Tafuta

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa wadhambi, wanaohitaji kutubu na kuongoka, ili kupyaisha maisha yao! Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa wadhambi, wanaohitaji kutubu na kuongoka, ili kupyaisha maisha yao! 

Tafakari Jumapili 31 Mwaka: Huruma ya Mungu kwa wakosefu!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa inatualika tutafakari juu ya kiu ya mwanadamu ya kumtafuta Muumba wake, toba, wongofu wa ndani, malipizi ya dhambi na furaha ya upya wa maisha yanayofumbatwa katika neema ya utakaso kama mwitikio wa upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Zakayo Mtoza ushuru ni mfano bora wa kuigwa katika hija ya toba.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunatafakari leo masomo ya dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa. Masomo ya dominika hii yanatualika tutafakari juu ya kiu ya mwanadamu kumtafuta Muumba wake, toba, wongofu wa ndani, malipizi ya dhambi na furaha ya upya wa maisha yanayofumbatwa katika neema ya utakaso kama mwitikio wa upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Somo la kwanza (Hek 11:22-12:2 ) ni kutoka katika kitabu cha Hekima ya Sulemani. Sulemani alikuwa mfalme wa tatu wa Israeli baada ya Sauli na Daudi. Ni yeye ambaye Mungu alimtokea katika ndoto na kumwambia aombe chochote anachotaka (1 Fal 3:1-15) . Yeye aliomba Hekima, tena hekima itokayo kwa Mungu. Ombi lake hili lilimpendeza Mungu kwa maana hakuomba maisha marefu wala utajiri wala maangamizi ya maadui wa ufalme wake. Naye Mungu akamjalia hekima. Wayahudi waliifuata hekima hii na ndiyo iliyowaongoza katika kujitambua wao ni akina nani na hasa iliwapa mwelekeo katika maisha yao.

Katika somo la leo, hekima inauweka ulimwengu wote chini ya maongozi ya Mungu. Inawaonesha wayahudi kuwa ulimwengu huu ni Mungu aliyeuumba na hata baada ya kuuumba hakuuacha ujiendeshe wenyewe bali anaendelea kuudumisha, anaendelea kuuongoza na kuuhifadhi. Anafanya hivi kwa sababu anaupenda ulimwengu na anampenda mwanadamu aliyemuumba. Upendo huu wa Mungu kwa mwanadamu na kwa ulimwengu mzima ni upendo wenye huruma. Ndio maana mwanadamu anapomkosea Mungu kwa dhambi, Mungu hauondoi upendo wake kwake, hamuadhibu sawa sawa na madhambi yake bali anamuachilia ili apate kutubu na kurudi katika mahusiano naye. Somo hili linatupatia mafundisho mawili makubwa. La kwanza ni juu ya kazi ya Mwenyezi Mungu katika ulimwengu. Kazi hii haikuwa tu kuuumba ulimwengu na kuuacha uende kwa jinsi yake wenyewe. Ulimwengu bado unamuhitaji Mungu ili uendelee kuwapo. Kwa maneno mengine ulimwengu unamuhitaji Mungu ili uendelee kuwa “ulimwengu”. Jambo la pili tunaloliona katika somo hili ni huruma ya Mungu kwa wakosefu. Mungu humtangulizia mkosefu huruma yake ili amvute afanye toba na asipotee.

Somo la pili (2 Thes 1:11- 2:2) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike. Ni katika kipindi ambacho kanisa la Thesalonike lilikuwa katika uvumi mkubwa juu ya siku ya mwisho. Walitokea watu waliopotosha mafundisho ya Paulo na kufundisha kuwa ujio wa pili wa Kristo na mwisho wa dunia vinakaribia, hivyo watu hawana haja ya kujihangaisha na chochote isipokuwa kuisubiri tu hiyo siku. Mafundisho haya yaliwafanya baadhi kukata tamaa ya maisha na hata kuacha kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kawaida katika maisha. Mtume Paulo katika somo la leo anawaandikia Wathesalonike kuwaonya na kuwatahadharisha juu ya uzushi na  mafundisho hayo potofu. Anawaambia “msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu wala msishtushwe kwa roho wala kwa neno”. Paulo anarudia kwa maneno mengine kile alichokwisha kisema Yesu kuwa hakuna aijuaye siku wala saa. Hivyo waendelee kutekeleza wajibu wao kama kawaida. Hili ni somo ambalo hata katika nyakati zetu linatualika tuwe makini na uzushi na mafundisho potofu yanayokuja bado chini ya mwamvuli wa injili. Utabiri juu ya mwisho wa dunia haujakoma na Watesalonike, upo hadi leo pamoja na mafundisho mengi yanayoendelea kuwatia watu hofu kwa malengo yanayopingana na Injili yenyewe. Injili maana yake ni Habari Njema. Ni habari njema ya wokovu na kamwe sio ya kuwafanya watu mateka wa hofu.

