Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili III ya Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa kutafakari umuhimu wa maji katika maisha ya mwamini! Maji kama chanzo cha uhai, utakaso na maafa! Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili III ya Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa kutafakari umuhimu wa maji katika maisha ya mwamini! Maji kama chanzo cha uhai, utakaso na maafa! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili III ya Kwaresima: Maji: Uhai, Utakaso na Kifo!

Masomo ya dominika hii yanatuonesha kuwa ni Mungu ndiye anayeanzisha ndani yetu kiu ya kurudi kwake. Ni yeye anayetuangazia kuona mahangaiko ya nafsi zetu pale tunapokuwa mbali naye kama walivyofanya Waisraeli katika maji ya Meriba na Masa au iwe ni kwa kuishi katika mazingira ambayo kwa asili yake yanatutenga na Mungu kama alivyokuwa yule mwanamke Msamaria.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumeingia katika dominika ya 3 katika kipindi hiki cha Kwaresima. Karibu katika kusikiliza masomo ya dominika hii na kupata tafakari yake fupi itakayotusaidia na kutuongoza kukiishi vema kipindi hiki maalumu cha neema kinachotuandaa kuiadhimisha Pasaka ya Bwana. Somo la kwanza (Kut. 17. 3-7) ni kutoka kitabu cha Kutoka. Somo hili la leo linaeleza tukio ambalo ni mojawapo ya matukio makubwa sana ya kukumbukwa kwa Waisraeli walipokuwa katika safari yao kutoka utumwani Misri kwenda katika nchi yao ya ahadi Kanaani. Katika safari hiyo, wanafika mahala ambapo baadaye paliitwa Masa na Meriba. Wakiwa mahali hapa, wanakosa maji. Wakaanza kumnung’unikia Musa kiongozi wao. Shida ya kukosa maji ni shida halali kwa sababu maji ni mojawapo ya mahitaji ya lazima kwa uhai. Lakini pamoja na hilo, ianonekana kuwa manung’uniko haya ya waisraeli yalivuka mipaka. Walianza kuhoji hata uhalali wa Musa kuwatoa Misri na hata wakatia mashaka kama Mungu aliyewatoa Misri bado yuko nao au la.

Wingi wa manung’uniko haya ukamfanya na Musa naye aingie katika dhambi ya kutafuta muujiza wa Mungu ili kuwathibitishia Waisraeli kinyume na manung’uniko yao. Akasahau muujiza mkubwa aliowafanyia Mungu kuwatoa Misri na akasahau ahadi zote Mungu alizokwisha waahidia. Hii ndiyo maana mahali hapo paliitwa majina mawili, kwanza paliitwa Masa, neno linalomaanisha manung’uniko au uasi na pakaitwa pia Meriba, neno linalomaanisha kumjaribu Mungu. Somo hili linaletwa kwetu leo kwa sababu linabeba dhana ya maji, dhana ambayo ina maana pana sana katika liturujia ya dominika ya leo. Waisraeli walikosa maji – wakaingia katika dhambi ya manung’uniko, uasi na kumjaribu Mungu – hata hivyo Mungu bado akawajibu kwa kuwapa Maji. Chombo hiki ambacho kwa waisraeli kilimaanisha uhai, nguvu ya uharibifu au pia utakaso, kinakuwa ni chombo kinachoalika utimilifu wa furaha ya kieskatolojia, yaani muungano kamili wa Mungu na watu wake.

Somo la pili (Rum. 5:1-2, 5-8) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Warumi. Paulo aliandika barua hii kwa wakristo waliokuwa Roma. Mji huu ambao ulikuwa ndio makao makuu ya dola ya kirumi ulikusanya makundi mbalimbali ya watu yaliyojumuishwa katika kundi la wayahudi na kundi la watu wa mataifa. Kwa makundi yote haya, Paulo aliwaandikia ili wampokee Kristo, njia pekee ya wokovu na tumaini lisilohadaa. Katika somo hili, Paulo anawatangazia ukombozi ambao Kristo amekwisha uweka tayari kwa ajili yao wote. Anawaonesha kuwa Kristo ameuweka ukombozi huu kwa kukubali kifo cha Msalabani katika kipindi ambacho watu wote walikuwa dhambini. Sasa kama alikufa katika kipindi ambacho wote tulikuwa dhambini na katika kipindi ambacho ubinadamu haukuwa na thamani ni dhahiri kwamba sasa ambapo ubinadamu umerudishiwa hadhi yake ataweza kuwapokea vizuri zaidi wanaomwamini na kumuongokea.

