Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Utukufu wa Kristo Yesu umetundikwa katika Fumbo la Msalaba! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Utukufu wa Kristo Yesu umetundikwa katika Fumbo la Msalaba! 

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Pili ya Kwaresima: Mateso na Utukufu wa Kristo Yesu!

Kugeuka sura kwa Kristo Yesu kunafunua umungu wake na kuonyesha kuwa yeye ni ukamilifu wa Sheria na Manabii kwa kuonekana na kutoweka kwa Musa na Eliya. Hitimisho la matukio haya ni sauti ya Baba iliyosikika na kudhibitisha kuwa Yesu Kristo ni nafsi ya pili ya Mungu na ni mwana wa Mungu akisema: “Huyu ni Mwanangu, mteule; Msikilizeni yeye.” Yaani tekelezeni ujumbe wake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, domenika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Wahusika wakuu katika ujumbe wa domenika hii ni wawili Ibrahimu Baba wa Imani ana Yesu mwana mpendwa wa Mungu. Kuitwa kwa Ibrahimu na kuambiwa toka wewe katika nchi yako, ni mwangwi wa kunaitwa kwa kila mmoja wetu kutoka katika dhambi kuingie katika utukufu unaojidhihirisha kwa Yesu kwa kugeuka sura. Leo ni siku ya kumi na mbili tangu tuanze kipindi hiki cha majiundo yetu ya kiroho kwa kusali, kufunga au kujikatalia na kujinyima yale tuyapendayo kwa ajili ya wengine hasa wahitaji ili tujipatanishe na Mungu. Masomo ya domenika ya kwanza ya Kwaresima yalitupeleka nyikani ili kutupa nguvu ya kuyashida majaribu ya shetani. Masomo ya domenika hii ya pili yanatutoa nyikani kwenye majaribu yanatupeleka juu ya mlima ili kukutana na Mungu katika utukufu wake na kutuonyesha uzuri wa kuyashida majaribu.

Kugeuka sura kwa Kristo kunafunua umungu wake na kuonyesha kuwa yeye ni ukamilifu wa Sheria na Manabii kwa kuonekana na kutoweka kwa Musa na Eliya. Hitimisho la matukio haya ni sauti ya Baba iliyosikika na kudhibitisha kuwa Yesu Kristo ni nafsi ya pili ya Mungu na ni mwana wa Mungu akisema: “Huyu ni Mwanangu, mteule; Msikilizeni yeye.” Tukio hili la kugeuka Sura kwa Yesu linatokea wakati Yesu anasali akiwa pamoja na wanafunzi wake watatu; Petro, Yohane na Yakobo mlimani Tabor. Hii inatonyesha dhamani na nguvu ya sala. Sala ina nguvu ya kuzifungua mbingu na kumfanya Mungu ashuke na kusema nasi. Ndiyo maana tunasema, sala ni kuongea na Mungu. Sala ni kuinua macho yetu ya akili na roho mbele za Mungu. Sala ni mawasiliano kati ya Mungu na Mwanadamu. Ndiyo maana moja ya nguzo kuu ya kipindi cha kwaresima na kusali kwa bidii tena bila unafiki. Katika tukio hili wanatokea Musa na Eliya na baadae wanatoweka na hapo Mungu anawaambia Mitume Petro, Yohane na Yakobo kuwa Yesu ni mwanaye mteule wamsikilize yeye.

Leo hii Mungu mwenyewe anatuambia tuwe wasikivu kwa Mwanaye. Nyakati zetu Yesu anaongea nasi katika Neno lake linaposomwa na kufafanuliwa tunaambiwa tulisikilize. Kama wanavyosema waswahili sikio la kufa halisikii dawa, domenika hii tumwombe Mungu atujalie neema ya kusikia na pia atujalie sikio la kuishi na sio la kufa! Kugeuka sura kwa Yesu kunakuja baada ya Petro kumkiri kuwa yeye ndiye Masiha, Mwana wa Mungu aliye hai {Mt16:13-15}, tena baada ya Yesu kuwatabiria juu ya mateso, kifo na ufufuko wake (Mt 16:21-22) na kuwapa masharti ya kumfuata yeye akisema anayetaka kuwa mfuasi wake, auchukue msalaba wake aubebe na kumfuata {Mt16:24}. Matukio haya yalikuwa kikwazo kwa wafuasi wake hata wengine wakataka kurudi nyuma na kuondoka hata Mtume Petro akamwambia, Bwana hili halitakupata, na Yesu akamkemea na kumwambia, rudi nyuma yangu shetani wewe. Hata sisi tunapopingana na mpango wa Mungu kwa namna yoyote ili Yesu anatuambia rudi nyuma yangu shetani wewe.

