Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kwaresima: Hofu ya Kifo!
Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.
Amani na Salama! Injili ya leo ingawa ni ndefu na inajulikana kama kufufuliwa kwa Lazaro, lakini tunaona muujiza wa kurejeshewa uhai Lazaro unasimuliwa kwa aya mbili tu ndizo za 43 – 44, na sehemu iliyobaki ni mahojiano yenye nia ya kumuwezesha msomaji kupata ujumbe kusudiwa. Naomba tangu mwanzo niweke wazi juu ya ukweli kuwa lugha yetu ya Kiswahili inakosa neno muafaka kuhusiana na ishara hii aliyoifanya Yesu na hivyo tunaona linatumika neno “kufufuliwa kwa Lazaro’’, labda niwaombe tusitumie neno hilo na badala yake tutumie neno: ”kurejeshewa uhai Lazaro’’. Labda utajiuliza kwa nini tusitumie ufufuko na badala yake ninawasihi tutumie neno ‘’Kurejeshewa uhai Lazaro’’, ni kwa sababu kubwa moja. Ufufuko ni pale tu tunapojaliwa uzima wa milele usio na mwisho na hivyo kuwa na miili ile ya utukufu isiyoweza kufa tena isiyokuwa miili ya nyama inayohitaji nafasi na muda, bali kwa Lazaro alirejeshewa sio mwili ule wa utukufu usioweza tena kufa bali alibaki na kuwa na mwili wa nyama na hivyo kuweza kufa tena. Baada ya ufufuko hakutakuwa tena na mwili wa nyama wala mauti. Ingawa pia tutaona hapa chini kuwa Mwinjili Yohane haikuwa lengo lake kutupa simulizi la kihistoria lililojiri bali ni katekesi ya kiteolojia ili kuwa na muono mpya juu ya mwisho wa maisha ya kibaolojia na mwanzo wa maisha mapya ya umilele.
Na pia tunaposoma sehemu ya Injili ya leo kama vile ile ya Dominika iliyopita tunaona kila mara Mwinjili Yohane anaposema juu ya ishara anatualika kwenda mbali zaidi ili kupata jumbe kusudiwa. Tunapoisoma kama vile anatueleza kweli ya kihistoria tunabaki na maswali yanayokosa majibu. Mwinjili anatutambulisha juu ya uwepo wa familia inayotushangaza kidogo kwani hatusikii juu ya wazazi, juu ya waume wa dada na mke wa Lazaro, na wala watoto au ndugu wengine wa familia ile, kiufupi ni familia inayoleta maswali mengi. Lakini hata Yesu baada ya kusikia kuwa rafiki yake Lazaro yu mgonjwa haendi mara moja kumponya na badala yake anakaa siku mbili zaidi, ni kama vile hajali juu ya rafiki yake na hivyo kumwacha afe. Kwa nini Yesu haoneshi kujali na kila mara tunamuona katika Injili ni mmoja anayeguswa na shida na mahangahiko ya watu, ni mmoja mwenye huruma? Na hata baada ya kupata taarifa juu ya kifo cha rafiki yake Lazaro tunabaki na swali kwa nini Mwinjili anatuonesha kuwa Yesu alifurahi kwa kuwa hakuwepo wakati rafiki yake Lazaro anapofariki?
