Tafakari Jumapili 33 Mwaka: Unabii: Hukumu na Matumaini!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunatafakari leo masomo ya dominika ya 33 ya Mwaka C wa Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu. Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya III ya Maskini Duniani ni tarehe 17 Novemba 2019 yaani Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya siku ya III ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2019 unaongozwa na kauli mbiu: "Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele" (Rej. Zab. 9:19). Mzaburi anaonesha imani na matumaini yake kwa Mwenyezi Mungu licha ya ukosefu wa haki, mateso pamoja na kukosa uhakika wa maisha. Tukiwa mwishoni mwa mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa, masomo haya yanatualika kujiandaa kuijongea siku ya Bwana, siku ya kutimilika kwa kazi nzima ya uuambaji na ukombozi wa mwanadamu. Somo la kwanza (Mal. 4:1-2 ) ni kutoka katika kitabu cha nabii Malaki. Jina lenyewe Malaki maana yake ni “mjumbe wa Mungu” (mjumbe wangu), naye anakuwa ni mjumbe kweli anayejikita kutangaza ujio wa Siku ya Bwana. Nabii Malaki ni nabii ambaye kwa namna iliyo wazi zaidi amewaalika waisraeli kuwa makini na mienendo yao kwa sababu Siku ya Bwana ipo na inakuja.
Katika somo la leo, nabii anawatahadharisha waisraeli kuwa siku hiyo ya Bwana itakuwa ni siku ya hukumu. Anasema “wote watendao maovu watakuwa makapi, siku hiyo itawateketeza na wala haitawaachia shina wala tawi”. Itakuwa ni hukumu kwa wenye kiburi na wote watendao maovu. Kwa wale wanaomcha Bwana, siku hiyo haitakuwa kwao siku ya hukumu bali itakuwa siku ya mwangaza wa haki, itakuwa siku ya kupokea tuzo. Anasema “kwenu ninyi maolicha jina langu, jua la haki litawazukia, jua lenye kuponya katika mbawa zake.” Katika somo hili tunaona mojawapo ya sifa kuu ya unabii: kutangaza hukumu na kutoa matumaini kwa watu. Hakuna unabii wa kimungu unaotangaza mabaya tu: hukumu, laana, adhabu, maangamizi na uovu tu wa watu. Hali kadhalika hakuna unabii wa kimungu unaotangaza neema tu: uponyaji, utajiri, fanaka na kadhalika. Yote mawili yanaenda pamoja. Hii ni kuwafanya watu waupokee ujumbe wa Mungu na kuishi mbele yake kwa tahadhari daima; wala si kwa kukata tamaa ya kufungiwa mlango wa matumaini na wala si kwa kubweteka kwa matumaini ya uongo.
Somo la pili (2 Thes 3:7- 12) ni kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike. Ni somo linalotupatia mojawapo ya kauli maarufu ya Mtume Paulo, “ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi asile chakula”. Mazingira ya kauli hii ni katika jamii ambapo waliibuka watu wakaanza kufundisha kuwa Siku ya Bwana ipo karibu kufika. Waliendelea kuwaaminisha watu kuwa hakuna haja ya kujisumbua na mipango wala mambo ya muda mrefu kwa kuwa siku ya mwisho imefika. Hawa hawakufanya tena kazi na walianza kuishi maisha kama walivyotaka wao. Mtume Paulo kisha kuwapa msingi wa mafundisho kuhusu Siku ya Bwana, katika somo la leo anaukemea mwenendo huu. Anakemea kuishi maisha bila kufuata utaratibu (utaratibu wa kijamii na hata wa kimaadili) na bila kufanya kazi. Anawakumbusha kuwa yeye mwenyewe alipokuwa kwao hakuishi bila utaratibu. Tena alifanya kazi na kula chakula kwa jasho lake mwenyewe. Ndipo akawaambia kuwa hao wasiopenda kufuata utaratibu wa kawaida wa maisha na wasiopenda kufanya kazi kwa kisingizio cha kuwa Siku ya Bwana ipo karibu basi hawapaswi hata kula chakula. Somo hili linaendeleza fundisho msingi la Paulo kwa watesalonike: kutokukubali kuyumbishwa katika imani na katika mwenendo mwema wa maisha. Imani yoyote iliyo njema hujimwilisha katika maisha mema ya yule anayeamini. Imani haiwezi kamwe kuwa kisingizio cha kumwondoa mtu katika ukawaida wa maisha na hasa katika uhalisia wa maisha.
