Tafuta

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huruma na upendo wa Mungu inayomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu katika hali ya unyenyekevu mkuu! Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huruma na upendo wa Mungu inayomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu katika hali ya unyenyekevu mkuu! 

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Sadaka ya Upendo na Huduma!

Ni katika karamu ile ya mwisho tunaona mategemeo na matarajio yao yanafika ukomo, ni Yesu anawafunulia kinagaubaga juu ya Umasiha wake. Ni katika kitendo cha kuwaosha miguu wanapata sasa kumtambua kuwa huyu ni mtumishi wa Bwana, ni mtumwa. Huyu ni Mungu anayekuwa mtumwa; ni Mungu anayemtafuta na mwenye kiu ya kuwa na mahusiano mema na mwanadamu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Kati ya majina mengi yanayoitambulisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambayo Mama Kanisa anatualika leo kukumbuka siku ile ya kuwekwa kwake rasmi, jina la ‘’ kuumega mkate’’ linabeba maana kubwa na nzuri kwetu mintarafu ujumbe wa Adhimisho la Ekaristi na amri kuu ya Upendo tunayosisitiziwa kuyatafakari leo. Wanafunzi wa Emausi walimtambua Kristo Mfufuka katika Kuumega mkate, Luka 24:35; Wanafunzi wa jumuiya zile za kwanza walidumu katika kushika mafundisho ya mitume na katika kuumega mkate. Matendo 20:7 Ilikuwa pia katika tamaduni za Kiyahudi kila mara walipokutana kwa mlo kwanza walibariki na pili kuumega mkate na ndipo mkubwa wa meza akaweza kuugawa kwa wote waliokuwa pale mezani. Tangu utotoni Yesu alishuhudia na kukuzwa katika tamaduni hiyo. Mpaka sile ile iliyotangulia mateso yake ndio naye alitwaa mkate na kuubariki na kuumega na kuwapa wanafunzi wake, na hapo ndio anabadili maana ya mazoea yale, siyo tena mkate bali ni mwili wake, sio tena divai bali ni damu yake azizi inayomwagika kwa ajili ya wokovu wetu na ulimwengu mzima.

Sehemu ya Injili takatifu kutoka Injili ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane inatuacha tunabaki na mshangao, kwani hatuoneshi jinsi Yesu alivyoweka rasmi Sakramenti ya Ekaristi, tofauti na masimulizi ya Injili Ndugu. Hotuba ya Yesu katika kalamu ile ya mwisho anatenga sura tano yaani Yohana 13-17 lakini bila kuonesha waziwazi jinsi Yesu alivyoiweka rasmi Ekaristi Takatifu, Kuumega Mkate. Badala yake katika sura ya 6 tunaona Mwinjili Yohane anatumia sura nzima ya sita kutuelezea mafundisho juu ya Yesu kama mkate wa uzima na pia karamu ya mwisho inachukua sehemu kidogo ya sura zile za Yohane 13-17. Swala ni kwa nini Mwinjili hatumii muda na nafasi ya kutosha kutuelezea juu ya Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu ambayo leo Alhamisi Kuu tunasherekea siku ile ya kuwekwa kwake?  Hakika haikusahaulika na wala si lengo la Mwinjili Yohane kuicha kwa bahati mbaya na badala yake kwa kuangalia tukio ambalo Mwinjili analielezea unaweza kupata maana na sababu za swali letu.

