Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Ujio wa Masiha ni chemchemi ya haki, amani na ustawi wa watu wake. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Ujio wa Masiha ni chemchemi ya haki, amani na ustawi wa watu wake. 

Tafakari Jumapili 2 ya Majilio: Masiha: Chimbuko la haki na amani!

Masiha tunayemngojea kama kweli tutajiandaa vyema kumpokea ndiye ataleta amani tunayoitafuta kama Waisraeli walivyoingoja kwa mda wa miaka mingi. Amani, pale ambapo dhambi imeleta mgawanyo, utengano na chuki. Ni amani inayotokana na msamaha. Amani kati ya Mtu na Mungu, amani kati ya mtu na mtu, amani kati ya mtu na Viumbe na amani kati yam tu na mazingira yake.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya majilio mwaka A wa Kanisa. Ujumbe wa domenika hii ni kuwa Masiha ataleta nyakati za Amani na haki. Atawabatiza watu kwa Roho Mtakatifu na kwa Moto ili kuondoa uovu wote unaoleta utengano na kuwapatia watu Roho wa Mungu, Roho wa upendo ambaye atawaleta watu pamoja katika haki na Amani; wakijaliana na kumcha Mungu. Katika historia ya waisraeli, baada ya kifo cha Solomoni, ufalme wa Israeli na ufalme wa Yuda ziligawanyika ikawa rahisi kuvamiwa na maadui zao na hivyo walipelekwa utumwani. Waliobaki nyumbani wakiwa ni wagonjwa na wazee, maskini na wanyonge. Hawa waliishi katika mateso mengi. Nabii Isaya anaonja mateso na mahangaiko yao. Anawatia moyo kuwa Mungu hajawasahau, atamtuma Masiha ambaye atawakomboa kutoka katika taabu zao na kuwapa amani na usitawi. Haya ndiyo mazingira ya somo la kwanza.

Nabii Isaya anasema siku ile litatoka chipukizi katika shina la Yese, yaani Masiha, na roho wa Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kufuata ayaonayo kwa macho yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Utabiri huu unamhusu Bwana wetu Yesu Kristo, mwokozi wetu. Hali hii ya nyakati za Nabii Isaya bado ipo hata nyakati zetu. Wanyonge bado wanagandamizwa sababu ya Rushwa, hhuluma, ufisadi wa aina mbalimbali. Waliopewa dhamana ya kutuongoza wanatumia nafasi yao kujinufaisha wao binafsi. Watu wananyimwa haki za msingi za maisha kama vile elimu, ajira, afya, makazi hata haki ya kuishi.

Kuna mpasuko mkubwa kati ya matajiri na maskini. Dhana ya ujirani mwema au undugu inapotea kwa sababu ya kuta kubwa zenye fensi ya Umeme, mbwa mkali pengine na ulinzi wa kimasai. Utamaduni wa ubinafsi na kifo ndio unaotawala.  Hali hii haina ubaguzi ipo hata ndani ya kanisa. Masiha tunayemngojea kama kweli tutajiandaa vyema kumpokea ndiye ataleta amani tunayoitafuta na kuingojea kama Waisraeli walivyoingoja kwa mda wa miaka mingi. Amani, pale ambapo dhambi imeleta mgawanyo, utengano, na woga au chuki. Ni amani inayotokana na msamaha. Amani kati ya Mtu na Mungu, amani kati ya mtu na mtu, amani kati ya mtu na Viumbe na amani kati yam tu na mazingira yake. Amani hii ni ile nguvu ya ndani inayomfanya mtu aweze kukabiliana na mateso, magumu, vishawishi, dhuluma na kubaki mwaminifu kwa Mungu. Lakini hii itatimia kama tutafungua mioyo yetu na kumpokea Masiha Bwana wetu Yesu Kristo. Na njia ni moja tu ndiyo ambayo Yohane Mbatizaji anasema katika Injili, “tubuni kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia.” Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.

