Sherehe ya Noeli ya Bwana: Huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu hauna mipaka!
Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, O.S.B., - Roma.
Maisha ya binadamu ni manyonge na dhaifu, yamejaa huzuni na hatima yake ni kifo. Kumbe ujumbe tunaoupata kwa Sherehe ya Noeli ni wa matumaini makubwa, kwamba Mungu ameamua kuingilia kati suala zima la maisha yetu. Yaani ameamua kuanzisha mahusiano ya upendo wa pekee na maisha haya. Unapomwangalia mtoto Yesu aliyelala pangoni na kumhoji kisa na mkasa wa Mungu kujidhalilisha na kuwa mtoto mchanga na kulala pangoni atakujibu: “Ninakupenda tu basi!” Anaendelea kukuthibitishia kwamba “Hata kama wewe binadamu ukiamua kuyasaliti mapendo hayo, potelea kwa mbali, mimi kwa upande wangu sitabadili msimamo. Mapendo yangu kwako hayatakoma kamwe.” Huu ndiyo ujumbe mzito wa kwanza anaokuambia mtoto Yesu pangoni. Hii ndiyo Noeli! Mwinjili Yohane kwa lugha ya utenzi anauelezea upendo huo wa mtoto Yesu. Mwinjili anafungua utenzi wake kwa kumpa mtoto jina la pekee: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno Alikuwa Mungu.”
Kumbe, jina la mtoto huyu ni Neno. Ndugu zangu ukitaka kuwasiliana na binadamu mwenzio huna budi kutumia maneno, kwa sababu maneno ni lugha ya mawasiliano. Mtu unayetamani kuwasiliana naye akikuambia analo neno analotaka kuongea nawe hapo unafurahi sana. Hali kadhalika Leo Mungu anataka kuwasiliana na wewe kwa njia ya Neno ambalo ni mtoto wake mchanga Yesu Kristu. Kwa hiyo kama hulifurahii Neno hilo, hapo ni dhahiri kwamba hajalielewa. Hii ndiyo Noeli! Kwa taarifa Yako lugha ya mtoto ya mchanga ina nguvu sana. Mathalani mtoto mchanga anaweza kulala usingizi mchana mzima na wazazi wakatulia na kufanya kazi zao. Lakini anaweza pia kulia usiku mzima na kuwafanya wazazi kukosa usingizi hata kuwazuia wasiweze kumwacha peke yake na kwenda wanakotaka. Kumbe leo Yesu ni Neno linaloongea nasi kutokana na hali yake ya uchanga. Neno la Mungu katika mtoto Yesu ni unyenyekevu wa Mungu anaotuonesha.
Mtoto Yesu anataka kutufundisha jinsi mtu aliyefaulu na kufanikiwa katika maisha anavyotakiwa kuwepo. Ukitaka kufaulu katika maisha uwe mnyenyekevu. Baadaye, atakapokua mkubwa atatueleza yeye mwenyewe kinaganaga zaidi jinsi ulivyo upendo wa Mungu kwetu binadamu. Kadhalika mtoto Yesu anafundisha kusoma ishara na alama za nyakati wanazoonesha watu ulimwenguni. Binadamu anaweza kuongea kwa kunyosha kidole, kwa kukunja uso, kwa kucheka, kwa kufyonya, kwa kutikisa mwili wake, kwa kujichora mwilini mwake, kwa ukimya wake, kwa kunywa vileo, kwa vichekesho vyake nk. Je unaweza kusoma lugha za vijana wa leo? Unaweza kusoma lugha ya viongozi mbalimbali wa siasa na wa serikali? Kwa hiyo mtoto aliyezaliwa leo ni Neno ambalo Mungu analitumia ili kuwasiliana nasi. Tulitafakari Neno hilo. Hii ndiyo Noeli. Mtoto huyu alikuwa nuru: “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu akija katika ilimwengu.”