Na labda tunajiuliza pia nyakati zile za Yesu hakukuwa na mawasiliano kama tunayokuwa nayo leo ya simu au mitandao ya kijamii na hata intaneti; Ni nini kilimpelekea Martha kujua kuwa Yesu anakaribia kufika kwao, na hata baada ya kufika na kukutana naye na kukimbia kwenda kumuita umbu lake Maria, tunaona tena Yesu anabaki njiani au kwa nini anasubiri na kubaki hapo njiani mpaka Maria anatoka Betania na kuja kukutana naye hapo njiani? Je, Yesu hakupaswa kwenda nyumbani kwa akina Martha na Maria na kutoa salamu zake za pole na rambirambi kama ilivyo katika desturi za jamii nyingi hata nyakati zetu leo? Na hata Martha kwa nini mwanzoni alitokea peke yake bila Maria kuwa na taarifa yeyote? ‘’Mimi ndimi ufufuo na uhai. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi; na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe’’. Maneno haya yana maana gani kwani tunajua kwa hakika hata na sisi tunaomwamini Yesu bado tunakufa kila siku na hasa labda nyakati hizi ambazo ulimwengu umegubikwa na hofu kubwa na tunashuhudia maelfu na maelfu ya watu wanakufa kwa janga la COVID-19? Yesu analia nalo ni neno linaloleta maswali, kwa nini alie wakati anajua kwa hakika kuwa atamrejeshea uhai rafiki yake Lazaro kwa kumtoa mle kaburini? Labda tunajiuliza tena kwa nini hatusikii tena juu ya familia hii ya Betania iwe katika Injili ya Yohana na hata Injili zile nyingine ndugu?
Kutokana na maswali haya na mengine tunayoweza kujiuliza tunaweza kusema kuwa Mwinjili nia na lengo lake ni kutupa katekesi iliyoshiba Taalimungu. Ni nia yake kutufundisha kuwa ‘’Yesu mfufuka, ndiye Bwana wa uhai’’ Tuanze kwa kuangalia kwa nini familia ya kaka na dada tu inayozungumziwa na Mwinjili Yohane. Mwinjili anataka tangu mwanzo kutuonesha kuwa familia inayozungumziwa hapa ndio jumuiya ya wakristo, jumuiya kama familia ya ndugu walio wote sawa, hivyo hakuna mmoja aliye mkubwa au mdogo kuliko mwingine. Ni jumuiya ya wote wanaokuwa wenye hadhi na hali sawa. Kinachowaunganisha hawa wote na Yesu ni upendo wa kirafiki. Na ndio mahusiano yetu kama wanakanisa hayana budi kuwa ya kidugu na pia tunaunganika na Yesu kwa upendo wa kirafiki. Yohane 15: 15. Ni katika familia ile tunaona wanapatwa na swahibu la kufiwa na kaka yao. Ni familia inayoingia katika mahangahiko na majonzi ya kufiwa na mpendwa wao, waliyependana naye kwa dhati, na mwenye nafasi na kuleta maana katika maisha yao ya kila siku. Ni mahangahiko ya haki kabisa kwani hata kati yetu leo tunapompoteza mmoja tunayempenda tunabaki na maswali na zaidi huzuni na majonzi makubwa.
Martha na Maria kama rafiki za Yesu na wakijua uwezo wa Yesu wanajiuliza kwa nini hakuzuia kifo cha rafiki yake Lazaro? Ni swali ambalo hata nasi tunajiuliza leo tunaposhuhudia vifo vya wapendwa wetu na hasa siku hizi za mahangahiko ya janga la COVID-19, kwa nini hazuii vifo vya wana wake na wakati tunajua Yeye ana uwezo wote wa Kimungu, kwa nini haingilii kati na kuponya watu wake na kutuepusha na balaa hili? Kwa kweli ni sala yetu kwani tuna imani na uwezo wake wa Kimungu. Na pia ni maswali ambayo leo ulimwengu unajiuliza. Yupo wapi Mungu wetu, yupo wapi Kristo mfufuka? Haya ni maswali tunajiuliza leo tunaposafiri katika kipindi hiki kigumu katika historia ya mwanadamu. Tukiwa tunakaribia kabisa maadhimisho ya Juma Kuu tunajiuliza kwa nini Mungu hatendi, kwa nini haoneshi uwezo na nguvu zake ili wote wapate kumwamini na kuokoka? Ni maswali waliyokuwa nayo pia Marta na umbu wake Maria kwa nini hata baada ya kupata taarifa ya mahangahiko na huzuni yao bado alichelewa kwa siku mbili zaidi? ‘’Bwana, kama ungalikuwapo hapa, kaka yangu hangalikufa!’’ Tunasoma Yohane 11:21, 32. Hakika kifo cha mmoja tunayempenda, mzazi, ndugu, rafiki au mjuani fulani mwenye nafasi katika maisha yetu kinatuachia si tu maswali bali maumivu makali pia, natumai wengi wetu tumewahi kufikwa na msiba wa mmoja anayekuwa mtu wa karibu na muhimu kabisa katika maisha yetu.