Badala ya simulizi la kuwekwa rasmi Ekaristi Takatifu, Mwinjili Yohane anatupa simulizi la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake. Tukio hilo linaachwa na Wainjili wengine ila tunaona ni Yohane peke yake anayelipatia kipaumbele na umuhimu mkubwa. Ni lengo la Mwinjili Yohane kwa jumuiya anayowaandikia kuwaonesha kuwa kuosha miguu na kusimikwa kwa Ekaristi ni matendo yanayoshabihiana na yenye maana moja. Si rahisi kuelewa maana ya moja kati ya haya matendo mawili pasipo kulihusianisha na lingine.  Kuosha miguu ni udhihirishaji wa kuumega mkate, ni tukio linaloonesha maana ya mfuasi wa Yesu Kristo kushiriki meza ile ya mwili na damu yake Kristo katika Ekaristi. Ilikuwa karibu na Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi, ambapo walikumbuka ukombozi wao kutoka utumwani Misri. Ni wakati huo huo pia Yesu anajiandaa kwa Pasaka yake, yaani kuukomboa ulimwengu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni kutoka katika ulimwengu huu na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, hivyo alipaswa kushiriki katika kina cha maji na giza la mateso na kifo ili kutupeleka sote katika uhuru wa kweli, yaani kuwa warithi pamoja na Mwana pekee wa Mungu.

Ni wakati wa ile saa yake, ambayo mara nyingi Mwinjili Yohane amekuwa akiizungumzia katika Injili yake. Katika harusi ya Kana (Yohane 2:4), alipogusia kuwa saa yake ilikuwa bado. Hata walipotaka kumkamata pale Yerusalemu walishindwa kwa kuwa saa yake ilikuwa bado. (Yohane 7:30; 8:20) Siku chache kabla ya mateso yake, Yesu anazungumzia juu ya kufika kwa saa yake. (Yohane 12:23,27). Saa yake ndio muda ule wa neema (Kairos) aliyoingojea kwa hamu na shauku kubwa, ni saa ile baada ya kuwapenda watu wake upeo, hivyo anajitoa yeye mwenyewe kama sadaka kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Mwinjili Yohane anaonesha juu ya Uungu wa Yesu, ndiye yeye aliyetoka kwa Mungu na kwa Mungu anarejea. Ndiye yeye anayejishusha na kujinyenyekeza kiasi cha kufanyika mtumwa, Mwana pekee ambaye kwa kumuona Yeye ni sawa na kumuona Baba. (Yohane 14:9).

Kwa desturi kabla ya kula milo ya Kipasaka, Wayahudi wachamungu walitawaza kwa maji safi. Kuanzia mkubwa wa meza mpaka kijana mdogo pale mezani walioshwa mikono na mtumishi na kama hayupo basi aliye mdogo kuliko wote aliweza kufanya utumishi huo wa kuwaosha mikono wakubwa. Wakati wa karamu ile ya mwisho kikatokea kitu au jambo ambalo halikuweza kufikirika kati yao. Mbele ya Mitume wake, Yesu anasimama na kuvua mavazi yake na kujifunga kitambaa kiunoni mwake na kuchukua chombo chenye maji na kuanza kuwaosha miguu wanafunzi wake na kuwakausha kwa mithiri ya taulo alilojifunga kiunoni mwake. Yote yanafanyika kukiwa na ukimya mkubwa. Wanafunzi wake walibaki kimya na hasa wakibaki na mshangao mkubwa, hivyo hawaamini wanayoyaona kwa macho yao. Yesu anafanya kama walivyokuwa wanapaswa kufanya watumwa au watumishi, na si tu anawaosha mikono bali anawaosha miguu, ni kujishusha na kukubali kuwa na hadhi hata chini ya ile ya mtumwa.