Injili (Yn. 4:5-42) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Yohane.na inaleta simulizi refu la Yesu na mwanamke Msamaria. Wakati wa Yesu, Uyahudi na Samaria yalikuwa ni mataifa mawili tofauti japokuwa hapo kabla walikuwa ni ndugu wa Taifa moja. Utofauti kati yao ulianza polepole hadi ukafikia kuwa uhasama ambao haukuruhusu mwingiliano wowote kati yao. Yesu leo anafika katika mji wa Samaria na anakwenda palipokuwa na kisima cha Yakobo, hapo anakutana na mwanamke Msamaria. Kiini cha mazungumzo kati yao ni maji. Mwanamke anakwenda kuteka maji lakini Yesu anamwambia kuwa Yeye ndiye atoaye maji yaliyo hai na kila anywaye maji hayo hataona kiu tena. Tayari hapo tunaona kuwa japokuwa hili linaweza kuwa simulizi la tukio linaloweza kuwa la kawaida, Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa kile kinachozungumzwa kina maana zaidi ya ile ya kawaida. Na maana hii ni ya kiteolojia.

Kwanza Yesu anavunja tamaduni ya Kiyahudi ya kutokukutana na tena kuongea na Msamaria. Myahudi ambaye Mungu alimteua awe taifa lake na ambaye kwa njia yake Mungu angeuunganisha na kuukomboa ulimwengu mzima, yeye alianza kuwagawa na kuwatenga watu. Kumbe, Yesu kuvunja mwiko huu ni kuonesha jitihada yake ya kuwafikia hata wale ambao ubinadamu uliwaweka mbali na mpango wa Mungu. Na ndio hao ambao mwanamke huyu Msamaria aliwawakilisha. Dhana ya maji ambayo ilidokezwa na somo la kwanza inajirudia tena katika injili hii. Yesu anapojitambulisha kama ndiye atoaye maji yaliyo hai anajitambulisha kuwa ndiye anayeitimiza kiu ya kuufikia muungano kamili kati ya mtu na Muumba wake. Muungano ambao ndio uzima wenyewe usiokufa. Katika nafasi nyingine mwanamke Msamaria anakuwa pia ni kielelezo cha wongofu na ukuaji wa imani. Anaposikia Yesu akimwambia kuwa ndiye atoaye maji ya uzima anamwambia “Bwana unipe maji hayo nisione kiu tena”. Na anakiri kwa Yesu kuwa hana mume kwa maana amekuwa tayari na waume watano naye aliyenaye sasa sio wake.

Hili haliwezi kuwa moja kwa moja suala la ukosefu wa maadili kwa mwanamke huyu na ndio maana Yesu hamuhukumu.  Kimapokeo, Wasamaria wanatajwa kuwa walikuwa na miungu watano waliokuwa wanawaabudu. Neno Baali lililomaanisha kwa Kiebrania “miungu ya kigeni”, kwa lugha hiyo hiyo lilimaanisha “mume”. Kumbe, inawezekana kabisa kuwa hapa mwanamke msamaria akawa anawakilisha mahangaiko ya kiimani ya taifa lake hasa walipokuwa wakitapatapa kuabudu miungu wengine na hata sasa hawana “mume” kwa sababu hawajamfungulia moyo Mungu wa kweli ambaye Kristo alikuja kuanzisha ufalme wake. Mwanamke msamaria kisha kupokea Neno, akaliamini alikwenda kuipeleka furaha hiyo kwa watu wa taifa lake na Wasamaria wengi walimwamini. Akawa shahidi wa imani ambayo yeye aliipokea kwa furaha.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, mwaliko usiokoma wa kipindi hiki cha Kwaresima, ni mwaliko wa kumrudia Mungu. Kwaresima inatualika kuuitikia mwaliko huu kwa njia ya mazoezi mbalimbali ya kiroho: kufunga, kusali, kutubu na kuzidisha matendo ya huruma. Masomo ya dominika hii ya leo yanatuonesha kuwa ni Mungu mwenyewe anayeanzisha ndani yetu kiu hiyo ya kurudi kwake. Ni yeye anayetuangazia kuona mahangaiko ya nafsi zetu pale tunapokuwa mbali naye iwe ni kwa kuasi kwetu wenyewe kama walivyofanya waisraeli katika maji ya Meriba na Masa au iwe ni kwa kuishi katika mazingira ambayo kwa asili yake yanatutenga na Mungu kama alivyokuwa yule mwanamke Msamaria.

Masomo ya leo yanatupa faraja na kutuhimiza tutambue kuwa kwa njia ya Kristo, Mwenyezi Mungu huijalia daima neema nafsi inayomtafuta. Ni yeye anayetimiza kiu kwa Maji ya Uzima, yaani kuijalia nafsi kuifikia furaha ya muungano kamili na Mungu wake. Neno hili la faraja na matumaini liwe pia nguvu na kitulizo katika kipindi hiki ambacho dunia nzima inapambana na tishio la ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona, COVID-19. Tukikumbushwa na maneno ya Mzaburi kuwa “Mungu asipoijenga nyumba waijengao wanafanya kazi bure na tena Mungu asipoulinda mji waulindao wanakesha bure” (Zab. 127),  tunamwomba Mungu aingilie kati na kutujalia uzima na amani kadiri ya mapenzi yake matukufu.

Liturujia J3 ya Kwaresima

 

13 March 2020, 15:00