Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Waamini wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na Siku ya Bwana, Siku ya Hukumu ya Mwisho. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Waamini wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na Siku ya Bwana, Siku ya Hukumu ya Mwisho. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 33: Hukumu ya Mwisho!

Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa ni Siku ya III ya Maskini Duniani inayoongozwa na kauli mbiu: Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele. Rej. Zab. 9:19. Liturujia ya Neno la Mungu inawaalika waamini kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na Siku ya Bwna, yaani Siku ya Hukumu, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu! Hapo sipati picha!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 33 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa domenika hii ni kuwa, fahari na mamlaka za kibinadamu zitapita, utawala wa Mungu utadumu hadi mwisho wa nyakati. Subirá yako itaiponya nafsi yako. Katika somo la kwanza Nabii Malaki anawaonya waisraeli baada ya kurudi kutoka utumwani Babeli, kwani walianza tena kuusahau wema wa Mungu na kutenda maovu. Nabii Malaki anawaambia ya kuwa ipo siku atakayofika Bwana na kutoa hukumu ya haki akisema, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru, na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake Hakika Mungu hataacha kamwe kuwanyeshea mvua ya neema na baraka wenye hofu Naye.

Wenye hofu ya Mungu kwa kuishi kwao kuliko kwa kweli na haki, watasitawi katika haki na kweli ya Mungu. Mungu humwelekea mwenye hofu naye kwa sababu ndani yake kuna unyofu wa moyo.  Huku ndiko kusitawi mbele za Mungu kuliko haki. Mzaburi anasema, “mwenye haki atasitawi kama mtende, atakua kama mwerezi wa Lebanoni,” Zab. 92:12. Mungu hawezi kukaa kimya kwa wonyofu wa moyo. Hakuna alichaye jina la Mungu, naye Mungu akaziba masikio kwa kilio chake. Yatupasa kudumu katika sala na maombi yetu tukiwa na matumaini kwamba tumekwisha pata kile tuombacho  Mtume Paulo katika waraka wake wa pili kwa Wathesalonike anatuasa kuwa wakati tunapongoja ujio wake Yesu, sisi wakristo haitupasi kufikiri ya kuwa ni kazi bure kufanya kazi. Ni lazima tufanye kazi ili tujipatie riziki zetu. Mtume Paulo anaonya; mtu asiyetaka kufanya kazi hastahili kula chakula akisema hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.

Si kwamba hatuma amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Na ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Paulo anatoa onyo kwa wale wasio na utaratibu katika maisha ambao hawana shughuli yao wenyewe, wanaojishughulisha na mambo ya wengine kwamba wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe. Injili ilivyoandikwa na Luka inatupa tumaini la maisha yajayo kwamba tunaposikia habari juu ya mwisho wa maisha yetu au mwisho wa dunia, sisi tulio wafusi wake Kristo haitupasi kuogopa bali tufurahi, turukeruke na kushangilia tukifanya sherehe kwani Kristo daima yupo pamoja nasi. Lengo letu ni kujitayarisha kwa ujio huo tukijiweka daima katika hali ya neema. “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyeyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7. Kilichopo mbele yetu leo na sasa ni kuihubiri habari njema hadi mwisho huo wa nyakati, Mdo 1:8. Na katika kweli hii, tusichoke wala kukata tamaa katika kutenda mema, 2The 3:13.

Uwepo wa matetemeko makubwa ya nchi, njaa na tauni, fitina na vita, mataifa na falme kupigana, usaliti kati ya wazazi na watoto, ndugu, jamaa na rafiki na mauaji ya kila aina sio ishara ya mwisho wa dunia kama Yesu anavyosema, msitishwe na mambo haya maana hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kuzuka kwa manabii wa uongo katika nyakati zetu ni utimilifu wa utabiri wa Yesu akisema “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule,” Mt 24:24. Tutambue kuwa uaskofu, ukasisi, mchungaji, mtumishi, hakuna anayejitwalia, bali hutwaliwa na Mungu peke yake, ikiwa ni hitaji la Kanisa mahalia kama Mwili wa Kristo inapoonekana inafaa na mhusika anastahili kadiri ya mamlaka iliyopewa Kanisa (Mwili wa Kristo) na Kristo mwenyewe (Kichwa cha Kanisa). “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1.

Hata Kristo hakujitwalia mwenyewe kuwa kuhani Mkuu maana maandiko yanasema, “Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa,” Ebr 5:5. Kutimia kwa utabiri huu wa Yesu usitukatishe tamaa, kwani katika hali hii ya kusalitiwa, Yesu anatuambia tuwe na furaha. “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Yatupasa kufurahi kwa sababu katika mateso na ugumu huu wa kusimama katika kweli na haki, hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyetu, Lk 21:18. Hakuna aliye wa bahati mbaya katika ulimwengu huu “kwa maana kama tunaishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8

Wahenga wanasema, “mficha uchi hazai, na mficha kidonda harufu humuumbua.” Kukiri udhaifu siyo kushindwa bali ni mwisho wa mwanzo mpya wa kule utakako kufika. Ukweli wa jambo huwezwa kufunikwa kwa wakati tu, bali kadiri ya muda uendavyo kweli hiyo hujifunua yenyewe. Kweli ni asili ya Mungu, nayo ni ya milele katika maana yake kama alivyo Mungu. Basi tujiandae kuanikwa na kuumbuliwa wakati utakapofika. Yesu anatuasa akisema, subirá yako itaiponya nafsi yako kwani mwenye subira hufikiri vyema tena kwa undani na upana wake. Mwenye subira huyatazama yote katika jana yake, leo yake, kesho yake, na umilele wake. Tumsifu Yesu Kristo. 

JP 33 ya Mwaka C
13 November 2019, 17:04