Yesu aliye Mwana wa Mungu; aliye mtu kweli na Mungu kweli anajishusha na kuwa mtumwa kwa wanafunzi wake. Wanafunzi wake wanabaki na mshangao mkubwa. Walikuwa na Yesu kwa miaka mitatu, walimtambua kama Kristo, na walikuwa wanangoja kwa hamu ili atawale kama ambavyo walitegemea Masiha kuwa mtawala kama watawala wa ulimwengu huu.  (Zaburi 72:8-11). Ni katika karamu ile ya mwisho tunaona mategemeo na matarajio yao yanafika ukomo, ni Yesu anawafunulia kinagaubaga juu ya Umasiha wake. Ni katika kitendo cha kuwaosha miguu wanapata sasa kumtambua kuwa huyu ni mtumishi wa Bwana, ni mtumwa, ni mtumishi na si mtawala kwa mantiki ya ulimwengu huu. Huyu ni Mungu kweli, Mungu anayekuwa mtumwa kwa mwanadamu, ni Mungu anayemtafuta na mwenye kiu ya kuwa na mahusiano mema na mwanadamu. Kinyume chake ni miungu tunayojiundia kichwani na hivyo kuwa mbali na sura halisi ya Mungu, Wengi wetu tangu utotoni labda kwa mafundisho au masimulizi tumejenga picha mbali mbali za Mungu, lakini ni katika kitendo cha kuosha miguu tunakutana na Sura halisi ya Mungu.Mungu anayekuwa na kiu na mwanadamu, anayejishusha ili mwanadamu aweze kupata hadhi ya kimungu.

Sasa tunaweza kuwelewa kwa nini Mwinjili Yohane anatoa nafasi na uzito mkubwa kwa tukio hili la kuoshwa miguu. Ni katika tukio hili kama nilivyotangulia kusema tunakutana na Sura halisi ya Mungu, Mungu anayejifanya mtumwa wa mwanadamu na si mtawala wa mabavu anayebaki katika viti vya enzi, anayengoja mwanadamu amuabudu na kumsujudu na kushindwa kufanya hivyo basi anajawa na hasira na hivyo kumwadhibu bila huruma mwanadamu, kwa kweli ni taswira potofu za Mungu ambazo tunaalikwa kubadili vichwa vyetu. Katika tafakari za Dominika 3 zilizopita nimerudia kusisitiza kuwa hatuna budi kuwa na Sura halisi ya Mungu na hasa siku hizi ambazo ulimwengu mzima umekumbwa na hofu kubwa ya janga la COVID-19. Yesu anamfunua kwetu Mungu ambaye tunakiri ni tofauti kabisa na sura ya Mungu tuliyoijenga katika akili na mioyo yetu. Mungu anayepiga magoti mbele ya mwanadamu, kiumbe wake na kumuosha miguu, kumtumikia. Huyu ndiye Mungu tunayealikwa kumwamini na kumfuata.  

Ni katika mazingira haya tunaalikwa hata nasi kutafakari nafasi za sifa ambazo mara nyingi tunapenda kujichukulia, kuitwa majina ya waheshimiwa, kuanza kuonekana na kuchukuliwa kuwa ni watu wa pekee na wa muhimu zaidi kuliko wengine, watu watusalimu kwa heshima na adabu na hata kutetemeka ikibidi, kubusiwa mikono au pete mikononi na mambo mengi ya namna hiyo. Kwa kweli ni kuwa kinyume na Injili ya Yesu Kristo, kinyume na sura halisi ya Mungu anayejifanya mtumwa na kumtumikia mwanadamu. Leo tunapoalikwa pia kuwaombea makuhani, tusali na kumwomba Mungu ili makuhani wetu waweze kutambua kuwa nao wamepakwa mafuta ili kuwa wadogo kama Kristo alite mpakwa mafuta wa kwanza, tuwaombee wavae daima vazi la udogo na utumishi katika utume wao wa kuwatumikia watu wote bila ubaguzi wala upendeleo wowote ule.

