Tafuta

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Mfano na kielelezo cha tunu msingi za maisha ya Kikristo na Utakatifu wa maisha. Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Mfano na kielelezo cha tunu msingi za maisha ya Kikristo na Utakatifu wa maisha. 

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Fadhila!

Upendo ndio katiba, ndio sheria, ndio mwongozo na ndio utambulisho wa maisha katika familia ya mkristo. Ni juu ya upendo ndipo zinajengeka fadhila nyingine anazozitaja. Katika nafasi ya pili, Paulo anautafsiri upendo katika hali halisi anaposema “enyi wake watiini waume zenu, enyi waume wapendeni wake zenu na enyi kina baba msiwachokoze watoto wenu”. Fadhila na Utakatifu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tunayatafakari leo Masomo ya sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ambayo ni mfano wa familia zetu zote katika fadhila za nyumbani na utakatifu. Somo la kwanza (Sir 3:2-6,12-14 ) ni kutoka katika kitabu cha Yoshua bin Sira. Kitabu hiki ni mojawapo ya vitabu vya Agano la Kale vinavyoitwa vitabu vya Hekima, vitabu ambavyo vinahifadhi mang’amuzi ya wayahudi kuhusu maisha: kuishi maisha yanayofaa, yanayowapendeza watu na Mungu. Yoshua bin Sira katika somo hili anazungumzia fadhila za kiutu zinazoongozwa na hekima. Ya kwanza anayoitaja ni heshima kwa wazazi. Na hiki ndicho inachofundisha amri ya nne ya Mungu. Kumbe hapa Yoshua bin Sira anaonekana kutumia hekima kuifafanua amri ya nne inafundisha nini katika lugha ya kawaida. “Waheshimu baba na mama, upate miaka mingi na heri duniani. Anaonesha kuwa neno “heshima kwa wazazi” ndani yake linaalika kuwapenda  wazazi, kuwasaidia kwa hali na kwa mali pamoja na kuwatii. Amri hii ya nne ya Mungu ndiyo amri pekee inayotaja moja ka moja tuzo “ili upate miaka mingi na heri duniani”. Tuzo hilo kama anavyolifafanua Yoshua bin Sira ni kustahili kusamehewa dhambi pale unapoomba upatanisho, ni kuwekewa akiba azizi, ni kuwafurahia watoto na ni kuongezewa siku.

Somo la pili (Kol 3:12-21) ni kutoka katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai. Somo hili linatoa mwongozo wa maisha ya kinyumbani kadiri ya Mtume Paulo. Huu ni mwongozo anaoutoa Paulo wa kuwasaidia wakristo wapya wa Kolosai kuishi katika familia zao kwa namna inayoendana na imani ya kikristo waliyoipokea kwa ubatizo. Anajikita juu ya maisha ya fadhila hasa fadhila ya upendo ambayo ndio kifungo cha ukamilifu. Kwa mtume Paulo maisha ya familia ya kikristo yanaongozwa na upendo. Upendo ndio katiba, ndio sheria, ndio mwongozo na ndio utambulisho wa maisha katika familia ya mkristo. Ni juu ya upendo ndipo zinajengeka fadhila nyingine anazozitaja. Katika nafasi ya pili, Mtume Paulo anautafsiri upendo katika hali halisi anaposema “enyi wake watiini waume zenu, enyi waume wapendeni wake zenu na enyi kina baba msiwachokoze watoto wenu”. Ni maneno yanayoonesha kuwa katika familia kila mmoja ana nafasi yake na majukumu yake. Kuuweka upendo katika matendo ni kila mmoja kuishi katika familia kwa kutambua nafasi yake ni ipi na majukumu yake ni yapi na hayo ayaishi na kuyatekeleza.

Injili (Mt. 2:13-15, 19-23) Somo la Injili ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Linaelezea tukio la Maria na Yosefu kumkimbiza mtoto Yesu Misri kumuepusha na hatari ya kuuwawa mikononi mwa Herode. Tukio hili la Injili ya leo tunaweza kulitafasiri kwa namna mbili. Namna ya kwanza ni kwamba Yesu anakimbilia Misri kama walivyokimbilia huko wana wa Yakobo kuepuka hatari ya baa la njaa lililoikumba nchi yao ya Kanaani. Wana hawa wa Yakobo baada ya kuteseka huko Misri Mungu aliwatoa na kuwarudisha katika nchi yao. Kitendo cha Yesu kwenda na kurudi kutoka Misri basi kinamuonesha Yesu akiipitia historia ile ile ya Waisraeli na hivi kinamtambulisha Yeye kuwa ndiye Israeli mpya. Ndiye anayeonesha namna ya kuyashika mapenzi ya Mungu na kwamba kwa njia yake taifa lote la Mungu linaingia katika ahadi zile zile ambazo Mungu aliwaahidia Israeli ya mwanzo.

