Tafakari Jumapili 32: Ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 32 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tukiwa ukingoni na mwishoni mwa mwaka wa kanisa kilitrujia masomo ya leo yanatuhimiza kutafakari nyakati za mwisho za maisha yetu yaani fumbo la maisha na kifo. Kifo ni ukweli katika maisha yetu na baada ya kifo kuna maisha. Mtu akikuuliza, Ebu nihakikishie kama kuna maisha baada ya kifo, nawe mwambie nihakikishie kwamba hakuna maisha baada ya kifo. Somo kwanza la kitabu cha kwanza cha Wamakabayo linatupa simulizi la habari ya ndugu saba pamoja na mama yao waliokubali kufa mashahidi ili kuishuhudia imani na dini yao wakisema wako tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wao. Simulizi hili latueleza kuwa baada ya kifo hapa duniani kuna maisha ya baadae yasiyo na mwisho. Ukweli huu anautamka ndugu wa kwanza akiwa kufani anasema kwa ujasiri, wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele.
Kumbe kwa walio waadilifu maisha yajayo yatakuwa ya heri na furaha, lakini kwa wadhambi yatakuwa maisha ya mateso. Ndugu wa tatu kufa alisema kwa ushujaa, kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena, na wa nne alisema, ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo. Katika somo la pili la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike, Paulo anamwomba Mungu Baba na Mwanae Yesu Kristo wawaimarishe Wethesalonike katika taabu zao na wazidi kuwa na upendo ili waweze kuvumilia wakingojea kuja kwake Kristo huku akiwaasa Wathesalonike wadumu katika sala akisema, hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee na kutukuzwa. Injili ya leo kama ilivyoandikwa na Luka ni sehemu ya mafunisho ya Yesu juu ya maisha yajayo kwa Wasadukayo ambao hawakuamini juu ya uwezekano wa kuwepo ufufuko wa mwili, kwa kutoa simulizi la mwanamke aliyeolewa na ndugu saba na wote wakafa bila kuacha uzao na wanauliza katika maisha yajayo atakuwa mke wa nani.
Jibu la Yesu ni kuwa maisha yajayo ni ya utukufu, hakuna kuoa wala kuolewa, vyote tulivyonavyo na tuvifanyavyo hapa duniani tutaviacha. Kila kiumbe hai kina sifa ya kufa. Sifa hii ni ya pekee kwani kila kiumbe hai huikimbia akiwemo binadamu. Mafundisho ya dini mbalimbali yanakiri kuwa roho ya mtu haifi. Dini asili za kiafrika zinafundisha kuwa Mababu zetu waliokufa zamani, roho zao zinaishi na sinamahusiano na maisha ya watu ndio maana kukiwa na shida mfano magonjwa ya ajabu, vifo vya ghafla wanasema mababu/mizimu/wamekasirika ili kujipatanisha nao wanatambika. Kwa Wagiriki na dini za kiyahudi imani hii ipo lakini si kwa wote maana watu kama masadukayo hawakusadiki juu ya maisha yajayo. Kwetu sisi wakristo tambiko letu ni sadaka ya misa takatifu, tambiko la milele. Kifo sio ukweli wa baadaye, ni ukweli wa kutwa kuchwa, kwa maana tunakikabili kila siku (1Kor.15:31). Asili na chanzo cha kifo ni adhabu waliyopewa wazazi wetu wa kwanza kwa kukosa utii kwa Mungu.
