Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili II ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu anageuka sura mbele ya wanafunzi wake. Utimilifu wa sheria na unabii! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili II ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu anageuka sura mbele ya wanafunzi wake. Utimilifu wa sheria na unabii! 

Tafakari Jumapili 2 ya Kwaresima: Utimilifu wa Torati na Unabii!

Mama kanisa katika Injili ya Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima kumsikiliza Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, utimilifu wa Sheria na Unabii kutoka katika Agano la Kale. Tukio la Yesu kugeuka mbele ya wanafunzi wake watatu ni kutaka kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, ili waweze kuwa imara kupambana na kashfa ya Msalaba: mateso, kifo na ufufuko wake!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Sehemu ya Injili ya Dominika ya leo tunasikia juu ya simulizi la kugeuka sura juu ya mlima mrefu akiwa pamoja wanafunzi wake watatu nao ni Petro, Yakobo na Yohana nduguye. Yafaa tangu mwanzo kuwa makini tunapokutana na masimulizi yanayohitaji maelezo ya kina ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa kwani kinyume chake tunaweza kuishia kudhani kuwa Mwinjili Mathayo anajaribu kutupa simulizi tu na jinsi lilivyojiri. Simulizi la kugeuka sura Yesu juu mlimani karibu linasimuliwa na wainjili wa Injili zote ndugu karibu katika mtindo na namna inayofanana sana. Leo tunasikia kutoka Mwinjili Mathayo. Mwinjili anaanza kwa kutueleza ‘’Baada ya siku sita’’ na hapo tunakuwa na maswali ni siku sita baada ya nini? Kwa kweli hasemi waziwazi ila yawezekana kabisa ni siku sita baada ya tukio la Yesu kuwapa mtihani wanafunzi wake wakiwa katika mji wa Kaisaria Filipo juu ya utambulisho wake. Ni katika mji ule wa kipagani Yesu anawauliza wanafunzi wake watu wanamsema Yeye kuwa ni nani na mwishoni anawageukia pia wanafunzi wake kutaka kusikia nao wanamtambua Yesu kama nani? Mathayo 16:13-20.  Lakini swali lingine kwa nini Yesu anaamua kwenda juu mlimani na wanafunzi wale watatu tu?

Katika Injili ya Mathayo tunaona kila mara Yesu anapotaka kutenda au kufundisha jambo lenye umuhimu mkubwa tunaona anapanda juu mlimani. Katika jaribu la mwisho la Somo la Injili ya Dominika iliyopita tunaona Yesu anajaribiwa akiwa juu ya mlima mrefu. (Mathayo 4:8). Mafundisho ya Heri yanatolewa juu mlimani. (Mathayo 5:1). Muujiza wa kulisha watu mikate unafanyika pia mlimani. (Mathayo 15:29). Na mwisho wa Injili ya Mathayo tunaona Yesu Mfufuka anakutana na wanafunzi wake na kuwatuma kwenda ulimwenguni kote wakiwa juu ya mlima ule walioagizwa. (Mathayo 27:16). Mlimani kadiri ya Agano la Kale daima ni sehemu inayoonesha ujumbe wa kiteolojia kuwa ni mahali pakukutana na Mungu. Juu ya mlima Sinai, Musa anapokea maagizo au amri zile za Mungu na pia Elia juu ya mlima Horebu anakutana na Mungu. Lakini tukizidi kusoma Agano la Kale tunaona hata Musa ilikuwa ni baada ya siku sita alipanda mlimani tunasoma Kutoka 24:16 na hapandi peke yake bali pamoja naye ni Aroni, Nadabu na Abihu na wakafunikwa na wingu tunasoma kitabu cha Kutoka 24: 1,9. Na wakiwa juu mlimani uso wa Musa ukageuka na kung’aa. Kutoka 34:30 ‘’Aroni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unang’aa’’.