Tafsiri ya pili ni ile inayoonesha changamoto za maisha ambazo familia ya Yesu kama familia nyingine yoyote ilizipitia. Zilikuwapo changamoto ndogondogo na zilikuwepo changamoto kubwa ambazo familia hii ilizipitia. Na somo hili linaonesha changamoto kubwa kabisa iliyokuwa inagusa uhai wa mtoto. Tunachokiona ni kwamba familia hii iliikabili changamoto hii kwa kulisikiliza Neno la Mungu. Yosefu, aliyechukua nafasi ya baba katika familia hii aliikimbiza Misri familia yake kwa kufuata agizo la Mungu na hata wakati ulipotimia aliirudisha familia yake kwa kufuata agizo la Mungu. Hili ni mojawapo ya fundisho kubwa la somo hili la injili, kuzikabili changamoto za kifamilia kwa kulisikiliza Neno la Mungu; kwa kung’amua ni nini Mungu anataka familia ifanye katika changamoto inayoikabili.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, sherehe ya Familia Takatifu ni sherehe inayoweka fumbo la kuzaliwa kwa Yesu katika mazingira ya kibinadamu. Yeye ambaye tangu mwanzo alitabiriwa na manabii kuwa “Emmanueli” yaani Mungu pamoja nasi ameshuka na kukaa kwetu katika mazingira na hali ya ubinadamu kama yetu na kuishi katika familia kama sisi.  Kama jinsi kuzaliwa kwake kulivyoikuza hadhi ya ubinadamu wetu vivyo hivyo familia yake ilivyozikuza familia zetu katika hadhi ya utakatifu. Kwa jinsi hii Sherehe ya familia Takatifu ni sherehe ya familia zote kwa maana familia zetu zote zinachukua mfano wa utakatifu kutoka katika familia ya Yesu, Maria na Yosefu.  Ni sherehe pia ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya familia zetu na ni sherehe pia ya kuomba neema ya Mungu kwa ajili ya familia zote ulimwenguni.

Sherehe inayotukumbusha kuwa familia ni tunu ya kimungu. Inatuonesha ni kiasi gani Mungu anazithamini familia hadi kujalia kuwa Mwanae Yesu azaliwe na kuuishi ubinadamu wake katika familia, tena familia ya kawaida kabisa. Ni hapo tunaona kuwa, Yesu ambaye ni mtu kweli na Mungu kweli, aliihitaji familia ili kudhihirisha kuwa mtu kweli. Alihitaji malezi, alihitaji uangalizi, alihitaji upendo na alihitaji kuonesha mshikamano wake na watu kuanzia katika hatua hii muhimu sana ya maisha ya jamii yaani familia. Na namna alivyoishi katika familia ametuonesha kuwa katika ukawaida wa maisha ya familia, ukawaida ulioungana na Mungu ndipo nasi kama yeye tutazifanya familia zetu kuwa takatifu na sisi wenyewe kuufikia utakatifu.

Tunaadhimisha Sherehe hii ya familia tukijua changamoto nyingi zinazozikabili familia zetu. Kila wakati, kila kipindi kimekuwa na changamoto zake. Katika kipindi chetu hiki huenda changamoto iliyo kubwa kuliko nyingine katika familia ni ile ya umoja. Umoja ambao ndio kielelezo cha undugu, upendo na fadhila zote za maisha ya nyumbani unakosa nafasi katika familia nyingi leo. Nguzo hii ya umoja haiwezi kukosekana bila kuleta madhara katika familia na kwa wanafamilia wenyewe. Umoja ni nguvu na utenganno ni udhaifu. Sherehe hii iwe kichocheo kwetu kuanza upya maisha katika familia zetu na kwa msaada wa Mungu tuweze kuujenga na kuuishi umoja katika familia zetu.

Liturujia: Familia Takatifu
28 December 2019, 08:07