Tafakari Jumapili 32 Mwaka C: Ufufuko na uzima wa milele!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Ndugu zangu wapendwa, karibuni katika tafakari yetu ya leo. Somo la kwanza na injili yaongelea juu ya kifo na hali baada ya kifo. Sote twafahamu fika kuwa kwa mwanadamu, kifo ni tatizo kubwa, ni shida. Pamoja na imani ya kikristo na hata mila na desturi zetu mbalimbali zinazoelezea uwepo wa maisha baada ya kifo, bado kifo hakipokeleki kama kitu kizuri au sehemu ya maisha ya mwanadamu kwa nanma yo yote ile. Ingawa tunatambua kuwa kila chenye mwanzo huwa na mwisho, lakini kifo bado si rafiki kabisa wa mwanadamu. Ujasiri wa kukipokea kifo kama namna ya kupata maisha mapya waonekana tu katika watakatifu walioishi mapenzi yake Mungu. Kwa hakika kifo cha Yesu msalabani kimeleta uzima kwetu na kutoa maana mpya inayotia moyo juu ya kifo cha mkristo. Wakati wa dhuluma ya Kabaka dhidi ya kina Karoli Lwanga na wenzake tunapata kuona kutoka kwa mashahidi hawa moyo wa ujasiri uliojaa imani kwa uzima katika Kristo.
Wakati wakielekea kuteketezwa kwa moto Karoli Lwanga alisikika akiwaambia wenzake ‘rafiki zangu kwa heri ya kuonana mbinguni’. Na wao akiwemo kijana shujaa Kizito na wale mashahidi wengine wanajibu wakiimba ‘kwa heri ya kuonana mbinguni’. Imani ya uzima ujao katika Kristo ina maana zaidi ya kitu kingine cho chote. Hawa wafiadini mashahidi walidhihirisha ushindi dhidi ya kifo. Katika KKK 990 tunasoma kuwali neno “mwili” laeleza mtu katika hali yake ya udhaifu na ya kufa. Tunasoma pia habari kama hiyo katika Mwa. 6:3; Zab. 56:5; Isa. 40:6. Hivyo iko wazi kuwa sote tutakufa. Tunaendelea kusoma katika Maandiko Matakatifu kuwa mwanadamu ndiye asili ya mauti – kinyume cha muumba wake – Mwa. 3. Kwenda kinyume na Muumba ni kutenda dhambi. Na katika KKK 1008 tunasoma kuwa kifo ni tokeo la dhambi. Hivyo kifo cha kweli ni kifo cha mwenye dhambi. Kadiri ya mafundisho ya Mtakatifu Paulo – Rum. 7:14-24 – tunasoma kuwa dhambi hukaa ndani ya mtu. Kimtokacho mtu humtia unajisi.
Kwa njia ya Adamu dhambi iliingia ulimwenguni na malipo ya dhambi ni mauti-kifo. Hata hivyo mamlaka ya ufundishaji wa kanisa, mfafanuzi halisi wa matamshi ya Maandiko Matakatifu na mapokeo hufundisha kwamba kifo kimeingia ulimwenguni kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu – Hek. 1:13 – yaani, Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Ingawa lakini mwanadamu ana hali ya kufa, Mungu alimweka asife. Kifo kilikuwa ni kinyume cha mipango ya Mungu Muumbaji, nacho kiliingia ulimwenguni kama tokeo la dhambi – Hek. 2:23-24, Rum. 5:12. Kifo cha kimwili, ambacho mwanadamu angekuwa huru nacho, ndiye adui wa mwisho wa mwanadamu ambaye lazima kumshinda – 1Kor. 15:26 – adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Kina Karoli Lwanga na wenzake wanadhihirisha hilo kwa kutoa maisha yao wakimshuhudia Kristo. Imani ya kikristo inatufundisha kuwa kwa njia ya Kristo tunapata uzima mpya – Rum. 8:29, - maana wale aliowajia tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu.
Katika 2Kor. 5:17, tunasoma kuwa hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. Katika hali ya dhambi mwanadamu anaalikwa na Mungu kuanza upya. Katika Yoh. 3:5 tunasoma kuwa Yesu akajibu, amini, amini, nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu na katika Mk. 16:16 tunaambiwa kuwa aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa Sasa fundisho kama hili Masadukayo hawakupata kulielewa. Na pengine sehemu kubwa ya uelewa wa imani yetu na mtindo wetu wa maisha na uelewa wetu juu ya maisha yajayo haina tofauti sana na Masadukayo. Wao walibaki katika ufahamu wao. Wanataka kujua hali ya wale wanaume saba na yule mwanamke itakuwaje baada ya kifo. Masadukayo wanataka kujua mambo yatakuwaje baada ya kifo. Yesu lakini anajibu akieleza ni kwa nini kuna ufufuko. Yesu anasema kuna ufufuko kwa sababu Mungu ni Mungu wa wazima. Mungu ametuumba ili tuishi hata kama tumetoka katika maisha haya ya hapa duniani.
Tena tunasoma hivi; ufufuko wa mwili huonesha kwamba baada ya kifo hakutakuwa na uzima wa roho peke yake bali kwamba hata miili yetu yenye hali ya kufa itapata tena uzima – katika Rom. 8:11 tunasoma kuwa lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Ijulikane kuwa maisha yajayo si mwendelezo wa maisha ya hapa duniani bali hupata hali nyingine kabisa ya maisha. Jibu la Yesu lajitosheleza – lakini wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, wala hawawezi kufa tena, kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuko. Yesu anakataa kibonzo cha masadukayo wasemao au wanaomini katika uwepo wa mwendelezo wa maisha ya kindoa kama walivyokuwa wanaishi hapa duniani.
Ieleweke wazi kuwa katika muungano wa ndoa kuna kifungo cha upendo. Kwa hakika kifungo hiki hakiishii tu hapa duniani. Maisha mapya ya kimbingu ni ukamilifu wa yale maisha ya upendo ambayo wanandoa waliishi hapa duniani. Maandiko yasema ndoa ni sakramenti kubwa kwa sababu inaonesha umoja kati ya Kristo na kanisa lake. Katika Efe. 5: 31-32 – tunasoma – kwa hiyo mume atawaacha baba na mama na kuambatana na mke wake. Nao wawili watakuwa mwili mmoja. Mtume Paulo anasema kuwa fumbo hili ni kubwa, lakini anasema, nasema hayo juu ya Kristo na kanisa. Kwa mtazamo huu ndoa haimaliziki tu kwa kifo cha duniani bali hupata mtazamo mpya wa kiroho zaidi. Katika misa ya wafu tunasali hivi; Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, tunapata makao ya milele mbinguni.
Padre Munachi, mhubiri maarufu anatushirikisha tafakari hii. Mtalii mmoja toka Marekani alimtembelea Rabi Hofetz Chaim huko Poland. Huyu mtalii alishangaa sana kumkuta mtu huyu maarufu katika chumba cha kawaida kabisa kikiwa na vitabu, meza ndogo na ubao wa kukalia. Yule mtalii akamwuliza yule Rabi kwa mshangao mkubwa ziko wapi samani zako? Yule Rabi akamwuliza za kwako ziko wapi? Yule mtalii akiwa bado anashanga alimjibu mimi ni mtalii hapa Poland na samani zangu ziko nyumbani kwangu. Hapa ninapita tu. Ni mtalii. Ndivyo nilivyo na mimi pia hapa duniani. Alijibu yule Rabi. Hapa ni mtalii na napita njia tu. Sisi sote hapa tunapita njia tu. Tumsifu Yesu Kristo.