Lakini kwa kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu kristo, kifo si adhabu tena bali ni njia ya kwenda mbinguni na hakuna njia ya mkato zaidi ya kifo, ukweli ndio huo na habari ndiyo hiyo. Lakini tutambue kuwa maisha ni suala la uhai na kifo. Kifo ni mabadiliko kutoka hali fulani, kuingia hali nyingine. Mtu anayekufa, amekuwa anaishi, na anakufa ili aishi tena. Tena kila hatua ya maisha ni kifo na maisha, kuanzia mbegu za kiume na yai la kike vikifa mimba inatungwa, mimba inakufa kichanga kinazaliwa, uchanga unakufa, utoto unazaliwa; utoto unakufa, ujana unazaliwa; ujana unakufa, utu uzima unazaliwa, utu uzima unakufa, uzee unazaliwa na mwisho wa yote, maisha huingia kifo na kifo huingia maisha. Kumbe, ni katika kuishi tunakufa na katika kufa tunaishi; lakini mwisho wa yote, kifo kitaangamizwa na uzima utatawala, kama anavyosema nabii Isaya, “Bwana atakiangamiza kifo milele,” (Isa. 25:8) na Yohane katika ufunuo anasema, kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto,” (Ufu. 20:14).
Kifo ni lile tukio la Roho na Mwili kutengana; lakini maisha yanaendelea baada ya utengano huu. Mwili na roho vikitengana ndipo mwanadamu anakufa, lakini mtu anaendelea kuishi, akiwa amevaa mwili mpya wa kiroho wenye uzuri wa pekee kabisa. Katika mabadiliko haya, Mungu yupo nasi maana “kama tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana, na tukifa tunakufa kwa ajili ya Bwana,” (Rum.14:18). Ndiyo maana Mzaburi anasema, “Nijapopita katika bonde la giza kuu, sitaogopa hatari yeyote, maana wewe ee Mwenyezi Mungu u pamoja nami; gongo na fimbo yako vyanilinda. Kifo ni mapambazuko ya maisha mengine, maisha ya umilele. Kama giza linavyoupisha mwanga vivyohivyo kifo hupisha maisha, maana kifo ni nukta ya pekee kati ya maisha ya muda na yale ya umilele hivyo ni vizuri kufurahia kifo, kwani ni mlinzi yupi anayechukia mapambazuko ya siku nyingine? Hakika kama mlinzi angojeavyo kwa hamu kubwa mapambazuko ya siku nyingine (Zab. 13o:6) ndivyo tunavyopaswa kukisubiria kifo. Kama usiku ulivyo sehemu ya siku nzima, nacho kifo ni sehemu ya mpangilio wa maisha yetu kwa asili.
Mtakatifu Francisko wa Assisi, anasema, “Usifiwe, ee Bwana wangu, kwa ajili ya huyu dada yetu kifo cha mwili, ambapo hakuna mwanadamu yeyote, aweza kumkwepa. Ole wao watakao kufa katika dhambi ya mauti! Heri wale watakaokutwa katika mapenzi yako, kwani, kifo cha pili hakitawadhuru KKK 1014”. Ukiwa na dhamiri nyeupe huwezi kuogopa kufa; mwenye dhamiri safi, nyeupe; wakati wote anatamani na kungojea siku ya kufa kwake, kwa hamu kubwa; mtu wa namna hiyo, kwake “kufa ni faida” (Fil.1:21), ili aende kukaa na Mungu, ajiunge na watakatifu mbinguni. Mtakatifu Yahane Paulo II, katika uhai wake alisema, “ninapata amani tele ninapofikiria kuhusu wakati, ambapo Bwana ataniita kutoka maisha kwenda maisha, yaani anapata furaha na amani tele anapofikiria siku yake ya kufa, ambapo Mungu atamwita kutoka maisha haya ya duniani kuelekea Mbinguni kwenye maisha ya umilele. Mtu wa aina hii daima huimba moyoni mwake, nitakwenda mbinguni kwa Baba, kwani nasikia kuitwa naye, huko ndiko wanyonge hucheka, wenye kulia hufutwa machozi. Mt. Theresa wa Avila, anasema, “nataka kumwona Mungu, nakumwona Mungu, lazima nife.” Basi ndugu tumwombe Mungu atujalie ujasiri kama wa wale ndugu saba ili kukikubali na kukipokea kifo ili tukaishi naye milele yote mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.