Na ndio tunaona Petro anapingana na kitendo hiki cha Yesu, kwa kweli si Mtume Petro tu bali wengi hata nyakati zetu wasiokubali sura halisi ya Mungu, Mungu anayejifanya mtumwa na kumtumikia kiumbe wake, asiyejitafutia nafasi za mbele na sifa na kusujudiwa bali kutemewa mate, kuburuzwa na kudharauliwa. Nawaalika tunaposoma masomo ya Juma kuu, basi tuyasome na kufanya tafakari ya kina. Kwetu Makasisi ni nafasi pia ya kuutafakari wito wetu wa kuwa sio tu Kristo mwingine au ‘’Alter Christus’’ bali sisi tunaalikwa kuwa ‘’Ipse Christus’’, kuwa Kristo Mwenyewe. Kwa Sakramenti ile ya daraja tunafanyika kuwa Kristo Mwenyewe na ndio maana wakati wa mageuzi hatutamki, twaeni huu ni mwili wa Kristo bali tunatamka twaeni huu ni mwili wangu, twaeni hii ni damu yangu. Na ndio maana hatuna budi kila mara kukumbuka wito wetu ni kuwa Kristo mwenyewe anayejishusha na kuwaosha miguu wanafunzi wake miguu, wito wa kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza hata chembe!

Wewe hutaniosha kamwe miguu, huu ndio msimamo wa sote tunaobaki na sura isiyokuwa sahihi ya Mungu. Yesu hashangazwi na msimamo huo wa Petro ambao pia hata leo wengi wetu bado tunao. Ni kushindwa kufikiri pamoja na Mungu bali kwa kufuata mantiki ya ulimwengu huu. (Marko 8:33), tunaalikwa kuyawaza yaliyo ya Mungu na siyo ya wanadamu. Yesu anamtaadharisha Petro kuwa kama hatakubali basi hatakuwa na shirika na naye. Yesu anamwalika Petro kutozuia mpango wa Mungu wa kujifunua kwa watu wake. Ni tukio lenye katekesi kubwa ndani yake. Ni fundisho kwa vitendo, ni Mungu anayejifunua na kutuachia somo au fundisho sisi wafuasi wake. Kuokolewa ni kukubali mpango wa Mungu katika maisha yetu, kama tunavyosoma katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipo 2:5-8, ni kukubali kujishusha, kuwa ardhini na huo ndiyo unyenyekevu tunaoalikwa kuwa nao sisi wanafunzi wa Yesu.

Baada ya mazungumzo na Petro tunaona Mwinjili Yohane anatueleza hata matendo madogo madogo aliyoyafanya Yesu katika tukio la Karamu ya mwisho. Hivyo sasa anavaa tena mavazi yake na kuketi tena. Hivyo ndio kusema kila kitendo hata kama tunaweza kuona kwa nini anakitaja ni mwaliko kujua kuwa vyote vinabeba ujumbe. Yesu alivua mavazi yake kwani kwa watumwa ili kuweza kutoa huduma kirahisi walipaswa kuvaa mavazi machache na yasiokuwa marefu. Na ndio Yesu anavua kabla ili kuwa sawa na watumwa na kufanya kile wanachofanya watumwa wanapotumikia mabwana wao. Na kwa kuvaa tena mavazi yake na kuketi tena ndio kusema sasa ni mtu huru.  Watumwa kwa upande mwingine walipaswa kuwa na mavazi ambayo yanakuwa rahisi kuwa kufanya utumishi wao na hata walipaswa kuwa wanasimama tayari kwa kufanya kadiri ya matakwa ya mabwana wao. Yesu baada ya kuwa mtumwa na hata kuteseka na kufa pale juu msalabani, anapomaliza kazi ile anarejea tena katika utukufu wake wa milele na Baba yake kumfanya aketi kuume kwake.

Tulisema mwanzoni kuwa alijifunga kiunoni kitambaa mfano wa taulo ili kutumikia na baada ya kuwaosha hatusikii tena kama alikitoa kabla ya kuvaa vazi lake. Kwa kweli ndio kusema kitambaa kile cha kutumikia alibaki nacho. Ndio kusema hakuja duniani ili awe mtumishi na arudipo kwa Baba yake kurejea kuwa mtawala. Hapana anabaki daima na sura ile ile ya utumishi kwa mwanadamu! Ni fumbo la Upendo wa Mungu kwetu wanadamu! Anabaki daima mtumishi na hiyo ndio taswira sahihi ya Mungu. Kitambaa kile mfano wa taulo alilojifunga nalo kiunoni ni ishara ya utumishi wake, ni nguo ambayo kila mkristo anapaswa kulivaa daima. Kwani wakati wowote mwingine anaweza kuwa na uhitaji nasi, akihitaji utumishi wetu, upendo wa kujitoa kwetu kwa ajili ya wengine wahitaji.

