Mwanga na Nyota ni alama ambazo uyahudini zilihusishwa na ujio wa masiha!
Na Padre William Bahitwa - Vatican
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari masomo ya sherehe ya Epifania, sherehe ya Tokeo la Bwana. Tunaadhimisha tendo la Yesu kujifunua kwa mataifa kama mwanga na mkombozi. Somo la kwanza (Isa 60, 1-6) ni kutoka kitabu cha nabii Isaya. kwa uvuvio wa Mwenyezi Mungu, manabii walitoa daima unabii uliogusa moja kwa moja matukio na maisha ya watu. Lakini mara nyingi pia manabii walitoa unabii unaovuka yale mambo ya kawaida yanayoonekana, yale ambayo watu walikuwa wakikutana nayo moja kwa moja katika maisha yao. katika somo hili la leo, Nabii Isaya anatoa unabii wa namna hiyo.
Anauona mji wa Yerusalemu ukiwa umeangazwa kwa mwanga na mji wenyewe ukingàa na kuyaangaza mataifa yote kwa mwanga wake. Anawaona wana wa Yerusalemu waliokuwa wametawanyika na wameenda mbali sasa wanaurudia mji wao na sio hao tu, hata wana wa mataifa nao wanaujia mji wa Yerusalemu na wanaujaza kwa zawadi mbalimbali. Hapo anauambia mji wa Yerusalemu inuka sasa na uangaze pande zote, wote wanakusanyana wanakujia wewe. Mwanga ni alama ya utukufu. Nabii anaona katika Yerusalemu mahala ambapo patakuwa kitovu cha utukufu utakaowakusanya mataifa na hapo hapo utakaowaangazia mataifa. Anatabiri juu ya Epifania ya kweli ambapo katika mji huo, Mungu mwenyewe atajifunua katika utukufu wake; ndiye atakayekuwa mwanga halisi wa kuwaangazia mataifa na kuwaunganisha watu wa mataifa yote katika mpango wake wa ukombozi aliouanza na taifa la Israeli na kwa jinsi hii atayaangazia kwa mwanga halisi unaotokea Yerusalemu yaani Yesu Kristo Bwana wetu.
Somo la pili (Waef 3, 2-3. 5-6) ni kutoka katika waraka wa mtume Paulo kwa Waefeso. Ni somo linalotangaza ukombozi kwa wote. Mtume Paulo anawafunulia waefeso fumbo la Kristo ambalo anaeleza kuwa lilikuwa limefichwa tangu enzi lakini sasa Mungu mwenyewe amelifunua kwa njia ya Kristo kwa mitume wake na manabii wake. Paulo anaeleza kuwa katika mpango huo wa Mungu wa ukombozi, mataifa, yaani wote wasio wayahudi, walionekana wamewekwa kando, na Mungu alionekana kujihusisha tu na taifa la Israeli pekee. Lakini Mungu mwenyewe alikusudia awakusanye mataifa yote utakapofika utimilifu wa nyakati. Na sasa kwa njia ya Kristo, wote ni warithi na washiriki wa ahadi zile zile za ukombozi Mungu alizowaahidia taifa lake teule.
Injili (Mt 2, 1-12) Somo la Injili ni katika Injili ya Mathayo. Ni somo linaloeleza tukio lenyewe la Yesu kujifunua kwa mataifa. Kuzaliwa kwake kunaambatana na alama ya nyota isiyokuwa ya kawaida. Nyota hiyo inawaamsha mamajusi kutoka nchi za mbali, na kadiri ya elimu yao ya mambo ya anga, ni nyota inayoashiria kuwa kuna mfalme mkuu amezaliwa Bethlehemu. Nao wanafunga safari wanaenda kumsujudia. Ufalme huu wa Yesu au hasa upekee wa mtoto aliyezaliwa unatambuliwa na mamajusi kutoka mbali lakini wenyeji hawautambui. Wao wanafika na kumtolea mtoto Yesu zawadi za dhahabu, uvumba na manemane huku Herode anapanga mipango ya kumuangamiza.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Epifania ni sherehe iliyongana kwa karibu kabisa na Noeli. Inaendeleza furaha ya kuzaliwa Yesu na inazidi kulifafanua fumbo lenyewe la kuzaliwa Yesu. Siku ya Noeli tulisherehekea fumbo la Mwana wa Mungu kutwaa mwili na kuja kukaa kwetu katika hali yetu duni ya kibinadamu. Akawa kweli Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi. Sherehe hii ya Epifania inamtambulisha sasa huyu Yesu aliyezaliwa. Inatufafanulia kuwa huyu aliyeshuka akazaliwa na kukaa kwetu katika uduni wa ubinadamu wetu ana hadhi ya kifalme, hadhi ya umungu na ndiye mkombozi wetu. Hadhi hizi zinafunuliwa na zawadi alizopewa: zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.
Neno lenyewe Epifania kama lilivyotumika tangu hata kuzaliwa kwa Yesu lilimaanisha ziara rasmi ambayo mfalme au kiongozi aliifanya alipoenda kujitambulisha na kutembelea maeneo yaliyo chini ya himaya yake. Katika ukristo, Epifania imechukua maana hii hii na kuonesha kuwa ni “tokeo la Bwana” yaani Kristo anajitokeza na kujitambulisha kuwa ndiye Bwana.Masomo ya leo yanatumia alama nne katika kumtambulisha Yesu. Alama ya kwanza tumekwishaiona, nayo ni ya zawadi za dhahabu, uvumba na manemane zinazomtambulisha Kristo mfalme, kuhani (hadhi ya kimungu) na mkombozi (anayeukomboa ulimwengu kwa kifo chake msalabani). Alama nyingine ni mwanga, nyota na mamajusi.
Mwanga na Nyota ni alama ambazo katika uyahudi zilihusishwa na ujio wa masiha. Isaya ni nabii ambaye kwa namna ya pekee amehusianisha ukombozi wa kimasiha na mwanga. Katika Isa 9:1 anasema “watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; na wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti nuru imewaangazia”. Katika somo la leo inarudi tena alama ya mwanga “ondoka uangaze kwa kuwa nuru yako imekuja na utukufu wa Bwana umekuzukia” (Isa 60:1). Nyota hali kadhalika inamtambulisha masiha. Katika ufunuo Kristo ndiye “nyota ya asubuhi” (Ufu 2:28, 22:16). Alama hizi ambazo zilitumika kumtazamia masiha, leo zinaletwa pamoja zikimuelekea Yesu kuonesha kuwa yale yaliyotabiriwa na kuashiriwa kwa alama hizo sasa yametimia katika Kristo.
Mamajusi, kimapokeo, wanatajwa kuwa walikuwa watatu na majina yao yakiwa Gaspari, Melkiori na Baltazari. Hawa waliongozwa kutoka mashariki kuja kumsujudu mfalme aliyezaliwa. Mamajusi hawa wanawakilisha mataifa yote yasiyo wayahudi na kitendo chao cha kutoka mbali katika nchi zao kuja kumsujudia mtoto Yesu kinamtambulisha Yesu kama masiha wa mataifa yote. Yeye ni masiha wa ulimwengu mzima na ndiye anayewaita watu wote waupate wokovu kwa njia yake. Katika mamajusi hawa nasi tunajiona. Tunasema pamoja nao “tumeona nyota yake mashariki nasi tumekuja kumwabudu Bwana na zawadi zetu”. Adhimisho hili la Epifania liendeleze kwetu sote furaha ya kuzaliwa Bwana na kuzidi kuamsha ndani yetu kiu ya kumpokea kama masiha na mkombozi wetu.