Pasaka: Ufufuko wa Kristo Yesu ni msingi wa imani ya Kanisa!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Heri ya Pasaka! Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana, tuishangilie na kuifurahia. Kristo mkombozi wetu ameyashinda mauti na kutoka mzima kaburini, Aleluya! Nakukaribisha sasa katika tafakari ya masomo ya dominika ya Pasaka, masomo ambayo yanatutangazia na kutufafanulia Habari Njema ya ukombozi wetu kwa Fumbo la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la kwanza (Mdo. 10:34a,37-43) ni kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume. Somo hili ni hotuba au Mahubiri ambayo Mtume Petro aliyatoa katika tukio la kuongoka kwa askari mmoja aliyeitwa Kornelio. Hotuba hii ambayo ndiyo pia ilikuwa muhtasari wa mafundisho ya Mitume katika kipindi cha Kanisa la mwanzo, inaonesha kuwa kiini cha mafundisho waliyoyatoa kilikuwa ni Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo. Popote pale Mitume walipokwenda na katika mazingira yoyote walipofundisha, ujumbe walioutoa kwa nguvu zao zote ni kuwa; ‘yule Yesu wa Nazareti ambaye sisi tulimshuhudia na kukaa naye akifundisha na kutenda mema, ambaye wayahudi walimtesa na kumuua kwa kumtundika msalabani, sasa amefufuka katika wafu na sisi ni mashahidi wa Habari hiyo Njema.’
Mtume Petro anapotoa fundisho hili katika tukio la wongofu wa Kornelio anaonesha kwa namna ya pekee kuwa ndani ya Kristo kulikuwa na nguvu ya pekee kutoka kwa Mungu. Ni Mungu aliyemtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu na ni kwa nguvu hiyo Yesu alitekeleza utume uliomleta duniani. Petro anakazia kuwa nguvu hiyo ndani ya Kristo ilikuwa kubwa kiasi kwamba mabaya yote ambayo dunia iliyafanya dhidi yake hata kumuua msalabani hayakuweza kuishinda. Kristo ameyashinda yote. Hakuweza kuzimwa wala na ubaya wa dunia wala na nguvu ya mauti iliyotokana na ubaya huo. Hii ndiyo nguvu ambayo Petro anawaalika wasikilizaji wake waitegemee, waiamini na waipokee kama alivyoipokea Kornelio na kubatizwa. Pasaka tunayoiadhimisha inatangaza upya uwepo wa nguvu ya Kristo mshinda. Kama ilivyokuwa wakati wa mtume Petro, hata kwetu leo nguvu ya Kristo Mfufuka ni sababu ya furaha, uzima na matumaini ya wote wanaomkiri Kristo na kumshuhudia katika maisha yao.
Somo la pili (Kol 3:1-4) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai. Katika somo hili, Paulo anawaonesha wakolosai kuwa fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo tunaloliadhimisha wakati wa Pasaka ni fumbo ambalo kila mkristo analishiriki kwa njia ya ubatizo. Sakramenti ya ubatizo ni alama ya kila mbatizwa kufa na Kristo na alama pia ya kufufuka naye, ndiyo maana ubatizo huitwa pia sakrameti ya kipasaka. Kwa kuangalia namna ambavyo ubatizo ulikuwa unafanyika katika nyakati za mitume, alama hii itakuwa wazi zaidi. Katika nyakati hizo ubatizo uliadhimishwa kwa kumzamisha mtu, mwili mzima, katika maji na kisha kumuinua. Na baada ya hapo ndipo zilifuata alama za kudhihirisha ubatizo kama vile kupakwa Krisma takatifu, kuvikwa nguo nyeupe na kupewa mshumaa unaowaka. Kitendo cha kuzamishwa katika maji ndicho kiliwakilisha kifo kwa sababu maji mengi yalikuwa ni alama ya uharibifu na maangamizi. Kitendo cha kumuinua mbatizwa kutoka majini ndicho kiliwakilisha kufufuka pamoja na Kristo. Na ndivyo ilivyo kwa wote wanaobatizwa katika Kristo hata leo. Mtume Paulo anapowaandikia hivi Wakolosai analenga kuwaonesha kuwa ubatizo walioupokea umewapa hali na hadhi mpya katika maisha yao. Kwa ubatizo wameivaa hadhi ya Kristo au kama tusemavyo wamemvaa Kristo. Sasa, hali na hadhi yao hiyo mpya Paulo anawasisitiza waioneshe katika mwenendo ufaao wa maisha. Kwa namna ya pekee, Paulo analenga kusisitiza kipengele cha maadili yafaayo kwa mtu aliyemvaa Kristo.
