Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Ni Mfalme wa: Ukweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki na Amani. Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Ni Mfalme wa: Ukweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki na Amani. 

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu 2019

Sherehe ya Kristo Mfalme iliwekwa rasmi kuadhimishwa na Kanisa lote na Baba Mtakatifu Pius XI, 1925: lengo likiwa na kusherehekea utukufu wa Yesu Kristo. Katika Waraka wa Kitume – Quas Primas wa tarehe 11/12/1925 – aliandika hivi; watu watafute amani ya Kristo katika ufalme wa Kristo. Hivyo tunasherehekea sikukuu ya Yesu Kristo Bwana wa mbingu na nchi, enzi na utawala vyote ni vyake.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Yesu Kristo ni Mfalme wa: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki na Amani. Sherehe hii iliwekwa rasmi kuadhimishwa na Kanisa lote na Baba Mtakatifu Pius XI, 1925 na lengo likiwa ni kusherehekea utukufu wa Yesu Kristo. Hivyo tunasherehekea Siku kuu ya Yesu Kristo Bwana wa mbingu na nchi, enzi na utawala vyote ni vyake. Twaona katika masomo yetu, Pilato anamwuliza Yesu – ni mfalme wewe? Pilato anamshangaa Yesu aliye mbele yake. Jibu la Yesu ni rahisi. Ufalme wangu si wa dunia hii. Katika Waraka wa Paulo kwa Warumi: Rum. 10: 14 …. Tunaambiwa kuwa imani hutokana na kusikia. Ni tumaini langu kuwa kwa kuweza tena kusikia Neno la Mungu leo basi imani yangu/yako itakomaa zaidi.  Leo tunaadhimisha Jumapili ya 34 ya mwaka na kanisa linaadhimisha sherehe ya Yesu Kristo Mfalme, Bwana wa mbingu na nchi. Jumapili hii ni ya mwisho katika kalenda ya kanisa. Kadiri ya utaratibu wa kalenda ya kanisa, mwaka wa kanisa huanza na jumapili ya kwanza ya majilio na kilele chake ni jumapili hii ya leo tunapoadhimisha sherehe ya Yesu Kristo Mfalme.

Leo hii tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka salama, mwaka wa kanisa na tunamwomba tena baraka zake tunapojiandaa kuanza mwaka mpya wa kalenda katika Liturujia yetu. Sherehe hii iliwekwa rasmi kuadhimishwa na Kanisa lote na Baba Mtakatifu Pius XI, 1925 na lengo likiwa na kusherehekea utukufu wa Yesu Kristo. Katika Waraka wa Kitume – Quas Primas wa tarehe 11/12/1925 – aliandika hivi; watu watafute amani ya Kristo katika ufalme wa Kristo. Hivyo tunasherehekea sikukuu ya Yesu Kristo Bwana wa mbingu na nchi, enzi na utawala vyote ni vyake. Tunaona katika masomo yetu, Pilato anamwuliza Yesu – ni mfalme wewe? Pilato anamshangaa Yesu aliye mbele yake. Jibu la Yesu ni rahisi. Ufalme wangu si wa dunia hii. Katika KKK – 783 – tunasoma hivi; Yesu Kristo ndiye Yule ambaye Baba amempaka kwa Roho Mtakatifu na ambaye amemfanya kuhani, Nabii na Mfalme.

Taifa la Mungu, lote kabisa, linashiriki kazi hizi tatu za Kristo na linachukua madaraka ya utume na ya huduma unaotokana nazo. Uelewa huu wahitaji mafundisho sahihi, muda, tafakari na mwanga wa roho mtakatifu ili kupata ufahamu kamili. Angalia swali wa Pilato hapo juu. Waisraeli katika Agano la kale wanataka ufalme ili wafanane na mataifa mengine. Bahati nzuri kuhani wa Bwana anawaonya juu ya athari za madai yao. Wao wanasisitiza na Mungu anawaacha wafanye wanavyotaka. Mwisho wao ulikuwa maangamizi yao wenyewe. Bahati nzuri manabii wa Mungu wanaingilia kati na kusaidia kutoa mwongozo mpya wa namna ya kuhusiana na Mungu. Katika Isa. 9: 5-6 – tunasikia habari juu ya ujio wa mfalme; kwetu atazaliwa mtoto mwenye ufalme mabegani mwake, mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, mfalme wa amani. Wakati wa Yesu, Wayahudi walidhani ndiyo utimilifu wa maono hayo ya Isaya.

