Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Kwaresima: Mateso!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari masomo ya dominika ya 4 ya Kwaresima, Dominika ambayo huitwa pia Dominika ya furaha (Domenica laetare). Dominika hii imepata jina hili kutoka katika maneno ya wimbo wake wa mwanzo yasemayo “Furahi Yerusalemu na shangilieni ninyi nyote mmpendao”. Furaha hii pia ni dokezo la furaha ya Pasaka ambayo kwa dominika hii, safari ya Kwaresima inakuwa imevuka nusu ya maandalizi yake. Somo la kwanza (Sam. 16:1b,4,6-7,10-13) ni kutoka Kitabu cha Samweli. Ni somo linaloeleza namna ambavyo Mungu alimtuma Samweli kwenda kumpaka mafuta Daudi awe mfalme wa Israeli. Wafalme na makuhani walipakwa mafuta kama alama ya kuwatakasa na kuwaweka wakfu kwa Mungu. Mafuta matakatifu yaliwapa hadhi na nafasi ya pekee katika huduma walizotakiwa kutoa ndani ya taifa la Mungu. Lakini pia mafuta haya matakatifu yaliwaweka katika uhusiano wa pekee na Mungu aliyewaita katika huduma hiyo.
Somo linaonesha pia namna ambayo Mungu anawachagua watu kwa huduma yake. Yeye haangalii mambo ya nje, ambayo mara nyingi hugusa mambo ya nje ya mtu, bali Yeye huangalia moyo wa mtu. Ndivyo pia somo linavoonesha dhana hii kwa Mungu kumchagua Daudi ambaye ni mdogo kabisa kati ya wana wa Yese na ambaye hata Yese mwenyewe hakumfikiria. Kupitia picha hii ya udogo wa umri, somo linatupa maana pana zaidi ya kitaalimungu ya kuishi kwa kutokuwa na hatia mbele ya Mungu ili kustahili kupokea na kuziishi vema baraka zake. Somo hili linadokeza dhana ya ubatizo. Kipindi cha Kwaresima ni kipindi ambacho katika utamaduni kwa Kikristo hutumika pia kuwaandaa wakatekumeni kwa ajili ya kupokea ubatizo lakini pia kutupitisha sote tuliokwisha batizwa katika safari hiyo hiyo. Ndiyo maana sote kwa pamoja katika kusherehekea Pasaka ya Bwana, tunarudia ahadi za ubatizo na kunyunyiziwa tena maji ya baraka. Ni kwa jinsi hii, somo hili linatualika kukumbuka kuwa kama Daudi nasi tumeitwa, tumechaguliwa na kupakwa mafuta matakatifu, tukawekwa wakfu kwa ajili ya Bwana. Hivyo tunapewa mwaliko wa kuutunza ule udogo wetu, yaani kuyatunza maisha yasiyo na hatia mbele ya Mungu kama ulivyo mwito wetu wa kuwa wakristo.
Somo la pili (Ef. 5:8-14) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso. Somo hili pia linaendeleza dhana ya ubatizo ambayo tumeiona katika somo la kwanza. Hapa Paulo anaongelea hali ya wakristo wa Efeso kabla na baada ya kuwa wamebatizwa. Anawakumbusha kuwa kabla ya ubatizo walikuwa wanaishi gizani. Baada ya ubatizo sasa wanaishi katika mwanga, tena wao wenyewe wamekuwa mwanga. Hivyo anawaalika waishi kadiri iwapasavyo waana wa Mwanga. Mwanga huo ni Kristo ambaye licha ya kuwaangazia wote waliompokea kwa ubatizo, wote hao wanamvaa na kuwa Kristo mwingine. Jina lenyewe “Kristo” maana yake ni “mpakwa Mafuta”. Kumbe wote wanaobatizwa kwa jina lake na kupakwa mafuta wanakuwa kweli Kristo mwingine na ndiyo maana ya kuchukua jina “M-Kristo”.
Injili (Yn. 9:1-41) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa Mwinjili Yohane na inahusu tukio la Yesu kumponya mtu aliyezaliwa kipofu. Vipengele vichache vitatusaidia kulifafanua somo hili. Kwanza ni swali la wanafunzi kuwa ni yupi aliyetenda dhambi hadi mtu huyu azaliwe kipofu, Je, ni wazazi wake au ni yeye mwenyewe? Na Yesu anawajibu akisema “huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake bali ni ili kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”. Katika nafasi nyingine, ugonjwa wenyewe wa upofu ni ugonjwa ambao umetumika katika mapokeo ya mwanzo ya ukristo kama alama ya ukosefu wa imani. Hapo imani ilieleweka kama mwanga unaomuwezesha mtu kuona, yaani kuuona mkono wa Mungu katika yote yanayoonekana ulimwenguni. Kwa jinsi hii, muujiza huu wa kumponya mtu aliyezaliwa kipofu unaonesha muhtasari wa kazi nzima ambayo Yesu alikuja kuifanya duniani, yaani kuuamsha ulimwengu uliokuwa katika giza la dhambi ili uweze kuangazwa kwa mwanga wa imani na kumgeukia Mungu. Ndiyo maana mwisho wa majibizano yote Yesu anamuuliza yule aliyeponywa, “wewe wamwamini Mwana wa Mungu” naye akajibu “ni nani nipate kumwamini” na Yesu akamwambia “umemwona.” Hapo akasema “Naamini, Bwana” akamsujudia.
