Tafakari Jumapili 7 ya Mwaka A wa Kanisa: Sheria! Upendo! Utakatifu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Tafakari ya leo ni kutoka masomo ya dominika ya 7 ya mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza (Law. 19:1-2,17-18 ni kutoka kitabu cha Mambo ya Walawi. Hiki ni mojawapo ya vile vitabu vitano vya mwanzo vya Biblia ambavyo pia vinajulikana kama vitabu vya Musa. Kitabu cha Mambo ya Walawi ni kitabu cha sheria na tamaduni za wayahudi. Chimbuko la sheria na tamaduni hizi ni Amri 10 za Mungu. Kutoka katika Amri 10 za Mungu, sheria hizi ziliweka miongozo mbalimbali kuhusu mahusiano kati yao, mahusiano na wageni, kanuni za usafi na unajisi na mambo mengine mengi yaliyohusu ibada na mahusiano yao na Mungu. Sheria hizi walikabidhiwa Walawi ambao ndio walikuwa makuhani. Hawa ndio walikuwa watekelezaji na waangalizi wake wakubwa. Ni kwa sababu hii kwa mfano katika injili ya Luka, Yesu alipokuwa anawaponya wale wakoma kumi aliwaambia waende wakajioneshe kwa Makuhani ambao walikuwa ni Walawi ili wathibitishe kupona kwao kama sheria ilivyoamuru.
Somo la leo linaeleza sasa ni nini kilicho kiini cha sheria hizi na tamaduni ambazo Wayahudi walipaswa kuzifuata. Kiini hicho ni kulifanya taifa zima la Mungu kuwa takatifu; “Mungu akamwambia Musa.. waambie, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi Bwana Mungu wenu, ni Mtakatifu”. Na pamoja na kuwa Mungu amewapa sharia nyingi namna hii, somo la leo linaonesha kuwa njia ya kuufikia huo utakatifu ni njia ya upendo; upendo unaojionesha katika kutunza mahusiano mazuri kati ya ndugu. Hapo somo linasisitiza usimchukie ndugu yako moyoni, usifanye kisasi wala kuwa na kinyongo, panapokuwa na kosa ni lazima kumkemea lakini usichukue dhambi kwa ajili yake – yaani badala ya kurekebisha kosa lake, unajikuta unaongeza mnyororo wa makosa kwa wewe nawe kuongeza kosa lingine. Linahitimisha kwa mwaliko wa upendo: umpende jirani yako kama nafsi yako.
Somo la pili (1Kor 3:16-23) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorinto. Katika somo hili, Paulo anaendelea kukemea mgawanyiko ulolikumba kanisa la Korintho. Ni mgawanyiko uliosababishwa na wahubiri walioleta mafundisho potofu, kinyume na mafundisho ya kweli. Leo Paulo anatoa fundisho zito juu ya waamini na Kanisa. Anasema waamini ndio Hekalu la Mungu na Roho wa Mungu, Roho Mtakatifu anakaa ndani yao. Na yeyote anaekuja kuwatawanya au kuwagawanya kimafundisho analiharibu Hekalu hilo na Mungu atamharibu mtu huyo. Ndivyo Paulo anavyowaonya wale wanaotumia ujanja ujanja wanaouita hekima akisema hekima ya dunia hii ni upumbavu mbele ya Mungu. Mtume Paulo anaonesha leo umuhimu wa kulinda umoja kati ya waamini na anaonesha thamani kubwa na nafasi ya mkristo katika Kanisa.
