Tafakari Jumapili ya 1 Majilio: Roho ya Kipindi cha Majilio! Matumaini
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunayatafakari leo Maandiko Matakatifu ya dominika ya kwanza ya Majilio, dominika inayotuingiza katika mwaka mpya wa Kanisa, mwaka A. Baada ya kuyafafanua Maandiko, tafakari yetu itajikita katika roho ya kipindi hiki cha majilio ambacho tunakianza. Somo la kwanza (Isa. 2:1-5 ) ni kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Somo hili linazungumzia ufalme wa kimasiya ambao Mungu anaahidi kuuanzisha, ufalme ambao ndani yake atawakusanya na kuwaungamisha watu wote katika amani. Isaya alitoa unabii huu kama maono aliyoyapokea kwa ajili ya Israeli ya wakati huo. Kama ilivyo kawaida katika unabii, haya ni maneno yaliyoonekana kuwazungumzia waisraeli katika kipindi chao na katika yale waliyokuwa wakiyaishi na kuyapitia. Ni baadae sana waliporudi kuutafakari ujumbe wa unabii wanaona kuwa ulikuwa ni unabii ulioungumzia kitu kikubwa zaidi: unabii uliowahusu si waisraeli pekee bali mataifa yote ukiizungumzia enzi iliyopita mazingira ya wakati huo, na kuona kuwa ulikuwa ni unabii wa kimasiha.
Mlima wa nyumba ya Bwana anaouzungumzia Isaya ulikuwa ni mlima Sayuni ambapo juu yake lilijengwa Hekalu. Na hekalu hili licha ya kuwa ni sehemu ya kuabudia, kwa waisraeli lilikuwa pia ni alama ya uwepo wa Mungu kati yao. Nabii anasema ni katika Hekalu hili ambapo siku za mwisho mataifa yote wataenda. Katika hekalu hilo Mungu atawafundisha njia zake na hapo hapo Hekaluni, itatoka sheria. Neno “njia za Bwana” kwa Wayahudi ilikuwa ni namna nyingine ya kuzungumzia maadili. Na “sheria” au “sheria ya Bwana” namna ya kuzungumzia Torati. Nabii anaendelea kusema kuwa mataifa yatakayouendea mlima Sayuni, mataifa yatakayoliendea hekalu na kujifunza njia ya Bwana na sheria, yatafua panga kuwa majembe na mikuki iwe miundu. Mataifa hayo yatageuza silaha zao za vita kuwa zana za mafunfaa kwa ustawi wa mwanadamu kwa kumpatia chakula na uhai. Yatapata amani na ustawi. Nabii anaonesha kuwa kiini cha amani na ustawi ni kujifunza maadili na kuishika torati. Huu ni unabii wa kimasiya. Katika siku zake yeye, Hekalu halitakuwapo. Ni yeye atakayekuwa alama ya uwepo hai wa Mungu kati ya watu. Ndiye atakayewafundisha njia za Bwana na sheria yake. Nayo mataifa yatakayoishika njia yake na kuzifuata sheria zake yatapata amani na ustawi.
Somo la pili (Rum. 13:11-14a) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili Paulo anaalika wakristo kujua “tuko wakati gani” kama msingi wa kuuishi ukristo kiadilifu. Anatumia lugha ya “usiku na mchana”. Anaonesha kuwa usiku ni wakati katika maisha ambapo mtu anatawaliwa usingizi wa dhamiri na matokeo yake ni matendo ya dhambi ambazo anazitaja. Mchana badala yake ni alama ya nuru ya Kristo inayoangaza dhamiri ya mtu na kuiamsha kutenda mema. Anaalika kuzivaa silaha za nuru kwa maana wakati tuliopo ni wakati wa mapambazuko. Kristo jua la haki na masiya yupo karibu. Injili (Mt. 24:37-44) Somo la Injili ni kutoka kwa mwinjili Mathayo nalo linazungumza juu ya kukesha na kujiweka tayari. Yesu anatoa fundisho hili akijibu swali walilomuuliza wanafunzi wake kuhusu mambo ya siku za mwisho: utakuwa lini na ni nini dalili za ujio wake (Mt. 24:3). Anatoa mifano miwili, mmoja ni wakati wa Gharika enzi ya Nuhu na wa pili ni mwenye nyumba aliyevamiwa na mwivi bila kujua.