Kumbe, tukio hili la kugeuka sura kwa Yesu ni kielelezo wazi kwa wafuasi wake kwamba mateso na utukufu vinaambatana. Hawa wanafunzi watatu walichukuliwa ili wakija kuwasimuliwa wengine wengine waweze kukubali kuwa ni kweli kwani kwa Wayahudi ili jambo zito kama hilo liweze kukubalika lilihitaji mashahidi watatu tena wanaume. Kwa tukio la kugeuka sura, Yesu aliwaonesha wazi wafuasi wake utukufu atakaoupata kwa njia ya mateso na kifo. Hali hiyo ya utukufu iliwavutia sana wafuasi wake na kuwafanya wayapokee mateso ya Kristo kadiri ya mpango wa Mungu Baba. Wakawa tayari kumfuata Yesu katika njia hiyo ya mateso hata kukubali nao kufa vifo dini, kama mashuhuda wa imani ambayo sisi nasi tumeipokea.

Nasi leo, tunakumbushwa kuwa tayari kuyapokea mateso tunayopata katika kutekeleza wajibu wetu wa kumfuata Kristo. Wazazi muwe tayari kuyavumilia magumu yanayowapata katika kuutekeleza wajibu wa kikristo kama wazazi. Yawapasa kuvumiliana tofauti zenu kitabia, kimaweza, kiafya na katika magonjwa na taabu mbalimbali. Kwa uvumilivu na saburi mnapaswa kuwatunza na kuwalea watoto wenu ipasavyo bila kukata tamaa pale wanapokosa utii mbele yenu. Mapadre, walimu na walezi, tunawajibu mzito zaidi, wa kutumia nguvu, akili, muda, ili kuwalea watu wote, watoto, vijana na wazee kiroho, kimaadili, kifikra na hata kiakili ili wawe kweli watu wa Mungu waufikie utukufu wake.

Ndivyo alivyofanya Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Timotheo, akiwa gerezani Roma, anamhimiza Timotheo mhubiri chipukizi, Askofu kijana wa Efeso, aliyeitwa na kupewa neema ya Mungu kwa kuwekewa mikono na Paulo mwenyewe, asikatishwe tamaa katika utume wake bali avumilie mateso akizitumia nguvu alizojaliwa na Mungu kushiriki mateso kwa ajili ya Enjili. Na sisi tuliokombolewa, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi na neema zake Mungu, tunaitwa ili kwa neema hiyo tuliyoipewa katika Kristo Yesu kwa njia ya ubatizo, na umauti wetu ukabatilishwa na kufunuliwa uzima usioharibika hata milele yote tuishuhudie hii imani kama Ibrahimu Baba yetu wa Imani.

Katika somo la kwanza la Kitabu cha Mwanzo, Mungu anamwita Ibrahimu na kumwambia; Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Ibrahimu akatii, kwa imani akaondoka, akaacha yote, akajikabidhi mikononi mwa Mungu, akawa Baba wa Imani na chanzo cha baraka kwa mataifa yote. Nasi leo tunaitwa tutoke. Swali tutoke wapi na tuende wapi? Tutoke katika maisha tuliyoyazoea, maisha ya dhambi, twende tukamsikilize Yesu, Mwana wa Mungu ili tukawe warithi wa ufalme wake. Kila mmoja anaitwa kwa jina lake na kuambiwa, toka wewe katika tamaa zako, toka wewe katika dhambi zako, nenda ukapate neno la uzima wa milele. Na hii inawezekana kwa imani dhabiti. Tumsifu Yesu Kristo.

tafakari Jumapili 2 ya Kwaresima
06 March 2020, 17:08