Tafakari Jumapili 32: Baada ya kifo kuna maisha na uzima wa milele
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunatafakari leo masomo ya dominika ya 32 ya Mwaka C wa Kanisa, masomo yanayofundisha juu ya tumaini la ufufuko na maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Somo la kwanza (2Mak. 7:1-2, 9-11 ) ni kutoka katika kitabu cha Pili cha Wamakabayo. Linaeleza habari ya ndugu saba waliokubali kufa wakitetea imani na tamaduni zao njema walizorithi toka kwa wazee wao. Mazingira ya somo hili ni kipindi cha kihistoria ambapo Waisraeli walikuwa wanatawaliwa na dola ya Kiyunani chini ya mtawala Antioko Epifani. Mtawala huyu alikusudia kuifuta kabisa imani ya waisraeli na badala yake kuwaletea ibada za miungu ya kiyunani. Zaidi ya hapo alikusudia kufuta kabisa hata tamaduni za kiyahudi na mapokeo yao ili awaletee tamaduni na mapokeo ya kiyunani. Alichofanya sasa mtawala huyu Antioko Epifani ni kuwa; kile ambacho kwa mapokeo wayahudi hawakupaswa kufanya, hicho aliwalazimisha wafanye na kile ambacho kwa mapokeo walipaswa kufanya, hicho aliwakataza kufanya. Aliyekiuka alipaswa kuuwawa kwa kuteswa vikali.
Katika somo hili ndugu hawa saba wanateswa vikali na kulazimishwa kula nyama ya nguruwe. Suala hapa halikuwa nyama ya nguruwe kama nguruwe bali lilibeba maana pana zaidi ya kulazimishwa kufanya vitu ambacho kwa mapokeo yao kama taifa teule la Mungu, linaloishi chini ya Agano na Torati ya Musa, hawakupaswa kufanya. Wote saba wanakataa na wanakuwa tayari kukikabili kifo. Pamoja na uaminifu kwa imani na mapokeo yao, ndugu hawa pia wanaeleza msukumo wa uaminifu wao huo kuwa ni imani ya kuwa kuna na maisha baada ya kifo. Tunasikia yule kijana mkubwa anamwambia mtesi wake “unatuua katika maisha ya sasa lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake hata tupate uzima wa milele”. Somo hili ni kichocheo kwetu kuwa thabiti katika imani: kushika imani na mapokeo yake yote kiaminifu dhidi ya vitisho vya nguvu au ushawishi laini wa kufuata mkumbo bila kujali madhara yake kwa imani na mapokeo yetu. Zaidi ya hapo, somo hili ni mojawapo ya vifungu katika Agano la Kale vinavyozungumzia tumaini la ufufuko na maisha baada ya maisha ya hapa duniani.
Somo la pili (2 Thes 2:16- 3:5) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike, jumuiya ya Kikristo iliyokumbwa na mkanyanyiko na upotoshaji kuwa siku ya kurudi Bwana imekaribia. Paulo katika somo hili anahitimisha mafundisho na ufafanuzi wake kuhusu mkangayiko huo. Na ahahitimisha kwa kuwaasa watesalonike wasifadhaishwe na uvumi huo na wala wasivunjike moyo. Anawakabidhi kwa Kristo, faraja ya milele na tumaini jema ili awafariji na kuwaimarisha katika kuendelea na maisha yao. Anawaomba pia waombeane. Waombeane ili Mungu awalinde na yule mwovu kwa sababu hakuna mwingine anayeweza kuleta mkanganyiko na mvurugano katika jumuiya isipokuwa yule mwovu. Anawaomba wadumu kuombeana ili Mungu awakinge na mwovu na awaongoze mioyo ili walipate pendo lake na saburi ya Kristo.
