Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni njia, ufufuo na uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni njia, ufufuo na uzima wa milele! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili V ya Kwaresima: Ufufuo na uzima

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima. Yesu akamjibu Martha, dada yake Lazaro akisema: “Mimi ndimi huo Ufufuo na Uzima”. Maneno haya ya Yesu ambayo yanabeba kiini cha mafundisho ya muujiza wenyewe yalimaanisha kuwa yale ambayo Wayahudi walikuwa wakiyatazamia kuja siku ya Mwisho sasa yamekwisha timia. Tena yametimia katika nafsi ya Kristo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunayatafakari masomo ya dominika ya 5 ya Kwaresima. Kwa dominika hii tunaingia katika Juma la Kwanza la Mateso ambalo pia ni juma litakalotuingiza katika Juma Kuu. Ishara ya Kiliturujia ya kuingia katika Juma hili la Mateso ni kwamba kuanzia dominika hii Misalaba na anamu za watakatifu hufunikwa. Somo la kwanza (Eze. 37:12-14) ni kutoka kitabu cha nabii Ezekieli. Ujumbe mzima wa nabii Ezekieli umegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni ujumbe alioutoa kuionya Israeli dhidi ya hasira ya Mungu iliyokuwa inakuja. Ezekieli aliutoa ujumbe huu katika kipindi ambacho uasi wa waisraeli dhidi ya Mungu ulizidi kuongezeka. Watu hawakulijali tena Agano waliloweka na Mungu na walizidi kupuuzia amri na maagizo yake. Licha ya maonyo ya Nabii Ezekieli, Waisraeli hawakutubu, kuongoka na wala hawakumrudia Mungu. Mungu akaamua kuwaadhibu kwa mkono wa Babiloni.

Sehemu ya pili ya ujumbe wa Nabii Ezekieli ilikuja baada ya kuwa Waisraeli wameadhibiwa vikali na kupelekwa utumwani Babiloni. Wakiwa huko mbali na nchi yao wenyewe tena chini ya mateso na adha za utumwa waliyatambua makosa yao na kuona umuhimu wa kumrudia Mungu kwa toba. Dhamiri zao ziliwachoma wakaona jinsi ulivyokuwa mkubwa uasi wao kwa Mungu kiasi cha kukata tamaa kabisa hata ya Mungu kuwasamehe na kuurudisha upendo wake kwao.  Unabii wa Ezekieli katika somo hili la kwanza unakuja katika mazingira haya ya Waisraeli waliokata tamaa na kupondeka mioyo. Nabii anawaambia hata kama taifa zima limepoteza matumaini ya kuuonja tena upendo wa Mungu, hata kama limekuwa kama mtu aliyekufa na mifupa yake kukauka, Mungu mwenyewe atayafunua makaburi na kuirudishia mifupa uhai.

Ujumbe huu wa Nabii Ezekieli, katika nafasi ya kwanza kabisa, ni ujumbe unaoonesha nguvu ya toba ambayo mtu au taifa linaweza kuifanya mbele ya Mungu. Unaonesha nguvu ya toba kwa maana unaonesha kuwa kwa njia ya toba, Mungu anafanya uumbaji mpya juu ya mtu au taifa zima linalotubu. Ujumbe huu unakazia kuwa nafsi iliyo tayari kumrudia Mungu isikatishwe tamaa na ukubwa wa dhambi ilizotenda bali isukumwe na matumaini ya nguvu kubwa zaidi iliyo katika toba na maungamo ya kweli. Somo la pili (Rum. 8:8-11) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika waraka huu, mtume Paulo amekuwa na fundisho moja kubwa kuwa tunaokolewa kwa njia ya Imani na siyo kwa njia ya Matendo ya Sheria au Torati. Na neno hilo “kwa njia ya Imani” maana yake ni kwa njia ya “imani kwa Kristo” kwa sababu ni Kristo aliye njia pekee ya wokovu wa ulimwengu.

Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anazungumzia Imani na Torati katika lugha ya “Roho” na “Mwili”. Hii ni lugha ambayo tayari katika tamaduni za mwanzo za ukristo ilitumika kuelezea kanuni mbili za maisha zinazopingana. Roho ilimaanisha kanuni ya kimungu ambayo ni sawa na nguvu ya Mungu na Mwili ulimaanisha kanuni ya kidunia. Tena neno mwili lilitafasriwa sio katika maana ya mwili wa kibinadamu bali katika maana ya udhaifu wa kibinadamu. Kumbe Mtume Paulo katika somo hili anapotoa mwaliko kwa warumi kuwa “msiufuate mwili bali muifuae Roho”  anatoa mwaliko mpana sana wa kuwataka wayasimike maisha yao katika nguvu ya kimungu. Ndiyo maana anawakumbusha kuwa ni nguvu hiyo hiyo iliyomfufua Yesu kutoka wafu. Kwa jinsi hiyo wale wanaoyasimika maisha yao katika nguvu hiyo wataweza kuushinda udhaifu wa kidunia na kuupokea wokovu. Kwetu sisi tunaolisikiza somo hili leo, tunapewa mwaliko nasisi kutambua kuwa nguvu hizi mbili anazozungumzia Mtume Paulo, zipo kati yetu hata leo. Nidhamu tunayojiwekea katika kipindi hiki cha kwaresima ni hatua muhimu sana katika kutufundisha kuyasimika maisha yetu katika “kuifuata Roho” yaani nguvu ya kimungu inayookoa kwa njia ya Kristo.

