Tafakari Neno la Mungu Jumapili 3 Majilio: Jipeni moyo msiogope!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunayatafakari leo Masomo ya dominika ya tatu ya Majilio, mwaka A. Dominika hii ya tatu ya majilio huitwa pia dominika ya furaha (Gaudete) na inatualika tufurahi kwa sababu masiha mkombozi wetu yu karibu kuja. Somo la kwanza (Isa. 35:1-6a, 8a.10 ) ni kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya. Kiini cha ujumbe wake kinapatikana katika maneno ya nabii mwenyewe anaposema “waambieni watu walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope”. Ni ujumbe wa matumaini yanayoleta furaha kwa watu wa Mung. Nabii anautoa ujumbe huu kwa Israeli iliyokuwa chini ya vifungo vya utumwa wa Babiloni. Na matumaini anayowapa ni matumaini ya kuachiwa huru na kurudi katika nchi yao. Kipindi hiki cha majilio kwa namna fulani kinatupitisha katika historia ya Waisraeli na hatua mbalimbali walizozipitia. Somo hili la leo linazungumzia hali ngumu ya utumwa wao wakiwa Babiloni, mbali na nchi yao na tena wakiteseka.
Hili la taifa kupelekwa utumwani na taifa lingine lenye nguvu zaidi linaonekana kuwa ni tatizo la kisiasa na ni la kijamii pia. Pamoja na hayo, Nabii Isaya na manabii wengine hawakuliona hivyo. Kwao hili halikuwa tatizo lililokuwa na chimbuko la kisiasa wala la kijamii bali chimbuko lake ni katika imani na mahusiano ya Waisraeli na Mungu. Kwa sababu hii, tunaona kuwa ukombozi wao hautoki mahala popote isipokuwa kwa Mungu. Na ukombozi huu hautangazwi na mwingine yeyote isipokuwa nabii wake. Ni Mungu anayewakomboa watu wake. Anawakomboa ili kuwarudisha karibu naye: ili kuiamsha imani yao na matokeo ya watu kurudi kwa Mungu ndiyo furaha, amani na ukombozi wa kweli. Tukiwa na mawazo hayo, sisi tunaolisoma na kulitafakari somo hili katika kipindi hiki cha majilio tunaalikwa kumgoja masiha mkombozi wetu tukijibiisha kukuza imani yetu kwake na kujenga ukaribu naye kama msingi wa kuupokea ukombozi tunaoutazamia.
Somo la pili (Yak. 5:7-10) ni kutoka katika waraka wa Yakobo kwa watu wote. Waraka huu ambao umesheheni mausia na maonyo mbalimbali kwa watu wa Mungu, katika somo la leo unajikita katika mambo mawili: la kwanza ni kukazia juu ya uvumilivu na la pili ni kukumbusha kuwa Bwana yu karibu kurudi. Somo letu hili la pili linaanza katika aya ya 7 ya sura ya 5. Kuanzia aya ya 1 hadi ya 6 katika sura hii hii, Yakobo anawakaripia matajiri ambao wamejitajirisha kwa kuwanyonya wanyonge, wanatumia utajiri wao kwa anasa bila kujali wahitaji na kwa kukandamiza haki zao. Kumbe, Yakobo anazungumza katika jamii iliyokuwa na matabaka. Baada ya karipio kwa matajiri, somo la leo linaanza na ujumbe kwa tabaka la wanyonge. Ujumbe anaowapa ni kuwa Bwana yu karibu. Yakobo anahusisha ujio wa Bwana na siku ya hukumu. Anapowatangazia watu kuwa Bwana yu karibu anamaanisha kuwaambia kuwa imekaribia siku ya hukumu ya haki ambapo wale wanaojitajirisha kwa kuwanyonya wanyonge watapata hukumu yao na wale wanaonyonywa watarudishiwa haki na thamani yao. Hivyo anawaalika wawe na uvumilivu. Huu sio uvumilivu wa kukata tamaa bali ni uvumilivu wa matumaini. Ndiyo maana anamalizia kwa kuwaambia wajifunze uvumilivu huu kwa manabii ambao walistahimili mabaya kwa jina la Bwana na walimgojea yeye tu. Hata kwetu leo, ujio wa masiha tunayemgoja ni ujio unaotualika kusawazisha matabaka katika jamii. Ni ujio unaotualika kuyapima mambo tufanyayo kwa jicho la siku ya mwisho. Yote yana mwisho wake. Tujiandae kupokea mwisho mwema kwa kuanza tangu sasa kujiandalia mema.