Ni wakati mgumu wa majaribu hata ya imani pia, ni wakati hata tunashawishika kuona kuwa Mungu hayupo pamoja nasi, au kama yupo basi hatupendi na hivyo kuruhusu mmoja tunayempenda kufa. Marta na Maria pia walimwambia Bwana ungalikwepo, ndio kusema Bwana na Mwalimu wao aliwaacha? Ni katika kumwacha Lazaro afe, Yesu anatoa majibu kwa maswali ambayo mara nyingi tunakuwa nayo katika maisha yetu ya siku kwa siku. Si nia wala lengo la Yesu kuzuia kifo cha kibailojia cha kila mmoja wetu. Si lengo la ujio wake kuja kutufanya tubaki katika maisha ya dunia hii kuwa ya milele, yasiyo na mwisho, la hasha. Na badala yake amekuja ili tupate uzima wa milele baada ya maisha ya hapa duniani. Maisha ya hapa duniani hayana budi kufikia ukomo ili tuweze kuzaliwa katika maisha ya umilele, yasiyo na mwisho wala mauti tena. Ni kwa kuwa na muono na mtazamo huo tu imani yetu inabaki katika njia iliyo sahihi na kinyume chake ni kuanza kuingia katika ukinzani na mgogoro wa kiimani kama labda wengi wetu hata leo tunauingia tunapotafakari juu ya janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 na vifo vya wapendwa wetu na hata juu ya kifo changu mwenyewe. Kinyume chake ni kuishia kuona kuwa Mungu hayupo kati yetu au anatuadhibu, mawazo au fikra ambazo nikiri na narudia kusema ni kufuru kubwa kwa Mungu.
Ni mawazo yanayoendana kinyume na asili yake kwani Yeye ni ‘’Upendo usio na masharti’’, Mungu hatupendi kwa kuwa sisi ni wema au ni watakatifu, hapana bali anatupenda daima kwani sisi ni wana wake wapendwa hata tunapomkosea na kuwa mbali naye Yeye daima anabaki kuwa Ni Mungu na Baba yetu na hivyo anatupenda. Najua leo hii kuna mafundisho mengi na hata ya baadhi ya wahubiri wa ulimwengu wa leo yanayokuwa kufuru kwani ni kinyume na asili ya Mungu. Mungu ni upendo, naomba tusiongeze wala kupunguza kitu kama anavyotusihi Mtume Yohane katika Waraka wake. Mungu daima yupo pamoja nasi na anasafiri nasi hata katika nyakati ngumu kama hizi za janga la COVID-19, hayupo mbali nasi wala hawezi kutuacha kamwe. Kuna rafiki yangu mmoja ameniuliza; Je, Padre kwa nini Mungu ameruhusu hata tunapatwa na janga hili la COVID-19 na kujikuta leo tukiwa tumegubikwa na hofu na mashaka makubwa ulimwenguni kote? Ni swali la haki kabisa na uzuri linaakisi uhalisia na maswali ya wengi wetu leo. Ni kweli Mungu ameruhusu hilo na wala sina mashaka na labda tunaweza kujiuliza ni kwa nini Mungu ameruhusu, Je ni adhabu kwa mwanadamu, Je,ni kwa sababu gani nyingine? Hakika sio adhabu na wala hatuna Mungu anayeadhibu wana wake kwa kutuletea majanga na adhabu hapa duniani, ila ameruhusu na hakika ana sababu.
