Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Muhimu: Ushuhuda, Udumifu na hapa kazi tu! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Muhimu: Ushuhuda, Udumifu na hapa kazi tu! 

Tafakari Jumapili 33 ya Mwaka: Ushuhuda, Udumifu na hapa Kazi tu

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko wa kungojea utimilifu wa nyakati kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Jambo la pili ni waamini kudumu katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu licha ya madhulumu: Waamini waendelee kuchapa kazi kwani kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Vatican.

Amani na Salama! Tunapokaribia kuumaliza mwaka wa kiliturjia wa Kanisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari Neno la Mungu linalogusia juu ya mwisho wa nyakati au mwanzo wa dunia na mbingu mpya, kusema ujio wa utawala wa Mungu ambapo yule mwovu na maovu yote yatakuwa yamefikia mwisho. Hivyo ni mwaliko wa mwanzo mpya. Mwisho wa nyakati ni mwanzo mpya, mwanzo wa utawala wa ufalme wa Mungu kati kati yetu. Wazo la Siku ya Bwana kwa maana Siku ya mwisho wa nyakati lilianza kuzungumziwa na Nabii Amosi, likimaanisha ujio wa Mungu mwenyewe katika historia ya mwanadamu na kuanza mwanzo mpya na ndio ufalme wa haki na amani. Siku hiyo ya Bwana haiwezi kuonekana wala kutambulishwa katika kalenda zetu za kibinadamu ila itashuhidiwa pale ambapo jua la haki na matumaini litakapotuzukia ambapo maskini, wanaoteswa, wanaonyonywa na kunyanyaswa watakuwa huru kwani ni Mungu atabaki kuwa mtawala.

Na ndio wazo hili leo tunalisikia tena kwa Nabii Malaki aliyejulikana pia kama Mjumbe wa Bwana, naye anatualika juu ya siku ya Bwana.  Nabii Malaki anatupa picha ya kutisha ya moto unaoteketeza na kuangamiza kila aina ya uovu na waovu na pia jua la haki litawazukia wale wote wanaomcha Mungu. Ndio kusema mwanzo mpya ambapo sasa Mungu atatawala ulimwengu maana haki na amani itatawala. Ni mwanzo mpya kwani hakutakuwa tena na uovu wala yule mwovu. Katika Injili pia tunaona wazo la siku ya Bwana linabebwa na wazo la mwanzo mpya wa utawala wa Mungu aliye Mkombozi wa ulimwengu.  Na ndio wazo kuu la Injili ya leo kutuonesha kuwa mwisho ni mwanzo mpya na si kama wengi wetu tunakuwa na picha ile ya kiapokalipsia ambayo hata leo kuna baadhi ya madhehebu kama Mashahidi wa Yehova wanaihubiri. Yesu leo anatuonya wanafunzi na wafuasi wake kuwa makini na mafundisho ya namna hiyo.

Kristo Yesu anatuonya kutowafuata manabii wa uongo wanaohubiri juu ya ujio wa Ufalme wa Mungu na ujio wake wa mara ya pili. Mwinjili Luka naye katika mazingira ya jumuiya yake anawaandikia sehemu hii ya maneno ya Yesu wakati ambapo hekalu la Yerusalemu lilikuwa tayari limeharibiwa, hivyo ndio kusema ukamilifu wa maneno ya kinabii ya Yesu kuwa halitasalia jiwe juu ya jiwe. Ni katika muktadha huo ambapo jumuiya zile za wakristo wa Kanisa la mwanzo walishuhudia matendo mengi ya kutisha na kuogofya, vita na mapinduzi, njaa na maradhi mbali mbali na zaidi sana mateso yao wenyewe, hapo wanashawishika kuona kuwa mwisho umekaribia, yaani ujio wa pili wa Yesu Kristo. Na ndio Mwinjili Luka anaona kuna haja kuwaandikia na kuwakumbusha maneno ya Yesu mwenyewe ya kujihadhari si tu na mtazamo bali hata na wahubiri wa aina hiyo ambayo wanatambulishwa kama manabii wa uongo. Si kwamba Mwinjili Luka anakuwa tofauti au kupinga juu ya mwisho wa nyakati bali anatupa maana kusudiwa ya huo mwisho, sio mwisho kwa maana kama ile tunayoweza kuisoma na kuielewa kutoka katika Maandiko ya "Kiapokalipsia" bali ni mwanzo mpya, ni utawala mpya ambapo jua la haki na amani litawazukia ndio kusema wema utabaki kutawala milele yote.

