Tafakari Neno la Mungu: Jumapili ya Pili ya Kwaresima: Upendo wa Mungu umetundikwa Msalabani
Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, O.S.B., - Roma.
Kristo Yesu kwa Fumbo la Umwilisho wake amefanana tikitiki na Mungu Baba yake aliyemshuhudia alipobatizwa na alipong'ara sura kuwa: "Huyu ni mwanangu Mpendwa wangu." Kwa hiyo Yesu anayo Roho wa Mungu na mapaji yake kwa utimilifu wake wote. Paji la akili la Roho Mtakatifu ni kipawa cha kujua fumbo la upendo wa kimungu. Paji la Mungu la akili kwa Kristo unaliona katika utabiri wake kuwa: "Mwana wa Adamu hana budi kuteseka na kudharauliwa sana, kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka." (Luka 9:22-23). Akili yake ilishatambua kuwa Fumbo la upendo wa Mungu linadai kuteseka. Kwa hiyo Yesu anaposema "hana budi" au imempasa, inadhihirisha upakwa-wakfu wa ndani kabisa wa Yesu. Yaani kila kitakachomtokea kutokana na upendo kwa Baba yake na majitoleo ya upendo kwa wanadamu wote katika ilimwengu wa dhambi ni kuteseka na kufa tu hakuna jinsi nyingine.
Kwa hiyo akili za kimungu ni zile za Fumbo la upendo, Fumbo la Msalaba na la Kifo. Fumbo hili la upendo wa Mungu yanayotanguzana na mateso na Kifo unaweza ukalielewa lakini ni gumu sana kulifuata katika maisha. Ndiyo maana Yesu aliwasisitizia wanafunzi wake na kuwaambia: "yashikeni maneno haya masikioni mwenu" na kuwatabiria kuwa "Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu." Wanafunzi wakajidai hamnazo: "Hawakuelewa maana ya neno lile lakini wakaogopa kumwuliza maswali." Yaani, walielewa maana ya upendo lakini waliogopa ugumu wa kuwajibika ndiyo maana hawakuuliza swali. Binadamu tunahitaji kuwa na akili ya kujua mafumbo ya kimungu, yaani kujua kwamba maisha ya upendo wa kimungu yanaendana na Msalaba na hivi kuwajibika.
Ndugu zangu, utangulizi huu unalenga kutusaidia kuelewa ujumbe ulioko kwenye Injili ya leo ya Kung'ara Yesu mbele ya wanafunzi wake. Leo tutayashuhudia mang'amuzi ya kiroho ya wanafunzi hawa watatu waliyojionea mubashara. Ni dhahiri pia kwamba wanafunzi hawa waliandaliwa vya kutosha ili kwa njia ya paji la akili la Roho Mtakatifu waweze kulitambua Fumbo la upendo wa Mungu. Mwinjili Mathayo anatuletea lugha ya Kibiblia ili tupate akili ya kuweza kuwa na mang'amuzi kama ya wale wanafunzi watatu mlimani. Endapo hatutafaulu kufikia kiwango hicho cha akili walichofikia wanafunzi hawa, basi hatutakuwa na nguvu wala motisha ya kuweza kufasiri vyema ujumbe wa leo.
Kwanza kabisa tunaelezwa muda wa tukio kwamba ilikuwa "Siku sita baadaye". Hapa tunatakiwa tukumbuke kilichotokea siku hizo sita kabla pale Yesu na Mitume wake walipokuwa Chesarea Filipo. Yesu aliwauliza wanafunzi wake swali zito: "Watu wanasema mimi ni nani?" Petro akajibu: "Wewe ni Masiha." Yesu akampongeza na akaendelea kuwaeleza kuwa "ataenda Yerusalemu atakakoshikwa na wazee, waandishi na makuhani nao watamshtaki na kumhukumu kifo. Lakini hatimaye atafufuka." Kuonesha kwamba Petro alijibu “kikasuku”, kwa sababu alikosa akili ya kuelewa Fumbo la Mungu la Upendo na mateso, akamvutia Yesu chemba na kumwonya vikali kwamba hiyo ni nuksi, asilogwe kusema hivyo tena. Petro anaweka: vizingiti, vigingi au vizuizi katikati ya njia ambayo Mungu Baba amemtengenezea mwanae Yesu kuipita. Yeyote anayeweka vizuizi anaitwa Shetani, Ibilisi Ndiyo maana Yesu anamwambia Petro: "Nenda nyuma yangu Shetani, kwa sababu unafikiri kadiri ya ulimwengu huu." Onyo ili zito lilimkuna Petro, na kumtafakarisha sana, kama mtu mzima! Aidha yaonekana hata wanafunzi wengine baada ya kuishi na Yesu kwa takribani miaka mitatu waliposikia maneno hayo wakayatafakari.