Wakati wa Gharika Yesu anasema wale watu hawakujua ni lini gharika inakuja, na kwa sababu hawakujua iliwapasa kukesha na kujiweka tayari. Waliangamia kwa sababu badala ya kukesha na kujiweka tayari, wao waliendelea na maisha yao ya anasa kama kawaida. Kwa mwenye nyumba Yesu anasema kama angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha. Kumbe kujua saa na kutokujua saa vyote vinatoa mwaliko ule ule: kukesha na kujiweka tayari. Kwa maneno mengine Yesu anawaonesha wanafunzi wake kuwa lililo muhimu ni kukesha na kujiweka tayari kuliko mahangaiko ya kujua ni lini anarudi. Yesu anaendelea kuonesha katika injili hii kuwa kujiandaa kwa ujio wake ni muhimu kujikita katika undani wa maisha ya mtu binafsi kwa maana ndiko yeye anakoangalia. Anasema kwa nje watu wawili wataonekana kuwa sawa, lakini siku hiyo yeye anayeangalia undani wa maisha yao atabaini na kumtwaa yule aliyejiandaa akimuacha mwingine. Anasema “watu wawili watakuwako kondeni, mmoja atatwaliwa na mmoja ataachwa …. Kesheni basi kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu”.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Majilio ni kipindi kinachoufungua mwaka mpya wa kiliturujia wa Kanisa. Ni kipindi cha majuma manne ambacho kilele chake ni Sherehe ya Noeli. Kumbe ni kipindi cha maandalizi na matumaini ya ujio wa Kristo. Katika Mapokeo ya Kanisa, ujio wa Kristo umekuwa daima na sura mbili. Sura ya kwanza ni ujio wa kihistoria, yaani kutwaa kwake mwili na kuzaliwa na Bikira Maria. Huu pia huitwa ujio wa kwanza wa Kristo. Sura ya pili ni ile ya kieskatolojia ambapo katika mwisho wa nyakati Kristo atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu na kuuanzisha ufalme usio na mwisho. Majilio inafanya maandalizi ya ujio wa Kristo katika sura zote hizo mbili. Katika wiki mbili za mwanzo hadi tarehe 16 Desemba tafakari inaelekezwa kujiandaa kwa ujio wa pili wa Kristo na katika wiki mbili za mwisho kuanzia tarehe 17 hadi 24 desemba tafakari inaelekezwa kujiandaa kwa ujio wake wa kwanza tunaouadhimisha kwa sherehe ya Noeli.
Ni kipindi basi kinachotuonesha wazi kabisa kuwa sisi kama Kanisa tunaishi katikati ya ujio wa aina mbili wa Kristo, yaani katikati ya kuzaliwa kwake na kurudi kwake kwa mara ya pili. Kuzaliwa kwa Kristo kumetupa msingi wa enzi tuliyomo na ujio wake wa pili utakuwa ni ukamilifu wa enzi hiyo na sasa tunaishi katika matumaini hayo. Ni kwa sababu hii, rangi ya kiliturujia inayotumika ni rangi ya urujuani (zambarau). Hii sio rangi ya toba au maombolezo pekee, ni rangi hasa ya kuonesha matumaini. Ni katika mazingira haya tumeona masomo ya dominika hii yamejikita katika kuamsha matumaini yetu kwa siku za mwisho, siku za ujio wa pili wa Masiya na utimilifu wa ahadi za kimasiya. Mwaliko wake ni mmoja yaan: kujiandaa kumpokea masiya kwa kukesha na kujiweka tayari tukitumaini kutoka kwake amani na ustawi katika maisha yetu. Tuianze majilio kwa roho hii na Mungu atujaze wingi wa baraka na neema zake kwa ujio wa Kristo, masiya na mkombozi wetu.