Kila mmoja wetu anaalikwa kukaa mbele ya Mungu katika sala na tafakari yake kwani ana ujumbe kila dakika ya maisha na historia ya mwanadamu. Hatuwezi kusema kwa hakika kwani njia zake zinapita akili zetu ila anaongea na kila mmoja wetu katika nafsi na maisha yake. Sababu gani na kwa nini labda sio rahisi kujibiwa ila kila mmoja katika sala na tafakari tunaalikwa leo kukaa mbele yake Mungu na Muumbaji wetu na kuongea naye, tumsikilize Mungu anataka kusema nini na kila mmoja wetu. Kwa nini mateso na mahangahiko duniani? Ni swali ambalo limekuwa likitafakarisha si tu mwanadamu wa leo bali tunaona katika historia ya Kanisa walimu wa Kanisa kama Mtakatifu Augustino na Mt. Thomas Akwino na wengine wengi. Nawaalika tutumie kipindi hiki cha majaribu kutafakari vema kwa nini Mungu ameruhusu janga hili. Na kamwe isiwe muda wa kuanguka katika mtazamo finyu wa kutufanya tuanguke katika ‘’fallacies of non causa pro causa’’ ni ile kutoa majibu yasiyo sahihi ya sababu au kwa nini Mungu karuhusu hili, na hata pia ‘’fallacy of single effect’’ kubaki kudhani kuwa ni kwa sababu fulani moja tu basi Mungu ameruhusu haya tunayoshuhudia leo. Na ndio maana nimewaalika kila mmoja wetu kadiri ya mazingira yake achukue nafasi kusali na kutafakari.
Kipindi hiki kibaki kuwa cha matumaini makubwa kwa kumkazia macho Yesu na sio mawimbi yatokanayo na Virusi vya Corona au mengi ya kutisha na kukatisha tamaa. Tuzidi kuchukua tahadhari kwani kinyume chake kudai kuwa tuna imani na kumweka Mungu katika majaribu ni kumkufuru Mungu. Wapo hata viongozi wa dini wanaotualika tumjaribu Mungu kwa kuishi kana kwamba hatuna akili na utashi. Imani yetu daima haina budi kutopingana na akili na utashi tuliojaliwa na Mungu. Na ndio maana kwa maumivu makubwa utasikia baadhi ya sehemu mbali mbali za dunia viongozi wa Kanisa wamefikia maamuzi magumu ya kusitisha maadhimisho ya kiliturjia ya watu wengi. Tukumbuke Makanisa yapo wazi na tunaalikwa kusali na kumlilia Mwenyezi Mungu, lakini pia hata tunapobaki ndani kwa kuepuka maambukizi tutumie fursa hizo kusali zaidi na kumlilia Mungu. Kamwe tusione kuwa viongozi wetu wamefikia maamuzi hayo magumu kwa kuwa hawana imani kwa uwezo wa Mungu. Lazima kuzingatia kuwa Mama Kanisa ana wajibu wa kulinda maisha ya wana wake pale inapoona kuwa maisha yetu yanakuwa hatarini.
