Sherehe ya Noeli ya Bwana: Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Emmanuel, Mungu pamoja nasi. Leo ni siku ya furaha tunapoadhimisha kuzaliwa kwake Kristo Mwokozi wetu. Tumepewa mtoto mwanaume na uweza wa Kifalme u mabegani mwake. Tunafurahi kwasababu Mungu amezaliwa duniani akachukua hali yetu ya kibinadamu akawa mtu ili sisi tuwe kama Mungu. Kwa dhambi ya Adamu na Eva, utu wetu uliharibika. Dhambi iliingia duniani ikaleta doa katika utu wetu. Dhambi hii ilitutenga na Mungu. Ndivyo Maandiko Matakatifu yanavyotuambia, “Basi Mwenyezi Mungu akamfukuza Adamu nje ya bustani ya Edeni na kuweka mlizi upande wa mashariki wa bustani ya Edeni na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kulinda njia iendayo kwenye mti wa uzima wa milele” Mwa.3:23-24. Lakini Mungu ni mwenye huruma. Licha ya uasi huo Mungu ameendelea kumwita mwanadamu arudi kwake. Aliwateua Waisraeli ili kuanzia kwao awakusanye watu wa mataifa waliopotea.
Historia nzima ya Waisraeli ilikuwa ni juhudi zake Mungu za kumrudisha binadamu kwake. Walipokosea aliwatumia manabii kuwarejeza kwake. Licha ya juhudi zote hizo binadamu alidumu katika uasi wake. Mwishowe Mungu akaamua kumtuma mwanae wa pekee. Waraka kwa Waebrania unasema, “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana” Heb.1:1-2. Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yetu Mungu ameamua kuja mwenyewe. Ndivyo Yohane anavyotwambia katika Enjili “Hapo mwanzo kulikuwa Neno, naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” Yoh.1:1. Siku za Noeli ni siku za furaha tunapoadhimisha kuzaliwa kwake Kristo Mwokozi wetu. Katika sherehere za Noeli tunaadhimisha Fumbo la Umwilisho yaani Mungu kutwaa mwili. Kwa fumbo hili Mungu anakuwa mtu na anamfanya mtu kuwa kama yeye; ubinadamu na umungu vinakutana; dunia na mbingu zinaungana.
Tunamshukuru Mungu kwa kuthamini hivyo ubinadamu wetu na tumuombe jinsi yeye alivyoshiriki ubinadamu wetu atusaidie na sisi tushiriki Umungu wake. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatualika tupige kelele za furaha, tuimbe pamoja kwani Bwana anakuja kutufariji, Bwana anakuja kutukomboa, anatuletea wokovu. Furaha yetu itakuwa na tija pale ambapo tutatimiza yale anayoagiza kupitia amri zake. Somo la pili, la Waraka kwa Waebrania linafafanua umwilisho wa Kristo. Neno wa Mungu kutwaa mwili, na jinsi ambavyo Mungu alivyojishusha na kuja kutwaa mwili na kukaa kwetu na kutufundisha yote yale ambayo yanapaswa kufanywa kwa ajili ya kujenga uhusiano mzuri na Mungu wetu ambaye tunamwita BABA. Yeye anakuja kutufundisha njia ya kufika kwa Baba kupitia kwake. Katika Injili mtume Yohane anaelezea asili ya Yesu kuwa ni Mungu mwenyewe, naye ni Mungu kwa asili. Kuwa ndiye aliyekuja kulishinda giza na kutujalia nuru, kutufanya sisi tuweze kuona Mwanga wa Mungu na kuufuata kikamilifu. Yohane anashuhudia kuwa neema zilikuja kwa mkono wa Kristo, naye ndiye aliyemfunua Mungu kwetu.
Yesu amekuja ili tusamehewe dhambi zetu. Amekuja ili kutufuta machozi yetu. Amekuja ili kutusafisha mioyo yetu, kutununua toka utumwa wa shetani kwa gharama ya uhai wake. “Mganga hamtafuti mtu mzima, bali mgonjwa” Kwa hiyo: Mpe moyo wako uliojaa tamaa za makuu kuzidi kiasi ili abomoe majivuno yako. Mpe moyo wako uliojaa tamaa za mali kuzidi kiasi ili amfukuze shetani huyo pamoja na madanganyo ya mali zake. Mpe moyo wako uliojaa tamaa za mwili kuzidi kiasi ili ausafishe na ayafukie mabonde ya matope ya tamaa za mwili wako. Haya yanawezekana tukiwa na moyo wa sala kwani sala ndio mfereji wa neema, neema ndizo ziletazo nguvu za kukwepa mabaya na kutenda mema. Tumwombe Mtoto Yesu aliyezaliwa ambaye ni mfalme wa haki na amani, Mshauri wa ajabu atuletee amani mioyoni mwetu na katika jumuiya zetu na jamii kwa ujumla, ili kazi aliyokuja kuifanya hapa duniani ionekane kwa ulimwengu mzima.
Kuzaliwa kwake Kristo sio tu tukio la kihistoria, bali tukio halisi katika maisha yetu. Kristo yupo nasi katika maisha yetu: Yesu amekuja kujiunga nasi katika magumu ya maisha na katika udhaifu wetu. Yesu ni Emanueli “Mungu pamoja nasi, kwa hiyo, hatuko peke yetu katika maisha na mahangaiko yetu. Tunachotakiwa kufanya, ni kumpokea, kwa kubali mwenendo wa maisha anaotufundisha, tumkabidhi maisha yetu, shughuli zetu, mahangaiko yetu, magonjwa yetu. Kristo yupo nasi katika njia hii ya maisha ili ahakikishe anatufikisha huko alikotoka yeye yaani kwa Baba Mbinguni. Tuanze upya katika maisha yetu, kama tulikuwa na mahusianao mabaya, hatuelewani, tuanze upya. Kama tulikuwa na tabia mbaya, tuanze upya. Krismasi ni mwanzo mpya. Tuthamini utu wetu na miili yetu: Kama Mungu amethamini utu wetu na kutwaa mwili kama sisi lazima sisi pia tujithamini na tuuthamini ubinadamu wetu na kuiheshimu miili yetu.
Tusiudhalilishe ubinadamu wetu au kuwadhalilisha wengine. Mtu ana thamani, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na Mungu amejiunga naye katika ubinadamu wake. Kwa hiyo, tuondoe yale yote yanayodhalilisha utu wa. Tuthamini miili yetu kwa kuitunza vizuri kwa heshima, tuvae vizuri, tusiiharibu kwa dawa au pombe. Tukubali kuacha: Jambo lililoharibu uhusiano wetu na Mungu ni dhambi ya asili ambayo kwayo wazee wetu walikataa kuwa wao ni binadamu wakataka kubaki hapa duniani kula tunda la dunia kufurahia mambo ya ulimwengu. “Mwanamke akaona huo mti kuwa ni mzuri kwa chakula na unapendeza kwa macho” (Mwa.3:6). Kristo amekuja ili kutufundisha kuwa tunsing’ang’anie ya ulimwengu hata tukapoteza uzima wa milele. Kwa asili sisi ni binadamu, tusione kuwa kule kuwa mwanadamu ni kitu cha kushimamana nacho kwa nguvu bali tuachilie hayo yote tujichukulie hali ya kimungu na tuonekane kama watoto wa Mungu.