Ni kwa kuvaa vazi hilo kiunoni nasi tunatambulika kama wanafunzi na wafuasi wake Yesu Kristo.  Na ndio hapo tunaona baada ya kuwafundisha kwa matendo sasa anawaachia amri mpya ndio kupendana kama anavyotupenda yeye, ni kwa kupendana tu sisi tunatambulika kuwa ni wanafunzi wake Yesu. (Yohane 13:34-35). Mfuasi ni yule anayefuata nyao za mwalimu wake. Ni kuenenda kadiri ya mafundisho iwe ya vitendo au kwa maneno ya mwalimu. (Wafilipi 2:5; Marko 10:45). Hivyo ili kuelewa vema juu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, hatuna budi kuelewa maana ya fundisho la kuosha miguu kwa wanafunzi wake Yesu. Kushiriki Meza ya Ekaristi ni kukubali kwa hiari kamili kufuata mfano ule wa Yesu Kristo aliyejifunga kitambaa kile kiunoni ili apate kuwatumikia wengine kwa upendo. Hivyo kushiriki Mwili na Damu yake ni kukubali kuwa mwili mmoja naye. Ni kushiriki sadaka yake ya upendo kwa ajili ya wengine. Yesu anatuachia amri mpya katika Siku ya leo na ndio ya Upendo. Anatualika kupendana na kipimo cha upendo si mwingine bali ni yeye mwenyewe. Kupendana kama Yeye anavyotupenda sisi. Yohana 13:34-35.

Sisi tutajulikana kuwa ni wafuasi wake Yesu sio kwa ishara au kitu kingine chochote bali kwa kupendana. Na ndio mwaliko wa Yesu wa kujifunza kutoka kwake, kwa kuenenda kama Yeye alivyotufundisha kwa kutumikiana kwa upendo, Ekaristi Takatifu ni kukubali nasi kupendana kama Yesu anavyotoa mwili na damu yake kwa ajili ya kila mmoja wetu bila ubaguzi, anatoa mwili na damu yake si kwa ajili ya wale wanaokuwa wema tu bali ni sadaka ya upendo wa kimungu kwa kila mwanadamu, kwani Mungu anatupenda upeo, upendo usio na masharti wala ubaguzi. Mtume Paulo katika somo la pili anatualika kabla ya kushiriki kalamu ya Mwili na Damu wake Yesu kujihoji nafsini au dhamiri zetu kama kweli tunastahili na ndio kujihoji kama nasi tumejifunga kitambaa kile tayari kwa kumtumikia kwa upendo aliye mhitaji, ndio dada na kaka zetu tunaokutana nao kila siku. Petro pale ziwani aligundua kuwa yu uchi na hivyo anakosa mastahili ya kuwa mbele ya Bwana na ndio mwaliko kwangu na kwako kila mara tunapoalikwa kushiriki na kuwa Mwili mmoja na roho mmoja pamoja na Kristo. Nawaalika kwa namna ya pekee leo Alhamisi Kuu kuwaombea watumishi wote wa Ekaristi Takatifu ili daima wavae vazi la utumishi na udogo na kamwe wasifuate mantiki ya ukubwa ya ulimwengu huu.

Pasaka na tafakari njema! Mshirikishe pia jirani yako! Utamu wa tafakari ya Neno la Mungu! Kizuri wakati wa Pasaka, unakula na jirani yako!

09 April 2020, 17:02