Injili hii pia kwa namna ya pekee, inaonesha utimilifu wa unabii wa Simeoni kuwa Yesu atakuwa ni “alama ya kunenewa”. Hii inaonekana katika mabishano yanayoibuka kati ya Mafarisayo na yule mtu aliyeponywa. Kitu ambacho kingeweza kuwa wazi kabisa, yaani tendo jema la kuponywa mtu kipofu, kwa Mafarisayo kinakuwa ni kitu ambacho hakiwaingii akilini. Mabishano ya kauli yanayotokana na kazi njema ya Yesu ndiyo yatakayokuzwa na kuwa mashtaka ambayo yatapekekea kushtakiwa kwa Yesu, kusulubiwa na kuuwawa Msalabani. Kwetu tunaoisikiliza injili hii leo, tunapewa mwaliko wa kuomba kuimarishiwa imani yetu. Tuzidi kuipokea imani kama mwanga unaotuwezesha kuuona vema ulimwengu na kuyatafsiri yote katika mpango mwema wa Mungu kwa ulimwengu na kwa viumbe vyake vyote.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo na kupata ufafanuzi wake, nawaalika sasa tuingie katika tafakari yake kwa fupi. Katika tafakari ya leo, nawaalika tujikite katika Injili na kwa namna ya pekee katika lile swali ambalo wanafunzi walimuuliza Yesu kuhusu yule mtu aliyezaliwa kipofu; “Je, ni yupi aliyetenda dhambi hadi mtu huyu azaliwe kipofu? Ni yeye mwenyewe au ni wazazi wake?” Swali hili lilitokana na mapokeo ya Wayahudi kuwa magonjwa na majanga yanayompata mwanadamu huja kwa sababu ya dhambi za mwanadamu. Mapokeo haya yalikuwa na chimbuko lake katika sheria ya Musa, sheria ambayo baada ya kuelekeza yote ambayo waisraeli walitakiwa kuyafanya na baada ya kuaninisha yote ambayo hawakutakiwa kuyafanya, ilihitimisha kwa kusema kuwahakikishia kuwa wataishi kwa amani na furaha endapo tu wataishika kiaminifu sheria hiyo. Kinyume chake watakaribisha hasira na laana ya Mwenyezi Mungu.
Mungu mwenyewe katika mwendelezo wa ufunuo kwa watu wake alianza kuwaonesha kuwa si lazima kila wanapomwona mtu anayeteseka au aliyekumbwa na majanga waseme kuwa yamempata kwa sababu ya dhambi zake. Tena si kila wanapoona mtu amefanikiwa wakasema amefanikiwa kwa sababu ya uadilifu wake na hivo yote ayafanyayo yamepata kibali mbele ya Mungu. Katika kisa cha Ayubu na katika sura za Mtumishi wa Bwana katika kitabu cha Nabii Isaya, Mungu alianza kuwaonesha kuwa wapo wanaoteseka si kwa sababu ya dhambi bali wanateseka kama sehemu ya Mapenzi ya Mungu. Jibu la Yesu kwa wanafunzi wake linaendeleza ufunuo huo wa Mwenyezi Mungu juu ya Fumbo la mateso ya mwanadamu, jibu ambalo litapata utimilifu wa ufunuo pale ambapo yeye mwenyewe, mtu asiye na dhambi, atateseka na kufa msalabani. Ni jibu ambalo linafungua mlango kwa Taalimungu ya Kikristo juu ya Fumbo la mateso na hivi kutoa mwono wa Kikristo.
Katika Taalimungu hii, tafsiri ya mateso, magonjwa au majanga mbalimbali yanayomkuta mwanadamu haipatikani sana kwa kujiuliza ni nini au ni nani kayasababisha bali katika kutafakari Mungu ana lengo gani kwangu au kwetu katika haya tunayopitia. Ndiyo maana Yesu hawajibu wanafunzi wake kama ni mtu huyo au ni wazazi wake au ni majirani zake ndio waliotenda dhambi. Yeye anapojubu anasema “yametokea ili kazi za Mungu zidhihirike ndani yake”. Tafsiri ya Fumbo la mateso ni katika mwisho wake, sio katika mwanzo. Taalimungu hii isaidie kutupa mwanga hasa katika kipindi hiki ambacho dunia nzima inahangaika dhidi ya maambukizi na vifo vinavyotokana na virusi vya Corona. Kama anavyotualika Baba Mtakatifu Francisko, tuendelee kushirikiana na kuzingatia miongozo ya kiusalama na tuzidi kudumisha mshikamano wa sala. Pale ambapo upeo wa mwanadamu unakoma, ni nguvu ya imani tu inayoweza kuendelea kutoa matumaini ya kusonga mbele. Dominika hii iliyo pia dominika ya furaha, iijaze mioyo yetu na furaha ya uwepo usiokoma wa Mungu katika maisha yetu.