Siku ya Mwisho si kwa maana ya kuangamiza matendo mema bali kuangamiza uovu wote na hapo tutabaki na utawala wa wana wa Mungu kwani mwovu na uovu wote utaangamizwa, utafikia mwisho wake. Na ndio maana Yesu anatualika kuwa ufalme wake upo tayari katikati yetu. Ufalme wa Mungu utayari kati yetu. Na ndio mana Yesu leo anatuhadharisha wanafunzi na rafiki zake juu ya maisha yetu hapa duniani. Jibu la Yesu kwetu tukiwa tungali hapa duniani ni jibu pia kwa jumuiya iliyokuwa inateseka ya Luka Mwinjili. Wafuasi wa kweli watateseka, watasalitiwa, watachukiwa, na kupata kila aina ya udhia. Jumuiya ile ya Luka Mwinjili ndio tunaona ilichukiwa na kutengwa na wale wafuasi wa dini ya Kiyahudi (Masinagogi), na hata watawala warumi (mbele ya wafalme na maliwali), na hata kati ya ndugu wa karibu wa familia moja (wazazi, ndugu na hata marafiki). Mazingira na changamoto zile zipo bado hata katika nyakati zetu leo, labda kila mmoja niwaalike kuingia ndani na kuona yale yote yanayokuwa makwazo kwetu kuweza kushuhudia Injili katika mazingira yetu, ni wazi kila mmoja na mazingira yake.

Mwinjili Luka leo anatualika kutafakari juu ya fadhili kuu tatu tunazopaswa kuwa nazo kama wafuasi wake Yesu Kristo. Ya kwanza ni utayari wa kuwa mashahidi bila kujali mazingira na changamoto zake. Ya pili ni ustahimilivu au udumifu katika ufuasi wetu bila kujali magumu tunayopitia katika maisha ya ufuasi na ya tatu kubaki tukifanya kazi kama ambavyo Mtume Paolo anawakumbusha waamini wa Kanisa la Thesalonike. Fadhila hizi za ushuhuda, udumifu na kazi zinaakisi fadhila kuu za Kimungu yaani, imani, matumaini na mapendo. Ni fadhila za imani, matumaini na mapendo daima zinapaswa kumulika na kuongoza maisha ya kila mwamini, ziwe nguzo za maisha yetu ya siku kwa siku kwani ni katika hizo tunaujenga ulimwengu mpya, ulimwengu unaoruhusu Mungu atawale leo na hata milele. Ulimwengu mpya unaanza ndani mwa na katika maisha ya kila mmoja wetu. Yesu leo anamalizia sehemu ya Injili kwa msemo uliokuwa unatumika sana katika nyakati zake kuwa hautapotea hata unywele mmoja wa vichwani mwenu. 

Ndio kusema mateso na mahangaiko wanayopitia daima wanafunzi au wafuasi wa Yesu hayapotei bure, kila mateso yana thamani kubwa kwa wokovu wetu na ulimwengu mzima. Hata kama katika macho ya ulimwengu huu wanafunzi wa Yesu wataonekana kupoteza na kudharauliwa ila kuteseka kwa ajili ya Yesu na Injili yake ni kito cha thamani kubwa mintarafu wongofu wetu. Nawatakia tafari njema na Dominika njema.

16 November 2019, 12:49