Haja ya ufalme wa kimasiha ukaanza kuingia katika mawazo yao. Ndiyo maana katika macho ya Wayahudi, Yesu alipouawa hata matumaini yao yalifika mwisho. Aidha matumaini yao yalianza upya kwa wanaoamini baada ya kupaa Bwana (mitume) na kupokea Roho Mtakatifu aliyewafunulia pole pole kilichotokea. Hakika Israeli alitambua umuhimu wa ufalme wa kimasiha utumwani Babeli – Isa. 40-55 yazungumzia juu ya mtumishi anayeteseka. Hali hii yaonesha matumaini ya wale wanaomtumainia Mungu – watashinda pamoja naye. Fundisho lililo katika somo la Injili kwa kifupi ni kuwa kiti cha enzi cha Kristo ni utukufu wa msalaba. Yesu hana wasiwasi kwa kuwa ajua afanyalo. Kutoka katika utukufu huo wa msalaba, Kristo anatawala na atatawala milele juu ya mbingu na nchi. Hakika Pilato hakuelewa maana ya ufalme huo wa Kristo kama ilivyo bado leo kwa wapinga Kristo. Yaelezwa pia kuwa hata wale wanaoungama jina la Kristo lakini bila kutekeleza mapenzi yake wako katika mshangao kama ule wa Pilato – uko wapi ukuu wako?

Ye yote yule anayelitaja jina la Bwana, lakini hatimizi mapenzi yake huyo si mfuasi wa kweli. Yesu hana eneo la utawala, hana chama na wala hana jeshi. Ufalme wa Yesu kama tunavyofundishwa ni wa upendo kwa Mungu na kuwa tayari kutimiza mapenzi ya Baba yake. Utumishi mwingine wo wote ule kwa mtu au vitu ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Utumishi wetu ni kuwa waaminifu na watiifu katika upendo kwa Mungu. Daima Kristo anatupa mfano. Katika KKK 908, tunasoma hivi; kwa utii wake hadi mauti, Kristo aliwapa wafuasi wake paji la uhuru wa kifalme, ili kwa njia ya kujikatalia wenyewe, na kwa njia ya maisha matakatifu, waushinde utawala wa dhambi ndani yao. Yule anayeutiisha mwili wake na kujitawala mwenyewe, bila kuzamishwa na tamaa ni bwana wake mwenyewe; anaweza kuitwa mfalme kwa sababu anaweza kutawala nafsi yake; yu huru na anajitegemea, na hajiachii kufungwa katika utumwa wa dhambi.

Ndugu mpendwa, sherehe hii ya leo inagusa moja kwa moja katika ujumla wake, maisha yetu ya ufuasi kama watoto wa Mungu. Tumalizie tafakari hii kwa kujiangalia tena;

-         Tunafunga mwaka na tunaalikwa kuangalia tumefanya nini. Salio letu likoje. Kuna cho chote?

-         Je, tutavikwa vilemba vya ushindi?

-         Je, tunalo salio la kuanza mwaka mpya pamoja na Bwana?

-         Je, tumeshinda pamoja na Bwana?

-         Je, tuna kibali cha kuingia katika jumba la kifalme?

-         Je, kadi yetu ya ufalme iko vizuri?

Tunapoadhimisha sherehe hii leo, kweli sisi tunamtumikia, tunamtii, tuko chini ya mamlaka yake? Kwetu sisi kutawala na kutumikia ni kumtumikia Kristo. Mtakatifu Leo Mkuu anaandika hivi; ishara ya msalaba inawafanya wafalme wale wote waliozaliwa upya katika Kristo na mpako wa Roho Mtakatifu unawatakasa kama makuhani, licha ya utumishi wa pekee wa huduma yetu, wakristo wote wa kiroho na wanaotumia akili yao wanajitambua kama viungo vya ukoo huu wa kifalme na wanashiriki kazi ya kikuhani. Ni nini kweli kilicho cha kifalme kwa roho kama kuweza kutawala mwili wake katika utii kwa Mungu? Na nini pia kilicho cha kikuhani kama kujitosa kwa Bwana na kumtolea juu ya altare ya moyo wake sadaka zisizo na doa za ibada? Tumsifu Yesu Kristo.

23 November 2019, 13:48