Tuwe mwanga na chumvi:bila imani ni vigumu mtu kupambanua yampendezayo Mungu!
Na Padre William Bahitwa – Vatican
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tafakari ya leo ni kutoka masomo ya dominika ya 5 ya mwaka A. Somo la kwanza (Isa 58:7-10) ni kutoka kitabu cha nabii Isaya. Mazingira ya somo hili ni kipindi ambacho waisraeli wametoka utumwani, wamejitambua kama taifa lililo chini ya mkono wa Mwenyezi Mungu na hivi wameanza kushika dini kwa nguvu ikiwa ni pamoja na kufutata taratibu za ibada na uchaji kama ilivyoamuru Torati. Pamoja na kushika hayo yote, waisraeli bado wanajiona wako mbali na Mungu. Hawaioni neema ya Mungu katika maisha yao na hawamsikii Mungu akiitika wanapomuita. Katika aya ya tatu ya sura hii hii wanasikika kusema “mbona tumefunga lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu lakini huangalii? Wanashindwa kujua tatizo liko wapi.
Katika mazingira haya, Mungu anawajibu kwa kinywa cha nabii Isaya na anawaambia kuwa kushika dini, kufunga na kufuata taratibu zingine za uchaji kama wanavyofanya kunapaswa kuendana na kipengele kingine muhimu ambacho wao wamekuwa wanakipuuzia. Na kipengele hicho ni kuwajali wahitaji na kusikiliza kilio cha wanyonge na kuwasaidia. Nabii anataja mifano ya matendo waliyoyapuuzia huku wakijiona wanashika dini. Anataja kuwapa wenye njaa chakula, kuwakaribisha wageni, kuwavika wasio na nguo na kutowakana ndugu. Na anasema anayeshika dini huku akiyafanya haya, nuru yake itapambazuka kama asubuhi na atakapoita Bwana ataitika na kusema “mimi hapa”. Hili ni somo linalotukumbusha kuwa imani tunayoikiri ni lazima tuiweke katika matendo ya maisha yetu ya kila siku.
Somo la pili (1Kor 2:1-5) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa wakorinto. Mtume Paulo baada ya kuhubiri kwa wakorinto na kuondoka, walifika wahubiri wengine na mafundisho tofauti na yale ya Paulo. Zaidi ya hilo, wahubiri hawa walikuwa ni mafundi wa kuongea katika hadhara na walikuwa na ujuzi wa falsafa. Na kwa falsafa yao walitaka wakorinto wampuuzie Paulo na injili aliyokuja kuwahubiria. Katika somo hili la leo Paulo anawaandikia wakorinto kuhusu suala hili. Paulo hahangaiki kujifananisha na wajuzi hao bali anasisitiza kwa wakorinto kuwa alikuja kuwahubiria mafumbo ya Mungu kwa unyenyekevu wote, sio kwa ujuzi wa maneno wala hekima ili watakachobaki nacho kisiwe hiyo hekima yake wala utaalamu wake bali wabaki na ujumbe wenyewe wa Mungu. Katika somo hili Paulo anatukumbusha kuwa kazi ya mtumishi wa Mungu ni kujishusha ili kazi ya Mungu ionekane. Kadiri mtumishi wa Mungu anavyojishusha ndivyo ukuu wa kazi ya Mungu unavyozidi kuonekana lakini pia kadiri mtumishi wa Mungu anavyojikuza mwenyewe vivyo hivyo ndivyo anavyouficha ukuu wa kazi ya Mungu.
Injili (Mt. 5:13-16) ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Ni mafundisho kuhusu chumvi ma mwanga ambayo Yesu anawapa wanafunzi wake baada ya kuwafundisha Heri nane. Anapowaambia ninyi ni chumvi ya dunia, anawaalika ili kama chumvi inavyoleta ladha katika chakula, wao nao waipe ladha dunia kwa imani yao. Jambo jingine ni kwamba uzoefu wao pamoja na mafundisho y arabi wao viliwasadikisha kuwa chumvi haiwezi kamwe kupoteza ladha. Yesu anawapa kitu kipya anapowaambia kuwa chumvi inaweza kupoteza ladha. Na mwisho wa chumvi iliyopoteza ladha ni kutupwa na kukanyagwa na watu njiani. Yesu pia anawafundisha kuwa wao ni nuru ya ulimwengu. Kazi ya nuru ni kuangaza na kuvutia. Hapa anawaalika kuuangaza ulimwengu kwa matendo yao mema na kwa jinsi hiyo kuushawishi ulimwengu kugeuza mwenendo kwa kuuelekea mwanga wao wa matendo yao mema. Mafundisho haya ya Yesu yanayofuata baada ya fundisho la Heri nane, ni kuwaalika wafuasi kuviweka katika matendo vigezo vya kiimani na kimaadili kama vinavyofundishwa na Heri nane.
Tafakari
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya leo yanatupatia changamoto ya kuhusisha imani yetu ya kikristo na maisha yetu ya kawaida ya kila siku. Imani na matendo ni vitu vinavyotegemeana na kukamilishana. Mtume Yakobo katika waraka kwa watu wote alihoji “yafaa nini mtu akisema ya kwamba anayo imani lakini hana matendo? Je imani ya namna hii yaweza kumwokoa? Na akahitimisha kuwa imani ni kitu kisichoonekana waziwazi, huonekana kwa njia ya matendo ya mtu. Mafundisho haya yametufikia katika wakati wetu huu ambapo ni rahisi kuona mpasuko unaotofautisha kile tunachoweza kukiita ukristo na maisha ya kawaida. Ipo jitihada kubwa ya kumtafuta Mungu, ipo bidii ya kushiriki kwa moyo ibada, mazoezi ya kiroho na matakwa mengine ya uchaji wa Mungu lakini wakati huo huo kinachoonekana katika jamii ni kushamiri kwa matendo yanayopingana na bidii ya kiimani tuliyonayo. Masomo ya leo yanatualika turudi katika nafsi zetu na imani tunayoikiri tuibebe na ituongoze hata katika maeneo mengine ya maisha yetu: katika biashara, katika utumishi wa umma, katika siasa na nafasi nyingine zozote Mungu anazotujalia. Huku ndiko kuwa chumvi na nuru. Na hii ndiyo, kadiri ya nabii Isaya, dini inayompendeza Mungu. Yaani dini isiyokomea kutangaza ukuu wa Mungu madhabahuni ilhali ikifumbia macho upotevu mahangaiko ya kila siku ya watu wa Mungu.
Katika tafakari hii, wapo waliokwenda mbali zaidi hata wakaipuuzia imani na kushika dini. Hawa husema hakuna haja ya kwenda kanisani wala kuwa mwamini, inatosha tu kuishi vizuri na watu na kuwatendea mema. Huku nako ni kujidanganya na kutafuta kuficha ukana dini katika kichaka cha kuwa mwema kwa watu. Bila dini na bila imani kuna hatari ya mtu kujigeuza yeye kuwa mungu. Badala ya kumuona Mungu kuwa ndio kipimo cha kuamua lipi ni jema na lipi ni baya, mtu ndio anakuwa kipimo hicho na hapo hapo akijitangaza kuwa hamuhitaji Mungu katika maisha yake. Imani na matendo ni kama pande mbili za sarafu moja. Bila imani hawezi mtu kuyapambanua yanayompendeza Mungu na watu na bila matendo imani ya mtu haiwezi kudhihirika na imani hiyo haiwezi kumuokoa mtu. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuishika imani kwake na atupe ujasiri wa kuiishi imani hiyo katika maisha yetu ya kila siku.