Tafakari ya Neno la Mungu, Kesha la Sherehe ya Noeli ya Bwana: Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa. Tafakari ya Neno la Mungu, Kesha la Sherehe ya Noeli ya Bwana: Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa. 

Sherehe ya Noeli ya Bwana: Yesu Mwanga wa Mataifa!

Nabii Isaya aliwafariji Waisraeli kuwa wafurahi kwani kwa ajili yao Mtoto amezaliwa mtoto huyu ndiye Yesu Kristo ambaye sisi leo tunafurahi kuzaliwa kwake. Mtoto huyo ni mtoto wa kiume, ana uweza wa kifalme mabegani mwake, jina lake ni Emmanueli, mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, mfalme wa amani, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Noeli ya Bwana!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, katika misa ya mkesha wa kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, hayuko mbali, bali yu pamoja na watu wake. Yupo pamoja nasi ili atuokoe. Katika usiku mtakatifu, Kanisa linasherehekea, Krismasi, Noeli, sherehe ya umwilisho, yaani Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa binadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo: Mkombozi wa ulimwengu. Sikukuu hii ni mwanzo wa utimilifu wa ufunuo wa Mungu na ya fumbo la ukombozi wetu. Hivyo kumuona Mtoto Yesu ni kumwona Mungu Baba. Tena, Noeli yatujulisha sababu ya kuwako kwetu duniani: Kama Yesu alivyotoka kwa Baba kuja duniani na kurudi tena kwa Baba, vivyo hivyo binadamu anatakiwa ajijue kuwa yu msafiri: ametoka kwa Mungu kuja duniani na atarudi tena kwa Mungu. Kwa kuzaliwa Kristo, mbingu na dunia vinagusana, Mungu na binadamu wanaungana! Kwazaliwa kwake kunatuwezesha kufahamu upana na urefu, kimo na kina cha upendo wa Mungu: kuwa ameupenda ulimwengu hivi hata akamtoa mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16).

Tunaalikwa kufurahi kwa sababu kuzaliwa kwake kumeleta mwanga duniani kama Nabii Isaya anavyotuambia katika somo la kwanzaWatu waliokwenda katika giza, wameiona nuru kuu.” Maneno haya ya nabii Isaya ni maneno ya faraja na yana msingi wake. Historia inatueleza kuwa Nabii Isaya aliishi miaka 720 KK. Kipindi hiki Palestina iligawanyika katika Falme mbili. Ufalme wa Kaskazini, yaani ufalme wa Israeli ulichukua maeneo ya Galilea na Samaria. Ufalme huu ulikuwa na makabila kumi. Ufalme wa Kusini ni ufalme wa Yuda ambao ulichukua eneo la Yudea. Huu ni ufalme uliokuwa dhaifu na mdogo kwa kuwa na makabila mawili tu. Ijapokuwa falme hizi mbili zinaundwa na ndugu wana wa Israeli, lakini hawakuwa na mahusiano mazuri kwani palikuwepo na ugomvi na vita vya mara kwa mara. Ahazi mfalme wa Yuda akawa na hofu na kuanza kuomba msaada wa ulinzi kwa mataifa mengine hasa kutoka Assyria. Jeshi la Assyria likaushambulia ufalme wa kaskazini wakateketeza kila kitu wakapofusha watu, wakawaua wote walioonesha upinzani na kuwachukua wengine mateka.

Nchi yote iligeuka kuwa Bwawa la Damu, giza na wasiwasi. Ili kuokoa maisha, watu wengi walichimba mahandaki ili kujificha huko. Na wale waliopofushwa waliishi katika giza nene na uvuli wa mauti. Katika hali hii ya mateso, vita, na upofushaji wa macho, ndipo anajitokeza Nabii Isaya kuwapa matumaini mapya kwamba Nuru inakuja, waliokwenda katika giza na katika uvuli wa mauti nuru hiyo itawaangaza. Anawaalika wafurahi kama mkulima afurahiavyo mavuno yake ya kwanza, kama mwindaji afurahiavyo mawindo. Mkulima hufanya sherehe akiwaalika watu wale, wanywe na wacheze ngoma akifurahia kujaa kwa ghala zake. Wawindaji nao hufurahia mawindo yao, hukaa chini ili kugawanya mawindo yao. Nabii Isaya alimwambia Ahazi kuwa asiogope Mungu atamlinda. Ahazi hakuamini, Isaya anampa ishara ya kuzaliwa mtoto mwanamume atakayeuimarisha ufalme wake na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Huyu Masiha ataleta amani na ukombozi kati ya watu. Nabii Isaya aliwafariji Waisraeli kuwa wafurahi kwani kwa ajili yao Mtoto amezaliwa mtoto huyu ndiye Yesu Kristo ambaye sisi leo tunafurahi kuzaliwa kwake.

Mtoto huyo ni mtoto wa kiume, ana uweza wa kifalme mabegani mwake, jina lake ni Emmanueli, mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, mfalme wa amani, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Matukio yanayoambatana na ujio wake ni kwamba, wote wanapata Uhuru, kunakuwa ni mwisho wa vita chuki na ugomvi, atasimika Ufalme wa Amani, Upendo na Haki. Kumbe kwa wanaosherehekea kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, chuki, vita mapigano na machukizo kwao ni mwiko, amani upendo na haki ndilo vazi lao. Katika somo la pili Paulo anatuambia kuwa, Neema ya Mungu imefunuliwa katika fumbo la umwilisho yaani Mungu kujifanya mtu. Tuwajibike kumtambulisha Kristo kwa maisha yetu. Utambulisho wetu uwe ni sisi kuwa watu wa amani, upendo, uaminifu, haki na usitawi unaobubujika katika Kristo. Tuwe ni watu wanaojitawala, tukiepuka tamaa za dunia na dhambi. Katika simulizi la kuzaliwa kwake Kristo katika Injili, tunaambiwa kwamba kulikuwa na sensa ya kuhesabu watu, naye Yusufu na Maria mkewe walienda Bethlehemu katika mji wa Daudi wakahesabiwe huko na ndipo Bikira Maria akajifungua mtoto wa kiume katika hori la kulishia ng’ombe kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.

