Sherehe ya Noeli ya Bwana: Fumbo la Umwilisho! Mshikamano!
Don Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Noeli ni sherehe ya Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu. Ni sherehe ya umwilisho wa Neno la Mungu. Injili ya Yohane inaanza na wimbo juu ya Neno wa Mungu au kwa kigiriki λογος (Logos) na Kilatini Verbum. Mwinjili Yohane anamtambulisha Yesu Krsito kuwa ni NENO la MUNGU ametumwa kutoka kwa Baba, ni asili ya maisha, mwanga wa ulimwengu, aliyejaa neema na kweli, mwana pekee wa Mungu anayeufunua kwetu utukufu wa Mungu Baba. Neno, kwa lugha rahisi, ni mojawapo ya nyenzo ya mawasiliano kwani kwa neno au maneno tunaweza kuwasiliana. Mtoto aliyezaliwa bado ni mtoto mchanga na hivyo bado hawezi kuongea au kutumia maneno kama njia ya mawasiliano. Lakini bado mtoto huyu anaongea nasi kwa nafsi yake kama zawadi ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote. Huyu mtoto ndiye NENO LA MUNGU (λογος). Ni Upendo wa Mungu kwetu.
Neno(logos) la Mungu ndio hekima ya Mungu ambayo kwayo Mungu ameumba ulimwengu. Neno halikuumbwa bali lilikuwepo pamoja Mungu na kwako Mungu akauumba ulimwengu. Ni katika Neno Mungu anaumba ulimwengu. Ni Neno linaleta nuru duniani na kututoa katika maisha ya dhambi na giza. Hivyo ni nuru kwetu wanadamu. Yohane Mbatizaji sio ile nuru bali ametumwa na Mungu kuja kushuhudia hiyo nuru yenyewe. Amekuja ili kuwaelekeza wanadamu nuru yenyewe. Alikuja ulimwenguni ile nuru yenyewe ila watu hawaikutambia ile nuru, ila wale walioitambua na kuipokea wakafanyika wana wa Mungu. Ni kwa njia ya Neno nasi tunafanyika kuwa wana wa Mungu.
Neno alifanyika mwili na kukaa kwetu. Noeli ni sherehe ya Fumbo la Umwilisho. Mwili katika lugha ya kibiblia ni ishara ya uduni na unyonge wetu kama wanadamu, tunaweza kurejea nabii Isaya 40: 6-8. Huyu Neno anafanyika mwili sawa na sisi katika yote isipokuwa hakuwa na dhambi. Ni upendo wa Mungu kutaka kufanana na mwanadamu ili mwanadamu aliye mnyonge na dhaifu aweze kushirika utukufu na utakatifu wa Kimungu. Mwanadamu anayekufa na kupotea katika uso wa nchi apate kuishi milele pamoja na Mungu, ni upendo wa namna gani huu? Nasi tutaona utukufu wake. Katika Biblia, mwanadamu hawezi kumuona Mungu kwa macho ya kibinadamu. Mwanadamu anaweza tu kuutafakari utukufu wa Mungu, yaani ishara za uwepo wa Mungu, na ukuu wa kazi zake kama alivyoonesha ukuu na uweza wake kwa wamisri na Farao na jeshi lake. Kutoka 14:17. Ila katika nafsi ya Yesu Kristo tunamuona Mungu. Anayemwona Yesu Kristo anamwona Mungu Baba kama alivyosema Yesu kwa Filipo. Rej. Yoh 14:9
Ni Mungu kwa mara ya kwanza anajifunua na kujidhihirisha kwa mwanadamu katika nafsi ya Mwana pekee wa Mungu na hivyo huyu mtoto aliyezaliwa amejaa neema na kweli. Neema na kweli katika Maandiko Matakatifu ni sawa na upendo wa kiaminifu wa Mungu kwa watu wake. Ni uwepo wa Mungu mwenyewe kati yetu. Katika nafsi ya Yesu Kristo kuna ukamilifu wa upendo wa Kimungu kwa watu wake. Mtoto aliyezaliwa ni zawadi isiyo kifani ya Mungu mwenyewe kwa watu wake. Ni Mungu mwenyewe anajitoa zawadi kwetu. Yohana mwinjili mara nyingi anatueleza kuwa hakuna aliyemwona Mungu (Yoh. 5:37; 6:46; 1 Yoh. 4:12,20) na pia Kutoka 33:20 ila hapa anatueleza kuwa aliyemwona Yesu amemwona Mungu. Yatosha kumtafakari Yesu Kristo, kuangalia yale anayoyafanya, anayofundisha na kutuelekeza kuweza kukutana na Mungu mwenyewe. Nuru ya kweli inayotupelekea kuuona utukufu wa Mungu Baba ni nafsi ya huyu mtoto aliyezaliwa. Rej. Yoh 14.
Fumbo la umwilisho linatuacha na mshangao mkubwa juu ya Upendo wa Mungu kwetu wanadamu. Mungu aliye wa milele anakubali kuchukua ubinadamu wetu wenye kuharibika, Mungu asiyeonekana anajifunua kwetu katika nafsi ya Mtoto Yesu. Ni rahisi labda kueleweka kwa Mungu anayebaki juu mbinguni na kutoa hukumu zake kali kwa wadhambi na wakosefu. Ila ni upendo wa namna gani aliye Muumba wetu anashuka na kukaa kati yetu, na ndio mwaliko wa Noeli kumkaribisha Masiha na kuishi naye katika maisha yetu ya siku kwa siku. Somo la 1 kutoka kwa Nabii Isaya linatupa pia habari ya furaha kwani sasa utumwa na mateso ya kila aina umefika mwisho. Kutoka utumwa wa Babeli ni ishara ya ukombozi wa kiroho sio tu kwa wanawaisraeli bali pia kwa ulimwengu mzima. Kutoka Waraka kwa Waebrania tunaona mwandishi anatueleza kuwa Mungu ananena nasi sasa sio kwa njia ya manabii kama hapo zamani bali kwa njia ya Mwana pekee mwenye utukufu wa Mungu Baba na zaidi ya malaika kwani huyu ni Mwana pekee wa Mungu.
Ni zaidi ya malaika kwani ni Mwana wa Mungu. Mwandishi anarejea Zaburi 2:7 Wewe ndiwe mwanangu mimi leo nimekuzaa. Mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto mwanamume. Noeli njema kwenu nyote na Mtoto Yesu azidi kuzaliwa katika maisha yetu, afanyike mwili na kukaa nasi. Kwa Lugha ya Kilatini: Puer natus est nobis, et filius datus est nobis: Cuis imperium super humerum eius: et vocabitur nomen eius magni consilii angelus. Cantate Domino canticum novum, quia mirabilia fecit. Huu ndio utamu wa Sherehe ya Noeli.