Natumaini sasa tumepata mwanga kuwa Mwinjili Mathayo anamtambulisha Yesu kama Musa mpya anayekwenda mlimani ili kuwaletea watu wake sheria mpya akiwa na wanafunzi wake watatu kama alivyofanya Musa. ‘’…Uso wake ukang’aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga’’. (Mathayo 17:2) Hata ishara hizi pia tunakutana nazo katika Maandiko Matakatifu yaani Agano la Kale. Zaburi 104:1-2 ‘’Umsifu Mwenyezi Mungu ee nafsi yangu! Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu mno! Umejivika utukufu wa fahari. Umejizungushia mwanga kama vazi…’’ Hivyo ni ishara zinazotumika kuonesha uwepo na hasa ukuu wa Mungu na ndio Mwinjili anazitumia pia kutuonesha kuwa ni katika Nafsi ya Yesu tunakutana na Mungu katika ukuu na utukufu wake. Wingu jeupe lililowafunika tunaweza kufanya rejea pia katika Kitabu cha Kutoka 13:21 ambapo Mungu aliwaongoza watu wake mchana na usiku katika ishara hiyo ya wingu. Musa akiwa mlimani tunaona pia mlima ulifunikwa na wingu, Kutoka 24:15-16 na hata wakati anashuka kutoka mlimani sura ya Musa iling’aa Kutoka 39:29-35. Hivyo ishara za wingu na kung’aa sura nazo ni ishara zenye kuonesha uwepo wa Mungu.

Ndio kusema Mitume wale watatu Petro, Yakobo na Yohane wanatambulishwa juu ya utambulisho halisi wa Yesu ‘’His true identity’’ lakini hasa lengo la ujio wake ulimwenguni. Siyo Masiha kwa jinsi walivyokuwa wanafikiri wao bali baaada ya kukataliwa na wakuu wa dini alipaswa kupitia mateso na kifo na mwisho kufufuka. Na hata wao kama wanafunzi wake hawana budi kupitia njia ile ile kama ya Bwana na Mwalimu wao. Sauti kutoka mbinguni (Mathayo 17:5), ilikuwa ni aina ya uandishi iliyotumiwa pia na Marabi katika kufanya hitimisho la kuonesha kuwa ni mawazo ya Mungu mwenyewe. Sura iliyotangulia ile ya 16 ilikuwa ni juu ya utambulisho wa Yesu. Yesu alianza kuwauliza wanafunzi wake watu wanamnena kuwa ni nani? Baada ya kusikia majibu au mitazamo ya watu wengine mwishoni anawauliza pia wanafunzi wake na Simoni Petro anajibu kuwa ni Masiha. Sauti kutoka mbinguni leo inamtambulisha Yesu kuwa; ‘’Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni.’’ Ni Mwana mpendwa aliyependezwa na Baba kama tunavyoweza kusoma katika Kitabu cha Nabii Isaya 42:1

Siku ile ya Ubatizo wa Yesu pale mtoni Yordani ilisikika pia sauti kuwa ‘Huyu ni Mwana wangu niliyependezwa naye’, (Mathayo 3:17), ila leo unaongezeka ujumbe zaidi wa ‘’msikilizeni’’ hata pale anapotualika kupitia njia ngumu na mateso na madhurumu bado mwaliko wa Mungu Baba kwetu ni kumsikiliza Yesu. Na ndio safari yetu ya Kwaresma kila mara ni kukaa karibu naye kwa sala na tafakari ili kila mmoja wetu aweze kutambua ni misheni gani ninayoitiwa na Bwana na Mwalimu wetu. Ni Neno wa Mungu, hivyo hatuna budi kumsikiliza. Nafasi ya Injili katika kipindi cha Kwaresma, si tu kuisoma bali tutenge muda wa kuwa rafiki daima wa Maandiko Matakatifu na tusikubali kuongozwa kwa akili zetu bali mang’amuzi tunayoyapata kutokana na sala na tafakari za kweli. Katika Maandiko Matakatifu kitenzi kusikiliza hakimaanishi tu kusikia kwa masikio yetu bali zaidi sana kutii, kukubali kuenenda kadiri ya Neno la Mungu. (Kutoka 6:12 na Matayo 18:15-16) Hivyo mwito wa Mungu kwa wanafunzi wale watatu ni mwito kwa kila mmoja wetu, kulisikiliza Neno na kulitii kwa maana ya kulishika, kuliweka katika maisha yangu ya kila siku. Musa na Elia ni akina nani? Musa ndiye aliyepokea sheria na amri za Mungu kwa watu wake na Elia alitambulika kama nabii wa kwanza, na hivyo watu hawa wawili kwa waisraeli walitumika kama kuwakilisha Maandiko Matakatifu.

