Tafuta

Tarehe 8 Desemba 1854 Papa Pio IX alitangaza kwamba, Bikira Maria amekingiwa Dhambi ya Asili kuwa ni sehemu ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Tarehe 8 Desemba 1854 Papa Pio IX alitangaza kwamba, Bikira Maria amekingiwa Dhambi ya Asili kuwa ni sehemu ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa. 

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Utenzi wa Sifa

Tarehe 8 Desemba 1854 Papa Pio IX katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. - Roma.

Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba mwaka 1854 katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba. Sherehe haitukuzi tu usafi, uzuri na utakatifu wa Bikira Maria bali ni fundisho la imani ambalo waamini wanapaswa kuliamini kina. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tenzi ni tungo za ushairi zinazoakisi kifasaha dhana za kifalsafa na za kitaalilimungu. Tenzi hueleza itikadi zinazohusiana na falsafa na teolojia ya watu fulani katika kipindi fulani cha maisha.

Leo tunakaribishwa kupata chakula cha kiroho kutoka utenzi mzuri uliosheheni mawazo mazito ya kiteolojia yenye dhana ya sikukuu ya Mama Bikira Maria Imakulata. Dhana mojawapo inayoonekana katika mapokeo ya Kanisa Katoliki inaakisi fasuli ya Injili yenye wazo la Bikira Maria Imakulata. Wazo hilo ni amkio la Malaika kwa Maria: “Salamu (furahi) Maria umejaa neema.” Neno hili Salamu kwa Kigiriki ni Kaire. Halafu umejaa neema ni kekaritomene kutoka neno tendo “Kekaritoum”. Neno hili lina maana nzito iliyo ngumu kuifasiri kirahisi. Tungeweza kusema: “Furahi, wewe uliyebarikiwa, uliyependwa na Mungu, uliyepata mazawadi mengi na hivi umetulizwa sana.” Kumbe, salamu hizo unazikuta pia katika utenzi wa leo. Waefeso wanaungana na Mama Maria katika upendo huu kamili wa Mungu. Kila mfuasi wa Kristu ameitwa kuwa Imakulata. Kwa hiyo hata sisi tunaosherekea sikukuu ya Bikira Maria Imakulata tumeitwa kuwa akina imakulata.

Hebu tujaribu kutafiti kwa kina ujumbe wa utenzi huu. Kihistoria utenzi huu uliimbwa huko Efeso katika maadhimisho ya sakramenti ya ubatizo. Paulo akauchukua na kuutumia katika kuanza kuandika karibu barua za kichungaji. “Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu, kwa watakatifu walioko Efeso, wanaomwamini Kristo Yesu. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu  Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.” Kumbe watakatifu hao Waefeso walikuwa waamini wa kawaida tu walioamua kuupokea ujumbe wa Injili (Habari njema) na kuumwilisha katika maisha yao. Sisi pia tunaweza kuingia katika kundi la watakatifu hawa katika imani na kumwimbia Mungu utenzi huu. Utenzi ni sala ambayo mwamini anaongea na Mungu anayehusika na maisha yake. “Mwenye furaha anaimba, anapiga vigelegele, anapiga mluzi na kucheza…” Tujiunge na waamini wanaomwimbia kwa shangwe Baba yao anayehusika kwa undani kabisa na maisha yao: “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.”

Neno kutukuza, lina maana ya kubariki yaani, kutakia mema, kutakia uhai na uzima. Kinyume cha kutakia mema ni kulaani yaani kutakia kifo. Paulo anawaandikia Warumi: “Wabarikini wote wanaowadhulumu, wabarikini daima. Msilaani kamwe.” Mtume Petro anasema: “Msimlipe yeyote ovu kwa ovu, bali daima lipeni uovu kwa baraka, daima kumtakia mwingine uhai na uzima.” Mtu anakuwa kamili pale anapotambua kuwa inambidi amtukuze Mungu yaani aseme mema tu juu ya Mungu. Kwa kawaida binadamu tunamshukuru Mungu kwa sababu ya kufanikiwa katika mambo yanayoonekana katika maisha. Kumbe Waumini wa Efeso wanamtukuza Mungu kwa vile wameona uso wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristu mwanae. Siyo tu kwa vile ametutendea maajabu bali ni kwa sababu pia: “Ametubariki kwa baraka zote za roho katika Kristo.” Yaani, siyo tu kwa sababu ametupatia uzima wa kibaolojia (uhai wa duniani hapa) bali pia uzima ule aliotuletea Kristo, yaani maisha ya Baba wa mbinguni.

Kwa hiyo kama maisha ya Yesu hayatugusi hapo tutafanana na Wakristo wale wanaosifu maajabu ya Kristo lakini hawaelewi maana ya maisha hayo. Mungu ametuchagua kutokana tu na upendo wake: “Katika yeye ametuchagua kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.”  Baada ya uchaguzi huo tumetumwa kupeleka ujumbe wa upendo wa Mungu kwa watu wote. Sisi waamini tumechaguliwa kisha tumetumwa kwa malengo mawili: “ili tuwe watakatifu na safi mbele yake katika mapendo.” Lengo la kwanza la utume wetu ni kuwa Watakatifu mbele ya Mungu na mbele ya watu wote katika upendo. Yaani tumeitwa kuwa tofauti na wale ambao bado hawajautambua upendo huu mkamilifu wa maisha ya utu mpya katika Mungu kwa njia ya Kristu. Hivi sisi tumechaguliwa ili kuwa Jumuiya Takatifu iliyo tofauti na ile ya ulimwengu wa kipagani. Lengo la pili la utume wetu ni kuwa safi yaani imakulata. Tuwe imakulata mbele ya Mungu na mbele ya watu wote katika upendo kama Mama yetu Bikira Maria Imakulata. Mwito wa kuwa bila doa katika mapendo naana yake ni kujisadaka kujitoa kwa ndugu bila ubinafsi yaani safi (Imakulata) katika upendo wa Kikristo.

Mungu hakutuchagua kwa kubahatisha bali “Kutoka mwanzo aliazimu kutufanya waana wake kwa ajili ya Yesu Kristo jinsi alivyonuia na kutaka.” Azimio hilo la Mungu liliwahusu watu wote bila ubaguzi. Kila mtu ameitwa kuwa mwana mrithi siyo kwa mastahili yake bali kutokana na upendo wa Mungu. Hivi neno hili mrithi linataka tu kutujulisha kuwa hiyo neema ni ya zawadi ya bure. Utukufu wa Mungu ni ule unaoonekana waziwazi, yaani upendo wake. “Ili usifiwe utukufu wa neema yake, aliyotujalia katika huyo mpendwa.” Wakristo wa awali wa Efeso waliishi maisha safi yaliyoakisi utukufu wa Mungu. Hivi utenzi huu unaonesha kwamba wakristu wenzetu wa Efeso walitambua mwito wao kuwa katika jumuiya yao ilitakiwa ing’are upendo huo wa Mungu. Kwa hiyo Jumuiya ya kikristu inapoonesha upendo safi (Imakulata) bila alama ya ubinafsi hapo inaonesha jinsi ulivyo ukubwa wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Tuige maisha ya Bikira Maria Imakulata yanayong’ara upendo wa Mungu.

Bikira Maria Mkingiwa Dhambi Asili
07 December 2019, 10:29