Ni vema kukumbuka hata Yesu alivunja amri ya siku ya Sabato kwa kutenda mema, kwa kuokoa maisha. Na ndicho kinachofanywa na Mama Kanisa, ni kuvunja amri ya Sabato kwa kusukumwa na Upendo. Upendo kwa Mungu na kwa jirani ndio amri kuu kuliko sadaka na mengine tunayoweza kuyafikiria. Yesu ametolea maisha yake pale juu msalabani si kwa sababu tulikuwa wema hapana ili aweze kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na kuwa wana huru na rafiki na ndugu zake Kristo Mfufuka. Leo tunaposhuhudia kipindi kigumu katika maisha ya wanakanisa kwa kukosa Ibada za wazi kwa watu wote na hasa Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu. Ndio kusema kuna kilio kila kona ya ulimwengu, ni kuonesha kwa haki kiu na njaa yetu ya Mungu, kiu na njaa ya Neno lake, kiu na njaa ya Ekaristi Takatifu, kiu na njaa ya kuwa naye kwa namna ya pekee kabisa katika maadhimisho yetu ya kiliturjia na yale yasiyo ya kiliturjia, ni njaa na kiu ya kuwa karibu na jirani, rafiki, ndugu, wazazi, walimu, wanafunzi, kuwa tumeumbwa sio kuishi mbali na Mungu bali pamoja na Mungu na jirani. Leo tunakiri na kutambua hatuwezi kuishi bila Mungu na hatujaumbwa kuishi kama kisiwa bila wengine. Leo tunaona tunavyomhitaji Mungu na mwingine.
Sote tuna hofu ya kifo kama ambavyo wanafunzi wa Yesu walivyokuwa na hofu hiyo, ni hofu ya haki kwa kila mwanadamu tukibaki kuangalia maisha kwa kuongozwa na mantiki ya ulimwengu wetu wa leo. Mfuasi wa Yesu lazima aondokane na hofu ya kifo, ni kukubali kupoteza maisha yetu ya sasa kwa kuyatoa kwa upendo, kufa kama mbegu ya ngano, na kwa kuzikwa tu inaweza kuota na hivyo kuzaa matunda mengi na mema. Yohane 12:24-28 Ni katika maneno ya Yesu anatufundisha kuwa na muono mpya na ulio sahihi juu ya kifo. Yesu anafurahi kutokuwepo wakati wa kifo cha rafiki yake Lazaro. ‘’ Lazaro amekufa, lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwepo huko, ili mpate kuamini.’’ Yohane 11: 15 Yesu anafurahi kwa kuwa kwake kifo sio uharibifu bali ni mwanzo mpya wa maisha mapya ya umilele tofauti na maisha ya sasa ya hapa duniani. Yesu anakutana na Martha na kufanya naye mahojiano. Lazaro alishakuwa amekaa kaburini kwa siku nne sasa ndio kusema nyakati zile wayahudi waliamini kuwa ni siku ya nne kusingekuwa na matumaini tena ya mmoja ingewezekana kuwa amezimia na hivyo kurudi katika maisha ya kawaida. Ni siku ya nne ambapo hakukuwa tena na matumaini ndipo Yesu anapofika pale.
Ni katika mahojiano yake na Martha, Yesu anajaribu kumuelekeza si tu Martha bali kwa kila mfuasi wake kujua nini maana ya kifo kwa yule anayemwamini Yesu Kristo. Kama ungalikuwepo ndio msemo wa Marta lakini yawezekana ni wa kila mmoja wetu kila mara tunapokutana na nyakati ngumu na kushawishika kuona tupo peke yetu kwani Mungu ametuacha, ametupa kisogo. Kama Mungu yupo kwa nini kifo, maradhi na mahangahiko? Martha anaonekana kuwa ni kati ya wale wanaoamini katika ufufuko siku ya mwisho wa ulimwengu. Labda ndio muono wa baadhi yetu wakristo kuwa tunaamini siku ya mwisho Bwana atawafufua wapendwa wetu. Lakini bado tunaona muono wa namna hii bado hauleti ahueni, wala faraja, wala nafuu yeyote kati ya mahangahiko ya kifo. Kwa nini basi Mungu anaruhusu tufe halafu mwishoni anaturejeshea tena uzima? Kwa nini asituache tukaendelea kuishi maisha haya bila kifo, kwani kutengana na wapendwa wetu kunaleta mahangahiko na huzuni kubwa. Kwa nini kusubiri basi mpaka mwisho wa ulimwengu? Na je roho inakuwa wapi bila mwili kipindi chote cha kusubiri ufufuko?