Kama nilivyowaalika tangu awali kuwa ili kupata ujumbe kusudiwa hatuna budi kuelewa aina ya uandishi ya Mwinjili Mathayo ambaye daima anatuonesha ili kumwelewa Yesu hatuna budi kusoma kwa kuhusianisha na Agano la Kale. Na hivyo hivyo hatuwezi kuelewa Agano la Kale kama hatutalisoma kwa kulihusianisha na Yesu. Bila Yesu, Agano la Kale linabaki bila kueleweka, na pia bila Agano la Kale, Yesu anabaki kuwa fumbo lisiloeleweka kwetu. Siku ila ya Pasaka, Kristo Mfufuka anapokutana na wafuasi wale wawili wa Emausi tunaona ili waweze kuelewe fumbo la mateso na kifo na ufufuko wake anaanza kuwaeleza Maandiko yote kuanzia Agano la Kale.  Luka 24:27 Ishara ya vibanda vitatu anayosema Petro sio rahisi sana kupata maana yake. Anayefanya kibanda ni mmoja anayetaka kubaki hapo bila kutoka kwa kufanya makazi ya kudumu, yawezekana Petro alitaka waendelee kubaki katika hali ile ya utukufu. Lakini Yesu anatuonesha kuwa daima yeye ni msafiri, daima yupo safarini, na ndio maisha ya kila mkristo, tu wasafiri kila siku ya maisha yetu.Tunaalikwa kutoka iwe katika ubinafsi wetu ili tuweze kumwelekea jirani aliye muhitaji zaidi yangu.

Na hili ndio lengo la mazoezi ya kiroho kwa kipindi hiki cha neema cha Kwaresima ili tutoke katika hali zetu tunazozipenda na kufurahia kwa kumpenda Mungu zaidi na jirani. Sala, Kufunga na Matendo ya Huruma vyote lengu na shabaha lake ni kutualika kutoka katika ‘’comfortable zones’’ zetu na kuwa daima safarini. Hata baada ya kukutana na Mungu kwa namna ya pekee katika Maadhimisho yetu ya kiliturjia au sala binafsi tunaalikwa daima kutoka na kwenda kutumikia wengine, kwenda kuwashirikisha wengine mema na ukuu wa Mungu. Kishawishi cha kujenga vibanda vitatu kwa maana ya kutaka kuendelea kubaki katika “comfortable zones” zinampata kila mmoja wetu, Kwaresma ni mwaliko wa kushuka kutoka mlimani ili nasi tuweze kwa maisha yetu kupanda mlimani ule wa Kalvari pamoja na Yesu kwa kutumikia ndugu zetu wanaokuwa wahitaji zaidi wa upendo na huruma ya Mungu. Muda wa sala na Maadhimisho ni nafasi za kutusaidia kukutana na kumsikiliza Mungu nini na wapi anatutaka kwenda na kutumika.

Kama tulivyoona kuwa hatuwezi kuelewa Agano la Kale ikiwa hatutalisoma kwa kumuhusianisha Yesu na ndio tunaona Petro anakosa bado kuelewa ‘’Identity’’ ya Yesu hata kama alimkiri kuwa ni Kristo, ni Masiha. (Mathayo 16:16). Kwake alibaki kumuona Yesu ni Masiha ila kwa mantiki ya dunia hii, mtu mkubwa na muhimu sawa kama walivyo Musa na Eliya. Na ndipo tunaona Mungu anaingilia kati kwa kumtambulisha Yesu.  Yesu si tu nabii au mmoja wa manabii bali ni ‘’Mwana mpendwa wa Mungu Baba’’. Kutaka kujenga vibanda vitatu kwa Yesu, Musa na Eliya ni sawa na kusema wanafanana kwa hadhi: Mara baada ya mazungumzo yao tunaona anabaki Yesu peke yake. Mungu alinena na watu wake mwanzoni kwa njia ya Musa na manabii ila sasa anabaki Mwana pekee wa Mungu anayenena nasi.  Ni Yeye pekee tunaalikwa na kupaswa kumsikiliza kwani Ni Neno wa Mungu.  Musa na manabii walishamaliza misheni yao tunabaki na tunaalikwa sasa kumsikiliza Mwana pekee wa Mungu Baba.  Nawatakia tafakari na Dominika Njema na Mfungo mwema wa safari ya Kwaresima jangwani kwa siku hizi za neema 40.

04 March 2020, 14:43