Injili (Yn. 11:1-45) Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Yohane. Inaleta kwetu simulizi la muujiza wa Yesu kumfufua Lazaro. Katika injili nzima ya Yohane, ni miujiza 7 tu ya Yesu inayosimuliwa. Wa kwanza ni ule wa harusi ya Kana na wa mwisho ni huu wa kumfufua Lazaro. Mwinjili Yohane anauweka muujiza huu kama ndio kilele cha alama hizi kuu ambazo Yesu alizifanya kabla ya kuingia katika mateso yake. Na tena kwa kufuata tafsiri ya kibiblia ya namba 7, huu tunaweza kuuita kuwa ndio ukamilifu wa miujiza yote aliyoifanya Yesu, yaani kuurudisha uhai kwa yule aliyekuwa amekufa. Ufafanuzi wa vipengele vichache juu ya simulizi lenyewe utatusaidia kuelewa fundisho lake. Yesu alipopewa taarifa kuwa Lazaro rafiki yake ni mgonjwa, hakwenda mara moja kumwona wala kumponya kama ambayo ilitegemewa. Hata baadaye alipoambiwa amekufa, alisubiri mpaka baada ya siku 4 ndipo akaenda. Hapa tunaona kuwa Yesu alijua ni kitu gani anachotaka kufanya. Na aliamua kusubiri hadi siku 4 baada ya Lazaro kuwa amekufa ili kuondoa mashaka kama alikuwa amekufa kweli au la. Hii inatokana na mapokeo ya kiyahudi kuwa baada ya kufa, roho ya mtu hubaki katika mwili kwa siku tatu. Yesu alisubiri hadi hizo siku 3 zikaisha.

Martha alipokwenda kumpokea, alimwambia Yesu kwa uchungu kuwa “Bwana kama ungalikuwapo hapa ndugu yangu asingalikufa”. Tena akaongeza “najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho”. Maneno haya ya Martha yaliwakilisha imani ya wayahudi ambao waliamini juu ya ufufuko wa wafu. Miongoni mwa walioamini kuhusu ufufuko walikuwa ni wafarisayo. Lakini wote hao waliamini kuwa ufufuko haupo hadi siku ya mwisho. Sasa namna Wayahudi walivyoamini juu ya siku ya mwisho ni tofauti na sisi wakristo tunavyoamini juu ya siku ya mwisho. Kwa wayahudi siku ya mwisho ilikuwa ni siku ambapo Masiha waliyemtegemea atakuja. Hawakuamini kuwa masiya huyo ndiye Kristo. Kwetu sisi wakristo ambao tunaamini masiya tayari ameshakuja, Siku ya Mwisho ni siku ya ujio wake wa pili. Baada ya maneno hayo ya Martha, Yesu akamjibu akisema “Mimi ndimi huo Ufufuo na Uzima”.

Maneno haya ya Yesu ambayo yanabeba kiini cha mafundisho ya muujiza wenyewe yalimaanisha kuwa yale ambayo wayahudi walikuwa wakiyatazamia kuja siku ya Mwisho sasa yamekwisha timia. Tena yametimia katika nafsi ya Kristo. Maneno haya yanaonesha kuwa muujiza ambao Yesu anaufanya ni ufunuo mkubwa juu ya Umasiha wake. Naye Martha anapojibu anatumia maneno kama yale aliyotumia Petro kukiri umasiya wa Kristo. Anakiri “Naam Bwana , mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni”.Tendo lenyewe la kumfufua Lazaro linakuwa ni tendo linalothibitisha fundisho hilo kubwa alilolitoa Yesu kuwa Yeye kweli ndio ufufuo na uzima.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kwa dominika hii tunaingia katika Juma la Kwanza la Mateso ambalo pia ni juma litakalotuingiza katika Juma Kuu. Ishara ya Kiliturujia ya kufunika misalaba na sanamu za watakatifu, ni ishara inayopambanua roho ya toba ambayo kwa namna ya pekee ndio mwaliko wa Juma hili. Ishara hii inalo chimbuko lake katika liturujia za kitubio zilizoambatana na maadhimisho ya Kwaresima. Katika kipindi ambacho kitubio cha wadhambi sugu kilitolewa wakati wa Kwaresima, waungamaji walitengwa wasiione altare katika kipindi chote kilichotangulia kitubio chao. Hii ilikuwa ni kuwaalika waingie zaidi nafsini mwao na pia kuwajengea kile kilichoitwa “kiu ya macho” ya kupaona patakatifu pa Bwana.

Leo kanisa halitofautishi wadhambi sugu na wadhambi wa kawaida. Sote tunaalikwa kutambua kama anavyofundisha mtume Yohane kuwa “tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe”. Ni kwa mantiki hiyo Misalaba na Sanamu za watakatifu zinafunikwa kwetu sote kwa lengo lilelile la kutualika tuingie zaidi ndani yetu kuona yasiyotustahilisha kuutazama utakatifu wa Mungu na pia ili kutujengea “kiu ya macho” ya kutamani kuuona tena utakatifu huo tukiwa tumetakaswa. Masomo tuliyoyasoma na kuyafafanua yametupa matumaini kuwa toba yetu ina nguvu ya kutuumba upya. Inaweza kutuumba upya sio kiroho tu bali hata kimwili na kutufufua kutoka upotevu wa maisha kuelekea katika uzima wa wokovu wetu.

Liturujia J5
27 March 2020, 15:11