Yesu leo anatualika sisi wafuasi wake kuwa na mtazamo na mwono mpya, sio ule kama wa Martha na baadhi yetu bali tukimwamini Yeye tutaishi milele. Anayemwamini Yeye hata kama atakufa ataishi milele. Yafaa hapa tutafakari maana yake maneno haya maana kama nilivyosema mbona tunashuhudia kila siku tena bila mashaka kuwa hata na wale wanaomwamini Yesu wanakufa na tunawazika na tena siku hizi za COVID-19 maelfu ya wafuasi wa Yesu wanakufa kila siku tena kwa wingi wa kutisha. Nawaalika tutumie japo lugha ya picha na mfano ili kuweza kuelewa lugha ya Yesu. Maisha yetu ya dunia yanafumbatwa na ukweli kuwa ni maisha ya kuingia na kutoka. Kutoka kutokuwepo tunatungwa mimba katika tumbo la mama zetu, tunabaki tumboni kwa miezi tisa na kuzaliwa katika ulimwengu huu wenye ishara nyingi za umauti. Ni ishara za umauti kama vile, upweke, kutengwa, umbali na wengine, kusalitiwa, ujinga, magonjwa, na maumivu. Maisha yetu hapa duniani tunaona wazi kuwa hayajakamilika, kila mara tunajiona kuwa na mipaka mingi. Hivyo haiwezekani kuwa mwisho wetu ni ulimwengu huu kadiri ya mpango wa Mungu, hivyo kuweza kuishi maisha ya ukamilifu na ya milele hatuna budi kutoka katika maisha haya.
Tuchukulie mfano mwingine, wa mapacha wawili wanaokuwa katika tumbo la mama ambao wawe wanaweza kuona, kuelewe na hata kuzungumza kwa miezi ile tisa wakiwa tumboni mwa mama yao, na hivyo kujenga urafiki wa karibu na upendo mkubwa kati yao. Wakiwa tumboni mwa mama yao huo ndio ulimwengu wao wanaoujua na kuufurahia kwani hawajui ulimwengu mwingine nje ya tumbo la mama yao. Hawajui yanayojiri nje ya tumbo la mama yao kuwa watu wanazaliwa, wanakua na kuoana, wanaofanyakazi, wanaosafiri, wanaofurahi na kuhuzika, kuna wanyama, mimea, maua na fukwe na kadhalika na kadhalika. Wanajua ni maisha yale tu wanayoishi kwa muda ule wa miezi tisa wanapokuwa tumboni mwa mama yao. Inakamilika miezi tisa na pacha wa kwanza anazaliwa. Yule anayebaki tumboni kwa muda kabla ya kuzaliwa kwa hakika anawaza kwa muda ule kabla ya kuzaliwa kuwa, pacha na ndugu yake amefariki, hayupo tena, amepotea na kumuacha peke yake, hivyo kulia na hata kuhuzunika. Ukweli ni kuwa pacha wake hajafa. Ametoka na kuachana na maisha yale yasiokuwa na uhuru mkubwa, mafupi ya miezi kadhaa tu yenye kila aina ya mipaka na sasa ameingia katika maisha mapya.