Injili (Yoh 20:1-9) Injili ya dominika ya Pasaka ni kadiri ya mwinjili Yohane. Ni Injili inayoleta ushuhuda wa mwanzo kabisa waliokuwa nao wakristo juu ya ufufuko wa Yesu. Ushuhuda huu unajijenga juu ya utamaduni unaoeleza tukio la kukuta wazi kaburi alimokuwa amezikwa Yesu. Maria Magdalena, Petro na yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda hawakuweza kuelewa wala kueleza ni nani aliyeliondoa jiwe kubwa lililokuwa katika mlango wa kaburi. Hawakuweza kuelewa na kueleza ni nani aliyetoa sanda na vitambaa vilivyoufunga mwili wa Yesu na akaviweka kando. Katika simulizi hili la ufufuko wa Yesu, Mwinjili Yohane alalenga kutoa fundisho kubwa kupitia mwanafunzi ambaye hamtaji kwa jina bali anasema tu ni “yule ambaye Yesu alimpenda”. Ni mwanafunzi huyu ambaye anakimbia upesi kuliko Petro lakini haingii kaburini hadi alipoingia Petro. Ni yeye alipoingia “akaona na kuamini”. Ni kana kwamba Petro na Maria Magdalena hawakuwa bado wamefumbuliwa macho ndiyo maana injili inapoendelea inasema “kwa maana hawajalifahamu bado andiko ya kwamba imempasa kufufuka”.
Mwanafunzi huyu ni nani? Katika Injili ya Yohane, mwanafunzi huyu ambaye Yesu alimpenda anadhaniwa kuwa ni Yohane mwenyewe aliyeandika Injili hii. Lakini pia inaonekana ni kiwakilishi cha wote wanaomwamini Kristo, wote ambao Kristo alikuja kwa ajili yao na ndio hao ambao Kristo anawapenda. Mara zote ambazo Yohane anamtaja mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda ana lengo la kutoa mwaliko wa pekee kwa wote wanaomwamini Kristo. Katika Injili ya leo, mwanafunzi huyu anahusika na mambo mawili. La kwanza ni kwamba hakuingia kaburini kabla ya Petro. Hii ilikuwa ni alama ya kutambua mamlaka ya Petro kama kichwa cha mitume. Huu ni mwaliko kwa wote wanaomwamini Kristo kushikamana na uongozi wa Kanisa na kujiweka chini yake katika mang’amuzi ya kiimani. Jambo la pili ni kupokea zawadi ya imani kama ufunuo unaoweza kuliangaza giza linalozisonga akili za mwanadamu katika kuyapokea mafumbo ya kimungu. Yale waliyoyaona kaburini, yaani kaburi wazi na vitambaa vimesongwa pembeni, kwa akili ya kibinadamu hayatoshi kuthibitisha ukweli juu ya Kristo mfufuka. Na ndivyo pia yalivyo mafumbo yote ya kimungu, yanahitaji akili iliyoangazwa kwa mwanga wa imani na ufunuo kuyaelewa.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Pasaka ndiyo sherehe ya sherehe zote linazoziadhimisha Kanisa katika mzunguko wa mwaka mzima wa liturujia. Ni katika fumbo hili maadhimisho mengine yote yanatoka na katika fumbo hili yanapata kilele chake. Ni sherehe ya umuhimu na umaana mkubwa sana kwa ukombozi wa mwanadamu. Katika sherehe ya Pasaka tunaadhimisha utimilifu wa ahadi za Agano la Kale na za Yesu Kristo mwenyewe wakati wa maisha yake duniani. Ni ufufuko wa Yesu unaothibitisha ahadi hizo za kale na unaothibitisha kazi zote na mafundisho yote aliyoyatoa Kristo mwenyewe. Ni hiki tunachokikiri tunaposema “akafufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko”. Mtume Paulo naye katika waraka wake wa kwanza kwa wakorinto anakiri na kusema “kama Kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure” (1Kor 15:14). Ufufuko wa Kristo haukuwa kurudi katika maisha ya kidunia kama ilivyokuwa ufufuko mwingine alioufanya kabla ya Pasaka: kama ule wa binti Yairo au wa Lazaro. Hawa waliyarudia maisha ya kawaida ya ubinadamu na baadaye iliwapasa kufa kama binadamu wengine wowote.
Ufufuko wa Yesu ulikuwa tofauti. Ulikuwa ni kupita kutoka hali ya kifo na kuingia katika maisha mengine, maisha ya umilele yasiyofungwa na mipaka ya wakati au mahali na maisha yasiyokufa kamwe. Na ni kwa njia hiyo ametufungulia nasi waamini wake njia ya kuyaendea hayo maisha. Ufufuko wake unakuwa ni msingi na asili ya ufufuko wetu pia. Kwa kufuata mafundisho ya masomo ya leo, tumwombe Mungu atujalie neema ili kwa ufufuko wa Kristo dunia iangazwe na nguvu ya Kristo mshindi na kuwajalia watu wake wote furaha, amani na usalama. Mungu atujalie pia tutwae jukumu la kuwa mashahidi wake, tuishi kwa kuyatafuta yaliyo juu Kristo aliko na kwa nguvu ya kimungu iliyomfufua Kristo tuzishinde hofu mbalimbali zinazoyasonga maisha yetu ya kibinadamu kwa kuitumainia nguvu ya Kristo ambayo kwayo ameyashinda mauti. Heri ya Pasaka!