Tumefanywa kuwa chumvi na mwanga wa dunia katika Sakramenti ya Ubatizo!
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 5 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa leo ni kwamba sisi kwa sakramenti ya ubatizo, tumefanywa kuwa chumvi na mwanga wa ulimwengu.
Katika somo la kwanza Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya anawaonya Wayahudi waliorudi toka utumwani Babeli, kwamba kufunga na kusali kwao ni kazi bure kama hawatendi haki kwa ndugu zao, kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako. Kumvika nguo mtu aliye uchi kunatupatia nuru itakayopambazuka kama asubuhi kuwa na afya njema kwani utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukikulinda kwani utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Hata kwetu sisi, mahusiano mema na wenzetu ndiyo hasa yanayodhihirisha kuwa Kristo yu kati yetu. Kusali sala ndefu na kufunga kwa mda mrefu hakutufai chochote kama hatuwajali wenzetu.
Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho, anatukumbusha kuwa msalaba wa Yesu Kristo ndio kiini cha habari njema. Pia Mungu anachagua viumbe dhaifu kwa kuhubiri neno lake ili kuonyesha kwamba nguvu ya Injili si katika ufasaha wa maneno au hekima ya mhubiri bali katika nguvu ya Mungu anayefungua mioyo ya watu ili wasadiki. Paulo anasema, nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima zangu, neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa nguvu ya Roho wa Mungu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
Katika somo la Injili ilivyoandikwa na Mathayo, Yesu anatufundisha kuwa kama ilivyo kazi ya chumvi kukoleza na kuongeza ladha ya chakula na kazi ya mwanga kuangaza gizani, ndiyo inavyotupasa wakristo kuishi hapa duniani. Matendo yetu mema yakoleze na kuangaza wengine ili wafuate mfano wetu na kumtukuza Mungu. Tusipotimiza huu wajibu mwisho wetu ni kutupwa kwenye moto wa milele.
Chumvi ni kikolezo cha chakula na ni dawa. Mwandamu anatumia chumvi apate kuweka ladha katika chakula, anaitumia chumvi kutunza na kuhifadhi chakula kisioze, pia anatumia chumvi kama dawa. Chumvi ni alama ya hekima na busara itokayo kwa wazee ndiyo maana tunasema mtu amekula chumvi nyingi maana yake ameishi miaka mingi. Mwanga hutumika kuondoa giza ili watu wapate kuona au kitu chochote kipate kuonekana. Kwa ubatizo, mkristo anafanywa kuwa mwanga apate kuwamulikia wengine wamfikie kristo.
Katika Biblia giza au usingizi ni hali ya kuwa na dhambi ni hali ya kukosa uwepo wa Mungu ni hali ya kutokuwepo na neema ya Utakaso. Mwanga ni ishara ya uwepo wa Mungu, ni ishara ya Neema ni ishara ya uwepo wa neema ya utakaso. Mwanga huu unaweza kuelezwa kuwa ni Neno la Mungu kama Mzaburi anavyosema “Neno lako ni taa ya kuniongoza na mwanga katika njia yangu” Zab. 119:105. Hivyo, mtu anapojua neno la Mungu na amri zake anakuwa na mwanga na anaweza kufuata njia nzuri ya kuishi. Yeyote yule anayewajulisha watu neno la Mungu na Amri zake anaeleweka kuwa analeta mwanga kwa watu. Watu wamuone Mungu na waone njia ya kuweza kumfikia. Anawatoa watu gizani.
Hivyo, basi kuwa mwanga ni kuishi maisha ya mfano. Ili watu wayaone matendo yetu wamtukuze Mungu. Kwa matendo yetu watu waone wanavyopaswa kuishi. Kila mmoja katika ngazi yake anapaswa kuhakikisha kuwa anakuwa mfano wa kuigwa na wengine. Iwe katika masuala ya kiroho au hata katika mambo ya kawaida ya maisha. Kila mara ujihisi kuwa na wajibu na kujiuliza “je, wengine watajifunza nini kwangu?” Hili si jambo rahisi. Linahitaji kujisadaka, kwa sababu utatakiwa kuacha baadhi ya mambo ambayo ni halali kwako ili usiwakwaze wengine unaamua kuyaacha kwa sababu ya hadhi uliyonayo. Basi tumuombe Mungu atujalie ujasiri na moyo wa kujisadaka ili tuweze kuwa kweli nuru, mwanga na chumvi kwa mataifa.