Tafakari Jumapili 33 Mwaka: Siku ya Bwana, Kesheni na Kusali!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Mtu mmoja aitwaye Tillotson anasema – ni mjinga sana anayehangaikia maisha yake hapa duniani bila kujali ya mbinguni. Ni busara ya muda, lakini ni upumbavu wa daima. Tunasoma habari juu ya siku ya Bwana katika Biblia. Katika Amos 5:18 – na maelezo yake tunaambiwa kuwa katika nyakati za mwanzo msemo huu ulirejea kwenye ushindi wa Israeli ambapo Mungu angekuja kuyashida mataifa ya maadui. Kwa Amosi ilimaanisha siku ambapo Mungu angekuja kuwawajibisha watu wake. Katika Mal. 3:19 tunasoma – kwa maana tazama, siku inakuja, inawaka kama tanuru. Watu wote wenye kiburi, na ye yote atendaye uovu, watakuwa kama makapi. Na siku ile inayokuja itawateketeza, ambapo haitawaachia shina wala tawi. Na katika Sef. 1:14 tunasoma – siku hiyo kuu ya Bwana i karibu, ni karibu na inakuja haraka sana. Sikilizeni! Kilio cha siku ya Bwana kitakuwa kichungu, shujaa atapiga yowe huko. Katika Agano Jipya inamaanisha siku ya hukumu ya mwisho. Katika Rum. 1:18 tunasoma – hasira ya Mungu yafunuliwa kutoka mbinguni juu ya watu wote wenye kumwasi Mungu na kukosa haki wakiipinga kweli kwa ukosefu wao. Siku ya Bwana ina maana ni siku Kristo atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu.
Ndugu zangu Neno la Mungu dominika hii ya leo latualika kutafakari sana ufahamu wa uwepo wa Mungu katika maisha yetu na uhusiano wetu na huyo Muumba. Pia tunaalikwa kutafakari juu ya hatima ya maisha yetu baada ya maisha yetu hapa duniani. Tunakumbushwa kuwa sisi sote tumeshakombolewa na hivi sisi ni mali yake Mungu. Swali ambalo tunatakiwa sote kujiuliza ni kuwa je tunaishi kama watu ambao tumeshakombolewa tayari? Je maisha yetu yanaakisi huo utukufu wa Mungu au tunaishi bado kama watu ambao wanasubiri ukombozi? Tunapohitimisha mwaka wetu wa kiroho tunapata nafasi leo ya kuangalia tulikotoka ili tuone kama tuko salama huko tuendako au tunakotarajia kwenda, yaani mbinguni. Na masomo yetu ya leo na zaidi sana injili yazungumzia Kristo atakayekuja kwa hukumu, yaani ile iitwayo siku ya Bwana. Hii ni nafasi ya kutafakari juu ya hukumu hii. Mt. Paulo katika 1Kor. 11:31 – anasema – kama tungejichunguza wenyewe vizuri, hatungeadhibiwa hivyo …. kujihoji ni kujihukumu na ndiyo namna ya kujiweka tayari kwa hukumu ya pekee.
Mtu mmoja akiwa kwenye kiti cha hukumu, aliambiwa na malaika, jina lako haliko katika orodha ya waingiao mbinguni. Hivyo nenda motoni. Yule mtu aling’aka kwa ukali, mbona sijafanya kitu? Malaika akamwambia na hii ndiyo hukumu yako. Kwamba hukufanya cho chote. Ndugu zangu, tukumbuke kuwa mkristo hana budi kuwa mtendaji. Kristo alikuja ili kuuleta ufalme wa Mungu na ufuasi wetu hauna budi kuutangaza huo ufalme kwa ushuhuda wa maisha. Wengi wetu hudhani kwamba kutokufanya kitu ndilo jibu. Tunasahau kuwa sisi tunawajibu wa kufanya kitu na zaidi sana kwa mkristo ni wajibu si hiari. Hiki ndicho alichokuja kufanya Bwana wetu Yesu Kristo Mwokozi. Sisi tulikuwa tumetindikiwa, tumetenda dhambi. Akawa kwetu sababu ya msamaha. Hata katika hukumu yetu ya mwisho, tutahukumiwa kwa matendo yetu. Angalia Mt. 25 – nilikuwa na njaa ukanipa chakula nk. Aliyehukumiwa ni yule ambaye anasema ni lini ulikuwa na njaa – tutahukumiwa kwa kutokuona na kutokufanya cho chote. Tukumbuke kuwa tukiyatimiza mapenzi yake Mungu, tunaadhimisha kila siku ya maisha yetu hii siku ya Bwana.
Mtakatifu Gaspari anasema kwa Mungu hatuna budi kufanya mambo mengi, vizuri na haraka. Mengi kwa sababu mambo ya Mungu ni mengi, vizuri kwa sababu ndivyo inavyompendeza Mungu na haraka wa sababu maisha yetu ni mafupi. Kifupi ni kuwa hatuna budi kufanya kitu. Katika mkutano wa bodi ya mashetani uliohusu upungufu wa wateja wanaofika motoni mazungumzo yalikuwa hivi; mawazo yakawekwa mezani namma ya kupata wateja. Ibilisi mmoja akasema nitumeni mimi na ujumbe wangu kwa watu ni kuwa hakuna mbingu. Shetani akasema hilo halitafanya kazi. Ibilisi mwingine akasema nitumeni mimi na ujumbe wangu ni kuwa hakuna jehanamu. Shetani akasema hata hiyo haitafanya kazi. Akajitokeza ibilisi mzee na mzoefu akasema nitumeni mimi na ujumbe wangu ni kuwa hakuna haraka. Akatumwa. Katika somo la kwanza tunaona jinsi nabii Malaki anavyoongea badala ya Mungu na analaani dharau na kutojali kulikoingia kwenye ibada iliyokuwa ikifanyika hekaluni na kushutumu dhambi nyingine ambazo zilivunja agano la Mungu na hivyo kuifanya ibada ya hekaluni kuwa ya bure. Nabii anasema jua la haki litawazukia.
Haki ya Mungu itatawala daima. Huyu aliona na kutenda kwa kusema waziwazi ule uovu uliokuwa ukiendelea. Sote tuna deni hili mbele ya Mungu na watu wake. Nimalizie mahubiri haya kwa tafakari ya maneno yaliyopo katika lango kuu la Kanisa kuu la Jimbo kuu la Milano, Italia. Katika lango kuu la Kanisa la kiaskofu la Milano nchini Italia kuna milango mitatu katika hilo lango kuu na katika milango hiyo kuna maneno mazuri sana kwa tafakari yetu leo. Katika mlango mmoja kuna maneno haya – yote yafurahisha ila ni kwa muda. Katika mlango mwingine yameandikwa maneno – yote husumbua ila kwa muda na katika mlango mwingine yameandikwa maneno – kwa yote yaliyo muhimu ambayo ni kwa umilele. Katika hali hii hatuna budi kuchuchumilia ya umilele. Tafakari ya Mt. Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa kuwa hakuna upendo bila matumaini, hakuna matumaini bila upendo na hakuna upendo wala matumaini bila imani ituongoze ili siku ya Bwana itukute tukikesha. Tumsifu Yesu Kristo.