Injili (Mt. 11:2-12) Somo la Injili ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani anasikia anayoyafanya Yesu. Anawatuma wanafunzi wake kwenda kumuuliza, “wewe ndiwe yule ajaye au tumtazamie mwingine”? Swali hili kidogo linashangaza. Linashangaza kwa sababu masimulizi mbalimbali katika injili yanaonesha Yohane Mbatizaji alimfahamu Yesu kabla. Bikira Maria alipokwenda kumtembelea Elizabeti na kumuamkia, Yohane akiwa tumboni aliruka kuonesha furaha ya kumtambua Yesu masiha anayekuja. Mtoni Yordani ni Yohane Mbatizaji aliyemtambulisha Yesu akatoa ushuhuda kuwa ndiye mwanakondoo wa Mungu na akambatiza. Swali lake hili linamaana gani? Israeli yote ilikuwa ikimgoja masiha lakini wazo kwamba masiha huyu atakuwa ni wa namna gani halikuwa wazi kwa wote. Kulikuwa na mitazamo tofauti tofauti kuhusu masiha aliyekuwa akingojewa. Ilikuwapo mitazamo ya kidini lakini pia ilikuwapo mitazamo ya kiutawala, mitazamo ya kijamii ambapo alitegemewa masiha mfalme. Ndani ya mitazamo ya kidini wapo waliokuwa wanamtegemea masiha kuhani, wengine masiha nabii na wengine masiha anayekuja kuuhukumu ulimwengu na kuleta kisasi cha Mungu yaani kuweka utofauti kati ya wateule wa Mungu waliopokea ujumbe wa manabii na wale ambao hawakuupokea.
Katika Mt 3:11-12 Yohane Mbatizaji alimtambulisha Yesu “…yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika”. Utambulisho huu unamuonesha Yohane Mbatizaji kuwa naye alishiriki mawazo ya watu wa wakati wake kuhusu masiha anayekuja na licha ya kumkiri na kumtolea ushuhuda kuwa ndiye mwanakondoo wa Mungu na licha ya kumbatiza, anashitushwa bado na utendaji wa Yesu na anatuma watu kumuuliza kama ni yeye au wangoje mwingine. Yohane Mbatizaji kama watu wa wakati wake alitegemea masiha mwanamapinduzi, masiha asiyewakaripia wadhambi, Masiha anayetangaza kisasi na kuhukumu badala yake anasikia juu ya masiha anayehubiri habari njema, anayeponya na anayefufua wafu. Somo hili kwetu linatualika kumtambua Masiha tunayemgoja ni Masiha wa namna gani. Lakini pia ni somo linalokazia umuhimu wa kulinda imani isichafuliwe na mitizamo ya mazingira tunamoishi. Yohane Mbatizaji pamoja na ukuu wake alifika mahala akatia shaka katika Kristo. Kumbe hata sisi hata tukishapiga hatua namna gani katika ukristo tuendelee kujilinda na kuilinda imani yetu.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kipindi cha Majilio ni kipindi ambacho kina uhusiano wa ukaribu sana na unabii katika Israeli. Manabii ambao kimsingi walikuwa ni wajumbe wa Mungu katika hali na mazingira mahsusi, katika ujumla wao wameamsha tumaini la ujio wa Masiha katika Israeli. Ni wao wamewafundisha watu kuutumainia wokovu na hapo hapo wakawaandaa watu kumpokea Yesu, Masiha na mkombozi. Kwa jinsi hii, Majilio inatusaidia pia kuuelewa unabii katika Biblia. Ni sawa na kuiangalia filamu kutoka mwisho kwenda mwanzo kunavyoweza kusaidia kujua makusudi ya baadhi ya vipengele vyake. Kristo ambaye ni kiini au mwisho wa unabii wote, kwa mwanga wake tunapata kujua roho ya unabii ni kitu gani hasa. Katika nyakati zetu za sasa, kutokana na mazingira ya kijamii au hata ya kisiasa tunamoishi kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa uanaharakati. Na kwa mwamko huu wa uanaharakati msisitizo umewekwa zaidi juu ya haki, juu ya hukumu, juu ya misimamo mikali ya kiitikadi na juu ya utatuzi wa mambo kwa haraka na tena kwa njia fupi iwezekanavyo.
Na kwa bahati mbaya mitazamo hii ya kiuanaharakati imeanza kutafuta uhalali wake katika unabii wa kibiblia. Matokeo yake ni moja kwa moja kuupotosha unabii kwa kuusoma na kuutumia si kama unabii wenyewe ulivyo bali inakuwa ni kuusoma na kuutumia kadiri ya mitazamo yetu ya sasa. Kama kiini na mwisho wa unabii wa kibiblia ni Kristo na Kristo ndiye Masiha anayekuja kuokoa basi lengo la kwanza la unabii na roho yenyewe ya unabii ni wokovu. Wokovu huu ambao ni wa kiroho na wa kimwili hauji kwa kuwajaza watu hofu wala kwa kuwatangazia mapambano na vitu vingine kama hivyo bali huja kwa kuendana na fadhila na tunu zile zile alizoziishi na kuzifundisha Kristo. Kumbe kuukataa ujumbe unaohubiri juu ya upendo, haki, amani, uvumilivu, ustahimilivu na fadhila kuwa ni ujumbe usio wa kinabii ni kuukataa unabii wenyewe, kinyume na unabii na ni kinyume na mafundisho ya Kristo, aliye kiini cha unabii wenyewe. Tunapoendelea kumtazamia Masiha mkombozi wetu anayekuja, neema ya Mungu ituongoze kuuewa na kuuishi ujumbe wa manabii wake.