Hadi hapo yaonekana mafundisho ya Yesu yalianza kuzama akilini mwa wanafunzi wake na yalianza kufanya mageuzi mioyoni mwao. Ndipo Yesu alipowachagua wachache walioonekana akili zimefunguka kidogo kuweza kulitambua fumbo hilo jipya litakalomtokea Kristo, yaani kung'ara kwake. Anawachukua na kwenda nao mlimani. Katika Biblia mlimani maana yake ni ulimwengu wa Mungu. Huko juu Mlimani unakutana na Mungu na kutafakari, kutathmini na kuhukumu kadiri ya mawazo ya Mungu. Tofauti na maisha au fikra za bondeni kwenye machozi au sehemu ya uwanda walikojaa watu wengi na kwenye mzunguko mkubwa wa mawazo yasiyo na uhusiano wowote na fikra za kimungu.
Yesu anawaongoza Petro, Yakobo na Yohane kwenda mlimani ili sasa wakaione sura ya Kristo kwa mtazamo (mwanga) wa akili ya Kimungu. "Kwa mwanga wako tunaona mwanga" (Zab. 36:9). Kwa hiyo ukitaka kuwa na mang'amuzi ya akili na mawazo ya Roho wa Mungu, yabidi kujitenga kidogo na maisha ya kawaida, kujitenga na pilika pilika, vurugu za maisha na kuingia katika ulimwengu wa ukimya na kufikiria juu ya maisha yako. Wale wanaomfuata Yesu na kuingia katika akili ya Mungu wanafanikiwa kuwa na mang'amuzi kama waliyokuwa nayo wanafunzi hawa watatu. Wanafunzi hawa wanamwona Yesu amebadilika yaani "anang'ara". Kwa mtazamo wa watu wa ulimwengu huu (watu walioko bondeni) hatima ya Yesu ya kushindwa kabisa ilionekana kunyata kama buu lisilo na sura ya kupendeza. Wasijue kwamba hatua hiyo ya kuwa buu ni ya mpito tu. Kumbe hali halisi ya Yesu ni kama ya kipepeo kinachopendeza yaani ni kung'ara. Kwa hiyo wanafunzi wanashuhudia wenyewe mabadiliko hayo y kupendeza. Yesu anaonesha utukufu halisi wa mtu anayependa.
Aidha kuna picha nyingine mbili ya Kibiblia inayoambatana na kung'ara. Mosi, "Sura yake iling'aa kama jua." Jua ni picha ya utukufu wa Mungu, wenye kujaa mwanga usiofifia. Pili, "Mavazi yalimeremeta, yakawa meupe mno," rangi nyeupe inamaanisha ulimwengu wa Mungu. Kama ilivyokuwa Pasaka, Malaika wa Bwana mwenye mavazi meupe na uso wake uking'ara kama barafu alishuka kutoka mbinguni, akaja akaliviringisha lile jiwe akalikalia. Kadhalika mavazi ni kitambulisho cha mtu. Yesu aliyevaa vazi la ubinadamu sasa vazi hilo linang'ara mwanga wa akili ya kimungu. Kwamba fumbo hilo la upendo wa Mungu sasa unang'ara katika Yesu. Ama kweli hakuna binadamu mwingine zaidi ya Yesu aliyeonesha upendo wa Mungu unaong'ara. Picha nyingine inayoonekana ni Manabii Musa na Eliya. Kila mmoja wa Manabii hawa aliwahi kukwea mlimani ili kuuona utukufu wa Mungu, lakini hawakuuona. Musa alimwuliza Mungu "nioneshe utukufu wako." Mungu akamjibu "Wewe huwezi kuona uso wangu, kwa sababu hakuna anayeweza kuona uso wangu halafu akabaki mzima." Hapo Musa anaingia pangoni. Mungu anaweka uso wake kwenye mkono wake na kumwambia utauona mgongo wangu tu na siyo uso wangu, kwani huwezi ukautafakuri utukufu wa Mungu.
Kadhalika Nabii Eliya baada ya kumtoroka mfalme Jezebel baada ya kuwaua makuhani wa Baal. Kwa vile Mungu wa Agano la kale ni mkali, hivi Eliya alidhani amefanya jambo linalompendeza Mungu. Akadiriki hata kumkasirikia Mungu kwa vile hakumpigania. Ndiyo maana Eliya alipanda mlimani ili kuiona sura ya Mungu. Alitegemea kuiona katika tetemeko, katika moto mkali, katika kimbunga. Lakini asijue Fumbo la upendo wa Mungu limo katika upepo mwororo. Eliya anapofumba uso wake ndipo hapo unapita utukufu wa Mungu ambao hawezi kuuona. Sasa watu hawa watatu wanatafakari pamoja juu sura halisi ya Mungu. Kwa hiyo sasa hata Manabii inawabidi wabadili fikra na kukubaliana na ukweli mpya juu ya picha halisi ya Mungu ya upendo. Kwamba uso kweli wa Mungu, siyo ule wa nguvu, mabavu, moto, mtetemeko, kimbunga, wa Mungu anayeadhibu wahalifu. La hasha, bali ni huruma na upendo. Ukiwa na Yesu tu ndipo unaweza kuuona utukufu wa Mungu uking'ara. Kama sisi hatuwi na mang'amuzi haya ya mabadiliko (metamorphos) kama utukufu haupo katika upendo katika kutoa maisha yetu, hapo hatuwezi kuelewe uso unaong'ara wa Yesu.
