Tafuta

Mwandishi wa Kitabu cha Yoshua Bini Sira anawawakumbusha kuwa tangu mwanzo Mungu ameweka mbele yao njia mbili:njia ya uzima na ya mauti;ndiyo njia ya maji na moto au ya amri zake na ya utashi wa mwanadamu. Mwandishi wa Kitabu cha Yoshua Bini Sira anawawakumbusha kuwa tangu mwanzo Mungu ameweka mbele yao njia mbili:njia ya uzima na ya mauti;ndiyo njia ya maji na moto au ya amri zake na ya utashi wa mwanadamu. 

Tufuate hekima ya kimungu ili tuukamilishe ufahamu wa kibinadamu

Tusiridhike au kubaki katika ufahamu wa kidunia:si mambo yote yanayoweza kujibiwa na teknolojia,si mambo yote yanayoweza kuamuliwa na siasa,si mambo yote ambayo utendaji wake unapaswa kuangalia uchumi pekee. Mwono wa kiimani na utashi wa kuifuata hekima ya kimungu ni ya msingi katika kuukamilisha ufahamu wa kibinadamu na kumsaidia kuishi kama anavyokusudia Mungu muumba wake.

Na Padre William Bahitwa – Vatican

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu.  Tafakari ya leo ni kutoka masomo ya dominika ya 6 ya mwaka A.

Somo la kwanza (YBS 15:15-20 ni kutoka kitabu cha Yoshua bin Sira. Hiki ni mojawapo ya vitabu saba katika Agano la Kale, vinavyoitwa vitabu vya Hekima. Katika ujumla wake, ni vitabu vinavyobeba mapokeo ya muda mrefu ya waisraeli juu ya namna walivyoyakabili maisha. Ndani ya mapokeo haya ulikuwemo ufunuo wa Mwenyezi Mungu. Na hiki ndicho kilichotofautisha hekima kwa waisraeli na hekima kama mataifa mengine walivyoitambua na kuiishi. Kitabu hiki cha Yoshua bin Sira kimeandikwa baada ya kuwa umepita muda mrefu sana kati ya vizazi vya kwanza kwanza vya waisraeli hadi wakati huo. Tena kimeandikwa kipindi ambacho waisraeli walikuwa chini ya utawala wa Wayunani.  Mambo mengi yalikuwa yamekwishabadilika na tena utawala wa wayunani ulikuwa ni mwiba kwa tamaduni za kiyahudi kwa sababu uliwataka wazisahau zote na waanze kuishi kwa kufuata tamaduni za kiyunani.

Kwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu, mwandishi wa kitabu hiki anaandika kuwakumbusha waisraeli juu ya mapokeo ya hekima ya mababu zao. Anawakumbusha kuwa tangu mwanzo Mungu ameweka mbele yao njia mbili: njia ya uzima na ya mauti; ndiyo njia ya maji na moto au ya amri zake na ya utashi wa mwanadamu. Njia hizi ni mwaliko kwa mwanadamu kutumia dhamiri yake na kuchagua mema na yafaayo. Kwa maneno haya anawakumbusha kuwa tangu mwanzo Mungu hajayaweka maisha ya mwanadamu yaende kama maji yanayofuata mkondo yaliyopangiwa. Amemweka mwanadamu katika ulimwengu ulio na “mikondo” mingi ili mwanadamu atumie utashi wake kuyachagua mema na kuyafuta. Na hii ndiyo hekima ya kimungu.

Somo la pili (1Kor 2:6-10) ni kutoka katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorinto. Paulo anaonekana kuandika sehemu hii akiwa kichwani na mafundisho ya Yoshua bin Sira kama tulivyoyaona katika somo la kwanza. Kama alivyofundisha Yoshua bin Sira, Paulo anawaandikia wakorinto kuwaonehs kuwa hapa duniani ipo hekima ya kidunia na ipo pia hekima ya kimungu. Anaendelea kusema kuwa mfano wa hekima ya kidunia ni ya watawala batili wa dunia hii. Anawaita batili kwa sababu kwa kufuata hekima yao walishindwa kumtambua Kristo wakamsulibisha. Kwa bahati mbaya hekima hii ya kidunia bado inazidi kupata wafuasi na inaendelea.