Hivyo ndivyo Yesu anavyomwalika Martha kuwa na muono mpya kuwa kifo, kwa kufa mmoja anazaliwa katika maisha mapya, anaingia katika kuunganika na Mungu, maisha yasiokuwa tena na mipaka wala muda wala nafasi, maisha yasio na mwisho. Ni maisha ambayo kama asemavyo Mtume Paulo kwa Wakorinto wa kwanza, 1 Wakorintho 2:9 “Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona, wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndio Mungu aliyowatayarishia wale wampendao.’’ Hivyo kwa mkristo maisha ya ulimwenguni ni sawa na kipindi kile cha kuwa tumboni mwa mama kabla ya kuzaliwa kwetu, hivyo kifo kinabaki kwa wale wanaobaki ila kwa yule aliyetanguli, yeye anakuwa amezaliwa katika ulimwengu wa milele, katika maisha mapya. Ni hapo tunaona kwa nini Yesu alifurahi kwa kifo cha rafiki yake Lazaro na akaruhusu kifo chake ambacho kwa hakika angeliweza kukizuia kwa uwezo wake wa Kimungu. Yeye anaona kifo kwa jicho la Kimungu, kama nafasi muhimu na adimu kabisa katika safari ya maisha yetu ya hapa duniani. Na ndio maana tunaona jumuiya za wakristo za mwanzo hawakuita kifo bali walitumia msemo wa ‘’siku ya kuzaliwa’’. Ni kuzaliwa katika maisha yale ya milele, maisha ya utukufu na furaha ya milele, hivyo kifo ni kupita kutoka maisha ya kuharibika na kuingia na kuvaa kutokuharibika. Ni baada ya kusikiliza mafundisho ya Yesu tunaona Marta anakiri imani; “…Je waamini hayo? Marta akamwambia, Ndiyo Bwana! Mimi naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.’’ Yohane 11:27
Na pia Yesu alikuwa na mahojiano yanayofanana pia kati yake na Maria, ndio kusema Yesu anafanya mahojiano hayo hayo na kila mmoja na hivyo kutualika sote kuwa na muono mpya juu ya maana ya kifo kwa maisha ya mfuasi wa Yesu Mfufuka. Ni kutualika kufika kukiri kuwa ni Yeye aliye Bwana wa uzima. Tunaona kuwa Yesu haingii kijiji cha Martha na Maria pale Betania, ambapo Wayahudi walifika ili kuwafariji umbu wale wawili. Ndio kusema Yesu hakuja kutoa salamu za rambirambi na kuomboleza bali kutoa uzima lakini ili kuweza kutoa uzima na uhai anataka ndugu wale watoke Betania, watoke katika nyumba ile iliyojaa watu wenye uzuni na maombolezo, yenye watu wanaobaki katika muono na mtazamo wa kipagani. Na ndio mwaliko wa Yesu katika Dominika ya leo kwetu kutoka katika muono ule wa kale na wa kipagani wa kulia na kuhuzunika na kuomboleza kifo kama watu wasio na imani.
Yesu anafika mahali pale walipomweka Lazaro; alipoona huzuni ya Maria na wale waombolezaji naye alilia. Ni haki kulia na kuomboleza sio kwa sababu aliyekufa amepotea na kuangamia bali ni vile tunatengana naye kwa muda katika maisha ya hapa duniani. Lakini naomba niseme kuwa kuna aina mbili za kulia na kuomboleza hapa. Ya kwanza ndio ile ya kuona kuwa kifo ndio mwisho wa kila kitu, hakuna tena matumaini mengine wala maisha mengine yasiyo na mwisho bali ndio ni kuangamia kwa milele. Aina ya pili ya kulia ndio kama ile ya Yesu ambayo kila mmoja wetu anajikuta kuwa nayo hasa dakika ile ya kumzika mmoja tunayempenda sana. Hata katika Maandiko Matakatifu tunaona yanatumika maneno mawili tofauti ya Kigiriki. Kilio cha Martha, Maria na Wayahudi linatumika neno ‘’klaiein’’ Yohane 11:33 ndio kilio cha mmoja asiye na matumaini, anayeona kifo ni mwisho wa kila kitu. Kilio cha Yesu kinyume chake linatumika neno la kigiriki ‘’edàkrusen’’ likimaanisha machozi yanayotiririka kutoka machoni, Yohane 11:35. Ni kilio hiki cha pili cha Yesu, ni kulia tukiwa bado na matumaini, tunahuzunika wakati tumejawa na matumaini tele, tukijua kifo sio mwisho bali ni kutengana kwa muda mfupi tu.