Kristo, Emanueli, Mungu pamoja nasi anazaliwa katika hali ya kibinadamu; amezaliwa kama binadamu wengine katika mazingira ya kawaida na amehesabiwa katika ukoo wa Daudi. Kwa hiyo anaitwa “Mwana wa Daudi” (Lk.18:38), anakuja kuturudishia utu wetu na kutufundisha jinsi ya kuwa watu. Kihistoria Kristo alizaliwa katika utawala wa Mfalme Augustus aliyetawala kuanzia mwaka 44 BC mpaka 14 AD. Katika utawala wake amani ilienea katika uso wa nchi. Kwa hiyo Kristo anazaliwa katika mazingira ambapo kuna amani duniani. Hiyo ilikuwa ni ishara kwamba atakuwa Mfalme wa Amani kama alivyoagua nabii Isaya “naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa Amani” Isa.7:6. Wachungaji wanapewa taarifa: Msiogope, leo katika mji wa Daudi, amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana.” Mantiki ya Mungu ni tofauti kabisa na fikara ya mwanadamu. Habari za uzao wa mfalme huyu hazikutolewa kwa wafalme au wasomi na watu mashuhuri, bali kwa wachungaji walioonekana machoni pa watu kuwa wadhambi, wapagani na wadanganyifu. Mfalme huyu wa ajabu hakuzaliwa, Hekaluni, Ikulu au mahali pazuri, bali horini katika hali ya umaskini na ufukara.

Alizaliwa mfalme asiye na ulinzi, mamlaka na madaraka, jeshi la nguvu, wala fecha, hana marafiki na umaarufu. Ishara wanazopewa wachungaji ni za kawaida kabisa. Mtoto mchanga, aliyevikwa nguo za kitoto, akiwa amelazwa katika hori la kulishia wanyama. Hana mavazi ya hariri au maridadi, ana uso wa kung’ara kama malaika, hana kilemba wala taji la kifalme. Kwa nini habari hizi zapelekwa kwa wachungaji: Hawa ni watu wasio na nafasi katika jamii, wapagani, ambao hawakuruhusiwa kusali Hekaluni, na ushahidi wao haukukubalika mahakamani, watu walioonekana daima kama wezi waongo na matapeli pamoja na watoza ushuru walioonekana wako mbali na wokovu wa Mungu. Wachungaji kupewa taarifa wa kwanza ni ushuhuda kuwa ujio wa Kristo ni kwa ajili yao na wale wote wanaoangukia katika kundi lao yaani wadhambi kama Kristo mwenyewe anavyosema nimekuja kwa ajili ya wadhambi ili wapate kuokoka. Kwa ajili ya hawa Kristo amezaliwa. Hawa ndio waliomngojea masiha, wakampokea, wakafurahi na kumtukuza ili katika Kristo waonje Upendo, furaha, amani na haki. Hawa ndio waliohitaji uponyaji na neno la uzima. Kristo ataambatana nao katika hali zao ili awarudishie hadhi. Kristo atawajalia uhai na uzima. Ataongea lugha yao katika kuwapigania.

Sisi tutambue matendo yanayodhuru uhai na kuyakemea. Tupambane na yote yanayoathiri utu wa mtu kimwili na kiroho. Tutazame kwa makini matendo yote yanayovunja heshima ya mwanadamu hususani, utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu hasa watoto wa kike, ukahaba, hali nyonge za kazi zinazowafanya wafanyakazi watumike kama vyombo vya kuleta faida tu. Haya na mengineyo huchafua ustaarabu wa mwanadamu na ni kinyume na heshima ya Muumba ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anapambana nayo hasa adhabu ya kifo. Kwa kuwa tunaishi nyakati za Kristo, tunapaswa kuishi kwa amani, furaha, haki na upendo kwa watu wote. Wazazi wanawajibike ili mtoto azaliwe, akue na adumu katika familia na sio kumzuia kuzaliwa kwa kumuua kwa kutumia sumu za uzazi wa mpango. Leo tunaalikwa kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Tuanze kuishi maisha ya utakaso. Tutambue utambulisho wetu wa wana na warithi wa uzima pamoja na Kristo unaoanza hapa duniani na ukamilifu wake huko mbinguni. Tukitambua ya kuwa wokovu wetu si kwa mastahili yetu bali ni huruma na upendo wa Mungu tujawe na moyo wa upendo na shukrani kwa kila jambo.

Basi tujiombee sisi wenyewe; tuziombee tawala mbalimbali duniani ziondoe sheria zinazotetea mambo ya giza na kila aina ya uovu. Tuzingatie maadili ya utu na kutetea haki na amani. Tushikilie mafundisho ya Kanisa yatupatie mwelekeo wa Maisha kama anavyotushauri Mtume Paulo akisema, “Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana… Bwana wetu Yesu Kristo awe vazi lenu” Rum.13:12-13. Kwa namna hiyo Krismas itakuwa na maana na tutakuwa na haki ya kuimba Aleluya na huku ndiko kuzaliwa tena kwa Kristo katika maisha yetu.

Noeli: Mkesha

 

23 December 2019, 15:45