Injili (Lk 20:27-38) Somo la Injili ni kutoka kwa mwinjili Luka. Ni somo linalotoa fundisho juu ya ufufuo wa wafu na maisha baada ya kifo. Injili inaleta fundisho hili kupitia majibizano kati ya Yesu na Masadukayo. Katika uyahudi kulikuwa na vikundi mbalimbali vyenye mitazamo tofauti katika masuala ya kidini. Wasadukayo walikuwa ni mojawapo ya vikundi hivyo. Hawa walipokea vitabu tu vitano vya Musa kama Biblia. Vitabu vingine kama vile Wafalme na Manabii hawakuvipa uzito. Hivyo mambo ambayo hayakufundishwa katika vitabu vitano vya Musa hawakuyapokea. Hivyo walikataa uwepo wa malaika na hawakuamini juu ya ufufuko na maisha baada ya kifo. Kitovu cha dini kwao kilikuwa ni ibada za hekalu na ni humo tu waliamini Mungu yumo na wala si mahala pengine. Hawa bila shaka walikwishamsikia Yesu akifundisha juu ya ufufuko na maisha baada ya kifo. Kuhusu maisha baada ya kifo, nadharia iliyokuwapo kabla ya Kristo ni kuwa mtu akifa aliendelea kuishi katika uzao wake.
Hata hivyo nadharia hii haikuwa juu ya ufufuko bali kama kumbukumbu tu ya maisha ya mtu. Wanamfuata Yesu na kumuuliza huo ufufuko anaoufundisha utakuwaje na mtu ataendeleaje kuishi iwapo hatakuwa hata ameacha uzao duniani? Yesu anawafundisha akiwaonesha kuwa maisha baada ya kifo sio mwendelezo wa vipengele vya maisha ya hapa duniani na wala hayapimwi kwa vigezo vya maisha ya hapa duniani. Anasema “wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa lakini wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule na kule kufufuliwa katika wafu, hawaoi wala hawaolewi”. Hayo ni maisha ya utukufu na ndiyo maana anasema watakuwa sawasawa na malaika. Hali kadhalika Yesu anawaonesha kuwa Mungu mwenyewe alikwisha jifunua kuwa ni Mungu wa walio hai pale anapojitambulisha kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, wa Isaka na wa Yakobo kwa maana wote wamwaminio kwake huishi, wako hai daima.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo ya leo yanatualika tutafakari imani ya Kanisa juu ya ufufuko na uzima wa milele. Tunaposali kanuni ya Imani huwa tunaihitimisha kwa kukiri “nangojea na ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo. Amina.” Kwa kifo mwili na roho ya mtu hutengana. Mwili huoza lakini roho yake huenda kukutana na Mungu ikingojea kuunganika na mwili uliotukuka. Ufufuko ni pale ambapo Mungu kwa uwezo wake mkuu atairudishia kwa hakika miili yetu uzima usioharibika kwa kuiunganisha na roho zetu kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu (Rej. KKK. 997). Namna ya ufufuko itakuwa ni namna ile ile ya ufufuko wa Kristo. Alifufuka na mwili wake lakini hakuurudia uzima wa kidunia. Kumbe wote watafufuka pamoja na miili yao waliyo nayo sasa lakini mwili huo utageuzwa katika mwili wa utukufu, mwili wa kiroho (Rej. KKK. 999).
Imani hii juu ya ufufuko na uzima wa milele ambayo masomo ya leo kwa namna tofauti tofauti yameonesha chimbuko lake, imeungana kabisa na imani kwa Mungu mwenyewe hivi kwamba anayeamini juu ya uwepo wa Mungu anayo kila sababu ya kuamini pia juu ya ufufuko na uzima wa milele kwa sababu Mungu mwenyewe sio Mungu wa wafu bali ni Mungu wa walio hai. Tafakari hii, ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, inatuonesha kuwa maisha yetu binadamu yana lengo, na lengo hilo ni kurudi kuungana na Mungu. Tofauti kabisa na viumbe wengine, maisha ya binadamu hayapotei baada ya maisha ya ulimwenguni, “mwishowe ni uwinguni” kama inavyotukumbusha antifona ya ule wimbo wa matumaini ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko sasa wa kuishi maisha yetu ya hapa duniani katika namna itakayotuwezesha kustahili kulifikia lengo letu hilo.