Na ndipo sasa Yesu anawaamuru kuliondoa jiwe kaburini. Ni jiwe linalokuwa katika akili na mawazo yetu kuwa kifo ni mwisho wa kila kitu, ni jiwe la kuondoa kupoteza kwetu imani na matumaini, ni jiwe la upofu wa maisha mapya ya umilele pamoja na Mungu. Anayemwamini Yesu anajua kuwa hata kama tunakufa bado tunaishi ingawa katika mtindo na maisha mengine. Vizuizi na kila aina ya jiwe linaondolewa siku ile ya Pasaka, kuwa kuanzia sasa kifo ni mpito kutoka maisha haya na kuzaliwa katika maisha yasiyo na mwisho, maisha ya umilele, maisha pamoja na Mungu kwa namna ya pekee zaidi. Yesu anasali sio kwa nia ya kutaka Mungu Baba afanye muujiza, la hasha bali ni kwa kuombea wale wote wanaomzunguka pale ili waweze kumwamini, kubadili vichwa na kuwa na muono mpya juu ya kifo. Yesu alipaaza sauti: Lazaro!, toka nje! Imefika saa ile ambapo wafu watasikia sauti ya Mwana wa Mungu na kupata kuishi. Wote wanaokuwa makaburi wataisikia sauti yake na kutoka katika makaburi yao. Yohane 5:25-29 Hata baada ya Yesu kumwamuru atoke nje bado alibaki na ishara zile za mfu kwani miguu na mikono yake ilikuwa bado imefungwa.
Yesu anawaamuru kumfungua na kumwacha aende zake. Ndio kusema ni mwaliko kwa wale wanaoomboleza kifo cha mmoja wa waamini huku wakikosa imani, wamfungue aliye mfu na kumwacha huru aende katika maisha mapya, maisha ya milele. Na ndio unaona hata leo tamaduni ya Mama Kanisa tunawafungua wafu watu kwa sala na hasa kwa kutolea sadaka ya Misa, ndio kusema kuwafungua miguu na mikono ili waweze kusamehewa dhambi na adhabu zao za dhambi na kuanza kuishi maisha ya umilele, maisha yasiyo na mwisho, maisha mapya bila kifo, bila magonjwa, bila huzuni wala shida iwayo yote ile. Lazaro hafunguliwi vizuizi vile na kukumbatiwa na rafiki yake au na dada zake bali aende zake. Ndio mwaliko kuwa nasi hatuna budi kuwafungua wafu wetu na kuwaacha huru waingie katika maisha mapya ya umilele pamoja na Mungu na watakatifu wake, hivyo huzuni yetu haina budi kuwa yenye imani na matumaini. Kifo hakina neno la mwisho, siyo mwisho wa mwanadamu bali ni hatua ya mpito kutoka maisha ya sas ana kuzaliwa katika maisha ya umilele.
Tunajua hata kati yetu waamini kuna namna nyingi za kuendelea kuwafunga mikono na miguu ndugu zetu waliotwaliwa kutoka maisha haya kwa namna ya tabia zetu zinazoonesha kuwa hatuna imani kwa Kristo mfufuka. Ndio kusema kutaka wapendwa wetu kuendelea kuishi pamoja nasi katika ulimwengu huu na hivyo kukosa kuzaliwa katika maisha mapya. Tuzidi kusali na kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie nasi kukua katika imani, imani kwake kwani ndiye Bwana wa uzima wa milele. Nawatakia tafakari njema na maandalizi mema ya Juma Kuu litakaloanza Dominika ijayo ya Matawi, tutolee sala na maombi yetu kwa imani kipindi hiki na Kwaresima hii tunayopitia jaribu gumu kabisa la imani yetu ili jaribu hili lisiwe chanzo cha kupoteza imani na matumaini bali kuimarika zaidi katika imani na matumaini kwa wema na huruma ya Mungu kwetu. Dominika na tafakari njema.