Injili (Lk 19:1-10) Injili ya leo ni kutoka kwa mwinjili Luka. Inaelezea simulizi la Zakayo: mkuu wa watoza ushuru, tajiri, mfupi wa kimo na mtu aliyekuwa na kiu ya kumwona Yesu. Kwa sababu ya ufupi wa kimo alipanda juu ya mti wa mkuyu ili Yesu anapopita yeye apate kumwona. Naye Yesu alipomwona akamwambia ashuke na akaenda naye hadi nyumbani kwake. Hili ni simulizi juu ya wongofu, juu ya namna mtu mwenye dhambi anavyoweza kuupokea mwaliko wa Kristo na kuanza kutembea katika maisha mapya ndani ya Kristo.  Anayechukua nafasi ya kwanza katika safari yoyote ya wongofu ni Kristo. Alipomwona Zakayo juu ya mti akamwambia “Zakayo, shuka upesi” na hapo hapo Yesu akamwonesha kuwa anahitaji kushinda nyumbani kwake, anahitaji kupewa nafasi katika maisha yote ya yule anayemuokoa. Na hivi anamwambia Zakayo “leo imenipasa kushinda nyumbani kwako”. Kitendo hiki kinawakasirisha watu waliomfahamu fika Zakayo na wanajiuliza kwa nini Yesu anaenda mpaka nyumbani kwa mwenye dhambi. Yote haya anayoyafanya Yesu anayafanya kwa kuwa “alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea”.

Zakayo kwa upande wake anaipokea neema ya wongofu. Na anaipokea kwa kupiga hatua kumwelekea Yesu aliyetayari kumpokea na anakuwa tayari kurekebisha makosa yake na kushika mwenendo mpya wa maisha. Kitendo cha kukimbia, licha ya kuwa kwa mtu mzima na tena tajiri ni kitendo cha kujidhalilisha, ni kitendo kinachoonesha utayari wa Zakayo kumpokea Yesu. Kupanda juu ya mkuyu ni kushika njia ngumu ya toba. Mkuyu ni mti ambao hauna magamba na hivyo kuukwea si kazi rahisi kwa sababu unateleza, unahitaji jitihada ya pekee, uvumilifu na nia thabiti. Na ndivyo vitu vinavyohitajika katika toba. Na hatimaye, kitendo chake cha kugawa kwa masikini nusu ya mali na kurudisha mara nne ya kile alichokuwa amechukua isivyo halali ni kurekebisa makosa ya maisha yake na kuanza njia mpya ya wongofu. Zakayo anakuwa tayari kufanya kile ambacho yule tajiri kijana alishindwa: kuuza alivyonavyo, kuwapa masikini na kumfuata Yesu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo ya leo yanatualika tutafakari juu ya wongofu kama mwitikio wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Somo la kwanza limetuonesha upendo mkubwa wa Mungu kwa mwanadamu na kwa ulimwengu mzima. Ni kwa upendo Mungu alimuumba mwanadamu na kuumba ulimwengu. Na hata baada ya kuumba Mungu anaendelea kuutegemeza ulimwengu kwa upendo wake. Ni Mungu ambaye anavipenda vitu vyote vilivyopo na wala hakichukii kitu chochote alichokiumba. Ni kwa sababu hii upendo wa Mungu kuiamsha huruma yake kwa ajili ya binadamu anayeanguka katika dhambi. Humuonesha huruma yake kama mlango wa kupitia kufanya wongofu, kurudi katika upendo wa Mungu na hivi kupata wokovu. Zakayo katika injili anakuwa ni mfano wa namna binadamu aliyezongwa na mazingira ya dhambi anaweza kuuitikia upendo wa Mungu na kuishika njia ya wongofu.

Wongofu huu ni mwaliko wa kudumu hadi siku ile atakaporudi Kristo. Tukiwa bado hapa duniani ukamilifu wetu unapatikana kwa njia ya kujitakasa mara kwa mara. Hakuna namna ambavyo mmoja anaweza kusema amekamilika na hahitaji wongofu. Tunahitaji uthabidi wa dhamiri, kuifungua mioyo yetu daima na kuuona ukweli wa maisha yetu na kuichukua njia ile inayotupeleka katika wongofu ili tuendelee kudumu katika upendo wake Mungu Muumbaji wetu. Amina.

Liturujia J31
01 November 2019, 15:16