Katika uhalisia wa maisha ya kawaida iwe kwa mtu mmoja mmoja, familia, jumuiya au nchi nyakati zetu kuna kutoelewana, magomvi, utengano, chuki na vita. Mke na mume hawaongee, mama mkwe hasalimiani na mkwewe, watoto hawasalimiani na wazazi wao, ndugu wanagombana hata kuuana, majirani hawatembeleani, hata katika jumuiya moja kuna wasiosalimiana. Hii ni dalili wazi ya uwepo wa dhambi katika nafsi zetu. Yakobo anashuhuida hili akisema, “Mapigano na ugomvi wote kati yenu vinatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana ndani yenu. Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mnatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati; hivyo mnagombana” (Yak 4:1). Dhambi inaleta utengano kati ya mtu na Mungu wake na kati ya mtu na jamii inayomzunguka. Dhambi inaondoa neema ya utakaso ndani mwa mtu yaani uzima wa Kimungu; inaondoa Roho wa Mungu inayetuongoza katika umoja na uelewano.

Hivyo, dhambi ikishaondoa taa hiyo ndani mwa mtu, mtu anakosa mwelekeo. Mzaburi anatuambia, “Dhambi huongea na mtu mwovu ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya.” (Zab.36:1-4). Hayo ndiyo yampatayo mtu akitenda dhambi na kumfukuzia mbali Roho wa Mungu. Kumbe, kama mafarakano yanaletwa na dhambi na kwa vile Kitubio kinatuondolea dhambi; basi kitubio kitaondoa mafarakano na kuleta Amani. Ndiyo maana Yohane Mbatizaji amesema: “Tubuni, kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia”, “Pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika”. Akasisitiza, “Shoka limekwishawekwa katika shina la miti, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa”.

Yohane anaendelea kutuasa katika waraka wake wa kwanza akisema, “Tukisema kwamba hatuna dhambi tunajidanganya wala kweli haimo ndani mwetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu hata atusamehe dhambi zetu” (1Yoh 1:8). Ataondoa uchafu wote na kutia Roho wa Mungu ndani yetu tuliyempoteza kwa dhambi. Hapo ndipo tunaweza kuishi kwa pamoja na amani kama alivyoagua Nabii Isaya. Mtume Paulo pia ametuombea, “Mungu atujalie kunia mamoja sisi kwa sisi”, anatusihi tukaribishane sisi kwa sisi. Hivyo, anayeungama, anarudishiwa neema ya Utakaso na Roho wa Kimungu ndani yake. Lakini pia kwa maungamo yake anarudisha Roho wa Kimungu katika jumuiya. Kuungama ni tendo la mapendo, kwa mtu binafsi, kwa Mungu na kwa jumuiya. Kuungama ni tendo la kinafsi lakini pia la kijumiya. Hivyo, hata kama hutaki kuungama kwa ajili yako binafsi, walau uungame kwa ajili ya jumuiya maana dhambi yako inaleta mafarakano katika jumuiya.

Tutambue kuwa maisha yetu yanapata maana na ukamilifu wake katika Kristo. Tunapoyalinganisha au tunapoyatathmini maisha yetu kwa vigezo vya kibinadamu, vigezo vya kidunia, tunaweza kujiona kuwa tumekuwa wakamilifu, hatuna dhambi. Lakini kama kigezo chetu cha ulinganifu kikiwa ni Kristo mwenyewe tutatambua tu wadhambi na tunahitaji kufanya toba. Hivyo, tuhimizane kuungama. Kila mwana familia mwenye dhambi akiungama; kwa pamoja tunashirikiana kurudisha neema ya utakaso katika familia zetu, katika jumuiya zetu na katika dunia kwa ujumla. Hii itatusaidia kumaliza mafarakano na ugomvi na kuleta furaha na amani hata mbwa mwitu atakaa pamoja na mwanakondoo.

Jumapili 2 ya Majilio
04 December 2019, 18:07