Paulo lakini anaonesha kuwa ipo hekima ya kimungu. Hekima hii ilikuwa katika siri, ilikuwa imefichwa ili mwanadamu aitafute kwa kutumia utashi wake aliyopewa; kwa kuisikiliza dhamiri. Hata hivyo Mungu mwenyewe ameamua kuifunua hekima yake hii kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hivyo Paulo anaongeza katika mafundisho ya Yoshua bin Sira nafasi ya Roho Mtakatifu katika katika kuitambua hekima ya kimungu maishani. Mbele ya njia mbili, njia ya uzima na ya mauti; njia ya maji na moto; njia ya mema na mabaya, ni muhimu kuomba msaada wa Roho Mtakatifu ili kung’amua vema.

Injili (Mt. 5:17-37) ni kutoka kwa mwinjili Mathayo. Ni sehemu ya hotuba ndefu ambayo Yesu anaitoa kwa wanafunzi wake akiwa ameketi mlimani. Katika injili ya Mathayo huitwa “hotuba ya mlimani”. Katika somo hili la leo, Yesu anawaonesha wanafunzi wake uhusiano uliopo kati ya mafundisho ambayo amekuwa anawapa na Torati ambayo kwa miaka mingi imeongoza maisha yao. Anasema “msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au Manabii; sikuja kuitangua bali kuitimiliza”.  Analenga kuwaonesha kuwa mafundisho anayowapa, pamoja na upya wake wote, hayapingani hata kidogo na ufunuo wa Mwenyezi Mungu uliomo katika Torati. Bila kuipinga Torati, mafundisho ya Yesu yanaikamilisha, yaani yanaisisitiza na kuipa nguvu zaidi.

Torati ni nini? Torati ni sheria na kanuni ambazo Mungu aliwapa waisraeli wazishike ili waendelee kuwa katika Agano aliloweka nao mlimani Sinai.  Kumbe chimbuko la Torati ni Agano. Lakini Agano hili kiini chake ni wema na upendo wa Mungu kwa watu wake. Kwa jinsi hii Torati haipaswi kupingana na tunu za wema na upendo wa Mungu kwa watu wake. Mbeleni katika injili hii Yesu anawaonesha ni nini kilicho kiini cha Torati katika masuala halisi yahusuyo kulinda uhai, uaminifu katika ndoa, talaka na viapo.  Na hapo Yesu anaonesha kuwa kipimo cha hayo yote kinaanzia moyoni mwa mtu katika nia zake na makusudi yake kabla hata tendo lenyewe halijaonekana nje.  Kumbe kuishika Torati kama anavyofundisha Yesu ni kuanza kuisafisha mioyo dhidi ya nia mbaya.

Tafakari

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, ninawaalika tuingie katika tafakari ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa dominika hii tukiongozwa na somo la kwanza, somo ambalo linatoka katika kitabu cha hekima ya Yoshua bin Sira. Yoshua bin Sira anazungumza na jamii iliyo  sawa kabisa na mazingira yetu ya sasa na changamoto zake. Katika changamoto zao hizo, Yoshua bin Sira aliwaalika waisraeli wenzake kuigeukia hekima ya kimungu iliyo ndani ya mapokeo yao. Anaamini kuwa ni hekima hiyo pekee iliyo na uwezo wa kuwavusha katika changamoto za wakati zinazowakabili. Anachowaonesha Yoshua bin Sira ni kuwa mtu hawezi kujikwamua kutoka katika matatizo aliyomo kwa kutegemea udhaifu ule ule uliomwingiza katika matatizo hayo. Anapaswa kujikita katika nguvu iliyo kuu zaidi. Sisi tulio wakristo, mwaliko wa Yoshua bin Sira kwetu ni mwaliko wa kuigeukia imani.

Ni mwaliko wa kuishikilia imani. Ni imani yetu inayotuelekeza katika hekima ya kimungu na kwa imani hiyo tutapata maana na majibu ya changamoto zetu za sasa. Tusiridhike au kubaki katika ufahamu wa kidunia: si mambo yote yanayoweza kujibiwa na teknolojia, si mambo yote yanayoweza kuamuliwa na siasa, si mambo yote ambayo utendaji wake unapaswa kuangalia uchumi pekee. Mwono wa kiimani na utashi wa kuifuata hekima ya kimungu ni ya msingi katika kuukamilisha ufahamu wa kibinadamu na kumsaidia kuishi kama anavyokusudia Mungu muumba wake.

TAFAKARI NENO LA MUNGU

  

14 February 2020, 16:00