Injili (Lk. 21:5-19) Somo la Injili ni kutoka kwa mwinjili Luka. Ni somo linalotoa hotuba ndefu ya Yesu kuhusu mambo ya siku za mwisho. Wayahudi walikuwa na matumaini tofauti tofauti kuhusu siku ya mwisho. Kutoka katika mafundisho ya manabii waliamini kuwa siku hiyo ipo na tena ujio wake utatanguliwa na ishara na alama zisizo za kawaida. Hapo walimtegemea daima yule ambaye anaouwezo wa kusoma alama hizo aje na awaambie ni lini kwa uhakika, itakuja hiyo siku ya mwisho. Ni kwa mawazo haya haya walipomsikia Yesu anazungumza juu ya mwisho wa hekalu, kwamba siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe, basi wakajua ni yeye anayepaswa kuwapa majibu ya maswali yao. Na wakamuuliza “mwalimu mambo haya yatakuwa lini? nayo ni nini ishara ya kuwa siku hiyo ipo karibu?” Kwa Yesu, kujua siku na alama ya matukio siyo namna ya kuingojea siku ya Bwana. Ndiyo maana mara moja anawaambia “angalieni msije mkadanganyika”. Namna ya kuingojea siku ya Bwana ni kwa saburi na matumaini. Matukio ya kuogopesha, ujio wa manabii wa uongo, ishara za kutisha, mateso na vifo vya mashahidi wa Kristo na mambo mengine kama hayo vinapaswa kupokelewa kama mwaliko wa kudumu wa kuwa na saburi na matumaini katika kuuishi ukristo na ufuasi wa imani. Anasema Yesu mwenyewe kuwa mambo hayo hayana budi kutokea kwanza lakini ule mwisho hauji upesi. Hayana budi kutokea kwa sababu ni sehemu ya njia ya ufuasi na ushuhuda wa imani. Siku ya mwisho ni siku ya wokovu na siku ya kuiponya nafsi iliyoishi kwa saburi na uvumilivu. “nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu”.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tupo mwishoni kabisa mwa mwaka wa kiliturujia wa kanisa na Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanazungumzia habari za mambo ya mwisho – ujio wa siku ya Bwana na tafakari nzima ya mambo ya mwisho. Lugha hii ya mambo ya siku za mwisho ni lugha inayoendana kabisa na fikra za kawaida za binadamu kuyapima mambo katika mizani ya “mwanzo na mwisho”. Na fikra hii inajieleza vizuri katika msemo wetu uliozoeleka: “kila chenye mwanzo, kina mwisho”. Na hii wakati mwingine huleta huzuni na masikitiko hasa pale tunapoona kuwa jambo au hali fulani njema ambayo mtu anaifurahia itafikia mwisho wake na haitakuwapo tena. Hisia zinakuwa ngumu zaidi hasa tunapofikiria juu ya maisha yenyewe. Lakini mtazamo au fikra ya kiimani ambayo hasa ni fikra ya kimungu haiko hivyo. Fikra ya kimungu haipo katika mizani ya “mwanzo na mwisho”. Badala ya “mwisho” wa mambo, yanyewe imejikita katika “ukamilifu” au utimilifu wake. Katika fikra hii ya kimungu mambo hayaelekei kufikia mwisho bali kufikia ukamilifu. Ujio wenyewe wa Kristo ni ujio uliokuja kukamilisha ufunuo wa Mungu ulioanza na uumbaji na kufunga na mwanadamu Agano Jipya na la milele. Amekuja kutimiliza. Mwanzo kabisa wa mahubiri yake alisema “leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Lk. 4:21), kuhusu Torati anasema “sikuja kutangua”..kuihitimisha “bali kutimiliza”(Mt. 5:17) na hata alipokuwa anakata roho pale msalabani neno lake lilikuwa “yametimia” (Yn 19:30).
Ni katika mwanga huu, imani yetu inatualika tuijongee Siku ya Bwana kama ni siku inayokuja kuukamilisha ulimwengu na kutukamilisha sisi wenyewe. Na ukamilifu huu ni kufananishwa naye na kumuona Yeye kwa jinsi alivyo. Tukiwa na imani na matumaini haya, tafakari ya siku ya Bwana na kuhusu mambo ya siku za mwisho haiwezi kuwa kwetu sababu ya hofu, vitisho wala kuvunjika moyo bali mwaliko hai daima wa kujiandaa kuufikia ukamilifu wa uumbaji na ukombozi wetu kwa njia ya Kristo.