Kisha Petro anabwabwata maneno yafuatayo baada ya kuyashuhudia hayo: "Rabi ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako, wewe, kimoja cha Mungu na kimoja cha Eliya. Kukasikika sauti ikatoka uwinguni. Huyu ni Mwanangu Mpendwa wangu msikieni yeye." Petro alibaki anashangaa juu ya uzuri wa Mungu unaoonekana katika Kristo. Hapa hata sisi tunaalikwa kuutambua na kuushangaa uzuri huu wa Mungu kwa kukwea mlimani, tubandukane na picha potofu ya Mungu tuliyo nayo. Bali tumwangalie Mungu katika uso wa Kristo. Petro anataka kujenga vibanda ili abakie hapo. Asijue kwamba hapo siyo mwisho wa reli “kama ilivyo Kigoma”. Inabidi kushuka bondeni kwenye maisha ya kawaida, kutoka Kanisani na kuingia kazini, lakini sasa kwa namna tofauti, ili kutumikia na kutotafuta utukufu wa ulimwengu huu kunakowapelekea wengi kumeza na malimwengu. Bali ni kurudi ulimwengu ukiwa na uso unaong'ara.
Wakati Petro anaendelea kuongea "Wingu likaja kuwafunika." Wingu lugha ya kibiblia linamaanisha uwepo wa Mungu kama wingu lile lililowatangulia Waisraeli jangwani. Yaani mhubiri yambidi ajisikie kuwa amefunikwa, ametandwa na uwepo na ulinzi wa Mungu unaomwongoza katika maisha halisi ya hapa ulimwenguni. Kisha tunasikia "sauti kutoka mbinguni". Kadhalika katika Biblia "sauti" inadhihirisha uwepo wa Mungu unaothibitisha kitendo kinachoonekana. Yaani, sauti hii ina mtambulisha Yesu kuwa mwana mpendwa mwenye DNA au Roho inayofanana kabisa na Mungu Baba yake. Katika Injili sauti hii ya Mungu inajitokeza mara mbili: Mosi wakati wa ubatizo wa Yesu. "Huyu ni mwanangu mpenzi niliyependezwa naye." Kwa vile hadi hapo hakuwa ameanza kuhubiri hatusikii maneno haya "Msikilizeni yeye" Kwa vile hakuwa amedhihirisha uso wake. Lakini leo anapong'ara sura, tunamsikia Mungu anaongeza kusema: "Msikilizeni yeye." Kwani ameshahubiri tayari.
Siku sita kabla Yesu alishatoa tamko zito: "Jikane mwenyewe. “Pambana na hali yako”. Fanya maamuzi magumu ya kuwa mtumwa, utoe maisha yako kwa ajili ya upendo." Kwa hiyo sasa Mungu anatoa pendekezo kuwa: "Tafadhali mumsikilie huyo anayeng'ara upendo." Kisha hali ya "wanafunzi kulala kifudifudi wakiogopa mno." inadhahirisha kwamba walichokiona kimewagusa, na sasa wanayo akili ya kutambua fumbo la Mungu la upendo kuwa linadai sadaka ya kujitoa maisha yao. Hata kwetu pia, kama hatushangai na kushtuka tunaposikia mabadiliko hayo, hapo ni dhahiri kwamba hatujalielewa fumbo hili la upendo wa Mungu. Kisha tunamwona Yesu anawakaribia, anawagusa na kuwaambia amkeni. Neno la Kigiriki “egerthete” lililotumika hapa linamaanisha kufufuka. Yesu anawaambia wanafunzi wake badilikeni, fufukeni kutoka wafu, muwe watu wapya waliopitia mang'amuzi mazito ya maisha. Ndipo wanafunzi wanafungua macho na wanamwona Yesu yuko peke yake. Mwito kwetu kipindi hiki cha Kwaresima ni kuinua uso na kumwona Yesu na kumtafakari yeye, na tusiwe watu wa kushangaa-shangaa mbwembwe nyingine za duniani. Hii ndiyo akili ya Mungu. Amkeni kumekucha! Yaani hadi raha inatikisa na kugusakatika undani wa maisha! Huu ndio utamu wa Neno la Mungu wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima! Mrushie Jirani yako!