudie kwa dhati maneno aliyotufundisha Yesu katika sala ya Baba Yetu: “Ufalme wako ufike.”