Mungu alishuka duniani kulikokuwa na giza. Gizani watu tunashindwa kuonana, kutambuana na kuthaminiana kama binadamu. Kumbe Nuru ilifika ili kupambana na hilo giza. “Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Daima giza linatafuta mbinu za kuizima nuru. Lakini Nuru inabaki kuangaza ili iweze kulishinda giza lililotanda duniani. Mapambano bado yanaendelea lakini kwa njia ya mtoto huyu ushindi ni dhahiri. Hii ndiyo Noeli! Kwa njia ya mtoto Yesu, kizazi cha binadamu hakitaweza tena kujidai kuwa miungu kama ilivyo kwa baadhi ya wafalme, wakuu na watawala wanaojifanya mianga yaani miungu na kuwatawala wengine. Mungu mwenyewe ametuondolea uvivu kwa kujifanya binadamu na kuwa sawa kama sisi. Hii ndiyo Noeli! Aidha, hapa duniani wanaweza kutokea watu wanaong’ara na kuonekana kama mwanga wenyewe. Hao wanaweza kuwa watu wa dini, wa serikali, wa siasa walio na mvuto mkubwa kwa watu. Wataonekana kuleta mwanga wa matumini kwa watu.
Katika kipengele hiki mwinjili anatuletea Yohane anaposema: “Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane.” Huyo alikuwa, aling’ara na kuwapa watu matumaini hadi wakamwona kuwa ndiye nuru yenyewe iliyokuja kutukomboa. Kumbe Yohane alimwakisi tu Yesu aliye mwanga. Hivi akakana heshima hiyo na kusema: “Yeye siyo nuru hiyo.” Yohane ni shahidi wa Mwanga yaani Yesu aliye neno. Mwinjili anasema: “Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye.” Yesu anatuambia: Ninyi yabidi muangaze lakini muangaze. Hapa tunapata ujumbe Mkubwa sana kwa wale wanaoibuka kila kukicha na kuonekana kuwa mwanga na kuwapatia watu matumaini. Mwinjili anataka tujihoji kwamba hata kama tunang’aa lakini mwanga huo umwakisi na kumshuhudia Kristo aliye mwanga wenyewe. Hii ndiyo Noeli! Ujumbe mkuu na muhimu wa Injili ya leo unasema: “Bali wale wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.”
Umuhimu wake umelala katika kuyapokea mapendekezo hayo ya uso wa Mungu katika mtoto mchanga. Yaani ukimpokea mtoto huyu, nawe utakuwa mtoto wa Mungu. Kumbe sasa tunatambua kwamba ulimwenguni kumeingizwa roho ya Mungu iliyokuwa imepotea kwa njia ya mtoto Yesu. Hii ndiyo Noeli! Neno hilo limechukua mwili wetu, limekuwa sawa nasi ili tuweze kumwona tena Mungu. Ugumu umelala katika kumpokea mtoto huyu na kumwona kuwa ni Mungu kweli aliyejifanya binadamu kweli. Kumbe ni rahisi sana kutambua hilo kama utakumbuka kuwa “Kipenda moyo hula nyama mbichi.” Yaani Mungu anaweza tu kukaa nasi kutokana na upendo wake mkuu kwetu. Sisi leo tunaweza kumwona Mungu kwa kutafakari uso wake kwa njia ya mtoto Yesu. Hii ndiyo Noeli! Ndugu zangu, unapomwona mtoto yeyote yule amezaliwa, hapo ujue Mungu bado anaupenda ulimwengu. Leo tumepata Yesu kama kitoto kichanga, yeye ni alama ya kwamba Mungu sasa siyo anatupenda tu bali ameamua kuwa kama sisi na kukaa nasi.
Basi tusiogope tena giza la maisha, bali tumpokee na tuangazwe na mwanga wake wa kweli, ili nasi tuweze kung’aa kwa nuru yake katika bonde hili la giza. Kule kujua kwamba Kristu ni Nuru inayoniangaza gizani mwa maisha yangu ndiyo faida kubwa ya kusherekea Noeli kwa mkristo. Yesu ni Nuru ya ulimwengu. Heri kwa Sherehe ya Noeli ya Bwana!