Injili (Mt. 5:38-48) ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Katika injili hii Yesu anaurudia kwa namna ya pekee mwaliko wa kuwa watakatifu. Mwaliko huu ambao ndio ulikuwa kilele cha sheria ya Musa kama kinavyoonesha kitabu cha Mambo ya Walawi, Yesu anautoa kama matokeo ya kuuishi upendo katika ukamilifu wake. Ukamilifu huu wa upendo Yesu anauonesha njia mbili katika injili ya leo: njia ya kwanza ni njia ya msamaha na ya pili ni njia ya kumpenda adui. Yesu anafundisha msamaha pale anaposema “akupigaye shavu la kuume mgeuzie na la pili, anayetaka kuitwaa kanzu yako mpe na joho pia na anayekulazimisha mwendo wa maili moja nenda naye mbili”. Msamaha anaofundisha Yesu leo ni msamaha wa kutokulipiza kisasi kwa ovu mtu alilotendewa. Kwa vyovyote vile hatuwezi kuchukua tafsiri sisisi kwa mfano katika “akupigaye shavu la kuume mgeuzie na la pili”, ila fundisho linabaki lile lile, kutokujenga moyo wa kulipiza kisasi. Katika kumpenda adui, Yesu anafundisha kuwa matendo mema tunayoalikwa kuyafanya yasiwe ndani yake na ubaguzi, yasiwaelekee wale tu walio upande wangu wa kimawazo, kiitikadi au vinginevyo na kuwaacha kando nisioshibana nao au ninaotofautiana nao kimawazo, kiitikadi au vinginevyo. Wema wa namna hiyo sio wema na haumpi utakatifu yeye anayeuendeleza. Wema mkamilifu ni wema ulio na upendo usio na mipaka.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza masomo ya dominika hii pamoja na ufafanuzi wake, ninawaalika sasa tuingie katika tafakari yake fupi. Tafakari ya leo itaongozwa na somo la Injili. Katika Injili, Yesu ameanza kwa kunukuu sheria ya kimapokeo ya wayahudi iliyojulikana kama sheria ya “Jicho kwa jicho na ya jino kwa jino”. Sheria ni kweli ilikuwepo. Mapokeo yanaonesha kuwa iliwekwa na Musa ili walau kupunguza uovu mkubwa uliofanywa kwa kisingizio cha sheria ya kulipizia kosa. Sura ya 4 ya kitabu cha Mwanzo inaonesha kiwango cha juu kabisa cha uovu huu. Hapo tunamwona Lameki akisema “nimemuua mtu kwa kunitia jeraha, nimemuua kijana kwa kunichubua” (Mwa. 4:23). Kwa kosa dogo kama kumchubua mtu, chini ya sheria ya kulipizia kosa mtu aliweza kufanya chochote hata kumuua aliyemchubua kama alivyofanya Lameki.
Katika mazingira hayo, Musa akaweka sheria ya kisasi. Sheria hii ilipunguza uovu kwa kuweka kiwango cha kulipizia kosa ili kama mtu amekuchubua unachoweza kufanya na wewe ni kumchubua, usimpe jeraha kubwa kuliko alilokufanyia. Kama mtu amekutoa jino moja, unachoweza kufanya na wewe ni kumtoa jino moja, sio kumi. Ndio maana sheria hii ikaitwa jino kwa jino. Na wayahudi wameitumia kwa muda mrefu. Yesu leo anachofundisha ni kuwa lengo la sheria hiyo ya Musa halikuwa kulipiza kisasi bali ilikuwa ni kupunguza uovu. Sasa uovu hauwezi kuupunguza kwa kuendeleza kisasi. Kutoka katika sheria ya Lameki ya kulipiza kosa, kwenda kwa sheria ya Musa ya kisasi, leo Yesu anafika katika ukamilifu. Anaondoa sheria ya kisasi na anausimika upendo. Ni upendo ulio na nguvu ya kupunguza kosa na kuliondoa kabisa na tena upendo huu humfanya anayeutenda kuwa mtakafitu kama Baba wa Mbinguni alivyo Mtakatifu.
Njia hii ya ukamilifu anayotufundisha leo Yesu, iliyo njia ya msamaha na ya upendo, sio njia rahisi hata kidogo. Katika baadhi ya hali na mambo tunayopitia, kibinadamu tunauona ugumu waziwazi lakini yafaa kujiuliza; nitabaki katika hali hii ya kutosamehe hadi lini? Na ni lini nitaacha kutojiangalia mwenyewe nianze kupiga hatua ya kwanza kuelekea kuuiga upendo huu wa Kristo. Yeye mwenyewe anaujua fika ugumu huu lakini bado ameweka njia hii ya Msamaha na upendo kuwa ndio njia ya kuufikia utakatifu. Tumwombe Neema na ujasiri wa kujiachilia katika mwaliko wake.